Na Ramadhan Juma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, ametoa msaada kwa kaya tano zilizoathirika na kimbunga katika kata mbili za Ifulifu na Bukima.
Msaada uliotolewa ni pamoja na mabati 105, mifuko ya saruji 105, mbao za kenchi 15 na misumari Kilo 56.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo vya ujenzi, Prof. Muhongo aliwataka wananchi waliokabidhiwa vifaa hivyo wavitumie kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuboresha makazi yao yaliyoharibiwa na kimbunga na si vinginevyo.
Mmoja wa wananchi waliopokea msaada huo, Tatu Richard alimshukuru mbunge kwa kuguswa na tukio lililompata na kusema kuwa pamoja na kuwa na watoto wengi bado hakuona mtoto wake hata mmoja aliyeguswa na tukio hilo.
“Mimi ni mzee, ninao watoto wengi, lakini hayupo hata mtoto mmoja kati ya wanangu aliyeguswa na tukio hili. Ninamshukuru sana mbunge wangu kwa kuniona na kunisaidia” alishukuru Tatu.
Naye Nyakaita Magati alishukuru kwa msaada wa mabati 24, saruji mifuko 40 pamoja na kilo 10 za misumari na kusisitiza kuwa hakuamini kwa kile alichokifanya Mbunge huyo kuwasaidia kurudisha nyumba zao kwenye hali nzuri baada ya kuharibiwa na upepo mkubwa.
“Siamini macho yangu kama hili linalofanyika hapa kwangu ni tukio halisi. Naona kama miujiza, hakika nina kila sababu ya kukushukuru mbunge wetu kwa kutujali, kumbe kura yetu tuliiweka panapostahili na leo tunayaona matunda yake” alisema Magati kwa furaha.
Mkazi mwingine Pili Mabele aliyekabidhiwa mabati 21, mifuko 5 ya saruji na kilo sita za misumari alimshukuru Mbunge kwa msaada aliompatia na kutoa somo kwamba ni vema kumheshimu na kumthamini kila mmoja bila kujali kama ni ndugu yako.
“Hakika ni jambo la kipekee na la kushukuru hata kama ni mbunge kuja kutoa msaada kama huu kwa mtu ambaye hana imani kama alimpigia kura. Hii imetuonesha njia kuwa kila mtu lazima amjali mwenzake hata kama siyo ndugu yake” alishukuru na kueleza Pili Mabele.
Sambamba na msaada huo, Prof. Muhongo amekabidhi Jefu Kibhisa taa moja inayotumia mwanga wa jua pamoja na chaja moja ya simu inayotumia mwanga wa jua.
Akikabidhiwa vifaa hivyo ambavyo vimeenda sambamba na msaada wa mabati 23, misumari kilo 20 na saruji mifuko 50, Jefu ameshukuru na kumpongeza Prof. Muhongo kwa jitihada za kuijali jamii ya jimbo lake.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi na uongozi wa kijiji cha Kiemba, Mwenyekiti wa kijiji hicho Golo Atanas alimshukuru mbunge kwa msaada alioutoa kwa watu walioathirika na kimbunga.
Akikamilisha ziara yake katika kijiji cha Bukima kata ya Bukima, Prof. Muhongo amemkabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi Perusi Turuka ambaye ni muhanga wa kimbunga katika kijiji cha Bukima kata ya Bukima.
Vifaa alivyokabidhiwa mkazi huyo wa Bukima ni Mifuko 5 ya saruji, mbao 15 za kenchi, mabati 10 na Kilo 10 za misumari.
Sambamba na msaada huo, Prof. Sospeter Muhongo amesisitiza suala la kilimo kuwa ndio mbinu pekee inayoweza kuondoa umaskini na njaa Tanzania hivyo wananchi wanatakiwa kulima mazao ya chakula kwa wingi na mazao ya biashara ili kuondokana na utegemezi.
“Ndugu zangu, mimi ninaamini kweli hali ya hewa haikuwa nzuri, lakini tunatakiwa tulime kilimo cha kisasa…” alisema Prof. Muhongo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Musoma vijijini, Yahana Mirumbe, alimshukuru mbunge kwa jitihada za kuwa karibu na jamii nzima ya jimbo lake na kuitaka jamii hiyo kujenga nyumba bora zenye hadhi ya kuwekwa umeme ili kuepuka madhara yatokanayo na umeme ikizingatiwa wakati wowote watawekewa umeme.