Na. Mwandishi Wetu
WANANCHI wa Jimbo la Musoma Vijijini wamempongeza Mbunge wao Profesa Sospeter Muhongo kwa kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo ndani ya mwaka mmoja.
Pongezi hizo zimetolewa na wananchi wa jimbo hilo wakati wa mkutano wa Tathmini ya Maendeleo na Uchumi ya jimbo uliofanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Murangi, Musoma Vijijini na kushirikisha wananchi wa jimboni humo, madiwani, wadau wa maendeleo na watendaji wa Halmashauri husika.
Awali akifungua mkutano huo mzee wa Kijiji cha Murangi, Musoma Vijijini, Clifford Biseko alisema wanamusoma vijijini wanajivunia maendeleo yanayodhihirika kila kukicha kutokana na mchango wa mbunge huyo.
Aliongeza kwamba Profesa Muhongo ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo na kuwa hawajuti kumchagua na wanamwombea afya njema ili azidi kushirikiana nao katika kusukuma gurudumu la maendeleo jimboni humo.
Alisema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, wameshuhudia masuala makubwa ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, sanaa na michezo.
Akizungumzia suala la afya, Biseko alisema, Musoma Vijijini haikuwahi kuwa na gari hata moja la wagonjwa, lakini tangu Profesa Muhongo awe Mbunge tayari jimbo hilo linayo magari manne.
Aliongeza kuwa Musoma vijijini haikuwahi kupata ugeni wa madaktari bingwa kwa ajili ya vipimo, ushauri na matibabu lakini kwa Profesa Muhongo hilo liliwezekana kwani alikaribisha madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi ambao walitoa huduma bila malipo.
Kuhusu suala la kilimo, Biseko alisema, tangu Profesa Muhongo achaguliwe, alisambaza tani kadhaa za mbegu za zao la mihogo na alizeti ili wananchi wajikwamue kwenye umasikini.
Aliongeza kuwa, Profesa Muhongo alipeleka wataalamu mahiri wa kilimo kutoka ndani na nje ya nchi ili kufanya tathmnini ya kilimo bora ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kilimo bora.
Aidha, suala la elimu, Biseko alisema kuwa kulikuwa na uhaba wa madawati 8,000 kwa shule zote zilizomo jimboni humo na hilo lilitatuliwa bila wao kuchangishwa pia kusambaziwa shehena ya vitabu vya sayansi kwa shule zote.
Biseko alimalizia kwa kuzungumzia sekta ya michezo na sanaa alisema kuwa Mbunge ameandaa mashindano mbalimbali na vilevile kugawa vifaa vya michezo kwenye vijiji mbalimbali jimboni humo jambo ambalo alisema limehamasisha sekta husika.