SHULE ZILIZOJENGA MAKTABA ZAPEWA ZAWADI YA KRISMASI NA MWAKA MPYA

Na. Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amegawa vitabu kwa shule sita za sekondari na shule 24 za msingi zenye maktaba ikiwa ni zawadi ya Krismasi na mwaka mpya.

Awali kabla ya kuanza zoezi hilo lililofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Etaro, Prof. Muhongo alisema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa maktaba kwa shule zote za sekondari na msingi, hivyo alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma kukutana na madiwani wake ili kuhakikisha vitabu vya awamu inayofuata shule zote ziwe zina maktaba.

“Mimi kwenye suala la vitabu nitazidi kuleta, ikiwa sisi hatuna maktaba, hawa ni watoto wa watanzania wote, nitawapatia watu wengine wavipeleke maeneo mengine” alisema Prof. Muhongo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma na diwani wa kata ya Mugango, Charles Magoma, alikiri kuwepo na mapungufu katika safu ya ufuatiliaji wa ujenzi wa maktaba kwani shule nyingi jimboni hazina maktaba.

“Ni kweli ni aibu kwetu mheshimiwa, kati ya shule 20 za sekondari tunapata shule sita  zenye maktaba na kati ya shule 111 za msingi tunapata shule 24 ambazo zina maktaba. Kwa kweli ni aibu na ni kazi ngumu tuliyonayo sasa. Sasa waheshimiwa madiwani, nadhani hili tulione kuwa ni changamoto kwetu sisi ndio wahamasishaji wa shuguli za maendeleo” alisema Magoma..

Magoma aliendelea kusema: “Mheshimiwa nimeshaamua kufanya kazi, na hili tumeshaliona kwenye halmashauri yetu, tutajitahidi ili tukuunge mkono kama ulivyoamua kulihudumia jimbo lako. Mheshimiwa tukuombe radhi, tunaenda kujipanga”