Na Ramadhani Juma
VIJANA 20 kutoka kata 6 za jimbo la Musoma vijijini walioshiriki mafunzo ya kutengeneza taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua, wamehitimu mafunzo yao katika kituo cha Bukima.
Mafunzo hayo yaliyowashirikisha vijana kutoka kata ya Rusoli, Bukima, Makojo, Bulinga, Bwasi na Bukumi yamehitimishwa rasmi 4, Machi mwaka huu katika ukumbi wa ofisi ya kata Bukima.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, vijana hao wameshukuru kupewa fursa hiyo muhimu ya kushiriki mafunzo hayo na kuahidi kuwa hawatowaangusha viongozi waliowateua na wananchi waliofanikisha uteuzi wao kwa kuhakikisha kilichofundishwa kitawasaidia kuwa walimu wa vijana wengine.
“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa viongozi na wananchi waliofanikisha kutupata, elimu na ujuzi tulioupata hapa ni njia bora ya kuwafundisha hata vijana wengine zaidi” alishukuru Anthony Zephania, mmoja wa vijana hao.
Kwa upande wake Ester Aloys alisema, Dkt. Choi amefungua njia nzuri kwao vijana kujiajiri bila kutegemea ajira kutoka serikalini kama ambavyo imezoeleka kwa vijana wengi.
“Dokta Choi umetuonesha njia nzuri, tumejifunza mengi ambayo mwanzo hatukuyajua na ametupatia ujuzi wa kudumu na sasa tunaweza kujiajiri na siyo kutegemea kuajiriwa tena. Vilevile endapo tutapata uwezesho kidogo wa vifaa, tutakuwa tumeisaidia sana jamii yetu ya kipato cha chini” alisema Ester.
Akizungumza wakati wa kuagana na wanafunzi wake Dkt. Hong-kyu Choi amewaambia kuwa, hana shaka na wao anaamini ipo siku watakutana tena Musoma vijijini na kuwasimika rasmi vijana wake na kuanza shughuli za uzalishaji zaidi kwani tayari wamejifunza na kuelewa nini kinatakiwa kifanyike.
Hata hivyo, Dkt. Choi aliongezea kuwa, haoni ugumu wa yeye kuagiza vifaa vya kutengenezea kutoka Korea kuja Tanzania endapo vijana hao wakiwa tayari na serikali ikawaunga mkono.