Na Mwandishi wetu
IDARA ya kilimo kupitia Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Musoma Godfrey Katima wamejiridhisha kuwepo kwa wadudu waharibifu wanaoshambulia zao la mahindi katika mashamba mbalimbali ya wakulima yaliyopo Musoma vijijini.
Hayo yamebainika kufuatia ziara ya afisa huyo kwenye mashamba ya mahindi na kukutana na baadhi ya wakulima kijijini Murangi katika kata ya Murangi ambapo alishuhudia kuwepo kwa tatizo hilo.
Awali akizungumza na afisa kilimo huyo, mmoja wa wakulima wa mahindi Christopher Magoti alisema, mahindi yao yameanza kupatwa na tatizo la kushambuliwa na wadudu mapema tu baada ya zao hilo kufikia katika hatua ya palizi.
Mkulima huyo alisema, wadudu hao wanashambulia zaidi majani laini yanayochipua, pamoja na kutoboa majani ya zao hilo jambo ambalo limekuwa endelevu na sasa linaonekana kuwa sugu kwani hawajapata ufumbuzi wowote wa kuweza kudhibiti tatizo hilo.
“Tukienda kwa maafisa kilimo wanatuelekeza dawa za shilingi arobaini elfu (40,000) wakati mimi hata chakula kwa siku ninashindia uji, tunaomba wakulima tusaidiwe hili, bila kusaidiwa basi hata hii mvua inayonyesha haitakuwa na faida kwetu na tutakufa na njaa kabisa” alisema na kuomba Mzee Magoti.
Mkulima mwingine Abel Biswalo alitahadharisha serikali kuwa endapo idara ya kilimo ya wilaya ya Musoma isipokuwa makini na kutimiza wajibu wake basi wilaya yao itakuwa na matukio ya njaa yasiyokoma kutokana na kupuuza majukumu yake, kwani kumekuwa na matukio ya muendelezo hasa katika sekta ya kilimo katika wilaya ya Musoma.
“Zao la muhogo lilishambuliwa, zao la viazi likavamiwa na wadudu kama ilivyo sasa kwenye mahindi na sasa mahindi nayo yamefikiwa na kama kawaida ya viongozi husika hatujajua tatizo hili litaisha lini” alibainisha Abel.
Kwa upande wake, Nyangai Ching’oro hakusita kulinganisha hali halisi iliyopo kwenye jamii zao na tatizo lililowakumba wakulima kwa sasa na kusema: “kwa kipindi kirefu jamii ya Musoma imekumbwa na tatizo la upungufu wa chakula uliosababishwa na ukame wa muda mrefu, lakini kwa sasa mvua imenyesha na wakulima wamelima kwa wingi. Tatizo kubwa lililopo ni mazao kushambuliwa na wadudu waharibifu kitu ambacho kitapelekea kuwepo na ukosefu wa chakula zaidi”
“Tumelia sana na tatizo la upungufu wa chakula kwani mvua ilikuwa hainyeshi. Mvua imenyesha, tumelima lakini mazao yanaharibiwa. Tusipokuwa makini tatizo la njaa halitokwisha na mimi naomba idara ya kilimo itimize majukumu yake kwetu wakulima ili matatizo haya yatatuliwe” alisema na kuomba Ching’oro.
Akizungumza baada ya kusikiliza vilio vya wakulima hao, Godfrey Katima aliahidi kuwasilisha taarifa ya tatizo hilo katika idara yao ya kilimo kwa ajili ya kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuokoa zao hilo huku akiwataka maafisa kilimo wa kata na vijiji kuwa karibu na wakulima kwa ajili ya msaada na ushauri zaidi.
“Poleni sana kwa tatizo hili linalowakabili. Kweli ni tatizo linalostahili hatua za haraka zaidi na mimi nitaliwasilisha kwenye idara yetu kwa ajili ya hatua zaidi. Pia niwatake maafisa kilimo wa kata na vijiji wawe karibu na wakulima na wawe tayari kutoa ushauri na msaada pale panapostahili” alisema na kuagiza Katima.