MIFUKO MINGINE 2,560 YA SARUJI YAKABIDHIWA MUSOMA VIJIJINI

saruji

Msaidizi wa mbunge Ramadhan Juma (kushoto) akiwakabidhi viongozi wa ngazi mbalimbali mifuko ya saruji. Kutoka kulia ni Mwalimu Biego Marogoi, Diwani wa Kata ya Bwasi Masatu Nyaonge na Mtendaji wa kijiji cha Busekera Dorica Togora.

Na Mwandishi Wetu

MIFUKO 2,560 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari za jimbo la  Musoma vijijini imekabidhiwa kwa walengwa.

Hiyo ni awamu ya pili ya mpango huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa unaofadhiliwa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, ambapo awamu ya kwanza mifuko 2,560 pamoja na mabati 1,296, yalitolewa kwa shule za msingi 39 na shule tatu za sekondari.

Katika awamu hiyo ya kwanza, zaidi ya vyumba 60 vimejengwa, katika awamu hii ya pili, shule za msingi 27 na shule za sekondari 4 zimepata mgao wa saruji hiyo ambapo utekelezaji wa ujenzi unaanza.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mifuko hiyo ya awamu ya pili, msaidizi wa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Ramadhani Juma, amewaomba viongozi wa vijiji na kata mbalimbali walioshiriki kuchukua saruji hiyo kuitumia kwa muda muafaka na kwa matumizi yaliyokusudiwa ambayo ni ujenzi wa vyumba vya madarasa na si vingine.

“Ndugu waheshimiwa viongozi mliochukua saruji hii, tunawaomba mjitahidi sana kuhakikisha inatumika kwa haraka sana na kwa kazi lengwa ikiwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa” alisema msaidizi huyo.

Aidha, aliongezea kwa kuwataka viongozi hao wajitume katika usimamiaji na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo ili kuendana na kasi ya awamu ya tano na hatimaye kukamilisha hatua hiyo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuingia kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

“Vile vile viongozi mjitahidi na mjitume sana kufuatilia na kusimamia kuhakikisha shughuli za maendeleo zinaenda kwa kasi ili tuweze kukamilisha hili zoezi la vyumba vya madarasa. Pia hatutakubaliana na ubadhilifu wowote utakaojitokeza juu ya matumizi ya saruji hii, atakayefanya vitendo hivyo atawajibika” alisisitiza.

Akizungumza baada ya kupokea mifuko hiyo, diwani wa kata ya Bwasi, Masatu Nyaonge alisema, mifuko 120 aliyopewa kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili ambazo ni shule ya msingi Bwasi B pamoja na kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi Kome B, utakuwa umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuahidi kusimamia matumizi sahihi ya saruji hiyo.

“Kwa idadi hii ya mifuko 120 mlionikabidhi, ujenzi wa shule hizi Kome B na Bwasi B utafanikiwa kwa kiasi kikubwa na ninakuhakikishia kuwa saruji hii itatumika kwa wakati na kwa matumizi sahihi” alisema diwani Nyaonge.

Naye Mtendaji wa kijiji cha Busekera Dorica Togora, ameshukuru kwa mchango huo wa mifuko 60 ya saruji na kusema ana uhakika wa kukamilisha zoezi la ujenzi wa vyumba viwili mapema mwezi wa nne kama hali ya hewa itakuwa nzuri.

Mtendaji Dorica aliongezea kuwa, ana imani na wananchi wake kuhusu ushiriki wao katika maendeleo kwani mpaka sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili na ofisi moja kwa nguvu na michango yao wenyewe.

Kwa upande wake, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Makojo Biego Marogoi kwa niaba ya viongozi na wananchi wa jimbo la Musoma vijijini, ametoa shukrani za dhati kwa Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini kwa jitihada zake za kuboresha miundo mbinu katika sekta ya elimu.

“Kwa niaba ya viongozi wote wa jimbo hili la Musoma vijijini na wananchi wote, napenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kabisa kwa mbunge wetu Prof. Muhongo kwa jitihada anazozifanya katika miundo mbinu ya elimu. Nasi tunaahidi kumuunga mkono na kuanza ujenzi huu mapema zaidi” alishukuru na kuahidi mwalimu Marogoi.

Baada ya awamu hii ya pili kukamilika, zaidi ya vyumba 100 vya madarasa vitakuwa vimejengwa. Upatikanaji wa vyumba hivi utasaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani hali inayochangia kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu.