MKUU WA WILAYA YA MUSOMA AHITIMISHA HUDUMA YA MATIBABU YA BURE

Madaktari bingwa kutoka China wakiwa katika maandalizi ya kuanza kutoa huduma ya matibabu katika zahanati ya Kwikuba.

Na. Fedson Masawa

MKUU wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amefunga huduma ya matibabu iliyokuwa ikitolewa na madaktari bingwa kutoka nchini China katika zahanati mbili za Musoma vijijini.

Huduma hiyo iliyoanza 7, Mei, 2017 katika zahanati ya Nyambono na kuendelea kwa muda wa siku nne, imehitimishwa rasmi 10, Mei katika zahanati ya Kwikuba.

Akitoa taarifa ya huduma hiyo kwa niaba ya Mganga mkuu wa zahanati ya Kwikuba, Elly Hassan ambaye ni mganga muuguzi katika zahanati hiyo, alisema wananchi waliojitokeza kupata vipimo na matibabu kwa siku nne ni 2,034 ambapo 844 walijitokeza kwenye zahanati ya Kwikuba na 1,190 zahanati ya Nyambono.

Akizungumza wakati wa kufunga huduma hiyo, Dkt. Anney kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameishukuru serikali ya China na timu ya madaktari hao kwa ushirikiano mzuri waliouonesha kwa kukubali wito kutoka kwa Prof. Muhongo kuja kutoa huduma ya matibabu ndani ya jimbo lake.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa, huduma iliyotolewa na timu hiyo ni huduma ambayo kwa asilimia kubwa isingekuwa rahisi kwa jamii ya watu maskini kuimudu, lakini wamefanikiwa kuipata bila malipo.

“Na nzuri zaidi wamekuja kutibu akina mama ambao wanaishi vijijini ambao kwa namna yoyote ile wasingeweza kupata hiyo huduma. Sasa tumewatembelea huku na wameonwa, na hiyo imesaidia wenzetu wachina kufahamu wananchi wenye matatizo makubwa ambayo wanakaa nayo nyumbani bila kupata matibabu. Mfano, akina mama 20 wamepata rufaa kwenda hospitali ya mkoa wakatibiwe” alisema Dkt. Naano.

Aidha, Dkt. Naano aliwasisitiza wananchi wa Musoma na Tanzania kwa ujumla kuuendeleza na kuudumisha uhusiano na urafiki uliopo baina ya serikali hizo mbili kwani wanatambua umuhimu na kazi kubwa inayofanywa na serikali ya China nchini Tanzania.

“Urafiki wetu kati ya China na Tanzania ulianza siku nyingi sana mpaka tukawa na kiwanda kinaitwa Urafiki, wachina walitujengea reli ya kati. Hili linadhihirisha kwamba urafiki wetu ni wa shida na raha na bado wanaendelea, wanajenga bandari ya Bagamoyo. Kwa hiyo hawajaishia tu katika kutoa matibabu” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.

Hata hivyo, katika kupiga hatua ya maendeleo zaidi ndani ya wilaya ya Musoma, Dkt. Naano amewasihi wananchi na viongozi kumuunga mkono kikamilifu mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutumia fursa zinazopatikana ndani ya wilaya yao ili kujihakikishia maendeleo chanya hasa katika mpango wa serikali kuu wa uchumi wa viwanda.

Dkt. Naano alisema, kutokana na serikali kupungukiwa katika sekta ya afya hasa upande wa madawa, wilaya ya Musoma imepewa fursa ya kujenga kiwanda cha kutengeneza bandeji na maji ya dripu ambayo yatakuwa yananunuliwa na MSD.

“Sisi serikali tunapungukiwa, hasa madawa na huduma mbalimbali, ndugu zetu wachina mlioko hapa, sisi tumepewa fursa kama wilaya tumeombwa tujenge kiwanda cha kutengeneza maji ya dripu, hicho kiwanda soko lake tumepewa na MSD. Tunahitaji tuwe na uchumi wa viwanda, sisi Musoma tunahitaji tuwe na kiwanda cha kutengeneza bandeji na maji ya dripu” alisema na kutoa changamoto kwa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya  Musoma vijijini kuandaa fedha kwa ajili ya kuanza zoezi la kujenga kiwanda hicho haraka iwezekanavyo.

“Kiwanda hicho, kitakuwa kimetengeneza fursa mbalimbali za ajira kwa jamii ya watu wa Musoma pamoja na Tanzania kwa ujumla. Vile vile kiwanda kitakuwa kimezuia kabisa hela nyingi zinazopelekwa nje kama vile Uganda na India ambako maji hayo yanayotumika kwenye hospitali zote nchini yanatoka huko” alisema.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Kwikuba Kamunyiro Kubega kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho na Jimbo la Musoma vijijini, ametoa shukrani za dhati kwa Prof. Muhongo kwa jitihada kubwa anazozifanya kwa wananchi wake ikiwemo kuleta madaktari bingwa na kutoa huduma ya matibabu.

“Ninamshukuru sana Prof. Muhongo kwa kutuletea madaktari bingwa ili kutoa huduma kwenye zahanati yetu, tuko pamoja na yeye. Naishukuru pia serikali ya Tanzania na China na timu ya madaktari bingwa kutoka China kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha huduma ya matibabu inawafikia wananchi na kuhudumiwa bure kabisa na huduma hii imewafikia karibu na tayari afya zao zitakuwa na auheni hivyo zitawawezesha kuendelea na shughuli zao za maendeleo.” alisema Mwenyekiti Kubega.