BUKIMA, BUTATA NA KASTAM WAHAMASISHWA KUSAKA MAENDELEO

Na. Mwandishi Wetu

ZIARA ya kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo imefanyika katika vijiji vitatu vya kata ya Bukima ambavyo ni Bukima, Butata na Kastam ambapo wananchi wametakiwa kujitokeza kuunga mkono jitihada zinazofanywa na mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo.

Viongozi mbalimbali akiwemo Diwani wa kata ya Bukima, viongozi wa serikali kutoka kata ya Bukima na vijiji vyote vitatu vya kata hiyo pamoja na wataalamu mbalimbali wa na msaidizi wa mbunge walishiriki ziara hiyo.

Akizungumza kwenye moja ya mikutano ilifanywa wakati wa ziara hiyo katika kijiji cha Bukima, msaidizi wa Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Fedson Masawa alisema kwa kipindi kifupi tangu alipochaguliwa, mbunge amechangia saruji mifuko 60, madawati 41 katika shule ya msingi majita A na madawati 95 katika shule ya msingi majita B.

Prof. Muhongo pia ametoa msaada wa mbegu za alizeti, mtama na mbegu za mihogo kwa wakulima mbalimbali wa kijiji cha Bukima sambamba na kushirikiana kwa ukaribu na wananchi wake katika matatizo mbalimbali kama majanga ya asili yakiwemo kimbunga na misiba.

Msaidizi huyo alisema, katika sekta ya afya Prof. Muhongo ametoa magari madogo manne katika zahanati nne za jimbo la Musoma vijijini ambazo ni Kurugee, Nyasulula, Mugango na Masinono magari ambayo yanafanya kazi jimbo zima kutokana na uhitaji wake.

Mbali na magari hayo manne, Prof. Muhongo ametoa gari moja kubwa ambalo lipo katika kituo cha afya cha Murangi huku akiahidi kutafuta gari jingine kubwa kwa ajili ya kubebea wagonjwa.

Akizungumzia suala la maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, afya na kilimo Fedson alisema ili mbunge aweze kufanikisha kuondoa changamoto zinazozikabili sekta hizo, wananchi wanapaswa kumuunga mkono kwa hali na mali katika utekelezaji huo kwa wakati muafaka.

“Ndugu wananchi wa kijiji cha Bukima, Mbunge wetu anahitaji ushirikiano mkubwa sana kutoka kwenu wananchi na viongozi, michango yenu, nguvu zenu na moyo wenu wa kujitolea ndio utakaomfanya mbunge kumaliza changamoto zinazowakabili” alisema.

Aidha, aliwataka wananchi wa kijiji cha Bukima kujituma katika kuchangia ujenzi wa wodi ya akina mama na watoto ili kuharakisha kasi ya ujenzi wa zahanati ya Bukima kuwa kituo cha Afya kutokana na wingi wa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika zahanati hiyo.

Katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, aliwashukuru viongozi na wananchi wa kijiji cha Bukima kwa hatua nzuri ambayo wamefikia ya kujenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya mwalimu katika shule ya msingi Majita B.

Kwa upande wa sekta ya kilimo, amewasisitiza wananchi kujituma katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kujikwamua kiuchumi huku akiwataka kuwa tayari kwa mtambo wa kusindika alizeti ambao unafanyiwa utaratibu wa kufungwa katika kata ya Suguti.

Kaimu Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Bukima Benarld Mirobo akizungumza kwa niaba ya serikali ya kijiji hicho alisema, wananchi kwa sasa wapo pamoja na watafanya kila linalowezekana kwa hali na mali kuanza mara moja ujenzi wa wodi ya akina mama na watoto kama walivyoanza katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.