MKUU WA WILAYA YA MUSOMA ATEMBELEA WAATHIRIKA WA MAFURIKO

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano (wa pili kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Bugunda Manyama Malembo (kulia) wakati alipofika kuangalia athari zilizosababishwa na kubwa iliyonyesha siku kadhaa zilizopita (Picha na Fedson Masawa).

Na. Mwandishi Wetu

MKUU wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amewatembelea waathirika wa mafuriko katika kijiji cha Kastam kilichopo kata ya Bukima wilaya ya Musoma vijijini.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya aliongozana na viongozi mbalimbali wa kata ya Bukima na kijiji cha Kastam pamoja na msaidizi wa Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini.

Awali akiwasilisha taarifa fupi ya uharibifu uliotokea, Mtendaji wa kijiji cha Kastam Joseph Phinias alisema,  jumla ya kaya 19 nyumba zao zimebomoka wakati kaya 17 zilikumbwa na mafuriko na nyingine zaidi zikipata nyufa kubwa huku akisisitiza kuwa, kaya zilizobomolewa nyumba zao tayari kaya mbili tu hadi sasa zimekwisha hama maeneo hayo.

Phinias alisema, pamoja na kuwepo kwa uharibifu katika majengo, mazao mengi yamesombwa na maji jambo ambalo linaweza kusababisha tatizo la njaa hapo baadaye.

Akigusia suala la barabara, mtendaji huyo alisema, barabara ya kuingia Kastam kwa sasa imekatika, hivyo hairuhusu tena gari lolote wala pikipiki kuingia na kushauri mamlaka husika kuiwahi barabara hiyo ili kuepusha kukwama kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Naye Diwani wa kata ya Bukima, January Simula alisema, mvua iliyonyesha kwa kipindi cha siku mbili, kata yake ilikumbwa na madhara makubwa, lakini kijiji cha Kastam ndicho kilichokumbwa na madhara makubwa zaidi kwani nyumba nyingi, mashamba yaliyokuwa na mazao takribani ekari 300 yameharibiwa na mvua.

Diwani Simula ameweka wazi kuwa, tayari serikali imeshawaagiza wananchi ambao nyumba zao zipo mabondeni wahame mara moja na kuelekea kwenye makazi mengine.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, amewapa pole wananchi na viongozi wa kata ya Bukima na kijiji cha Kastam kwa tatizo lililowapata na kuwaagiza wananchi walioko mabondeni wahame mapema ili kuepuka mafuriko yanayoweza kujitokeza zaidi.

“Nawaomba wananchi wenzangu, nawaagiza serikali ya kijiji na vitongoji wahame kwenye maeneo ya mabondeni mpaka mvua itakapopungua lasivyo watakuja kupata madhara makubwa sana” aliagiza Dkt. Naano.

Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza, wananchi ambao wanaendelea kuishi kwenye nyumba zilizo na nyufa pia wahame ili kuepuka madhara zaidi hasa kupoteza maisha ya jamii.

“Kwahiyo maeneo yote muwaambie wananchi serikali za vijiji, wenyeviti wa vitongoji wananchi wasikae kwenye nyumba zile zilizopasuka kwa maana zitaleta madhara makubwa na hata kupoteza maisha” alisisitiza Dkt. Naano.

Aidha, Dkt. Naano aliwaagiza watendaji kuorodhesha kaya zote zisizo na vyoo vya kudumu hasa kipindi hiki cha mvua na kuzifikisha kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua kwa lengo la kuepukana na madhara ya kipindupindu.

Hata hivyo, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Karebu Musululi ameishukuru serikali kwa wepesi wake na ushauri wao na kusema hali hiyo inaleta faraja na matumaini kwa watu wake na sasa wao wataufanyia kazi ushauri wa serikali ili kuokoa maisha yao

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amemuagiza Mhandisi wa wilaya ya Musoma kwa kushirikiana na wakala wa usimamizi na ujenzi wa barabara (TANROADS) kuharakisha ujenzi wa daraja kubwa lililopo mpakani mwa kijiji cha Bulinga (kata ya Bulinga) na kijiji cha Bugunda (kata ya Bwasi).

Mkuu wa wilaya ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo hilo na kushuhudia daraja hilo ambalo lilivunjika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha 7, Novemba na kusababisha barabara ya Bukima hadi Kome kutopitika.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Bugunda Manyama Malembo alisema, kuharibika kwa daraja hilo kumechangia shughuli nyingi za kiuchumi kukwama, hivyo ni muhimu serikali kuharakisha ujenzi mpya wa daraja hilo.

“Toka daraja hili livunjike, shughuli nyingi za kiuchumi zimekwama, tunaomba tu serikali itusaidie kulishughulikia suala hili.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi wa sekondari ya Nyanja wanaotoka kata ya Bulinga walisema, wana wasiwasi wa kukosa masomo na hata kuhatarisha maisha yao kwani barabara hiyo inapitika kwa shida na wengine ilifikia hatua wakaanza kutoa fedha kwa ajili ya kuvushwa hadi upande wa pili.