MBUNGE MUSOMA VIJIJINI AKAGUA MIRADI YA ZAHANATI NA SHULE

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini akisikiliza maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule ya msingi Nyausungu.

Na Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amefanya ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika vijiji vya Bukima, Kasoma na Nyasaungu inayotekelezwa kwa michango ya wananchi, fedha za mfuko wa jimbo pamoja na Mbunge.

Katika ziara yake hiyo, Prof. Muhongo amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Majita “B” iliyopo kijiji cha Bukima kata ya Bukima pamoja na jengo la akina mama na watoto linalojengwa katika zahanati ya kijiji cha Bukima ikiwa ni hatua ya awali ya upanuaji wa zahanati hiyo kuwa kituo cha afya.

Akiwa katika kijiji cha Kasoma kilichopo kata ya Nyamrandirira, Prof. Muhongo amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kasoma “A” na Kasoma “B” ambapo alitumia muda wa dakika 45 kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Kasoma kuhusu shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Prof. Muhongo alisema, wananchi hao wamefikia hatua nzuri kinachotakiwa sasa ni kuondoa makundi ya kisiasa, kujituma katika shughuli za maendeleo, kujitoa katika michango mbalimbali ya kimaendeleo ili kufanikisha shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa na zahanati bila kutegemea serikali kuu na wafadhili peke yao.

Akikamilisha ziara yake jimboni katika kijiji cha Nyasaungu kata ya Ifulifu, Prof. Muhongo alikagua miradi ya vyumba viwili vya madarasa ambavyo vinajengwa kwa nguvu za wananchi, saruji kutoka kwa mbunge, mabati kutoka kwa mbunge na fedha za mfuko wa jimbo; mchango ambao kwa pamoja umekamilisha ujenzi na upauji wa vyumba hivyo viwili vya madarasa shuleni hapo.

Kwa upande wa ujenzi wa zahanati, Prof. Muhongo ameahidi kupitia ofisi yake jimboni kufuatilia ili kupata ufumbuzi wa kufanikisha shughuli za ujenzi katika kijiji hicho na yeye yupo tayari kuungana na wananchi katika shughuli zote hizo.

Hata hivyo, amewaahidi wananchi wa jimbo lake kuwa, atatoa mchango wake katika shughuli yoyote ya maendeleo ambayo ni moja ya vipaumbele vyake jimboni.

Alisema, ni lazima wananchi waoneshe mfano kwanza kabla ya serikali au wafadhili wengine na kusema, yupo bega kwa na wananchi waliokwishaanza kazi hizo, sasa anasubiria taarifa ya kurudi tena ili aweke mchango wake katika maeneo yote yanayojenga zahanati na vituo vya afya na zahanati kama vile Bukima, Nyasaungu, Nyambono na maeneo mengine jimboni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa jimbo la Musoma vijijini wamemshukuru mbunge wao Prof. Muhongo kwa kuwaunga mkono katika kuboresha huduma ya afya jimboni pamoja na elimu na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikia maendeleo bora katika sekta ya elimu na afya.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Bukima, diwani wa kata ya Bukima January Simula alisema, jitihada za wananchi wa kijiji cha Bukima zimeanza kuonekana kwa vitendo, ndio maana tayari hatua za maendeleo zimeanza kwa kasi kubwa.

Diwani huyo alisema, tayari vyumba viwili vimekamilika katika ujenzi wa shule mpya ya Majita “B” kwa kushirikiana na Mbunge wao pamoja na upanuzi wa zahanati ya Bukima.

“Wananchi wangu wana hamasa kubwa ya kushiriki katika maendeleo na hata jitihada hizi za ukamilishaji wa vyumba viwili ni sehemu ya michango yao na michango ya mbunge. Tutaendelea kutoa ushirikiano Mheshimiwa mbunge na ujio wake hapa leo kama alivyosema ni lazima tumrudishe kama si kuweka jiwe la msingi basi vyote pamoja na msaada wake” alisema Simula.

Kwa upande wake Juma Maungo ambaye ni mwananchi wa kijiji cha Kasoma, amemshukuru mbunge wao Prof. Muhongo kwa jitihada ambazo ameshazifanya na anazoendelea kuzifanya katika jimbo la Musoma vijijini ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu, kilimo na afya na wamemuahidi mbunge wao kumpa ushirikiano mkubwa katika shughuli zote za maendeleo.

“Mheshimiwa mbunge kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu kwako kwa jitihada zote unazozifanya na hata unavyoendeleza shughuli za maendeleo jimboni. Kwa kusema hivyo, napenda nitamke wazi kwamba sisi tutakuunga mkono kwa nguvu zote ili tulisukume gurudumu la maendeleo jimboni” alishukuru mwananchi huyo.

Hadi sasa Prof. Muhongo tayari amechangia madawati 8,000 ambayo yameshasambazwa katika shule zote za msingi katika jimbo la Musoma vijijini, amechangia mabati na saruji kwenye shule za masingi na sekondari jimboni.

Aidha, mbunge huyo ametoa magari matano ya wagonjwa katika zahanati nne na kituo cha afya kimoja cha Murangi.

Hata hivyo, katika kuhakikisha hatua za mapambano katika kufanikisha maendeleo ya elimu jimboni mwake, Prof. Muhongo ameshagawa vitabu zaidi ya 10,000 katika awamu nne kwa shule zote za sekondari na msingi za jimbo lake na vitabu zaidi ya maboksi 2500 ambavyo aligawa kwa wabunge wengine wa mkoa wa Mara.