KABURI LA MWALIMU NYERERE LAFANYIWA UKARABATI

Msaidizi wa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini, Fedson Masawa akikabidhi vifaa kwa ajili ya ukarabati wa kaburi la hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa wafanyakazi na wanafamilia wa Mwalimu Nyerere.

Na. Mwandishi Wetu

FAMILIA ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kushirikiana na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo wameanza ukarabati wa kaburi la Baba huyo wa Taifa lililopo nyumbani kwake katika kitongoji cha Mwitongo, wilaya ya Butiama Mkoani Mara.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Prof. Muhongo kuitembelea familia hiyo mwishoni mwa mwaka jana ambapo pamoja na mazungumzo yao, familia hiyo ilisema rangi iliyokuwa imepakwa kwenye kaburi hilo imepoteza mvuto na wana mpango wa kulifanyia ukarabati kwa kupaka rangi (mausoleum) na kunyunyizia dawa kwa ajili ya kuua na kuzuia wadudu wanaokaa kwenye paa la kaburi hilo.

Kutokana na hilo, wakamuomba Prof. Muhongo aungane nao katika kufanikisha zoezi hilo ambalo limeanza rasmi Januari, 4, 2018 ambapo mbunge huyo amesaidia gharama za ufundi, vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na rangi kwa ajili ya kupaka kaburi na mawe yaliyomo ndani ya nyumba aliyokuwa anaishi Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Mwalimu Nyerere, Rehema Haruna alimshukuru Prof. Muhongo kwa mchango alioutoa ili kufanikisha zoezi la ukarabati na kusema wao kama wanafamilia watatoa ushirikiano mkubwa katika kukamilisha shughuli zote hizo na kutoa mahitaji mengine yatakayohitajika.