Na Fedson Masawa
HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Musoma Vijijini, Mkoani Mara imefanya kikao maalum kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wilaya hiyo na kukubaliana kuwaunganisha wananchi bila kujali itikadi zao za vyama.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya wilaya, pia kilihudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Musoma ambaye pia ni mjumbe, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini aliyewakilishwa na Msaidizi wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma na Madiwani wote wanaotokana na chama hicho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma na mwenyekiti wa kikao hicho Nyabukika Bwire, aliwataka viongozi wa kata kusimamia na kufuatilia utendaji kazi wa viongozi kuanzia ngazi ya mashina, matawi, kata hadi wilaya hasa katika uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mwenyekiti huyo alisema, ili kufanikisha hayo suala la mawasiliano baina ya viongozi katika chama na serikali ni muhimu katika kuondoa tofauti za utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney aliwashukuru wananchi wanaoendelea kuungana na serikali katika kufanikisha suala la kuchangia elimu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara pamoja na vyumba vya madarasa na kusema hatua hiyo imefikia pazuri.
“Shule nyingi za sekondari na msingi bado zina changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo kukaa chini na serikali inaendelea kufanya jitihada kwa kushirikiana na wazazi kuhakikisha tatizo hilo linakoma” alisema Dkt. Naano.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Charles Magoma alisema, kwenye shule za msingi na sekondari kumejitokeza changamoto ya upungufu wa madawati haswa kwa wanafunzi wapya wanaojiunga darasa la kwanza na kidato cha kwanza.
“Suala la madawati ni changamoto katika shule zetu za sekondari na msingi hasa pale wanafunzi wanapojiunga kidato cha kwanza na darasa la kwanza. Sisi halmashauri tumeshakubaliana tutashirikiana na wazazi katika kufanikisha suala la madawati katika shule zetu” alisema Magoma.
Akitoa taarifa kwa wajumbe wa kikao hicho, Katibu wa CCM wilaya ya Musoma Joseph Gatty alisema, katika kufanikisha kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo alichangia usafiri kwa wajumbe 108 ili kuhakikisha wanawahi kufika kwenye kikao na kurudi majumbani mwao kwa wakati uliopangwa.
Kutokana na mchango huo, Gatty alimpongeza Prof. Muhongo kwa jitihada anazoendelea kuzifanya katika kufanikisha shughuli mbalimbali za chama na serikali ndani ya Mkoa wa Mara.