PROF. MUHONGO AWATAKA WANANCHI KIJIJI CHA NYASAUNGU KUKAMILISHA UJENZI WA ZAHANATI

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika leo kwenye kijiji cha Nyasaungu.

Na. Verediana Mgoma

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amewataka wananchi wa kijiji cha Nyasaungu kuweka nguvu zao katika kumalizia ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho uliosimama kwa miaka sita.

Prof. Muhongo alisema hayo leo wakati wa ziara yake aliyoifanya kwenye kijiji hicho, ambapo aliwataka wananchi hao kujitolea kwa hali na mali kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo mapema na kuahidi iwapo watakamilisha ujenzi huo kufikia Juni, mwaka huu, atachangia mabati kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo ili wananchi wa kijiji hicho wawe karibu na huduma ya afya.

Aidha, katika mkutano huo Prof. Muhongo alichangia mifuko 100 ya saruji pamoja na shilingi 200,000 kwa ajili ya malipo ya fundi na wananchi waliendesha harambee na kufanikiwa kupata fedha ambazo zitatumika kununua mifuko 109 ya saruji.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyasaungu Magesa Chacha alisema, zahanati ya Nyasaungu ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2012, ambapo walikuwa wakichangia nguvu kazi na fedha, hata hivyo ujenzi huo ulisimama kwa muda baada ya kuwepo kwa changamoto za ukosefu wa fedha, vitendea kazi na wataalamu.

“Baada ya kilio chetu kufika ofisi ya mbunge, tulipata ushirikiano wa kutosha wa namna ya kufanikisha ujenzi wa zahanati ya Nyasaungu, mpaka sasa wananchi wameongeza nguvu zao na kukusanya mchanga, mawe pamoja na kufyatua matofali” alisema Chacha.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyasaungu Manyama Meru, alitoa shukrani za pekee kwa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini kwa kuweka nguvu kwenye sekta ya afya ndani ya kata hiyo na kuwasaidia wananchi wa kijiji cha Nyasaungu kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Musoma Thadeus Makwanda aliahidi kutoa ushirikiano kwa wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni pamoja na kumpeleka mkandarasi kutoka Halmashauri ili kuwaelekeza namna ya kujenga zahanati hiyo kitaalamu.