Na. Verdiana Mgoma
MAADHIMISHO ya siku ya wanawake duniani Jimbo la Musoma vijijini yameadhimishwa kwenye kijiji cha Bwai Kumsoma kwa kufanyika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza kwenye sherehe hizo mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney aliwataka wanafunzi wa kike wa shule ya msingi Bwai kusoma kwa bidii ili wakabiliane na vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike kwa kuzitambua haki zao.
Dkt. Naano alisema, Serikali inaendelea na jukumu lake la kumlinda na kutetea haki ya mtoto wa kike ili aweze kutimiza malengo aliyojiwekea bila kujali itikadi za kisiasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Musoma Flora Yongolo alisema, lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuongeza mshikamano wa wanawake na kuhimiza mapambano dhidi ya ukatili wa mtoto wa kike ili kutimiza malengo ya kufikia kwenye uchumi wa kati.
Mkurugenzi huyo alisema, kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kudhibiti baadhi ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya mwanamke kwenye jamii za vijijini, ingawa jitihada zaidi zinahitajika ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.
Akieleza jukumu la Serikali kwa kushirikiana na vitengo vya haki za binadamu alisema, wameendelea kutoa ushirikiano hasa kwenye usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke kisiasa, kiuchumi, kielimu na kiafya ili aweze kufikia malengo.
Mkurugenzi Yongolo aliendelea kusema, katika uundaji wa majukwaa ya kuwawezesha wanawake kiuchumi, wametoa elimu kwa vikundi vya wanawake vinavyojishughulisha na ushonaji, ubunifu, ujasiliamali kwa kutengeneza vitu vya asili na makundi mengine ya wanawake.
Aidha, Yongolo aliwataka akina mama kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kujiinua kiuchumi ambapo vikundi vya akinamama kutoka vijiji vya Suguti, Lyasembe, Nyambono na Mugango vilikabidhiwa mashine za umwagiliaji.
Mbali na mashine hizo, katika maadhimisho hayo shilingi milioni 23 zilitolewa kwa vikundi 10 vya akina mama na vijana kwa ajili kujiendeleza katika shughuli za kilimo na biashara.
Vikundi vilivyopokea fedha hizo ni Kikundi cha akinamama cha Mshikamano, We grow, Jitahidi ufaidike, Nyakabhungo, Juhudi, Jaribu, Bomafa, Amani na Upendo na kikundi cha Karpentas.
Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo aliungana na akinamama kuadhimisha kilele cha siku ya wanawake duniani kwa kutoa mchango wa miche ya miti ili kuwahamasisha watoto wa kike kulinda mazingira ambapo katika sherehe hizo miti 3,000 ilipandwa kwenye shule ya Msingi Bwai.
Prof. Muhongo pia alitoa mabati 54 kwa kikundi cha wanawake wa kijiji cha Bwai Kumsoma (We grow) kwa ajili ya kuezeka vyumba vya madarasa vilivyojengwa na kikundi hicho.