Na Fedson Masawa, Msaidizi wa Mbunge
18 – 09 – 2018
WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amefanya ziara ya Ukaguzi wa Utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini wa REA III ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini ambapo pia ametumia fursa hiyo kuzungumza na wananchi wa Jimbo hilo kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo Umeme Vijijini.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara leo Agosti 18, 2019 Kijijini Nyakatende, Dkt. Kalemani amewahakikishia wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini kwamba TAASISI, maeneo mbalimbali ya UWEKEZAJI na VITONGOJI vyote 374 vya Jimbo VITAPATA UMEME.
Awali akieleza kuhusu kero ya Umeme Musoma Vijijini, Waziri Kalemani amesisitiza kuwa Prof Muhongo aliomba Umeme kwenye Vijiji vyake vyote 68 na amepewa Vijiji vyote katika Mradi wa REA III
Akisisitiza juu ya jambo hilo, Dkt. Kalemani amesema kuwa kazi ya Mkandarasa ni kuhakikisha anapeleka umeme Vijiji vyote 68 vyenye VITONGOJI 374 katika awamu hii ya REA III
“Hakuna kijiji, hakuna kitongoji na hakuna mwananchi atakayerukwa katika Mradi huu” Amesisitiza Mhe Dkt. Kalemani
Aidha Waziri Dkt Kalemani ametoa maelekezo ya Uboreshaji wa Utekelezaji wa Mradi wa REA III mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Madiwani na WANANCHI wa Musoma Vijijini.
Dkt. Kalemani amewaagiza watendaji wake kufanya kazi bila kuondoka saiti hadi watakapokamilisha kazi hiyo.
“Mkandarasi nataka usihamishe genge, peleka genge kila kijiji. Badala ya kuhamishahamisha,” alisema Waziri wa Nishati Mhe Dkt Kalemani.
Vilevile, Dkt. Kalemani ameshiriki Tukio la Kuwasha Umeme Kijijini Nyakatende kuashiria Uzinduzi rasmi wa Mradi wa REA III Musoma Vijijini.
Katika Ziara yake hiyo, Dkt Kalemani aliongozana viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake ambao ni pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu TANESCO, Kaimu Mtendaji Mkuu wa REA, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mara, Engineer wa TANESCO Kanda ya Ziwa (Mwanza), Engineer wa Miradi ya REA Kutoka Makao Makuu, na Mkandarasi wa Mradi wa REA III Mkoa wa Mara.
Dkt. Kalemani amehitimisha ziara yake Jimboni kwa kutoa pongezi nyingi kwa Mbunge wa Jimbo, Prof Muhongo kwa Jitihada kubwa za Maendeleo anazozifanya. akishirikiana na Mkuu wa Wilaya, Dr. Vicent Naano na Viongozi wengine. Mhe Waziri amewataka Madiwani na Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha Jimbo la Musoma Vijijini linapiga hatua kubwa za kimaendeleo.