VIKUNDI VYA WATU WENYE ULEMAVU VYANUFAIKA NA MIKOPO KUTOKA HALMASHAURI NA BMZ

Baadhi ya Wanachama wa SHIVYAWATA ERUSULI wakiwa kazini kwenye MRADI wao wa UFUGAJI wa kuku wa kienyeji Kijijini Bwai Kumusoma, Kata ya Kiriba.

Jumatatu, 02.09.2019
Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma yenye Jimbo la Musoma Vijijini INAENDELEA kutekeleza AGIZO la SERIKALI la kutoa MIKOPO kwenye MAKUNDI 3, yaani VIJANA, WANAWAKE na WATU WENYE ULEMAVU. Mikopo inatolewa kila Mwaka.
Baadhi ya WATU WENYE ULEMAVU ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini WANAENDELEA kupokea MISAADA ya aina mbalimbali kutoka kwenye MRADI wa BMZ wa Serikali ya Ujerumani.
BMZ (Bundesministerium fuer wirtschaftliche Zusammenarbeit und Entwicklung, in English: The Federal Ministry of Economic Cooperation and Development) ina MRADI wa KUSAIDIA WATU WENYE ULEMAVU, wakiwemo WANAFUNZI, kwenye  Kata 10 za Jimbo la Musoma Vijijini. MISAADA hiyo ni pamoja na: Matibabu kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Rorya, KMT SHIRATI, Vifaa Maalum vya Kujimudu, Vifaa vya Shule kwa Wanafunzi, na Mikopo midogo midogo kwa Watu Wenye Ulemavu.
Kikundi cha Watu wenye Ulemavu cha SHIVYAWATA ERUSULI (Wanachama 15) kilichoko Kijijini Bwai Kumusoma, Kata ya Kiriba, kimeanzisha MRADI wa UFUGAJI wa KUKU wa kienyeji baada ya kupokea MKOPO wa Shilingi Milioni 2 kutoka HALMASHAURI ya Wilaya ya Musoma.
Akizungumza na Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Msimamizi wa Mradi huo, Ndugu Malandala Titi Masau ameeleza kwamba wametumia FEDHA za MKOPO huo kujenga banda la kuku, kununua vifaa vya kulishia kuku, chakula na madawa ya kuku. Malengo ni kuanza kufuga kuku 100 na hadi juzi walikuwa wameishanunua kuku 64.
Ndugu Titi Masau ameongezea kuwa, mbali ya MKOPO wa Halmashauri yao, SHIVYAWATA ni miongoni mwa Vikundi vya Watu Wenye Ulemavu vilivyo ndani ya MRADI wa BMZ ambao tayari  umetoa MKOPO wa Tsh 575,000/= kwenye Kikundi hicho. VIKUNDI vingine 9 navyo vimepokea MIKOPO kutoka kwenye MRADI huu.
Ndugu Hawa Daniel, Mwanachama wa Kikundi cha SHIVYWATA ERUSULI, kwa niaba ya Wanachama wenzake, ameshukuru sana HALMASHAURI yao na MRADI wa BMZ kwa kuwawezesha Watu Wenye Ulemavu kuanzisha MIRADI itakayowafanya WAJITEGEMEE ki-uchumi.