Jumatano, tarehe 4.12.2019, VIONGOZI wa MABARAZA ya WAZEE ya Ushauri, Ushawishi, Utamaduni na Maadili ya VIJIJI waliwasilisha TATHMINI za MIRADI YA UCHUMI na MAENDELEO ya VIJIJI vyao.
KIKAO hicho kilifanyika Kijijini SUGUTI chini ya Uenyekiti wa Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo.
TATHMINI za Vijiji zimewasilishwa na Mwenyekiti na Katibu wa Baraza la kila Kijiji. Jimbo lina Kata 21 na Vijiji 68. KIKAO cha VIONGOZI wa MABARAZA ya KATA kitakafanyika baadae.
TATHMINI zilifanyika kwenye SEKTA za: (i) Elimu, (ii) Afya, (iii) Kilimo, Uvuvi na Ufugaji, (iv) Mazingira na (v) Michezo na Utamaduni. Vilevile, TATHMINI zimeongelea MIRADI ya maji, umeme, barabara, vyombo vya usafirishaji na mawasiliano.
MAAZIMIO:
Baada ya uwasilishi na mjadala kukamilika, yafuatayo ni MAAZIMIO yatakayofikishwa Vijijini kwa UTEKELEZAJI:
(1) Hakuna Wanafunzi kusomea CHINI ya MITI. Kila Shule kijijini iwe na Vyumba vya Madarasa ya kutosha. MABARAZA yatashawishi na kushauri kazi hii ikamilike ifikapo 30 Juni 2020.
(2) MABARAZA yatashawishi na kushauri UPANDAJI wa MITI kwa WINGI kwa kila Kijiji. MICHE ya BURE inapatikana kwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Musoma.
(3) MABARAZA yatashawishi na kushauri Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kuunda VIKUNDI vya UCHUMI na kuomba MIKOPO kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma yenye Jimbo la Musoma Vijijini.
(4) MABARAZA yatashawishi na kushauri WAKULIMA na WAFUGAJI kuunda VIKUNDI VYA KILIMO vya kutumia PLAU (majembe ya kulimia yanayokokotwa na ng’ombe).
ZAWADI YA KRISMASI YA PLAU KWA VIKUNDI VYA KILIMO
Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo ATATOA ZAWADI YA PLAU (tarehe 24.12.2019) kwa VIKUNDI VYA KILIMO vilivyokuwa vya kwanza kuundwa na kuanza kazi.
VIKUNDI hivyo vinatoka Vijiji (14) vya: Bukima, Butata, Chitare, Chumwi, Kamguruki, Kwibara, Mabui Merafuru, Nyakatende, Nyegina, Mikuyu, Rusoli, Suguti, Tegeruka na Wanyere.