VIJIJI VYAGAWANA KAZI KUHARAKISHA UJENZI WA VYUMBA VIPYA VYA MADARASA NA OFISI ZA WALIMU

KIKAO (ndani ya Bugwema Sekondari) cha Mbunge wa Jimbo Prof Sospeter Muhongo na Wanavijiji wa Kata ya Bugwema.

Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
Wananchi wa Kata ya Bugwema WAMEAMUA kuharakisha UJENZI wa VYUMBA 4 VIPYA vya Madarasa na OFISI 2 za Walimu kwenye Sekondari yao ya Kata (Bugwema Secondary School) ndani ya MWEZI MMOJA (ifikapo tarehe 28.2.2020). UAMUZI huo ulitolewa na WANAVIJIJI wa Kata hiyo walipotembelewa na Mbunge wao Prof Sospeter Muhongo.
Kata ya Bugwena ina VIJIJI 4 – Bugwema, Kinyang’erere, Masinono na Muhoji.
Vijiji vya  Masinono na Kinyang’erere wako kwenye hatua ya UPAUAJI wa Vyumba 2 VIPYA vya Madarasa na OFISI 1 ya Walimu. Vijiji vya Bugwema na Muhoji navyo vinapaswa kukamilisha ujenzi wao unaofanana na ule wa Vijiji vya Masinono na Kinyang’erere.
Mwalimu Mkuu wa  Bugwema Sekondari, Mwl Ndaro Emmanuel amesizitiza kuwa Wananchi wa Kata ya Bugwema na Kata nyingine WANAPASWA kutatua mapema tatizo la UHABA wa Vyumba vya Madarasa ili WANAFUNZI ambao ni WATOTO wao waweze kupata ELIMU BORA wakisomea ndani ya Vyumba vizuri vya Madarasa vikiwa na idadi ya Wanafunzi wanaotakiwa badala ya KURUNDIKANA. Mwalimu huyo aliendelea kwa kusema kwamba tatizo la MIRUNDIKANO ya Wanafunzi madarasani likitatuliwa, UFAULU kwenye Mitihani ya Taifa ya  KIDATO CHA PILI NA CHA NNE utaongezeka.
Mwalimu Mkuu huyo  alieleza kuwa Jumla ya Wanafunzi wa Kata ya Bugwema waliochaguliwa kujiunga na masomo ya Kidato cha kwanza mwaka huu (2020) ni 249, na hadi sasa (wiki jana), Jumla ya Wanafunzi 114 (45.78%) walikuwa wameripoti shuleni na hao wote wamerundikana kwenye Chumba 1 cha Darasa la Form I.
Diwani wa Kata hiyo, Mhe Ernest Maghembe AMEOMBA WADAU mbalimbali WAJITOKEZE kuungana na Wananchi wa Kata ya Bugwema kujenga na kuboresha MIUNDOMBINU ya ELIMU kwenye Kata hiyo.
Diwani huyo na Wananchi kwa ujumla WANAMSHUKURU sana Mbunge wao wa Jimbo kwa kuisaidia Bugwema Sekondari kwa kutoa VITABU zaidi ya 1,000 (elfu moja), kuleta WADAU wa kuboresha MAABARA, kutoa POSHO ya Mwalimu wa Kujitolea wa Masomo ya Sayansi. MFUKO wa JIMBO umechangia Saruji Mifuko 70.