Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
SEKONDARI YA NYAKATENDE ilianzishwa Mwaka 2006 na kwa sasa ina Jumla ya Wanafunzi 737 na Walimu 23, akiwemo mmoja wa kujitolea. Jumla ya Walimu wa MASOMO ya SAYANSI ni 5.
Sekondari hii inahudumia KATA 2 za NYAKATENDE (Vijiji 4 – Kakisheri, Kamguruki, Kigera na Nyakatende) na IFULIFU (Vijiji 3 – Kabegi, Kiemba na Nyasaungu).
Mwalimu Mkuu wa Nyakatende Secondary School, Mwalimu Halima Yusuph Suleiman amesema jumla ya WANAFUNZI 269 wamechaguliwa kutoka VIJIJI 7 hivyo kuendelea na Masomo ya Kidato cha Kwanza (Form I) Shuleni hapo. Hadi sasa WANAFUNZI 213 wameisharipoti shuleni na tayari wako masomoni.
Mwalimu Mkuu huyo amesema kwamba vipo jumla ya Vyumba 5 kwa ajili ya Wanafunzi ya FORM I na kuna UPUNGUFU ya Chumba kimoja.
Mtendaji Kata (WEO) ya Nyakatende, Ndugu Martha Omahe Gagiri amesema kuwa Kata zote 2 (Nyakatende na Ifulifu) na Vijiji vyake vyote 7 wameamua kuunganisha nguvu ili kuharakisha ujenzi wa chumba hicho kimoja ambacho wanatarajia kukikamilisha kabla ya tarehe 15 Februari 2020.
Akiwa katika ZIARA ya uhamasishaji wa ujenzi wa Vyumba Vipya vya Madarasa Katani Nyakatende (6.1.2020), Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alisema atachangia SARUJI MIFUKO 50 na MABATI 27 ili kukamilisha ujenzi wa chumba hicho kimoja.
Wakati huo huo, Kata pekee ndani ya Jimbo isiyokuwa na Sekondari yake, yaani Kata ya IFULIFU, WANANCHI wake WAMEAMUA KUJITEGEMEA kwa kujenga Sekondari zao MPYA, yaani NYASAUNGU SECONDARY SCHOOL (inajengwa na Kijiji kimoja cha Nyasaungu) na IFULIFU SECONDARY SCHOOL (inajengwa na Vijiji 2 vya Kabegi na Kiemba). Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo anaendelea KUCHANGIA VIFAA VYA UJENZI kwenye ujenzi huu. Sekondari MPYA hizi zitakamilishwa kwa ajili ya kuchukua Wanafunzi wa Form I kabla ya Juni 2020.
Kwa upande wake, Kata ya Nyakatende inajenga SEKONDARI YA PILI kwenye Kijiji cha Kigera ambayo
inajengwa na Vijiji 2 vya Kigera na Kakisheri. Itakuwa tayari kuchukua Wanafunzi wa Form I mwakani (Jan 2021).
UJENZI HUO HAPO JUU UKIKAMILIKA utatatua matatizo ya UMBALI MREFU wa kutembea (Wanafunzi & Walimu) na MIRUNDIKANO madarasani kwenye Kata za Nyakatende na Ifulifu.