SERIKALI YATOA SHILINGI MILIONI 400 KUJENGA KITUO CHA AFYA NA WANANCHI WAJIONGEZA ILI KUPATA  MIUNDOMBINU ZAIDI

WANAVIJIJI wakiwa kwenye kazi za upanuzi wa ZAHANATI ya Masinono kuwa KITUO cha AFYA cha Kata ya Bugwema.

Jumamosi, 30.5.2020
Jimbo la Musoma Vijijini
Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge.
HALMASHAURI ya Musoma (Musoma DC) ina Jumla ya VITUO VYA AFYA 2 (Murangi & Mugango) na sasa inapanua ZAHANATI ya MASINONO kiwe KITUO CHA AFYA cha Kata ya Bugwema.
WANANCHI na VIONGOZI wa Kata ya Bugwema wakiongozwa na Diwani wao, Mhe Ernest Maghembe, na Halmashauri yote wanatoa SHUKRANI nyingi na za dhati kwa SERIKALI yao kwa kutoa Tsh MILIONI 400 kwa ajili ya MRADI wa kupanua Zahanati hiyo iwe KITUO cha AFYA cha TATU ndani ya Halmashauri yetu yenye Jimbo la Musoma Vijijini.
MIUNDOMBINU YA HUDUMA ZA AFYA JIMBONI MWETU
* HOSPITALI ya WILAYA inajengwa. Serikali imetoa Tsh BILIONI 1.5. Wananchi na Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo, nao wanachangia ujenzi huu.
* VITUO vya AFYA 2 (Murangi na Muganga). Kituo cha tatu (Bugwema) kinajengwa.
* ZAHANATI 24 za Serikali na 4 za Binafsi zipo zinatoa huduma.
* ZAHANATI MPYA 14 zinajengwa kwa ushirikiano wa Serikali, Wanavijiji, Wazaliwa wa Jimboni na Mbunge wa Jimbo.
KITUO CHA AFYA KIPYA CHA BUGWEMA
Kata ya Bugwema inaundwa na Vijiji vinne: Bugwema, Kinyang’erere, Masinono na Muhoji. Vijiji hivi 4 vina ZAHANATI moja tu ya Kijijini Masinono ambayo Mbunge wa Jimbo aliipatia GARI la WAGONJWA (Ambulance).
MGANGA MFAWIDHI wa Zahanati ya Masinono, Ndugu Mzalendo Wambura, ameeleza kuwa Zahanati yao imekuwa ikitoa huduma kwa jumla ya Wagonjwa wa Nje (OP) wapatao 17,000 (elfu kumi na saba) kwa mwaka. Kwa siku moja wamekuwa wakipokea Wagonjwa wa Nje kati ya 70 na 100.
Aidha, Mganga huyo ameendelea kufafanua kuwa katika shughuli za Ujenzi wa kupanua hiyo Zahanati kuwa Kituo cha Afya, wamepanga kujenga MAJENGO SABA (7):  (i) Wodi ya Mama na Mtoto, (ii) Maabara, (iii) Jengo la Upasuaji, (iv) Jengo la Kufulia, (v) Jengo la Maiti (mortuary), (vi) Vyoo vya nje, na (vii) Miundombinu/Mfumo wa kutolea Taka. Ujenzi umeanza kwa kasi kubwa.
AFISA MTENDAJI Kata ya Bugwema, Ndugu Alphonce Nyamgambwa  amesema kuwa Wananchi wa Kata hiyo wameupokea MRADI huo kwa furaha tele na utayari mkubwa wa kuutekeleza.
WANAVIJIJI wanachangia NGUVUKAZI (kusomba maji, mawe na mchanga) na FEDHA taslimu ambapo KILA KIJIJI kitachangia jumla ya Tsh MILIONI 33.5.
WANAVIJIJI watachangia TRIPU 600 za MCHANGA na nusu yake tayari imepatikana. MAWE yanapatika kwenye kimlima jirani na Zahanati inayopanuliwa.
MICHANGO YA MBUNGE WA JIMBO
Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo atachangia SARUJI MIFUKO 400 kwa MRADI huu wa Kata ya Bugwema. Mbunge huyo amechangia kiasi cha SARUJI kama hicho kwenye uboreshaji na upanuzi wa VITUO vya AFYA vya Murangi na Mugango.
Vilevile, Mbunge huyo ametoa MAGARI YA WAGONJWA (Ambulances) kwa VITUO vya AFYA vya Murangi na Mugango. Ambulance ya Murangi ni ya kisasa sana kwani UPASUAJI (operation) unaweza kufanyika ndani ya gari hilo.