Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
Tarehe, 18.11.2020
KATIBU MKUU wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Idara ya MIFUGO, Prof Elisante Ole Gabliel amezindua Kampeini ya UHIMILISHAJI wa NG’OMBE (Artificial Insemination) kwa WAFUGAJI wa Musoma Vijijini.
Tukio hilo lililofanyika Kijijini Bugwema, lilihudhuriwa na WAFUGAJI na VIONGOZI mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dr Vincent Naano Anney, Madiwani Wateule na Wasaidizi wa Mbunge. WANANCHI wasio Wafugaji nao walihudhuria uzinduzi huo.
Prof Elisante ole Gabriel alieleza kwamba LENGO KUU la UHIMILISHAJI ni UPANDIKIZAJI wa MIMBA kwenye NG’OMBE (wakiwemo wa kienyeji) kwa kuweka MBEGU ya NG’OMBE wa KISASA kwa njia ya MRIJA ili kuongeza UBORA na WINGI wa MIFUGO (ng’ombe) hiyo.
KATIBU MKUU huyo alisisitiza kuwa MIFUGO ni UTAJIRI, na kwamba WAFUGAJI wanapaswa kuwa tayari kutoa USHIRIKIANO mkubwa kwa WIZARA ili kuanzisha Miradi ya UFUGAJI wa KISASA wenye NG’OMBE BORA (maziwa mengi, nyama laini, ngozi nzuri, n.k.).
WAFUGAJI wa Kata ya Bugwema, kwa niaba ya Wafugaji wa Musoma Vijijini, wameishukuru sana SERIKALI kwa kuwasogezea huduma hiyo ya UHIMILISHAJI na wameahidi kutoa USHIRIKIANO mkubwa wa kuboresha UFUGAJI wao kwa njia hii ya UHIMILISHAJI wa ng’ombe wa kienyeji.
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini