HATIMAYE MUSOMA VIJIJINI WAANZA KUPATA BARABARA YA LAMI

Mradi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Musoma-Makojo-Busekera (km 92) unaanza kuweka matumaini.

KILOMITA 5 KUKAMILIKA OKTOBA 2022

Kampuni ya Gemen Engineering inayojenga kilomita hizo tano (5) imesema itakamilisha na kukabidhi kipande hicho cha kilomita 5 ifikapo tarehe 30.10.2022. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Injinia Andrew Nyantori.

Leo, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alikagua ujenzi wa barabara hilo ili ajiridhishe na ahadi ya Mkandarasi huyo.

UMUHIMU WA BARABARA HILI KIUCHUMI

Barabara hili ndiyo roho ya ukuaji wa uchumi wa Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, Vijiji 68 na Vitongoji 374.

Samaki wengi na wa aina mbalimbali wanaovuliwa Ziwa Victoria wanasafirishwa kutoka Musoma Vijijini kwenda kwenye masoko mbalimbali ya ndani na ya nje ya nchi yetu kwa kutumia barabara hili.

Mazao ya chakula ambayo nayo ni ya biashara (k.m. mihogo, mahindi, viazi vitamu, mpunga, na matunda) yanasafirisha kutumia barabara hili.

Musoma Vijijini ni maarufu kwa kilimo cha pamba. Barabara hili ndilo linatumika kusafirisha pamba kutoka vijijini mwetu kwenda sokoni.

Dhahabu na madini mengine yanayochimbwa Musoma Vijijini yanasafirishwa kwa kutumia barabara hili.

UMUHIMU WA BARABARA HILI KWA HUDUMA ZA JAMII

*Hili ndilo barabara kuu na pekee linalounganisha vijiji vyote 68 vya Jimboni mwetu. Kwa hiyo, hili barabara ni muhimu sana kwa usafiri wa wananchi ndani na nje ya Jimbo letu.

*Hili ndilo barabara kuu na pekee ambalo linatumika kwa usambazaji wa vifaa vya elimu, huduma za afya, kilimo, ufugaji, maji, umeme, n.k., ndani ya Jimbo letu.

*Wagonjwa wanaohitaji matibabu kwenye hospital kubwa za Musoma, Mwanza, n.k. wanatumia barabara hili.

OMBI KWA SERIKALI

*Kasi ya ujenzi iongezeke kwa kuongezewa bajeti ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara hili.

SHUKRANI KWA SERIKALI

Tafadhali sikiliza CLIP/VIDEO yenye shukrani nyingi kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan.

Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz

Tarehe:
Jumatano, 14.9.2022