BULINGA SEKONDARI KUKAMILISHA MAABARA YA FIZIKIA MWEZI AGOSTI 2024

Jimbo la Musoma Vijijini lina mradi kabambe wa ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi (fizikia, kemia na baiolojia) kwenye Sekondari zake zote za Kata. Wananchi na Serikali yetu wanashirikiana vizuri sana kwenye utekelezaji wa mradi huu.

Jimbo hili lina Sekondari za Kata 26 na wanavijiji wanajenga nyingine 10. Sekondari za Binafsi ni mbili (2).

Bulinga Sekondari ni ya Kata ya Bulinga yenye vijiji vitatu (3) ambavyo ni: Bujaga, Bulinga na Busungu. Ilianza kutoa elimu ya masomo ya sekondari Mwaka 2016, na kusajiliwa rasmi Mwaka 2019.

Bulinga Sekondari inazo maabara mbili (2) za masomo ya kemia na bailojia ambazo zinatumika. Maabara moja ya somo la fizikia hakijakamilishwa.

Sekondari hii yenye wanafunzi 610 ilitembelewa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, kwa lengo la kufuatilia ustawi wake na kupokea orodha ya mapungufu ya shule hii. Hiyo ilikuwa tarehe 12.4.2024

Vilevile, Mbunge huyo aliwakaribisha wananchi kutoka vijiji vitatu vya Kata ya Bulinga kwa lengo la kupokea na kutatua matatizo na kero zao.

Wananchi hao waligawiwa vitabu viwili viwili (Volumes III&IV) vinavyoelezea mafanikio makubwa yanayopatikana kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 ndani ya Jimbo letu.

Ukamilishaji wa Maabara ya Fizikia:
Kikao cha Mbunge wa Jimbo wa Jimbo, wananchi wa Kata ya Bulinga, walimu na baadhi ya wanafunzi wa Bulinga Sekondari kiliazimia yafuatayo:

(i) Maabara ya Fizikia iliyojengwa hadi usawa wa renta ikamilishwe kabla ya tarehe 30.8.2024

(ii) Mabati ya rangi 120 yanayohitajika:
* Kila kijiji kichangie mabati 24, jumla mabati 72
* Mbunge wa Jimbo achangie mabati 24
* Halmashauri yetu ichangie mabati 24

(iii) Mbao na misumari
Wanavijiji na Mbunge wao wamejiwekea utaratibu wa kununua vifaa hivi vya ujenzi.

Michango yote iliyoainishwa hapo juu iwasilishwe kwa Mkuu (Headmaster) wa Bulinga Sekondari ifikapo tarehe 15.8.2024

Michango kutoka kwa Wana-Bulinga na Wadau wengine wa maendeleo:

(i) Wanaopenda kuchangia vifaa vya ujenzi:
Wanaombwa waviwasilishe kwa Mkuu (Headmaster) wa Bulinga Sekondari

(ii) Michango ya fedha ipelekwe kwenye Akaunti ya Shule ambayo ni:
Benki: NMB
Akaunti Na: 30310029434
Jina: Bulinga Secondary School

KARIBUNI TUKAMILISHE UJENZI WA MAABARA YA FIZIKIA YA BULINGA SEKONDARI

Picha za hapa zinaonesha:
Wanafunzi wa Bulinga Sekondari wakiwa kwenye kipindi cha mafunzo kwa vitendo (practicals) ndani ya Maabara yao ya Kemia

Boma la Maabara ya Fizikia linalohitaji ukamilishwaji. Mbunge wa Jimbo alikabidhi Saruji Mifuko 100 ya ukamilishaji wa maabara hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini akiongea na wananchi wa Kata ya Bulinga kwenye eneo la Bulinga Sekondari

Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz

P. O. Box 6
Musoma

Tarehe:
Jumatatu, 15.4.2024