Na. Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Zahanati ya Kigeraetuma iliyopo Kijiji cha Kamuguruki, ikiwa ni zawadi ya sikukuu ya Krismasi.
Zawadi hiyo ilitolewa 25 Desemba kijijini humo katika hafla ya chakula aliyoiandaa kwa ajili ya wananchi wa Kijiji hicho pamoja na vijiji vingine.
Katika hafla hiyo Profesa Muhongo aliongozana na familia yake pamoja na rafiki zake kutoka Ujerumani ambao kwa pamoja walijumuika na wananchi wa Musoma vijijini kusherehekea.
Awali kabla ya hafla hiyo, Profesa Muhongo na ujumbe wake walishiriki ibada katika kanisa la Menonite lililopo katika kijiji cha Nyakatende na baada ya ibada hiyo walielekea katika kijiji cha Kamguruki kwa ajili ya chakula.
Mara baada ya kumalizika kwa ibada, Profesa Muhongo aliahidi kuchangia uendelezaji wa ujenzi wa kanisa hilo, na kuagiza tathmini ifanyike ya kubaini mahitaji ili achangie.
Akiwa katika kijiji cha Kamguruki, alielezwa changamoto na mahitaji mbalimbali ya kijiji hicho ikiwemo ya ukamilishwaji wa ujenzi wa zahanati husika.
“Ikiwa ni zawadi yangu ya Krismasi kwenu, nitatoa mifuko 300 ya saruji ili kuendeleza ujenzi wa zahanati,” alisema.
Profesa Muhongo alisema 26 Desemba kutakuwa na kikao cha wabunge wote wa Mkoa wa Mara kitakachofanyikia wilayani Butiama lengo likiwa ni kujadili kilimo na maendeleo ya pamoja ya Mkoa huo.
Alisema fedha za jimbo kiasi cha shilingi milioni 38 zimetumika kama ilivyokubaliwa kwa kununua mbegu za mihogo ambazo zitagawiwa kwa wananchi. “Nikimaliza huko kikao nitarudi huku kuwaletea mrejesho lakini pia kugawa mbegu za mihogo,” alisema.
Mbali na hilo, Profesa Muhongo alisema Balozi wa Korea Nchini, Song, Geum-Young anataka kutengeneza ajira kwa vijana waliohitimu Kidato cha Nne ambao hawakupata fursa ya kujiendeleza.
Alitambulisha teknolojia ya umeme jua kwa ajili ya taa na kuchaji simu ambayo alisema Balozi huyo kupitia mtaalamu wake anatarajia kuipeleka jimboni humo kwa kuwafundisha utengenezaji wake vijana hao.
“Hiki kifaa cha umeme jua kikitengenezwa gharama yake ni 15,000 kwa hiyo vijana watapewa mafunzo ya namna ya kuvitengeneza na watauza ili kujipatia kipato,” alisema.
Alisema Februari mwakani, Balozi huyo na mtaalamu wake watafika jimboni humo kwa ajili ya kutambulisha vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na kuandaa mafunzo na hivyo aliwataka wazazi wawaruhusu vijana wao kushiriki mafunzo husika.