Na Ramadhan Juma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amezindua mafunzo ya utengenezaji wa taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua.
Mafunzo hayo yanayofanyika kwenye kijiji cha Nyegina, yanawahusisha vijana 100 kutoka vijiji mbalimbali vya jimbo hilo, yana lengo la kutengeneza ujuzi na ajira kwa vijana hao.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Prof. Muhongo alisema mafunzo hayo mbali na kuzinduliwa Nyegina, yatafanyika kwenye kijiji cha Mugango, Bukima, Busekera na Saragana ambapo kila kituo kitakuwa na vijana 20 na mafunzo yatatolewa kwa siku tatu kwa kila kituo.
Prof. Muhongo alisema, baada ya mafunzo katika vituo hivyo vitano, vituo hivyo vitavunjwa na kuunda vituo viwili, kituo cha kwanza kitakuwa Nyegina na kingine kitakuwa Murangi ambapo kila kituo kitakuwa na vijana 50 kwa ajili ya kuwafanyia mazoezi ya mwisho.
Akizungumzia soko la vifaa hivyo, Prof. Muhongo alisema, baada ya vifaa hivyo kutengenezwa, vijana hao watakuwa wanaviuza kati ya 15,000 hadi 20,000 ambapo malighafi za kutengenezea vifaa hivyo watapelekewa, hivyo amewataka vijana jimboni humo kuchangamkia fursa hiyo.
Awali, Balozi wa Korea nchini Tanzania Song Geumyoung alisema, Korea itaendelea kudumisha uhusiano wao na Tanzania na sasa takribani miaka 20 toka mataifa haya yaingie katika uhusiano wao, bado wataendelea kudumisha uhusiano huo.
Aidha, Balozi Geumyoung alisema, vifaa hivyo vitasaidia kupunguza tatizo la umeme vijijini na hata mijini hususani kwa wale wasio na uwezo wa kupata umeme na kutoa ajira kwa vijana wengi.
“Miaka 20 ya uhusiano wa Korea na Tanzania, tutaendelea kudumisha uhusiano huu na tutasaidiana na Tanzania kusambaza umeme vijijini. Vilevile vifaa hivi vitawasaidia vijana hawa kujitengenezea ajira na pia vitasaidia wanafunzi kujisomea wakati wa usiku” alisema Balozi Geumyoung.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya Musoma Vincent Naano Anney, ameishukuru serikali ya Korea kwa hatua nzuri ya kuanzisha teknolojia ya utengenezaji wa taa na chaja zinazotumia mionzi ya jua kwani ni hatua pekee ya kuondoa utegemezi na umasikini kwa vijana wa Musoma na pia kuwaomba kuendelea na jitihada hizo ili kusaidia jimbo la Musoma vijijini na Tanzania kwa ujumla.
Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Choi Hong Kyu, alisema hatua ya kwanza ya mafunzo hayo ni kuwajengea vijana hao uwezo wa kujiamini na kisha watafundishwa ujuzi wa utengenezaji wa vifaa hivyo.
“Tunataka kuwatengenezea vijana ajira binafsi na hatimaye kuacha utegemezi na kuondokana na shughuli nyingine zisizo halali. Hivyo nawaomba waonyeshe ushirikiano wa hali ya juu katika kupokea kile watakachofundishwa” alisema Dkt. Choi Hong Kyu.