WANANCHI MUSOMA VIJIJINI WATAKIWA KUWEKA KANDO SIASA NA KUCHAPA KAZI

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo (wa kwanza kushoto waliokaa) akiwa na viongozi mbalimbali wa serikali, aliyesimama ni Thereza Rusweka, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kurugongo A.

Na. Mwandishi wetu

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ametaka wananchi na viongozi jimboni kwake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa linakwisha jimboni humo.

Prof. Muhongo ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kurugongo A na Kurugongo B zilizopo katika kata ya Bulinga ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kukutana na kuwapa pole wananchi walioathiriwa na kimbunga katika kijiji cha Musanja ambapo jumla ya nyumba 21 ziliezuliwa na upepo.

Akiwa katika shule ya msingi Kurugongo, Prof. Muhongo alishuhudia na kujiridhisha na hali halisi ya upungufu wa jumla ya vyumba 6 vya madarasa kwa shule zote mbili, hivyo kusababisha jumla ya madarasa 10 kusomea nje kwenye vivuli vya miti ya shule hiyo.

Awali akiwasilisha taarifa ya upungufu wa madarasa na mwenendo mzima wa taaluma ya shule hiyo, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kurugongo A, Thereza Rusweka alisema, shule hizo zote zina uhaba wa vyumba 16, na kusababisha madarasa 10 kupata elimu wakiwa katika vivuli vya miti.

“Kwa kipindi kirefu tumekuwa katika mazingira haya haya, wanafunzi wengi waliopita wamesomea kwenye madarasa haya haya…cha ajabu sasa mvua ikija hakuna shule tena” alisema Mwalimu Thereza.

Akiwa katika hatua ya kupambana na tatizo la upungufu wa madarasa, Prof. Muhongo amewataka wananchi wa kata ya Bulinga na kata zote za Musoma vijijini kuwekeza nguvu zao katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha wanamaliza tatizo sugu la upungufu huo wa vyumba vya madarasa.

Prof. Muhongo aliongeza kuwa, yupo bega kwa bega na wananchi wa Musoma vijijini katika kusukuma gurudumu la maendeleo jimboni mwao na kuwataka wananchi waachane na itikadi za kisiasa kwa kipindi hiki cha utekelezaji wa maendeleo kwani si muda wake, kwa sasa waungane pamoja katika kufanya maendeleo kwenye maeneo yao.

“Tuwekeze nguvu kwenye madarasa, mimi Mbunge wenu nipo pamoja nanyi kwa kila kitu. Saruji ikija chapeni kazi, mabati yakija chapeni kazi. Ndani ya miaka miwili au mitatu mtaona mabadiliko. Wakati wa maendeleo mfanye kazi ya maendeleo, siasa wekeni pembeni” alisema na kusisitiza Prof. Muhongo.

Kata ya Bulinga ni moja ya kata 21 za jimbo la Musoma vijijini ambazo tayari Prof. Muhongo amekwisha kuchangia vifaa vya ujenzi kwa ajili ya vyumba vya madarasa ambapo katika shule ya Msingi Kurugongo A, Prof. Muhongo amechangia jumla ya mifuko 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa. Shule ya msingi kurugongo “B” amechangia jumla ya mifuko 110 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa.

Pia, mbunge huyo amechangia jumla ya mifuko 60 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili katika shule ya msingi Busungu na kuchangia mifuko 70 ya saruji katika shule ya sekondari Bulinga ili kusaidia ujenzi wa jengo la utawala kwa ajili ya kukamilisha mahitaji ya sekondari mpya ya kata ya Bulinga kusajiliwa.

Aidha Prof. Muhongo amechangia vifaa vya uezekaji wa chumba kimoja cha darasa katika sekondari hiyo ambapo jumla ya mabati 52 na mbao 85 vimekwisha kutolewa na ofisi ya mbunge.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya Bulinga, Diwani wa kata hiyo Mambo Japan (CHADEMA), amemshukuru mbunge wa jimbo la Musoma vijijini kwa jitihada kubwa anazozifanya jimboni yeye na serikali ya awamu ya tano kwa ujumla katika kuhakikisha wanatekeleza na kusimamia vyema maendeleo ya jimbo, taifa na hatimaye kuleta mabadiliko ya kweli.

Diwani huyo alisema, mambo yanayofanywa na serikali ya sasa ndio hayo hayo waliyokuwa wakiyataka, hivyo wapo tayari kuungana pamoja na kufanya kazi za maendeleo kwa ushirikiano ili kuleta maendeleo wanayoyahitaji wananchi.