Na. Verdiana Mgoma
ZAO la Muhogo ni moja ya mazao muhimu. Zao hili ambalo hulimwa zaidi na wakulima wadogo, hutumika zaidi kwa matumizi ya chakula na biashara.
Wakulima walio wengi wamejikita kwenye zao hili kwasababu hustawi zaidi kwenye maeneo ya mvua ya wastani, ardhi yenye kichanga, pia hustahimili ukame.
Wakitoa sifa zaidi za zao hilo la Muhogo, wakulima wanasema ni rahisi kulima na hubaki ardhini kwa muda mrefu bila kuvunwa na upatikanaji wa mavuno ni wa uhakika zaidi kuliko mazao ya nafaka.
Kushamiri kwa kilimo hiki ni jitihada za Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, ambaye baada ya kutokea malalamiko ya kuwepo upungufu wa chakula kwenye vijiji mbalimbali ndani ya jimbo lake, aliamua kuhamasisha kilimo cha muhogo.
Prof. Muhongo aligawa mbegu za Mihogo kwa wananchi wake na kuwataka kuweka nguvu kubwa kwenye kilimo hicho chenye tija badala ya kuomba chakula cha msaada.
Mbali na wakulima wengi kujitokeza kulima muhogo, hamasa ilifanywa hata mashuleni ambapo shule nyingi zimelima na kutumia vizuri fursa ya mbegu kutoka kwa mbunge.
Yapo mashamba darasa yanayomilikiwa na shule, taasisi, vikundi na wananchi wa kawaida ambao ni wakulima wazuri, lakini pia lengo la kugawa mbegu hizo katika makundi ilikuwa ni kuandaa mbegu bora kwa matumizi ya kata nzima kwa baadaye.
“Tulipokea jumla ya kilo 50 mbegu za mtama na magunia 19 ya vipando vya mihogo kutoka ofisi ya mbunge” anasema Maricha Mgono, Afisa kilimo kata ya Murangi.
Mwalimu wa Kilimo wa shule ya msingi Lyasembe, Samora Manyika anasema lengo la shule hiyo kujikita katika kilimo ni kulima mazao ya chakula na biashara na kutumia mazao hayo kwa ajili ya wanafunzi.
“Endapo tutashirikiana vizuri na wananchi, tutatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi na hiyo itasaidia kupunguza tatizo la utoro shuleni na kuongeza pia kasi ya ufaulu wa wanafunzi” anasema mwalimu Manyika.
Mmoja wa wazazi waliopo kwenye kamati ya shule na mkulima wa kijiji cha Lyasembe, Sospeter Mfungo anasema, wamechangamkia fursa hiyo ya kilimo cha muhogo lengo ili mazao hayo yaweze kusaidia upatikanaji wa chakula shuleni na kuongeza maarifa ya uelewa kwa wanafunzi.
“Kilimo cha mihogo kina faida nyingi ikiwa ni pamoja na mizizi ya mihogo ni tegemeo kubwa la wakulima, majani ya mihogo hutumika kama mboga na miti ya mihogo hutumika kama kuni maalumu kwa kupikia. Tunamshukuru sana mbunge wetu kutusaidia katika upande wa kilimo, kwa sasa tumejipanga upya na mazao yanayo vumilia ukame tofauti na hapo nyuma tulilima kwa msimu” anasema Sospeter Mfungo.