Na. Mwandishi Wetu
WANANCHI wa kijiji cha Buraga, Kata ya Bukumi wamekubali na kuunga mkono agizo la Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney la kuwataka kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara.
Hatua hiyo muhimu imeonesha mafanikio chanya katika mkutano wa kwanza wa wananchi na viongozi mbali mbali wa kata na kijiji cha Buraga pamoja na ofisi ya Mbunge uliofanyika 10, Julai, 2017 ikiwa ni moja ya mikutano iliyopangwa kufanyika mfululizo kwenye kata ya Bukumi kuhamasisha zoezi la kuchangia maendeleo ya elimu.
Mtendaji wa kata ya Bukumi Leftinant Mukama akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara alisema, Mkuu wa Wilaya ameagiza watoe michango yao kwa nia njema ili kuungana na serikali pamoja na Mbunge wao katika kunusuru suala la elimu katika jimbo la Musoma vijijini.
Akichangia katika uwasilishaji wa agizo hilo, Fedson Masawa ambaye pia ni Msaidizi wa Mbunge alisema, endapo wananchi wakiwa na utaratibu wa uchangiaji huo, ni njia muafaka ya kuweka mfuko hai kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na maabara.
Masawa alisema, mfuko huo utatoa fursa nzuri katika utumiaji wa vifaa vya ujenzi vinavyotoka kwa Mbunge tofauti nasasa ambapo baadhi ya vijiji vinapokea vifaa hivyo mapema, lakini vinakaa muda mrefu bila kutumika kutokana na ukosefu wa fedha.
Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Mbega Kerenge akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Buraga alisema, agizo la Mkuu wa wilaya ni zuri kwa maana limelenga zaidi kuwasaidia na kuwaondolea usumbufu, hivyo wanalikubali na watalitekeleza.
“Mimi naona wazo hili ni zuri tu kwa maana litatusaidia kupunguza usumbufu, na sasa sisi wananchi wa kijiji cha Buraga tutachangia tu” alisema Kerenge.
Naye Msabha Matara, mkazi wa kijiji cha Buraga alisisitiza kuwa, wazo la kuchangia michango hii mapema ni zuri kwa kuwa litawapunguzia majukumu na kupoteza muda hasa wakati wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
“Tumekuwa tunapoteza muda mrefu kusubiria michango, kwahiyo tukienda na wazo hili la kuchangia mapema na kuhifadhi fedha kwenye mfuko maalum, tutapiga hatua nzuri tena ya pamoja” alisisitiza Msabha.
Kwa upande wake Abiudi Matekele alitoa tahadhari kwa viongozi wa kijiji na kata kuwa makini katika kufuatilia michango hiyo na kuhakikisha kila kaya inachangia bila kuacha kaya hata moja na kisha fedha zitakazopatikana zielekezwe kwenye matumizi sahihi.