KIKUNDI CHA ‘HAKI SAWA’ KURWAKI WAFURAHIA MAVUNO YA MAHINDI

Wanachama wa kikundi cha Haki sawa wakishiriki kuhifadhi mahindi waliyovuna (Picha Na. Ramadhani Juma)

Na. Mwandishi Wetu

KIKUNDI cha kilimo cha umwagiliaji cha Haki Sawa kutoka Kijiji cha Kurwaki wameanza kunufaika baada ya kuvuna zaidi ya magunia 50 katika msimu wao wa kwanza wa kilimo.

Wakizungumza kwa furaha mbele ya msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Ramadhani Juma wanakikundi hao wamesema kwa sasa wamegundua mbinu ya mafanikio ni juhudi na kujituma.

“Hakika hatukutarajia kama tungeweza kuvuna kiasi hiki cha mahindi, tumejifunza kuwa juhudi huzaa mafanikio, tulianza kimchezomchezo tu, lakini leo tuna furaha kwa kile tulichokipata” alisema Mwenyekiti wa kikundi hicho  Kudra Charles.

Katibu wa kikundi cha Haki Sawa Stephano Cosmas alisema, mahindi hayo nusu yake yatatumika kwa ajili ya chakula kwa wanakikundi na nusu yatauzwa ili kupata fedha za kutunisha mfuko wa kikundi.

“Tumekubaliana kugawana nusu ya mavuno yetu kwa maana kwa sasa tunakabiliwa na janga la njaa, hivyo mahindi haya yatatusaidia sana na yatakayobaki tutayauza kwa ajili ya kununua vitendea kazi ili tuweze kupanua kilimo chetu” alisema Cosmas.

Wakitoa ombi lao kwa msaidizi wa Mbunge la kusaidiwa vitendea kazi kutoka Ofisi ya Mbunge, mweka hazina wa kikundi hicho Selemani Minangi alimwomba msaidizi huyo amfikishie Mbunge ombi hilo.

“Sisi tumejitolea kufanya kazi ya kufa na kupona tutahakikisha tumeondoa umasikini katika familia zetu kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji kama tulivyofanya, tunakuomba mtusaidie japo mashine ya umwagiliaji kama mlivyotoa msaada kwa vikundi vingine” alisema mweka hazina huyo.

Kwa upande wake msaidizi wa Mbunge Ramadhani Juma, aliwaomba wanakikundi hao kuongeza juhudi na kutokuwa na tamaa ya kugawana mara tu wanapofanya uzalishaji.

“Kikundi chenu bado ni kichanga, mnahitaji kuzalisha kwa wingi ili muweze kufikia mafanikio, epukeni kuwa na tamaa, hivyo kiasi mtakachouza jitahidini kununua baadhi ya vitendea kazi ili muepukane na kazi za sulubu za kumwagilia kwa mikono” alisema.