Na Fedson Masawa
BODI ya shule ya sekondari Nyanja na Bulinga zimekubaliana na wazazi kuweka mikakati mipya ili kuinua kiwango cha elimu ya sekondari kwa shule hizo.
Makubaliano hayo yamefikiwa hivi karibuni kwenye kikao cha bodi za shule hizo, kilichofanyika katika shule ya Sekondari Bulinga.
Kikao hicho cha pili, kinafuatia kikao kingine kilichofanyika katika shule ya sekondari Nyanja iliyopo kata ya Bwasi, ambapo wazazi wote wa kata hizo wamekubaliana kuanzisha utaratibu maalum wa kuwaandalia watoto wao chakula cha mchana ili wanafunzi hao watumie muda wa kutosha katika masomo.
Wazazi hao wamekubaliana kuchangia Mahindi kilo 12, Maharage kilo 6, mafuta ya kupikia pamoja na chumvi, mchango ambao wazazi wamekubaliana kuutoa kwa awamu pamoja na vyombo vya kupikia na kulia chakula.
Sambamba na michango ya chakula, wazazi hao pia wamekubaliana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maabara kwa ajili ya kuboresha huduma ya masomo ya sayansi kwa watoto pamoja na kujenga jengo la utawala katika shule ya sekondari Bulinga.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hizo Abel Bogohe alisema, kamati ya bodi iliyopo kwa sasa ni kamati inayosimamia shule mbili;shule ya sekondari Nyanja iliyopo kata ya Bwasi na shule ya sekondari Bulinga iliyopo kata ya Bulinga ambayo kwa sasa inahesabika kama tawi la sekondari ya Nyanja.
Bogohe alisema, ni majukumu makubwa kwani kamati inayo kazi ya kusimamia shule mbili na hii yote ni kwa sababu shule ya sekondari Bulinga bado haijapata usajili kutokana na mapungufu ya jengo la utawala.
“Pamoja na majukumu yote hayo, ndugu wazazi hapa Prof. Muhongo haepukiki na ni lazima tumuombe atufikirie kwenye ukamilishaji wa maabara, kwani sekondari ya Nyanja tayari jengo la maabara zote tatu limekamilika na kuezekwa kwa nguvu za wananchi kilichobakia ni sakafu na miundombinu ya ndani. Bulinga bado jengo la maabara linaendelea kujengwa pia kwa nguvu za wananchi, tunaomba Mbunge atusaidie kuyafanikisha haya” alisema Bogohe.
Hata hivyo, Bogohe ameeleza pamoja na changamoto zote hizo wazazi, kamati na walimu wa shule hizo wanalo jukumu la kushirikiana pamoja ili kuinua taaluma ya wanafunzi wanaosoma katika shule hizo kwa kubuni, kupanga na kujiwekea utaratibu maalumu wa kuinua kiwango cha taaluma kwa watoto wao.
“Tunazo changamoto nyingi, lakini wazazi lazima mshiriki kikamilifu ili kuinua taaluma ya wanafunzi hawa. Tunapaswa sasa kuwatengenezea utaratibu wa kutumia muda mrefu katika masomo na wazazi kutumia muda mwingi kufanya maendeleo ya miundo mbinu ya watoto kujifunzia” alisema Bogohe.
Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo na Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Nyanja, Charles Ndebele amewaomba wazazi kuwaunga mkono walimu wao kwani walimu peke yao hawawezi kuleta mabadiliko katika elimu bila ushirikiano kutoka kwa wazazi hasa kuboresha miundo mbinu ya elimu kwa kuwa na maandalizi bora ya mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kutoa muda wa kutosha na uhuru wa mwanafunzi kujisomea.
Naye Mtendaji wa Kata ya Bulinga Gudrack Mazige ameieleza bodi na kumshukuru Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa jitihada zake za kupambana na changamoto za elimu na kusema, pamoja na kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa lakini bado ameisaidia kata ya Bulinga mifuko 70 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika sekondari ya Bulinga.
Mazige amewataka wazazi kuwa pamoja na kuwa na mwamko mzuri katika elimu, wanapaswa kujitahidi kumuunga mkono Mbunge wa jimbo lao kwa ajili ya kufanikisha mipango yao mizuri.
“Ndugu wananchi na viongozi wa bodi, sambamba na mapambano na kuinua kiwango cha elimu, shule ya sekondari Bulinga imepokea saruji 70 kutoka kwa Prof. Muhongo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala ili shule yetu iweze kusajiliwa. Tumshukuru sana Prof Muhongo lakini sasa tunao wajibu wa kumuunga mkono kwa kuwajibika kikamilifu hata kwa kuchangia nguvu kazi” alieleza Gudrack.