MILIONI 236 ZATOLEWA KUGHARAMIA UJENZI SEKONDARI YA KASOMA

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Anney akishiriki kuchimba msingi wa mabweni ya sekondari ya Kasoma ambao ujenzi wake umegharamiwa na Halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini.

Verdiana Mgoma

HALMASHAURI ya wilaya ya Musoma vijijini kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Nyamrandirira wamejitolea katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo shule ya sekondari Kasoma.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kufadhili mradi huo unaogharimu shilingi milioni 236 zitazotumika kupanua shule hiyo.

Mkuu wa Shule ya sekondari Kasoma Nelson Makaro alisema, kwa muda mrefu shule yao inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa ambapo wana wanafunzi 890 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, lakini wana vyumba vya madarasa 13 na wana upungufu wa vyumba vinane.

Makaro alisema, kwa upande wa mabweni upungufu ni mkubwa zaidi maana yapo mabweni mawili yanayotumika kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita tu, hivyo  wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha nne wanaishi majumbani mwao ambako ni mbali na shule, hivyo kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kupunguza changamoto hizo.

“Pia tunakabiliwa na changamoto nyingine ya uhaba wa walimu wa sayansi na nyumba za walimu na chakula kwa wanafunzi” alisema mwalimu Nelson Makaro.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamrandirira Ruteli Maregesi alisema, wananchi wa kata yake wamehamasika katika ujenzi huo na walianza ufyatuaji wa matofali na nasasa wapo kwenye hatua ya uchimbaji wa msingi.

“Tuliweka majadiliano na wananchi wangu tulipogundua kuna baadhi ya changamoto tunaweza kuanza kutatua ili kunyanyua kiwango cha elimu. Mabweni kwetu ni ya muhimu sana maana kuwepo kwa mabweni tutaondoa changamoto ya watoto kutoka umbali mrefu na kutumia muda mwingi kufika shule, hupunguza majukumu ambayo wakitoka shule mara nyingi hufanya nyumbani na kukosa muda wa kujisomea, lakini wakiwa shule watakuwa huru zaidi” alisema diwani huyo.

Aliongeza:”tutawakinga watoto wa kike na vishawishi wanavyokutana navyo na kukatisha masomo (mimba), itasaidia pia kwa matumizi ya lugha hasa ya kiingereza maana mazingira wanafunzi wanapotoka mara nyingi hutumia lugha ya asili”

Naye Mkuu wa wilaya Dkt. Vicent Anney aliwashukuru wananchi hao na viongozi kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya na kuwataka kuongeza bidii ili kukamilisha mradi huo mapema huku akitoa onyo kwa wanaogoma kushikiri kufanya shughuli za maendeleo kwamba, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hata hivyo, Dkt. Vicent Anney alisisitiza ushirikiano kati ya wadau wa elimu yaani walimu, wazazi, wanafunzi na viongozi wa kisiasa kuwekeza zaidi kwenye elimu ili kuinua sekta ya elimu na kusisisitiza: ‘ukimsomesha mtoto umesomesha jamii.’