Na. Ramadhani Juma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ametoa msaada wa chakula kwa kaya 57 zilizoathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha na kuambatana na upepo mkali katika kijiji cha Kabegi kata ya Ifulifu.
Prof. Muhongo ametoa msaada wa kilo 570 zenye thamani ya shilingi 456,000 ambapo kila kaya imepewa kilo 10 za mahindi.
Akizungumza na waathirika wa tukio hilo kabla ya kukabidhi msaada huo, Prof. Muhongo aliwapa pole wananchi wa kijiji cha Kabegi ambao nyumba zao zimeezuliwa na nyingine kubomoka na kuwahimiza kujenga nyumba bora na imara pamoja na kupanda miti mingi katika maeneo ya makazi kwa kata na vijiji vyao ili kuepuka dhoruba kama iliyokumba.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kabegi Pilly Waryoba alimshukuru Prof. Muhongo kwa msaada wa chakula aliowapatia na kusema ni hatua nzuri ya kuanzia, kwani mvua iliyonyesha ilisababisha kaya zao kupoteza chakula chote walichokuwa nacho.
Kwa upande wake Magori Maregesi alitoa shukrani kwa Prof. Muhongo kwa moyo wake wa kuitambua vyema na kuijali jamii yake hasa inapokumbwa na majanga, ambapo amewapatia chakula na siyo fedha kama ilivyokuwa imezoeleka kwa viongozi wengine.
“Kiongozi wa namna hii lazima tumtumie vizuri kwani anajali watu hasa wanapopatwa na matatizo makubwa kama haya na ni utaratibu mzuri wa kutupa chakula kuliko hela kama tulivyozoea kwa watu wengine” alishukuru Maregesi.
Naye Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kabegi Charles Choto alimshukuru Prof. Muhongo na kumtakia kheri na baraka katika kazi zake anazozifanya na kuendelea kuwakumbuka na kuwa karibu na wananchi wa jimbo lake la Musoma vijijini.
Choto aliongeza kuwa, wananchi wake wamebomokewa nyumba zao na wengine kuezuliwa nyumba na hivyo kaya nyingi hazina makazi na nyingine zimepoteza chakula, lakini kwa faraja aliyoionesha Prof. Muhongo imeleta matumaini kwa familia hizo.
“Namshukuru sana Prof. Muhongo na ninamtakia kheri katika kazi zake anazozifanya na aendelee na moyo huo wa kuwakumbuka wananchi wake. Ni nyumba nyingi zimebomolewa na kuezuliwa, lakini kwa msaada huu umetutia faraja” alishukuru Mwenyekiti Charles Choto.