Na Mwandishi Wetu
MSAIDIZI wa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Fedson Masawa ametembelea zahanati ya kijiji cha Mwiringo kilichopo kata ya Busambara kwa lengo la kujua sababu za kuchelewa kuanza kwa zahanati hiyo kutoa huduma za matibabu.
Zahanati hiyo iliyokamilika ujenzi wake tangu mwaka 2014, imejengwa kwa msaada wa mzaliwa wa kijiji hicho kwa kushirikiana na wananchi hadi kufikia kukamilika kwa ujenzi huo, lakini imeshindwa kutoa huduma za afya.
Akizungumza na msaidizi wa Mbunge, Mganga mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Makwanda amethibitisha kuwa zahanati ya kijiji cha Mwiringo tayari imekamilika na wao kama idara ya afya ngazi ya wilaya wameshaandaa mahitaji yote na watumishi wa zahanati hiyo wapo tayari kuanza kazi muda wowote.
Dkt. Makwanda alisema, jambo linalochelewesha zahanati hiyo kuanza kutoa huduma ni ukosefu wa meza nne na viti nane ambavyo gharama yake ni shilingi 2,400,000 na zinatakiwa kuchangwa na wananchi wa kijiji hicho ili kufanikisha mahitaji ya zahanti hiyo na kufunguliwa.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mwiringo Claudian Ihunyo Maganya amekiri kukosekana kwa meza na viti, jambo ambalo linasababisha wananchi hao kuendelea kukosa huduma ya afya na kulazimika kutembea umbali mrefu zaidi kwa ajili ya kuitafuta huduma ya afya kwenye vijiji vya jirani.
Mwenyekiti huyo alitoa ombi kwa Prof. Muhongo kuwaunga mkono wananchi hao, kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakielekeza michango yao katika kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Naye Mtendaji wa kata ya Busambara Victor Kasyupa alisema: “ipo haja ya zahanati ya Mwiringo kufunguliwa haraka ili kuwanusuru akina mama na watoto wanaolazimika kusafiri umbali usiopungua kilomita nne kuitafuta huduma ya afya.”
Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amekubali kushirikiana na Halmashauri na wananchi wa Mwiringo katika kukamilisha mahitaji ya zahanati hiyo na kuhakikisha inaanza kufanya kazi Mei, 1, 2018.