Na Fedson Masawa
WAKULIMA wa vijiji na kata mbalimbali ndani ya Jimbo la Musoma vijijini wamepokea mbegu za alizeti na ufuta kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Prof. Sospeter Muhongo ikiwa ni maandalizi ya msimu wa kilimo ambao tayari umeanza mwezi Februari, mwaka huu.
Zoezi hilo la ugawaji wa mbegu ambalo lilifanyika kwa kanda tano Bukwaya, Mugango, Murangi, Saragana na Busekera, liliongozwa na mbunge Prof. Muhongo, Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney pamoja na Kaimu Afisa kilimo wa wilaya ya Musoma Ismail Masogo.
Wakizungumza baada ya kupokea mbegu hizo, wakulima hao walisema wamefurahishwa na tukio hilo muhimu na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha wanapanda na kuvuna vizuri na kutumia mazao hayo kwa ajili ya kuinua uchumi wa familia zao na maeneo wanayotoka.
“Tunamshukuru sana Mbunge na Halmashauri yetu kwa kutupa mbegu bure. Tutapanda kwa wakati, tutayatunza mashamba vizuri hatimaye tutoe mavuno yaliyo bora ili kuinua kipato cha familia zetu” alisema Pili Julius, mkulima kutoka kijiji cha Mayani kata ya Tegeruka.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Kilimo Ismail Masogo alisema, ofisi yake kwa kushirikiana na Maafisa kilimo wa kata, watatoa usimamizi na elimu kwa wakulima kuhusu utayarishaji wa mashamba, upandaji, upaliliaji, uvunaji na utunzaji wa mazao hayo ili kuhakikisha msimu huu unakuwa na mafanikio makubwa Jimboni humo.
Aidha, katika kuimarisha soko na utunzaji wa zao la alizeti, tayari mitambo miwili ya watu binafsi imejengwa Jimboni katika kijiji cha Kusenyi na Saragana ambapo itasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo.
Hata hivyo, wakiwa katika ziara ya ugawaji wa mbegu hizo bila malipo, Mkuu wa Wilaya na Mbunge pia walitembelea shamba la pamba lililopo kijiji cha Kinyang’erere kata ya Bugwema.
Kwenye ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya Dkt. Naano aliwataka maafisa kilimo wa kata na vijiji wahakikishe wanawatembelea wakulima wa pamba kila mara ili kuona maendeleo yao na changamoto zinazowakabili na kuwatatulia kwa lengo la kuongeza mavuno na ubora wa zao hilo.