Na. Fedson Masawa
MAADHIMISHO ya sherehe za wiki ya Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) yatakayofanyika kimkoa katika wilaya mpya ya Musoma vijijini Mkoani Mara yameanza jana kwa kampeni maalumu ya upandaji miti katika ofisi za Taasisi mbalimbali na kwenye nyumba za watu binafsi.
Katika kufanikisha maadhimisho ya sherehe hizo ambazo zitafikia kilele chake Machi, 29, 2018, Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ameungana na wazazi wa Mkoa wa Mara kwa kuchangia ununuzi wa miche 5,555 kati ya miche 12,500 iliyopendekezwa na Jumuiya hiyo.
Aidha, Halmashauri ya wilaya ya Musoma nayo imenunua miche 5,555 ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za wazazi katika kupambana na majanga ya asili kama kimbunga na mengineyo huku miche 1,390 iliyobaki, itanunuliwa na Jumuiya hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kukamilisha idadi iliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, amechangia huduma ya kusafirisha miche yote 12,500 kutoka Musoma mjini na kusambazwa kwenye Kata tisa zenye vijiji 28 kama ilivyopangwa.
Awali, akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa Wazazi Mkoa wa Mara Robert Manjebe alisema, kata ambazo zimepewa kipaumbele kwenye zoezi hilo, ni zile zinazokumbwa na majanga ya kimbunga mara kwa mara na kusababisha maafa makubwa kwenye jamii.
Manjebe amezitaja kata hizo kuwa ni Nyegina, Ifulifu, Mugango, Kiriba, Bugwema, Musanja, Murangi, Bukima, Bukumi na vijiji viwili vya Bwasi na Chimati.
“Zoezi la upandaji miti pia ni kampeni ya kitaifa, hivyo kwa kata nyingine zitakazobakia, bado zitaletewa miche kwa ajili ya kuendelea kulinda mazingira yetu” aliongeza Manjebe.
Manjebe pia ametoa shukrani zake kwa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa kujitoa kwa hali na mali pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Halmashauri ya Musoma na wadau wengine katika kufanikisha maadhimisho ya sherehe za wiki ya Wazazi kimkoa.
Naye, Katibu wa wazazi wilaya ya Musoma vijijini Lucy John alisema, pamoja na zoezi la upandaji miti, maadhimisho ya sherehe za wiki ya wazazi pia zinalenga kuwatembelea na kuwapa pole wagonjwa na wazazi waliolazwa mahospitalini, watoto yatima na kuwatembelea watoto waishio katika mazingira magumu hasa katika taasisi za shule, dini na nyinginezo.
Wakipokea miche hiyo, viongozi wa Jumuiya ya wazazi katika ngazi ya matawi na kata, wameshukuru utaratibu wa ugawaji wa miche kuelekea kilele cha maadhimisho ya hayo na kuahidi kusimamia miti hiyo kwa manufaa ya jamii nzima ya Musoma vijijini.
“Tuwashukuru wote waliofanikisha kazi hii, nasi tunaahidi kuelekea kilele cha maadhimisho ya sherehe za wiki ya wazazi, sisi kama wazazi tutasimamia na kuilinda miti hii kwa manufaa ya jamii yetu” alishukuru na kusema Labani Kuboja wa kata ya Bukumi.