Na Fedson Masawa
WANANCHI wa kijiji cha Kigera Etuma kilichopo kata ya Nyakatende kwa kushirikiana na viongozi wa Kata na serikali ya kijiji hicho wamefikia hatua nzuri ya ujenzi wa zahanati na kuonesha matumaini ya kupata huduma ya afya kijijini hapo.
Diwani wa Kata ya Nyakatende Rufumbo Rufumbo alisema haikuwa kazi rahisi kwa wananchi na serikali ya kijiji cha Kigera Etuma kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo, lakini kutokana na nia, ushirikiano na mipango yao thabiti, wamekamilisha jengo la zahanati na sasa wameelekeza nguvu zao katika ujenzi wa nyumba ya mganga ili zahanati hiyo ianze kutoa huduma mapema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwiryanyo na Mjumbe wa serikali ya Kigera Etuma, Mnada Nyatago ameishukuru serikali na wafadhili mbalimbali wanaoendelea kuwaunga mkono ili kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo ambapo alisema wanatarajia ifikapo Machi, 26 mwaka huu nyumba ya mganga iwe imekamilika.
Kwa upande wake Albinusi Nyatago akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kigera Etuma, alitoa shukrani zake kwa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo katika kuunga mkono jitihada za ujenzi wa zahanati Jimboni.
Nyatago aliongeza kwa kutoa ombi kwa Mbunge kuwapa nguvu wananchi wa Kigera Etuma katika kukamilisha ujenzi wa nyumba ya mganga ili zahanati yao ianze kutoa huduma mapema kijijini hapo.