Leo, Jumanne, tarehe 25.12.2018 Mbunge wa Jimbo Prof Sospeter Muhongo kwa kushirikiana na Paroko Emmanuel Sylvester Haule wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bukima WAMEKARIBISHA WANANCHI kwenye Chakula cha Mchana cha Krismasi (Christmas Lunch) kwenye Kigango cha Bukumi.
Mbunge alipata fursa ya kutembelea MIRADI YA KANISA Parokiani Bukima na amevutiwa sana na MRADI wa UJENZI MAABARA YA AFYA. Kanisa linajenga Maabara ambayo itarahisisha matibabu (vipimo vya sampuli za damu, n.k.) kwenye Zahanati za Kata za Bukima, Bukumi, Bulinga, Makojo na Rusoli. Mbunge amehaidi kuchangia ujenzi huo ifikapo Februari 2019, na amependekeza kwamba Maabara hiyo ianze kutumiwa kabla ya Juni 2019.
Mahubiri ya Paroko Haule yamekazia umuhimu wa: (a) unyenyekevu, (b) upendo, (c) ufanyaji wa kazi kwa bidii, na kuwasihi waumini na wananchi kwa ujumla kuanza Mwaka Mpya wakiwa “watu wapya” wenye unyenyekevu, upendo, na wakiwa wachapa kazi.
Baada ya Ibada, Wanakijiji, Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa, na Waalikwa kutoka Madhehebu mengine (wakiwemo Waislamu) walikaribishwa kwenye chakula cha mchana ikiwa ndicho kilele cha Sherehe za Krismasi za Mwaka huu (2018) ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.