WANANCHI KIJIJI CHA NYABAENGERE  WAMEAMUA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU KWENYE SHULE YAO YA MSINGI – KILA KITONGOJI KUJENGA DARASA MOJA

Ujenzi na Ufungaji lenta wa Vyumba vya Madarasa na Ofisi za Walimu wa Shule ya Msingi Nyabaengere, Kijiji cha Nyabaengere, Kata ya Musanja

Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
Kutokana na idadi kubwa ya Wanafunzi wanaojiunga na ELIMU ya Msingi  kumekuwa na tatizo kubwa la UHABA wa Vyumba vya Madarasa kwenye Shule ya Msingi Nyabaengere iliyoko kwenye Kijiji cha Nyabaengere.
Ndugu Nashoni Manji ambae ni Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabaengere ameeleza kwamba Wanakijiji WAMEKIRI KWAMBA kuna TATIZO kubwa la UPUNGUFU wa Vyumba vya Madarasa. Kwa hiyo kwa kupitia Halmashauri ya Kijiji chao wamejiwekea UTARATIBU wa KILA KAYA kuchangia kiasi cha SHILINGI ELFU KUMI (10,000) na WAMEKUBALIANA kwamba KILA KITONGOJI kitajenga CHUMBA KIMOJA  cha Darasa.
Aliendelea na kusema, “Tumefanikiwa kunyanyua Maboma ya Vyumba Vinne na Ofisi mbili za Walimu kwa kushirikiana na Viongozi wenzangu wa Vitongoji vya Nyabaengere, Chakaroso, Kairo na Kamugea.”
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Nyabaengere, Mwalimu Steve Kihoko ameeleza kwamba MATATIZO yaliyopo hapo shuleni yatapatiwa tiba baada ya  kukamilika kwa Vyumba Vinne vya Madarasa. Hakutakuwepo na  mrundikano wa Wanafunzi Madarasani na hawatakuwepo Wanafunzi wanaosomea CHINI YA MITI.
Aidha Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Musanja, Ndugu Elias Ndaro amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa KUCHANGIA SARUJI MIFUKO 60 na Mabati 108. Hayo Mabati yamenunuliwa kutoka Mfuko wa Jimbo.
Mbunge wa Jimbo Profesa Muhongo ameishatoa MICHANGO ya Madawati, na Vitabu (mara tatu) kwenye Shule hii. Vilevile Profesa Muhongo amechangia Ustawi wa Kilimo kwenye Kata hii kwa Wanavijiji kuwapatia bure Mbegu za Alizeti (mara tatu), Mihogo na Mtama.
WADAU wa Maendeleo wakiwemo Wazaliwa wa Kata ya Musanja na Vijiji vyake WANAOMBWA WAJITOKEZE kuchangia ujenzi huu.