MIRADI YA TANROADS NA TARURA NDANI YA JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI YAKAGULIWA

Mhe Bupilipili akimsaidia Mama kwa kubeba Mtoto wa Mama huyo aliyekuwa akivuka Mto Nyamwifi kwenye eneo la Daraja lililokatika.

Jumatatu, 25.02.2019
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mara wametembelea na kukagua MIRADI inayotekelezwa na TANROADS na TARURA ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.
Kiongozi wa Wajumbe hao alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe Lydia Simeon Bupilipili. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Mhe Charles Magoma na Mbunge Prof Sospeter Muhongo walikuwa kwenye ziara hiyo iliyoratibiwa na Wataalamu (Wahandisi) kutoka TANROADS Mkoa na TARURA Wilaya.
Barabara zinazosimamiwa na TANROADS zinafanyiwa matengenezo mazuri na zinapitika kwa MWAKA MZIMA hata wakati wa MSIMU WA MVUA. Barabara kuu ya Musoma-Mugango-Murangi-Makojo-Busekela (km 92) iko kwenye hali nzuri na matayarisho ya kuwekwa LAMI yamekamilika.
Picha Na. 1 na 2 hapo chini inaonyesha Wajumbe wa Bodi, Wataalamu/ Wahandisi wa TANROADS na TARURA wakiwa pamoja na Mhe Bupilipili (mwenye cap ya njano) kwenye Daraja la Kijijini Kusenyi, mahali ambapo ujenzi utaanzia na kuelekea Makojo hadi Busekela.
TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (TARURA Musoma DC) ina Jumla ya BARABARA 85 zenye urefu wa km 474.32 (ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini).
Usimamizi wa BARABARA zilizo chini ya TARURA ni mzuri na matengenezo yanayafanywa kwa kiwango kizuri.
Viongozi wa TARURA wamewaonyesha Daraja kwenye Mto Nyamwifi lilokatika. Hili liko kwenye Barabara ya Bukima-Bulinga- Bwasi. Usanifu wa awali imefanyika na gharama zimekadiriwa kuwa Tsh Milioni 350 ambazo zimeombwa kwenye Bajeti ya 2019/2020.
Viongozi wa TARURA wameeleza kwamba Barabara ya Wanyere – Kataryo, kwenye Mto Suguti nayo inahitaji Daraja jipya.
WAJUMBE wa BODI ya BARABARA Mkoa wa MARA WAMERIDHIKA na kupongeza TANROADS na TARURA kwa kazi nzuri.