WANANCHI WA KIJIJI CHA ETARO WAMEDHAMIRIA KUKAMILISHA UJENZI VYUMBA 5 VYA MADARASA IFIKAPO MWISHONI MWA MEI 2019 

Wananchi wa Kijiji cha Etaro wakiendelea na Ujenzi wa Vyumba vya Madarasa ya S/M Etaro

Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
Wananchi wa Kijiji cha Etaro Kata ya Etaro, wanakamilisha Ujenzi wa Vyumba 3 vya Madarasa na tayari wameanza hatua za ujenzi wa Vyumba vingine Viwili (2) vya Madarasa kwenye Shule ya Msingi Etaro.
Awali akizungumza na Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo, Ndugu Fedson Masawa, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Ndugu Mangire Stephano Mahombwe alisema, “Shule ya Msingi Etaro ina Mahitaji ya Vyumba vya Madarasa 22, Vilivyopo 10 na kwa wakati huu tunakamilisha Vyumba 3, na baadae tunaanza ujenzi wa Vyumba vingine Viwili (2) ambavyo misingi (foundations) yake tumeishaiweka.”
Mwalimu Mkuu huyo aliendelea kueleza kwamba ifikapo mwishoni mwa Mei hii (Mei 2019), Vyumba vyote vitakuwa vimekamilika.
Mtendaji wa Kijiji cha Etaro Bi Sophia Charles Antone amewashukuru WADAU wa Maendeleo waliofanikisha kuchangia UJENZI wa Miundombinu ya Shule na Upatikanaji wa VIFAA muhimu vya Shule. WADAU hao ni pamoja na WANAKIJIJI wenyewe wa Kijiji cha Etaro waliosomba MAWE, KOKOTO, MCHANGA na MAJI. Mbunge wa Jimbo, Prof Muhongo alichangia MADAWATI 227 (walikuwa na upungufu wa Madawati 249), SARUJI MIFUKO 60, MABATI 54, na kutoa VITABU vingi.
Mkuu wa Wilaya (DC) Dr Vicent Naano Anney alichangia SARUJI MIFUKO 30, na Mchango wa Fedha za Mfuko wa Jimbo ni MABATI 144.
Wananchi wanategemea kwamba uboreshaji wa Miundombinu ya Shule yao, utaboresha ufaulu wa Mitihani ya Darasa la Saba (VII) na kuongezeka kutoka ule wa 33.11% wa Mwaka jana (2018). Wanatamani ufaulu uvuke Asilimia 50 (50%) na kufikia Asilimia 75 (75%).
KARIBU UCHANGIE UJENZI WA MIUNDOMBINU YA SHULE YA MSINGI ETARO.