Jumatatu, 20.05.2019
Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, Vijiji 68 na Vitongoji 374 LIMEAMUA KUKUZA KILIMO CHA UMWAGILIAJI
(A) BONDE LA BUGWEMA
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma yenye Jimbo la Musoma Vijijini IMEWEKEANA MKATABA na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuanza KILIMO KIKUBWA cha UMWAGIALIAJI kwenye Bonde la Bugwema. MAZAO Makuu yatakayolimwa ni Pamba, Alizeti, Mpunga, Mahindi na Kunde. Taarifa za Mradi huu zilishatolewa.
(B) KILIMO CHA UMWAGILIAJI CHA WAKULIMA WADOGO WADOGO
Vikundi vya Kilimo cha Umwagiliaji vimeweka wazi Mipango yao ya kushirikiana na Serikali za Vijiji na Kata zao ili kuongeza kasi ya UKUAJI wa Kilimo cha Umwagiliaji Vijijini mwao.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kikundi cha No Sweat No Sweet, Ndugu Goodluck Wambwe. Kikundi hiki kipo Kijiji cha Bugunda, Kata ya Bwasi.
Ndugu Wambwe alieleza kwamba wamepata mafanikio makubwa ambayo ni pamoja na kujihakikishia kipato cha kutosha kukidhi mahitaji ya kifamilia na mahitaji ya watoto shuleni. Ameendelea na kusema sasa wanalenga kushirikiana na Serikali za Vijiji na Kata kushawishi Wanavijiji wengine nao waanze Kilimo cha Umwagiliaji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugunda, Ndugu Manyama Bulerwa amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof Sospeter Muhongo kwa kukiwezesha Kikundi hicho (No Sweat No Sweet) kupata Vifaa vya Umwagiliaji kwa kutumia Fedha za Mfuko wa Jimbo. Aliendelea na kusema kuwa Kikundi hicho (No Sweat No Sweet) kimetoa hamasa kubwa, hadi sasa Kijiji chake kina jumla ya Vikundi 15 vya Kilimo cha Umwagiliaji.
Kikundi cha No Sweat No Sweet kimejikita zaidi katika Kilimo cha Mahindi, Matikiti Maji, Nyanya na Vitunguu.
FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO NA KILIMO CHA UMWAGIALIAJI JIMBONI
Kati ya Vikundi 15 vilivyokabidhiwa PAMPU, MIPIRA, MBEGU, n.k. kwa kutumia Fedha za Mfuko wa Jimbo, Kikundi cha No Sweat No Sweet ni moja kati ya Vikundi Vitano (5) tu vilivyoonekana vinafanya kazi vizuri na kukubaliwa kubaki na Vifaa vya Umwagiliaji. Vikundi vingine 10 vilinyang’anywa vifaa hivyo baada ya kuthibitika kwamba vimeshindwa kabisa kutumia vifaa hivyo ipasavyo. Vifaa hivyo vinatumika sehemu nyingine Jimboni penye mahitaji ya PAMPU za MAJI.
Vikundi vilivyofanikiwa kubaki na Vifaa vya Umwagiliaji ni: (1) Mwanga Farmers (Kata ya Nyambono), (2) KEUMA (Kata ya Busambara), (3) Angaza (Kata ya Bukumi), (4) Mkulima Jembe (Kata ya Bukima) na (5) No Sweat No Sweet (Kata ya Bwasi).
VIKUNDI hivi vinaomba Halmashauri iwapatie Wataalamu wa Kilimo cha Umwagiliaji na iwasaidie kupata MASOKO mazuri na ya uhakika ya bidhaa zao.