Jumatatu, 17.06.2019
Na: Hamisa Gamba
Msaidizi wa Mbunge
Serikali kupitia Mradi wake wa EQUIP imetoa Tsh Milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa SHULE SHIKIZI KAGURU, inayojengwa kwenye Kitongoji cha Kaguru, Kijijini Bugwema, Kata ya Bugwema.
Ujenzi wa SHULE SHIKIZI KAGURU ni muhimu sana kwa sababu watoto wa Kitongoji hicho na vile vya jirani wanalazimika kutembea umbali usiopungua kilomita 5 kwenda masomoni kwenye Shule jirani (S/M Bugwema) iliyoko Kijijini Bugwema.
Mbali ya MSAADA mkubwa uliotolewa na Serikali wa Tsh Milioni 60, NGUVUKAZI za Wananchi zinatumika kusomba mawe, kokoto, mchanga na maji kwa ajili ya ujenzi huu. Vilevile Wananchi wamekubali KUCHANGA fedha taslimu Tsh 16,000 kutoka kila KAYA.
Vyumba Viwili (2) vya Madarasa, Ofisi 1 ya Walimu Choo chenye Matundu 6 (Wanafunzi 4 na Walimu 2) vimeishajengwa.
Mwl Mkuu wa Shule ya Msingi Bugwema, Ndugu Esangya J. Bitta ambaye ni Msimamizi wa Ujenzi huu na Mlezi wa Shule Shikizi hiyo inayojengwa, ameeleza kuwa ujenzi ulianza rasmi Mwezi Machi 2019 na umepangwa ukamilike Juni 30, 2019. Aliongezea kuwa pamoja na ujenzi wa Vyumba 2 vya Madarasa, Ofisi 1 na Vyoo; kwa kuzingatia Usafi wa Mazingira na Afya Bora, MIUNDOMBINU ya MAJI inawekwa ikiwa ni jumla ya Matenki matano (5) ya Maji. Matenki 3 ni kwa ajili ya matumizi ya Vyoo na Matenki 2 kwa ajili ya matumizi mengine.
Diwani wa Kata ya Bugwema, Mhe Ernest Maghembe ametoa SHUKRANI nyingi sana kwa SERIKALI yetu na haswa kwa Mradi wa EQUIP, kwa kutoa MCHANGO huo mkubwa wa Fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule Shikizi hiyo mpya. Diwani huyo amesema WAMEPANGA kwamba Shule hiyo Shikizi ITAPANULIWA na kuwa Shule kamili ya Msingi yenye Darasa la I hadi la VII.