VIKUNDI VYA KILIMO KUPEWA ZAWADI YA KRISMASI YA KUBORESHA KILIMO CHAO

Wakulima wa Vijiji vya Bukumi (Kata ya Bukumi) na Kamuguruki (Kata ya Nyakatende) wakiwa mashambani mwao, kwenye Kilimo cha MSIMU huu (2019/2020), kwa kutumia MAJEMBE ya KUKOKOTWA na NG’OMBE (PLAU).

Na: Fedson Masawa
Msaidizi wa Mbunge
Zimebaki siku 2 kabla Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo kukabidhi ZAWADI ya KRISMASI ya PLAU (Majembe ya kukokotwa na Ng’ombe) kwa VIKUNDI VYA KILIMO 18 vya Wakulima ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini.
WAKULIMA Jimboni wanaendelea kuhamasika zaidi kwa kutambua umuhimu wa kutumia PLAU (na MATREKTA yakipatikana) badala ya JEMBE LA MKONO.
WAKULIMA wameeleza kuwa, tofauti na kipindi cha nyuma, ambacho Wakulima wengi walikuwa wakitumia Majembe ya Mkono  kwenye kilimo chao, kwa sasa Wakulima walio na MAJEMBE ya NG’OMBE (PLAU) wanatumia majembe hayo kulima eneo kubwa kwa muda mfupi.
Ndugu Majura Mbogora wa Kijiji cha Bukumi ameeleza kwamba Mkulima anaweza kulima EKARI MOJA kwa siku moja kwa kutumia PLAU MOJA wakati kulima shamba hilo hilo kwa kutumia JEMBE la MKONO, siku 5  hadi 7 zinahitajika kwa Familia ya watu wasiopungua watano (5). Hivyo, WAKULIMA wanaona kuna umuhimu wa KULIMA kwa kutumia PLAU ili kupanua ukubwa wa mashamba yao kwa kutumia muda mfupi zaidi.
ZAWADI ZA PLAU KWA VIKUNDI VYA KILIMO
Tarehe 24.12.2019, Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo atatoa ZAWADI YA KRISMASI YA PLAU kwa kila KIKUNDI cha KILIMO kutoka VIJIJI 18. Hii ni sehemu ya KAMPENI ya KUSHAWISHI Wakulima wapunguze kutumia JEMBE la MKONO na waanze kutumia PLAU kwa wingi.
VIONGOZI wa VIKUNDI vya KILIMO 18 vitakavyopewa ZAWADI YA PLAU kwa kila KIKUNDI wanatanguliza SHUKRANI zao za DHATI kwa Mbunge wa Jimbo lao kwa KUENDELEA KUBORESHA KILIMO Jimboni mwao.
Vilevile, WAKULIMA wanamshukuru sana Mbunge wao kwa kuwagawia bure MBEGU za mazao ya ALIZETI, MIHOGO, MTAMA na UFUTA kwa misimu kadhaa ya kilimo chao.
MATREKTA YA MKOPO
Jimbo la Musoma Vijijini lina jumla ya Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao (AMCOS) 35. Idara ya Kilimo ya Halmashauri (Musoma DC) yenye Jimbo hili IKO TAYARI kusaidia AMCOS hizo kutayarisha nyaraka za kutafuta MIKOPO ya kununua MATREKTA kwa manufaa ya Wanachama wao.