SIKUKUU YA KRISMASI KIJIJINI NYASAUNGU – WANAKIJIJI WASISITIZA SEKONDARI YAO KUFUNGULIWA MWAKANI (2020)

Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo akiendesha HARAMBEE ya ujenzi wa Nyasaungu Secondary School

SHEREHE YA KRISMASI Jimbo la Musoma Vijijini imetumika kuboresha UAMUZI  wa Wananchi wa Kijiji cha Nyasaungu wa kuhakikisha SEKONDARI MPYA inayojengwa Kijijini mwao INAFUNGULIWA Mwakani (Februari 2020).
SHEREHE za Eid al Fitr, Krismasi na Pasaka za Jimbo la Musoma Vijijini zinafanywa kwa mzunguko ndani ya Kata zote 21 za Jimbo hili.
Marafiki 2 (na wanafunzi wenzake) wa  Prof Muhongo wa kutoka Jijini Berlin,  Ujerumani (Magharibi) walihudhuria SHEREHE hiyo. Hao ni: Christa Werner (Dr.rer.nat.) na Wolfgang Zils (Dipl Ing, Dipl Geol).
Jimbo la Musoma Vijijini lina Jumla ya Kata 21. Kata 18 tayari zilishajenga Sekondari zao na zinatumika. Kata 3 (Bugoji, Busambara na Ifulifu) zisizokuwa na Sekondari zinakamilisha ujenzi wa Sekondari zao ili zianze kutumika mwakani (2020).
Kwa hiyo, ifikapo Februari 2020 KILA KATA Jimboni itakuwa inayo Sekondari yake. Kutokana na WINGI wa Wanafunzi na UMBALI wa kutembea, baadhi ya Kata zimeanza kujenga Sekondari ya pili kwenye Kata zao. Jumla ya Sekondari za Binafsi Jimboni ni mbili (2).
HARAMBEE YA KRISMASI – Nyasaungu Secondary School
Baada ya Ibada ya Krismasi, Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo aliendesha HARAMBEE ya kuchangia VIFAA VYA ujenzi vitakavyotumika ifuatavyo:
*Vyumba 3 vya Madarasa viezekwe ifikapo tarehe 15.1.2020
*Vyoo vya Wanafunzi  na Walimu vikamilishwe ujenzi wake kabla ya tarehe 30.1.2020
MFUKO wa JIMBO ulishachangia MABATI 54 ya kuezeka chumba kimoja cha darasa.
Tarehe 25.12.2019, Mbunge wa Jimbo Prof Sospeter Muhongo alichangia MABATI 54. Hapo awali, Mbunge huyo alishachangia SARUJI MIFUKO 35 na NONDO 20 kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari hii.