Jumatatu, tarehe 1.3.2021, MBUNGE wa JIMBO la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo alikagua ujenzi wa BARABARA KUU ya Jimbo hilo inayojengwa kwa kiwango cha LAMI – barabara ya KILOMITA 92 ya Musoma-Makojo-Busekera.
Mbunge huyo alifuatana na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Injinia Felix Ngaile na MKANDARASI wa Mradi, Injinia Getanyeri Nyantori.
Wataalamu wengine wa TANROADS walikuwepo na VIONGOZI wa Kijiji cha KUSENYI nao walikuwepo.
USHAURI ULIOTOLEWA
(1) Kasi ya ujenzi iongezeke na AGIZO la RAIS Mhe Dkt John Joseph Pombe Magufuli LITEKELEZWE, yaani ujenzi wa awali wa KILOMITA 40.
(2) Kazi kubwa ya awali kwenye kipande cha Kusenyi-Kwikonero imefanyika, yaani kunyanyua tuta na kudhibiti udongo mweusi uliochukua sehemu kubwa ya kipande hiki ambacho ni mkondo wa maji yaingiayo Ziwa Victoria.
Vilevile, ujenzi wa madaraja kwenye maeneo korofi umekaribia kukamilika, kwa hiyo kasi ya ujenzi wa barabara hii MUHIMU SANA kwa UCHUMI wa Jimbo letu na kwa Taifa letu kwa ujumla (madini, samaki, pamba, mihogo, maziwa, n.k.) iongezeke.
(3) Fedha za Mradi zitolewe kwa wakati baada ya maombi yote kutimiza masharti yaliyowekwa.
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini
www.musomavijijini.or.tz