Tarehe 17.5.2021
Jimbo la Musoma Vijijini
Na: Verediana Mgoma
Msaidizi wa Mbunge
HUDUMA za AFYA ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (Musoma DC) yenye Jimbo moja la Uchaguzi (Jimbo la Musoma Vijijini) ni hizi zifuatazo:
*Hospitali ya Wilaya ya Serikali: ujenzi unakamilishwa
*Vituo vya Afya 3 vya Serikali vinatoa huduma za Afya. Vituo hivi ni: Murangi, Mugango na Bugwema (Bugwema – ujenzi ni wa upanuzi wa Zahanati ya Masinono kuwa Kituo cha Afya, ujenzi unakamilishwa)
*Zahanati 23 za Serikali zinatoa huduma za Afya
*Zahati 4 za Binafsi zinatoa huduma za Afya.
*Zahanati Mpya 15 zinajengwa na Wanavijiji. Serikali imeanza kuchangia baadhi ya ujenzi wa Zahanati hizo.
JIMBO la Musoma Vijijini lina KATA 21 zenye VIJIJI 68 na VITONGOJI 374.
KIJIJI CHA NYABAENGERE CHAAMUA KUJENGA ZAHANATI YAKE
Wananchi wa Kijiji cha Nyabaengere kilichopo Kata ya Musanja wameanza ujenzi wa ZAHANATI yao wakiwa na LENGO KUU la kutatua tatizo lao la kutembea umbali mrefu wa zaidi ya KILOMITA 10 kwenda kutafuta HUDUMA za AFYA zilizoko Kata ya jirani ya Murangi – Kituo cha Afya Murangi.
DIWANI wa Kata ya Musanja, Mhe Ernest Mwira amesema ZAHANATI inayojengwa Kijijini hapo itakuwa na jumla ya VYUMBA 14.
HUDUMA za AFYA zitakazotolewa ni pamoja na:
*Kliniki ya Wajawazito na Huduma za Uzazi wa Mpango
*Huduma za Mama & Mtoto
*Matibabu mbalimbali na huduma nyingine za Afya
Diwani huyo amesema LENGO lao ni kukamilisha ujenzi wa ZAHANATI ya KIJIJI cha NYABAENGERE ndani ya MWAKA MMOJA.
MAMA Sophia Otieno, Mkazi Kijiji cha Nyabaengere amesema kukamilika kwa Zahanati hiyo kutaondoa adha wanayoipata AKINA MAMA kujifungulia nyumbani na njiani, na wengine kupoteza maisha wakienda kujifungulia mbali kwenye Kituo cha Afya cha Murangi.
MICHANGO YA UJENZI
MTENDAJI wa Kata ya Musanja, Ndugu Michael Tafuna amesema ujenzi wa Zahanati hiyo utafanikishwa kwa MICHANGO ifuatayo:
*NGUVUKAZI za Wanakijiji za kusomba mawe, kokoto, mchanga na maji ya ujenzi.
*Tsh 24,000 kutoka kwa kila Mwanakijiji mwenye nguvu za kufanya kazi
*MAPATO ya Kijiji yanatokana na uuzaji wa rasilimali zao ambazo ni mchanga, mawe na kifusi.
*MAPATO kutoka kwenye ushuru wa mifugo.
*MICHANGO ya DIWANI, Mhe Ernest Mwira – atachangia SARUJI MIFUKO 20. Ameanza kwa kuchangia Saruji Mifuko 5.
*MICHANGO ya Mbunge wa Jimbo, Prof Sospeter Muhongo.
Mbunge huyu atatumia mtindo wake wa kuchangia hatua zote za ujenzi kama afanyavyo kwingine Jimboni mwao, na kwa Zahanati hii ameanza kwa kuchangia ujenzi wa msingi kwa kutoa SARUJI MIFUKO 50.
OMBI KUTOKA KIJIJI CHA NYABAENGERE
Diwani na Wananchi wa Kijiji cha Nyabaengere wanawaomba WAZALIWA wa KIJIJI hicho na KATA ya MUSANJA kwa ujumla waungane na ndugu zao kuchangia ujenzi wa ZAHANATI hii. WADAU wengine wa MAENDELEO nao wanakaribishwa kutoa MICHANGO yao.
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Musoma Vijijini