Baadhi ya wananchi wa Musoma Vijijini waliohudhuria mkutano huo wakimsikiliza Mbunge wao, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
Na Fedson Masawa
MAMIA ya wananchi wamejitokeza kuhudhuria kikao maalumu cha kujadili uchumi na maendeleo ya jimbo lao kilichofanyika jana kwenye kijiji cha Murangi, Musoma vijijini.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wa serikali, madiwani, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wasomi mbalimbali wakiwemo waliozaliwa ndani ya jimbo hilo.
Waliowakilisha serikali kwenye kikao hicho ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk. Vincent Naano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma, Frola Yongolo.
Awali akizungumzia kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo aliwataka viongozi wa idara zote na madiwani wajipange kwa sehemu zao na kuhakikisha kila kitakachojadiliwa kinafuatiliwa ndani ya miezi minne kwa ajili ya kupima utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho.
Mambo yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na Elimu, Afya na kilimo kama yalivyoainishwa kwenye vipaumbele vya jimbo la Musoma Vijijini.
Elimu
Akianza na suala la Elimu, Prof. Sospeter Muhongo amefafanua kuwa, madawati bado hayajatosha kwani ukizingatia idadi ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba na wale walioandikishwa darasa la kwanza na upungufu wa madawati ya shule za sekondari, bado kutakuwa na upungufu wa madawati 5000 ndani ya jimbo zima.
Ili kufanikisha zoezi hili, Mbunge ameiagiza halmashauri kulisimamia na kuhakikisha hakutokuwa na upungufu wa madawati. Pia aliwaomba wote wenye moyo wa kuchangia wawasiliane na mkurugenzi wa halmashauri kupitia namba ya simu: +255754414441
“Kwa hiyo ndugu zangu hiyo kazi tunaiweka mikononi mwa halmashauri na watakaohitaji kuchangia, ni vizuri muwasiliane na mkurugenzi” alitoa utaratibu Prof. Muhongo.
Kwa upande wa ujenzi wa vyumba vya madarasa, Prof. Muhongo amebainisha kuwa, kuna upungufu wa vyumba 748 vya madarasa kwa shule zote za msingi na sekondari na tayari ameshafanya mazungumzo na JKT kwa ajili ya kupatiwa vijana watakaofanya shughuli za ujenzi wa vyumba hivyo jimboni.
Pia ameongeza kuwa vifaa ikiwemo saruji na mabati vitanunuliwa moja kwa moja kutoka viwandani na ameshakamilisha mazungumzo na makampuni mawili; TWIGA CEMENT kwa ajili ya saruji pamoja na ALUMINIUM AFRICA kwa ajili ya mabati.
Akizungumzia utaratibu wa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, Prof. Muhongo amesisitiza kuwa, fedha zote zitakazochangwa zinakwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya kampuni husika, jimboni vitaletwa vifaa tu na vifaa vikifika vielekezwe kwenye maeneo husika.
“Hatutoi hela mkononi, unapokea mabati na simenti, na simenti ikifika naomba iende moja kwa moja kwenye eneo husika isikae stoo” alisisitiza Prof. Muhongo.
Wakichangia kipengele cha ujenzi, wananchi na viongozi wa jimbo la Musoma vijijini wamekubaliana na Mbunge wao na kuahidi kuungana pamoja na pia kuacha malumbano ili kusukuma gurudumu la maendeleo ya jimbo hilo.
“Kinachotuumiza ni ubishi, lakini tunaamini tupo pamoja na wewe na tunaahidi kukupa ushirikiano. Pia hatutaweza kuwavumilia viongozi wazembe wa halmashauri watakaoonesha namna fulani ya kurudisha nyuma maendeleo ya Musoma vijijini” alisema Mambo Japan, Diwani wa kata ya Bulinga.
Kuhusu ujenzi wa shule za sekondari za elimu ya juu; Akigusia pia suala hilo, Prof. Muhongo amesisitiza ujenzi wa sekondari za mfano za sayansi; Mkirira, Mugango, Bugwema na Mtiro kuwa kasi iongezeke ili ifikapo mwaka 2018 ziwe tayari na ziwe zimeanza kutumika ambapo amesisitiza kuwa ni shule za masomo ya sayansi.
Kilimo
Suala la kilimo pia limezungumzwa ambapo Prof. Muhongo amesisitiza wananchi kuendelea kulima mazao ya biashara na chakula kwa ajili ya kuondokana na umaskini na kuongeza chakula kwa kila kaya.
Akizungumzia suala la mbegu za alizeti, Prof. Muhongo amesema tayari jumla ya tani 5 za mbegu za alizeti zimeshawasili jimboni na tayari wakulima wameshapewa mbegu hizo bure. Aliongeza kuwa endapo kutakuwa na wakulima wanaohitaji mbegu hizo basi watoe taarifa zinunuliwe nyingine.
“Tani 5 za mbegu za alizeti sawa na kilogramu 5000 zimeshagawiwa kwa wakulima. Kama kuna watu bado wanahitaji waseme mbegu ziagizwe tena” alisema Prof. Muhongo
Akizungumzia utaratibu wa soko la alizeti, Prof. Muhongo amewathibitishia wananchi kuwa soko la uhakika litakuwepo na pia mashine ndogo ndogo za kukamua zitatolewa kwa baadhi ya kaya ili wakamue na kuuza mafuta.
“Mwaka jana tuliuza, mwaka huu tutauza na tutakuwa na mashine ndogo ndogo za kukamua mafuta. Pia nimeshafanya mawasiliano na mmiliki wa kiwanda kikubwa cha mafuta na amenithibitishia kufika jimboni kwa ajili kununua alizeti” alithibitisha Prof. Muhongo.
Kilimo cha umwagiliaji na mbegu za mihogo; Prof. Muhongo mbele ya mamia ya waliohudhuria kikao hicho amependekeza fedha za mfuko wa jimbo Tshs. 38,479,000/= zielekezwe kwenye vikundi vya kilimo cha umwagiliaji pamoja na kununulia mbegu za mihogo na ameomba madiwani watayarishe orodha ya vikundi vitakavyonufaika na fedha hizo.
Aidha, Prof. Muhongo amependekeza pia kikao cha kuhidhinisha fedha hizo kifanyike 26, Disemba 2016 saa 9:00 alasiri kijijini Tegeruka.
Uvuvi, suala la ufugaji wa samaki; suala hili pia limesisitizwa kwa madiwani na halmashauri kutakiwa kuorodhesha maeneo ya ziwani yanayofaa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa wa samaki. Prof. Muhongo amependekeza kikao cha ufuatiliaji wa maazimio kifanyike kijijini Bugoji baada ya miezi minne kuanzia sasa.
Afya
Wakizungumza kuhusu ujenzi wa vituo vitatu vya afya jimboni; Bukima, Nyegina na Mugango, Madiwani wa kata hizo wamesema kuwa ujenzi wa vituo umeaanza na unaendelea vizuri.
“Nyumba ya mganga boma tayari limekamilika na maboma ya wodi yapo tayari hivyo naomba halmashauri itusaidie kuezeka kwani tunatarajia kufikia 2017 tutakuwa tumekamilisha” alifafanua Mchele Majira, Diwani wa kata ya Nyegina.
Kwa upande wake Prof. Muhongo ameongezea kuwa kila mwananchi awe mlinzi wa mali zinazoingizwa jimboni ili zitumike katika matumizi sahihi na kuendelea kuwapa moyo wale wanaojitolea kulisaidia jimbo la Musoma vijijini.
Alisema kwa wale madiwani watakaopewa msaada wowote kwenye kata zao ikiwa ni pamoja na magari na vifaa vya ujenzi na kushindwa kusimamia vizuri, hatosita kupeleka kata nyingine ambako wanajali.
Halmashauri kufanyia vikao vyote Murangi
Mbunge, Madiwani, Mkurugenzi kwa pamoja wamekubaliana kwa kauli moja mbele ya wananchi wa jimbo la Musoma vijijini kuwa vikao vyote vya halmashuri vitakuwa vinafanyika Murangi. Lengo kubwa ni kutaka kuijenga makao makuu ya halmashauri ya Musoma vijijini ambayo ni Murangi.
Akizungumza na wananchi na viongozi wa ngazi zote, Prof. Mukama Biswalo mwakilishi maalum wa umoja wa Afrika huko Sudan ya Kusini ambaye pia ni mzaliwa wa Musoma vijijini alisema: “hatuwezi kuijenga halmashauri yetu wakati vikao tunafanyia mjini badala ya Murangi. Bila kufanya hivi, haiwezekani kuijenga halmashauri ya Musoma Vijijini.”
“Mkurugenzi, make history kuwa mkurugenzi wa kwanza kuanzisha makao makuu ya Musoma vijijini Murangi. Hatuwezi kuijenga halmashauri wakati hatutaki kufanyia vikao vyetu Murangi” alisisitiza Prof. Biswalo.