WAKULIMA WAPOKEA MBEGU ZA ALIZETI NA UFUTA MUSOMA VIJIJINI

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo akizungumza na baadhi ya wakulima waliokabidhiwa mbegu za alizeti na ufuta, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney.

Na Fedson Masawa

WAKULIMA wa vijiji na kata mbalimbali ndani ya Jimbo la Musoma vijijini wamepokea mbegu za alizeti na ufuta kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Prof. Sospeter Muhongo ikiwa ni maandalizi ya msimu wa kilimo ambao tayari umeanza mwezi Februari, mwaka huu.

Zoezi hilo la ugawaji wa mbegu ambalo lilifanyika kwa kanda tano Bukwaya, Mugango, Murangi, Saragana na Busekera, liliongozwa na mbunge Prof. Muhongo, Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney pamoja na Kaimu Afisa kilimo wa wilaya ya Musoma Ismail Masogo.

Wakizungumza baada ya kupokea mbegu hizo, wakulima hao walisema wamefurahishwa na tukio hilo muhimu na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa ili kuhakikisha wanapanda na kuvuna vizuri na kutumia mazao hayo kwa ajili ya kuinua uchumi wa familia zao na maeneo wanayotoka.

“Tunamshukuru sana Mbunge na Halmashauri yetu kwa kutupa mbegu bure. Tutapanda kwa wakati, tutayatunza mashamba vizuri hatimaye tutoe mavuno yaliyo bora ili kuinua kipato cha familia zetu” alisema Pili Julius,  mkulima kutoka kijiji cha Mayani kata ya Tegeruka.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Kilimo Ismail Masogo alisema, ofisi yake kwa kushirikiana na Maafisa kilimo wa kata, watatoa usimamizi na elimu kwa wakulima kuhusu utayarishaji wa mashamba, upandaji, upaliliaji, uvunaji na utunzaji wa mazao hayo ili kuhakikisha msimu huu unakuwa na mafanikio makubwa Jimboni humo.

Aidha, katika kuimarisha soko na utunzaji wa zao la alizeti, tayari mitambo miwili ya watu binafsi imejengwa Jimboni katika kijiji cha Kusenyi na Saragana ambapo itasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo.

Hata hivyo, wakiwa katika ziara ya ugawaji wa mbegu hizo bila malipo, Mkuu wa Wilaya na Mbunge pia walitembelea shamba la pamba lililopo kijiji cha Kinyang’erere kata ya Bugwema.

Kwenye ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya Dkt. Naano aliwataka maafisa kilimo wa kata na vijiji wahakikishe wanawatembelea wakulima wa pamba kila mara ili kuona maendeleo yao na changamoto zinazowakabili na kuwatatulia kwa lengo la kuongeza mavuno na ubora wa zao hilo.

PROF. MUHONGO AWATAKA WANANCHI KIJIJI CHA NYASAUNGU KUKAMILISHA UJENZI WA ZAHANATI

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika leo kwenye kijiji cha Nyasaungu.

Na. Verediana Mgoma

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amewataka wananchi wa kijiji cha Nyasaungu kuweka nguvu zao katika kumalizia ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho uliosimama kwa miaka sita.

Prof. Muhongo alisema hayo leo wakati wa ziara yake aliyoifanya kwenye kijiji hicho, ambapo aliwataka wananchi hao kujitolea kwa hali na mali kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo mapema na kuahidi iwapo watakamilisha ujenzi huo kufikia Juni, mwaka huu, atachangia mabati kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo ili wananchi wa kijiji hicho wawe karibu na huduma ya afya.

Aidha, katika mkutano huo Prof. Muhongo alichangia mifuko 100 ya saruji pamoja na shilingi 200,000 kwa ajili ya malipo ya fundi na wananchi waliendesha harambee na kufanikiwa kupata fedha ambazo zitatumika kununua mifuko 109 ya saruji.

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyasaungu Magesa Chacha alisema, zahanati ya Nyasaungu ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2012, ambapo walikuwa wakichangia nguvu kazi na fedha, hata hivyo ujenzi huo ulisimama kwa muda baada ya kuwepo kwa changamoto za ukosefu wa fedha, vitendea kazi na wataalamu.

“Baada ya kilio chetu kufika ofisi ya mbunge, tulipata ushirikiano wa kutosha wa namna ya kufanikisha ujenzi wa zahanati ya Nyasaungu, mpaka sasa wananchi wameongeza nguvu zao na kukusanya mchanga, mawe pamoja na kufyatua matofali” alisema Chacha.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyasaungu Manyama Meru, alitoa shukrani za pekee kwa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini kwa kuweka nguvu kwenye sekta ya afya ndani ya kata hiyo na kuwasaidia wananchi wa kijiji cha Nyasaungu kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Musoma Thadeus Makwanda aliahidi kutoa ushirikiano kwa wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni pamoja na kumpeleka mkandarasi kutoka Halmashauri ili kuwaelekeza namna ya kujenga zahanati hiyo kitaalamu.

ZAHANATI NYASAUNGU

Ofisi ya Mbunge inapenda kuwataarifu kuwa, kesho tarehe 15/02/2018 saa 5:00 Asubuhi, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo atatembelea eneo la ujenzi wa zahanati ya Nyasaungu na kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kuhusu utaratibu wa kuendeleza ujenzi wa zahanati yao

Katika ziara yake hiyo, Prof. Muhongo ataambatana na Mganga Mkuu wa wilaya, Madiwani n.k.

KARIBUNI NYASAUNGU

Ofisi ya Mbunge
www.musomavijijini.or.tz

ZAHANATI YA KIJIJI CHA MWIRINGO KUANZA KUTOA HUDUMA MWEZI UJAO

Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo mapema leo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwiringo (wengine hawapo pichani) mbele ya jengo la zahanati ya Mwiringo ambayo itaanza kutoa huduma za afya Machi, 1, 2018.

Na. Mwandishi Wetu

WAKAZI wa Kijiji cha Mwiringo, Halmashauri ya Musoma vijijini na Mbunge Prof. Sospeter Muhongo, wamekubaliana huduma za matibabu kwenye zahanati ya kijiji hicho zianze kutolewa Machi, 1, mwaka huu.

Uamuzi huo umefikiwa kwenye mkutano uliofanyika kwenye kijiji cha Mwiringo, Kata ya Busambara ambapo Prof. Muhongo amechangia  meza, viti na vifaa vingine vinavyohitajika ili kuharakisha ufunguzi wa zahanati hiyo.

Wiki chache zilizopita, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Makwanda alisema, jambo linalochelewesha zahanati hiyo kuanza kutoa huduma, ni ukosefu wa meza nne na viti nane na vifaa vingine, hivyo kwa mchango huo wa mbunge kero ya muda mrefu ya wananchi wa kijiji cha Mwiringo ya kukosa huduma za afya inaelekea kupata ufumbuzi.

Zahanati hiyo ilianza kujengwa Mwaka 2011 kwa nguvu za wananchi na kwa mchango mkubwa wa vijana wasomi na wataalamu kutoka Kijiji cha Mwiringo, ujenzi wake ulikamilika mwaka 2014 na awali zahanati hiyo ilipangwa ianze kutoa huduma Mei, 1, 2018, lakini kutokana na hamasa iliyopo, itaanza kutoa huduma mwezi ujao.

KIKUNDI CHA AKINAMAMA WA LYASEMBE WAFURAHIA MAFANIKIO KWENYE KILIMO

Baadhi ya akinamama wa Kikundi cha kijiji cha Lyasembe wakiwa kwenye picha ya pamoja na Msaidizi wa Mbunge, Verdiana Mgoma alipowatembelea kwenye eneo wanalofanya mradi wao wa kilimo.

Na. Verdiana Mgoma

KIKUNDI cha akina mama wa kijiji cha Lyasembe wamesema wamepata mafanikio makubwa kiuchumi baada ya kujitosa kwenye kilimo cha umwagiliaji.

Kikundi hicho ambacho ni miongoni mwa vikundi vilivyopata ufadhili wa fedha za mfuko wa jimbo, kinajishughulisha na kilimo cha bustani za mboga mboga na matunda.

Katibu wa kikundi hicho Mawazo Jumbura alisema, baada ya kupokea mashine, mipira na mbegu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, walitambua kuwa wana jukumu kubwa katika jamii yao na kuamua kutumia vifaa hivyo kutafuta maendeleo yao, familia zao na jamii inayowazunguka.

Katibu huyo alisema, tangu wameanza kilimo hicho, hali zao kimaisha zimebadilika na wanamudu mahitaji ya familia zao ikiwemo kusomesha watoto na kununua mahitaji yao binafsi na wamejiwekea malengo ya kununua mashine nyingine za umwagiliaji na kuanzisha miradi mingine mbali na kilimo ili kujiongezea kipato zaidi.

Mbali na faida walizopata kupitia kikundi hicho, Katibu huyo pia ameelezea changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa eneo kubwa la kulima, ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa zao baada ya kuvuna, ugumu wa upatikanaji wa elimu kupitia matamasha, wahamasishaji na maonyesho kwa ajili ya kuboresha zaidi kilimo chao.

Hata hivyo, licha ya changamoto hizo wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa kuwaonyesha fursa hiyo ya kilimo cha umwagiliaji ambacho wanaamini kitawainua kiuchumi.

Naye, Afisa kilimo wa Kata ya Murangi Maricha Mgono akizungumza kijijini Lyasembe alisema, mpango wa kilimo cha umwagiliaji ni harakati zilizowekwa kuhakikisha akina mama na vijana wanajiajiri kupitia kilimo na kuinua hali zao kiuchumi.

Mgono alisema, hivi sasa kumekuwepo na muamko mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji katika kata hiyo tofauti na ilivyokuwa awali wakazi wa eneo husika walijikita zaidi kwenye uvuvi.

“Tumefanya jitihada za kuhamasisha uundwaji wa vikundi kwa maendeleo ya akina mama na vijana ili kuwepo kwa upatikanaji wa mikopo itakayowasaidia kuwainua kiuchumi na kufungua miradi mbalimbali” alisema.

Kwa upande wake Mtendaji wa kijiji cha Lyasembe Chikonya Chikonya alisema, kadri siku zinavyokwenda, mwitikio wa wananchi kwenye kilimo unazidi kutokana na hamasa ya Prof. Muhongo ambaye aliwahimiza kujikita kwenye kilimo hicho cha umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua ambazo hazina uhakika kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Kijijini hapa nimepokea mbegu za mtama, mihogo, alizeti kutoka ofisi ya mbunge na mpaka sasa kuna mikakati ya kilimo cha ufuta, kwa ujumla muitikio wa kilimo kwa wakazi wa eneo hili unakuwa siku hadi siku” alisema Chikoya.

MAADHIMISHO YA MIAKA 41 YA CCM YAPAMBA MOTO BUGWEMA

Baadhi ya akinamama wakiimba wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 41 ya kuzaliwa CCM yaliyofanyika kwenye kijiji cha Bugwema

Na. Mwandishi Wetu

DIWANI wa Kata ya Bugwema Ernest Maghembe amesema, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mageuzi makubwa kwa kipindi ilichokaa madarakani.

Akizungumza kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 41 tangu kuzaliwa CCM yaliyofanyika kwenye kijiji cha Bugwema, diwani Maghembe alisema, CCM imefanya mageuzi makubwa ambayo wanachama wake wanapaswa kujivunia hususani kwenye elimu, afya, na kilimo.

Aidha, diwani Maghembe alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia na watanzania wote kufuatia msiba wa mmoja wa waasisi wa chama hicho Mzee Kingunge Ngombale Mwiru aliyefariki wiki iliyopita na kuzikwa leo jijini Dar es Salaam.

“Tutakumbuka mchango wa mzee Kingunge kwa nchi yetu na chama, tutamuenzi kwa uzalendo wake” alisema diwani Maghembe.

Kwa upande wake msaidizi wa mbunge Hamisa Gamba aliwaomba wanachama wa CCM kuachana na makundi yanayoweza kuleta mgawanyiko ndani ya chama na badala yake maadhimisho hayo yatumike kuwajenga kifikra na katika uwajibikaji hasa kwenye kilimo, elimu na afya.

Msaidizi huyo pia aliwataka wanachama wa CCM na wananchi wote kujiandaa kwa kilimo cha alizeti na ufuta kwa kuwa mbegu zinatolewa bure na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini huku akisisitiza uwepo wa soko la uhakika kwenye mazao hayo.

Sherehe hizo ziliadhimishwa kwa michezo mbalimbali ya vijana ikiwemo kwaya na mpira wa mguu kutoka kwa timu zilizopo kwenye kata hiyo.

 

VIJANA WAHIMIZWA KUONYESHA VIPAJI VYAO KATIKA SOKA

Msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa akimpongeza nahodha wa timu ya Zahanati Mafuru Majogoro (kushoto) na kumkabidhi zawadi yao ya mbuzi watatu baada ya kuibuka mabingwa wa Ligi ya ‘Bashiri Vitongoji Ndondo Cup Bukima.’

Na Mwandishi Wetu

VIJANA wametakiwa kujitokeza kwa wingi na kuonyesha vipaji vyao katika mchezo wa mpira wa miguu na hatimaye kutumia vipaji hivyo kujiajiri kupitia timu kubwa za ndani na nje ya Jimbo la Musoma vijijini.

Hayo yamesemwa na msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa aliyekuwa mgeni rasmi katika fainali za Ligi ya vitongoji vya kijiji cha Bukima maarufu kama “Bashiri Vitongoji Ndondo Cup Bukima,” iliyoshirikisha timu kutoka vitongoji nane, ikiwa ni maandalizi ya ligi kubwa inayotarajiwa kuanza hivi karibuni kwenye kata ya Bukima.

Masawa alisema, kufanyika kwa mashindano hayo ni hatua nzuri ya kufungua njia kwa vijana wa Musoma vijijini katika kutumia vizuri  vipaji vyao na kumpongeza muandaaji wa mashindano hayo Bashiri Chirwa kwa jitihada anazofanya katika kuhamasisha mpira wa miguu kwenye kata hiyo.

Katika mashindano hayo, timu ya Zahanati ilichukua nafasi ya kwanza kwa kushinda magoli 2 dhidi ya Senta iliyopata goli 1 na kushika nafasi ya pili ambapo mshindi wa kwanza alipata zawadi ya mbuzi watatu na mshindi wa pili alipata mbuzi wawili.

WANANCHI NYASAUNGU WAFICHUA SIRI YA MAFANIKIO YAO

Wananchi wa kijiji cha Nyasaungu waliojitolea kushiriki ujenzi wa zahanati ya kijiji chao wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Na. Fedson Masawa

WANANCHI wa kijiji cha Nyasaungu wamesema siri ya maendeleo kijijini hapo ni umoja, mshikamano na kuheshimiana baina ya wananchi na viongozi ambao kwa kiasi kikubwa ndio wanahusika kusimamia shughuli hizo.

Wananchi hao walisema, maendeleo ni kuwa na mipango ya pamoja, kusikilizana na kuwajibika katika kuchangia shughuli yoyote ya maendeleo bila kusukumwa, hali ambayo inawapa moyo wafadhili mbalimbali na kuungana nao ili kuwapatia huduma bora kijijini hapo.

Katika hatua nyingine, wananchi hao wameishukuru Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini kwa namna ambavyo imewarudisha katika utaratibu wa maendeleo kupitia hamasa na kuwapa moyo wa matumaini ili kufanikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Nyasaungu.

Naye Kaimu Mtendaji wa kijiji hicho  Janas Itembe alisema, baada ya kukamilika kwa maandalizi ya kukusanya kokoto na mchanga, shughuli rasmi ya kurekebisha msingi wa zahanati itaanza Februari 5, 2018 baada ya mhandisi wa wilaya kufika kwa ajili ya maelekezo.

ZAHANATI YA MWIRINGO KUANZA KUTOA HUDUMA MEI MOSI

Msaidizi wa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini (Fedson Masawa) akipewa maelezo ya ujenzi wa zahanati ya Mwiringo na Mwenyekiti wa kijiji cha Mwiringo Claudian Ihunyo.

Na Mwandishi Wetu

MSAIDIZI wa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Fedson Masawa ametembelea zahanati ya kijiji cha Mwiringo kilichopo kata ya Busambara kwa lengo la kujua sababu za kuchelewa kuanza kwa zahanati hiyo kutoa huduma za matibabu.

Zahanati hiyo iliyokamilika ujenzi wake tangu mwaka 2014, imejengwa kwa msaada wa mzaliwa wa kijiji hicho kwa kushirikiana na wananchi hadi kufikia kukamilika kwa ujenzi huo, lakini imeshindwa kutoa huduma za afya.

Akizungumza na msaidizi wa Mbunge, Mganga mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Makwanda amethibitisha kuwa zahanati ya kijiji cha Mwiringo tayari imekamilika na wao kama idara ya afya ngazi ya wilaya wameshaandaa mahitaji yote na watumishi wa zahanati hiyo wapo tayari kuanza kazi muda wowote.

Dkt. Makwanda alisema, jambo linalochelewesha zahanati hiyo kuanza kutoa huduma ni ukosefu wa meza nne na viti nane ambavyo gharama yake ni shilingi 2,400,000 na zinatakiwa kuchangwa na wananchi wa kijiji hicho ili kufanikisha mahitaji ya zahanti hiyo na kufunguliwa.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mwiringo Claudian Ihunyo Maganya amekiri kukosekana kwa meza na viti, jambo ambalo linasababisha wananchi hao kuendelea kukosa huduma ya afya na kulazimika kutembea umbali mrefu zaidi kwa ajili ya kuitafuta huduma ya afya kwenye vijiji vya jirani.

Mwenyekiti huyo alitoa ombi kwa Prof. Muhongo kuwaunga mkono wananchi hao, kwani kwa kipindi kirefu wamekuwa wakielekeza michango yao katika kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Naye Mtendaji wa kata ya Busambara Victor Kasyupa alisema: “ipo haja ya zahanati ya Mwiringo kufunguliwa haraka ili kuwanusuru akina mama na watoto wanaolazimika kusafiri umbali usiopungua kilomita nne kuitafuta huduma ya afya.”

Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amekubali kushirikiana na Halmashauri na wananchi wa Mwiringo katika kukamilisha mahitaji ya zahanati hiyo na kuhakikisha inaanza kufanya kazi Mei, 1, 2018.

MKUU WA WILAYA AENDELEA NA ZIARA YA KIKAZI MUSOMA VIJIJINI

 

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano Anney (kulia) akikaribishwa kuzungumza kwenye mkutano uliofanyika kwenye kijiji cha Bukima.

Na. Verdiana Mgoma

MKUU wa wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano Anney ameendelea na ziara yake ya kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kusikiliza kero za wananchi wake.

Akiwa katika Jimbo la Musoma Vijijini, Dkt. Naano alifanya ziara katika kata ya Bwasi na Bukima na kufanya mikutano ya hadhara kusikiliza kero zinazowakabili wananchi wa kata hizo ikiwemo changamoto za elimu, maji, mradi wa kilimo cha umwagiliaji (Nyakanda) ambao umesimama na haufanyi kazi

Akijibu kero hizo Dkt. Naano kwanza aliwashukuru wananchi hao kwa kuungana na serikali kuhakikisha wanapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya vyumba vya madarasa hasa kwa msaada mkubwa kutoka kwa Mbunge wa jimbo hilo Prof. Sospeter Muhongo ambao umefanikisha ujenzi wa vyumba saba na kuviezeka.

Mkuu huyo wa wilaya aliahidi kushirikiana na wananchi hao na Mbunge wao katika kuhakikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyosalia na maabara kwenye kata hiyo vinakamilika mapema.

“Kwa juhudi mnazoendelea kuonyesha kwa kuipa elimu kipaumbele katika kata yenu, nitaungana nanyi na mheshimiwa Mbunge kuhakikisha tatizo la vyumba vya madarasa linakwisha kabisa” alisema Dkt. Naano.

Kwa upande wa sekta ya afya, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wakazi wa eneo husika kutoa ushirikiano zaidi katika kutimiza malengo yao hasa kwa upande wa ujenzi wa kituo cha afya cha Bukima ili kuboresha zaidi huduma za afya kwenye kata hiyo.

Mbali na hayo, Dkt. Naano amewataka wakazi wa eneo hilo kujikita zaidi katika kilimo hasa cha umwagiliaji kutokana na kuwepo kwa miradi ya kilimo na fursa ya upatikanaji wa maji kwa urahisi, hivyo amewataka kulima zaidi mazao ya nafaka.

WANAFUNZI WANYERE ‘A’ WAELEZEA CHANGAMOTO YA UPUNGUFU WA MADARASA

Na Hamisa Gamba

WANAFUNZI wa shule ya msingi Wanyere A, iliyopo kata ya Suguti, Jimbo la Musoma vijijini wanakabiliwa na uhaba wa mkubwa wa vyumba vya madarasa hali inayowalazimu kusoma wakiwa chini ya miti.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi shuleni hapo, wanafunzi wa darasa la tano wa shule hiyo walisema, hivi sasa hawana tatizo la madawati kama ilivyokuwa mwanzo, lakini wanakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Mmoja wa wanafunzi hao Jackson Malima alisema, mbali na changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa inayowafanya wasome kwenye mazingira magumu ikiwemo kuchomwa na jua kwa muda wote wa masomo, lakini bado darasa lao hilo la nje halina ubao wa kufundishia.

“Madarasa tuliyonayo ni machache sana, hivyo inatulazimu wakati mwingine kubadilishana chumba cha darasa na wanafunzi wa darasa lingine pale tunapohitaji kujifunza kwa maandishi hususani somo la hisabati ambalo ni lazima ubao utumike” alisema Malima.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Wanyere ‘A,’ Buriro  Manyama, alisema ukosefu wa madarasa ni changamoto kubwa inayowakabili shuleni hapo na kuchangia kwa kiasi kikubwa kushusha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wao.

Mwalimu Manyama alisema, sambamba na hilo bado shule yao haina vyoo, hivyo huwalazimu kuchangia choo cha shule ya msingi Wanyere ‘B,’ ambacho hakikidhi mahitaji ya wanafunzi 900 wa shule zote mbili.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi na mwalimu mkuu huyo waliomba msaada wa serikali, viongozi na wazazi ili kukabiliana na changamoto hizo za upungufu wa vyumba vya madarasa na vyoo.

KILIMO CHA ALIZETI NA UFUTA JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI

Wakulima wa Jimbo Musoma Vijijini wameendelea kupata uzoefu wa kulima ALIZETI na kwa sasa wanaingia msimu wa 3. Mbunge wa Musoma Vijijini, DC, DED na Afisa Kilimo wa Halmashauri wamefanya Kikao leo tarehe 25 Jan 2018 kukamilisha utaratibu wa upatikanaji wa mbegu za ALIZETI na UFUTA kwa ajili ya kilimo cha mazao hayo kwa msimu huu mpya.

Viongozi hao wamekubaliana kununua mbegu za ALIZETI kilo 4,974 zitakazonunuliwa na Mbunge wa Jimbo (Prof Sospeter Muhongo), na kilo 2,651 za UFUTA zitakazonunuliwa na Halmashauri. Imeazimiwa kwamba mbegu zote hizo zipatikane na kuwafikia Wakulima Jimboni kuanzia tarehe 10 Feb 2018. Jimbo la Musoma Vijijini limeazimia kuwa na ukulima mkubwa wa mazao ya PAMBA, ALIZETI, UFUTA, MUHOGO na mazao mengine ya chakula.

Ofisi ya Mbunge
www.musomavijijini.or.tz

WAZEE WA MUSOMA VIJIJINI WAUNDA BARAZA LAO

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wazee kutoka kwenye vijiji mbalimbali ndani ya jimbo lake ambao walikutana kwenye kijiji cha Murangi na kuunda baraza ambalo litafanya shughuli za kijamii ndani ya jimbo hilo.

Na. Mwandishi Wetu

WAWAKILISHI wa wazee wa vijiji 68 vya Jimbo la Musoma vijijini wamekutana na kuunda baraza lao ili kurahisisha na kuboresha mawasiliano baina ya wazee na jamii inayowazunguka.

Malengo mengine ya kuanzishwa kwa baraza hilo ni  kuweka pamoja mawazo ya wazee katika kusimamia maadili ndani ya jamii na kuishauri serikali katika suala zima la utekelezaji na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo.

Kikao hicho cha wazee hao kilichofanyika Januari, 23, katika kijiji cha Murangi, kilihudhuriwa na mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, madiwani na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Musoma pamoja na wazee wawili kutoka katika kila kijiji walio wawakilisha wazee wenzao kutoka vijijini.

Wakizungumzia muundo wa baraza hilo, wazee wa Jimbo la Musoma vijijini wamekubaliana kuwa, muundo wa baraza hilo uanzie ngazi ya kijiji, kata hadi jimbo ambapo kila muundo utakuwa na wajumbe wake watakaochaguliwa na wazee wenyewe kutoka kila ngazi husika.

Aidha, wazee hao wamemshukuru Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo kwa ubunifu wake na kwa kuwajali wazee na wananchi wote wa Jimbo la Musoma vijijini.

Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Muhongo alitumia fursa hiyo kugawa kwa uwazi milioni 26 fedha za mfuko wa jimbo ambapo jumla ya shule 15 zimenufaika na mgao huo.

Shule hizo zimetengewa fedha hizo za kununulia mabati 54 kwa kila shule kwa ajili ya kuezeka chumba kimoja cha darasa katika harakati za kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na sekondari ndani ya jimbo la Musoma vijijini.

Shule zilizonufaika na mgao huo kwa upande wa shule za msingi ni Nyegina, Kambarage, Mugango, Chanyauru B, Tegeruka, Rusoli, Busekera, Butata, Bugoji, Kamatondo, Kusenyi B na Kanyega, huku shule za sekondari ni Busamba, Bulinga na Mabui.

 

HALMASHAURI KUU YA CCM MUSOMA YAKUTANA KUJADILI MAENDELEO

Katibu wa CCM Wilaya ya Musoma Joseph Gatty (aliyesimama) akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (hawapo pichani) huku akisikilizwa kwa makini na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma Vijijini Nyabukika Bwire (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano (wapili kushoto) na Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini James Francis (mwenye fulana nyeusi) pamoja na viongozi wengine.

Na Fedson Masawa

HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Musoma Vijijini, Mkoani Mara imefanya kikao maalum kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wilaya hiyo na kukubaliana kuwaunganisha wananchi bila kujali itikadi zao za vyama.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya wilaya, pia kilihudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Musoma ambaye pia ni mjumbe, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini aliyewakilishwa na Msaidizi wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma na Madiwani wote wanaotokana na chama hicho.

Akizungumza wakati wa ufunguzi Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma na mwenyekiti wa kikao hicho Nyabukika Bwire, aliwataka viongozi wa kata kusimamia na kufuatilia utendaji kazi wa viongozi kuanzia ngazi ya mashina, matawi, kata hadi wilaya hasa katika uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mwenyekiti huyo alisema, ili kufanikisha hayo suala la mawasiliano baina ya viongozi katika chama na serikali ni muhimu katika kuondoa tofauti za utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney aliwashukuru wananchi wanaoendelea kuungana na serikali katika kufanikisha suala la kuchangia elimu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara pamoja na vyumba vya madarasa na kusema hatua hiyo imefikia pazuri.

“Shule nyingi za sekondari na msingi bado zina changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo kukaa chini na serikali inaendelea kufanya jitihada kwa kushirikiana na wazazi kuhakikisha tatizo hilo linakoma” alisema Dkt. Naano.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Charles Magoma alisema, kwenye shule za msingi na sekondari kumejitokeza changamoto ya upungufu wa madawati haswa kwa wanafunzi wapya wanaojiunga darasa la kwanza na kidato cha kwanza.

“Suala la madawati ni changamoto katika shule zetu za sekondari na msingi hasa pale wanafunzi wanapojiunga kidato cha kwanza na darasa la kwanza. Sisi halmashauri tumeshakubaliana tutashirikiana na wazazi katika kufanikisha suala la madawati katika shule zetu” alisema Magoma.

Akitoa taarifa kwa wajumbe wa kikao hicho, Katibu wa CCM wilaya ya Musoma Joseph Gatty alisema, katika kufanikisha kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo alichangia usafiri kwa wajumbe 108 ili kuhakikisha wanawahi kufika kwenye kikao na kurudi majumbani mwao kwa wakati uliopangwa.

Kutokana na mchango huo, Gatty alimpongeza Prof. Muhongo kwa jitihada anazoendelea kuzifanya katika kufanikisha shughuli mbalimbali za chama na serikali ndani ya Mkoa wa Mara.

UVCCM MUSOMA WATAKIWA KUTUMIA VIZURI FURSA ZA MAENDELEO

Wasaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini James Francis (kulia) Verdiana Mgoma na Hamisa Gamba wakifuatilia Kikao cha Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM ( UVCCM) kilichofanyika kwenye kijiji cha Suguti.  

Na. Verdiana Mgoma

UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Musoma umefanya kikao chake kwenye Kijiji cha Suguti na kujadili masuala mbalimbali ya kiuchumi na maendeleo.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara Jacob Mangalaya alisema, Jumuiya hiyo inapaswa kuachana na utegemezi na ili kufikia malengo hayo wanatakiwa kuunda vikundi vitakavyo wanufaisha kiuchumi, kijamii na kisiasa kulingana na fursa zilizopo.

Mwenyekiti huyo alisema, vikundi vitakavyoundwa vinatakiwa kupewa elimu ya kutosha, huku akisisitizia wajumbe kujitokeza kwenye suala la michezo na kugusia zoezi la uhakiki wa mali za UVCCM.

Kwa upande wake Katibu wa UVCCM Wilaya ya Musoma Joseph Mbogo alielezea jinsi ambavyo mfuko wa vijana ulivyowasaidia kuwapa mikopo na kuwawezesha katika miradi ya kilimo, uvuvi na urandaji mbao.

Katibu huyo alisema, mbali na mafanikio hayo waliyoyapata kutokana na mikopo, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utendaji wa kazi zao za kila siku ikiwemo kukosa usafiri, sare na kadi kwa wanachama wapya pamoja na upungufu wa vitendea kazi kwa watendaji ngazi ya kata na wilaya.

Hata hivyo, alimshukuru Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa juhudi na mchango wake kwenye chama na maendeleo ya jimbo kwa ujumla.

KILIMO CHA ALIZETI & UFUTA JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI – VIKUNDI VYA VIJANA – JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI – Msimu wa kilimo cha ALIZETI na UFUTA Jimboni umewadia. Vikundi vya Vijana vikiwemo vya UVCCM vinaombwa viwakilishe maombi ya mbegu za ALIZETI na UFUTA kwa Wasaidizi wa Mbunge au Madiwani wa maeneo yao kabla ya tarehe 25 Januari 2018.

Ofisi ya Mbunge.

www.musomavijijini.or.tz

KIKAO CHA UMOJA WA WAZEE WA JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI

Tarehe: 23 Januari 2018
Mahali: Kijiji cha SUGUTI
Ajenda: Uzinduzi Rasmi wa Umoja huo
Wajumbe wa Awali wa Umoja huo: Wazee wawili (2) kutoka kila Kijiji. Tunavyo Vijiji 68.
Wasaidizi wa Mbunge na Madiwani watayarishe orodha ya Wajumbe wa Awali wa Umoja huo. Wazee wajichague wenyewe kutoka Vijijini mwao.

Ofisi ya Mbunge

UKARABATI WA KABURI LA MWALIMU NYERERE WAKAMILIKA

Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Fedson Masawa (kushoto) akitoa maelekezo wakati wa zoezi la kunyunyizia dawa ya kuua wadudu kwenye paa la nyumba lilipo kaburi la Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Kulia ni William Elisha ambaye ni mmoja wa wanafamilia akiwa na mtaalamu aliyefanya zoezi hilo.

Na Mwandishi Wetu

UKARABATI wa kaburi la Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere umekamilika, ambapo shughuli zilizofanyika ni upakaji wa rangi, unyunyiziaji dawa kwenye paa la nyumba ya kaburi hilo pamoja na kupaka rangi kwenye mawe yaliyomo kwenye nyumba aliyokuwa akiishi Mwalimu Nyerere.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Mwalimu Nyerere mara baada ya kukamilika kwa ukarabati huo, mzee Iddi Selemani alishukuru ushirikiano uliotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika.

Mzee Selemani alisema, anaamini mahusiano ya familia ya Mwalimu Nyerere na viongozi mbalimbali wa nje na ndani ya Tanzania yataendelea kudumu daima na wao kama wanafamilia wataendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa kiongozi yeyote atakayefika kijijini hapo.

“Kwa niaba ya familia ya Mwalimu Nyerere, nitoe shukrani zangu nyingi kwa Prof. Muhongo kupitia ofisi yake kwa namna tulivyoshirikiana katika kulifanikisha zoezi hili. Nasi kama familia tutaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa kiongozi yeyote atakayetutembelea ili kuendeleza mahusiano aliyokuwa nayo Mwalimu iwe ndani hata nje ya Tanzania” alisema mzee Idd Selemani.

Kwa upande wake Fedson Masawa akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo alishukuru kwa ushirikiano aliopata kutoka kwa familia hiyo ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha zoezi hilo litakalosaidia kuendeleza mahusiano baina ya viongozi mbalimbali wa serikali na familia zao.

KABURI LA MWALIMU NYERERE LAFANYIWA UKARABATI

Msaidizi wa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini, Fedson Masawa akikabidhi vifaa kwa ajili ya ukarabati wa kaburi la hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa wafanyakazi na wanafamilia wa Mwalimu Nyerere.

Na. Mwandishi Wetu

FAMILIA ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kushirikiana na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo wameanza ukarabati wa kaburi la Baba huyo wa Taifa lililopo nyumbani kwake katika kitongoji cha Mwitongo, wilaya ya Butiama Mkoani Mara.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Prof. Muhongo kuitembelea familia hiyo mwishoni mwa mwaka jana ambapo pamoja na mazungumzo yao, familia hiyo ilisema rangi iliyokuwa imepakwa kwenye kaburi hilo imepoteza mvuto na wana mpango wa kulifanyia ukarabati kwa kupaka rangi (mausoleum) na kunyunyizia dawa kwa ajili ya kuua na kuzuia wadudu wanaokaa kwenye paa la kaburi hilo.

Kutokana na hilo, wakamuomba Prof. Muhongo aungane nao katika kufanikisha zoezi hilo ambalo limeanza rasmi Januari, 4, 2018 ambapo mbunge huyo amesaidia gharama za ufundi, vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na rangi kwa ajili ya kupaka kaburi na mawe yaliyomo ndani ya nyumba aliyokuwa anaishi Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Mwalimu Nyerere, Rehema Haruna alimshukuru Prof. Muhongo kwa mchango alioutoa ili kufanikisha zoezi la ukarabati na kusema wao kama wanafamilia watatoa ushirikiano mkubwa katika kukamilisha shughuli zote hizo na kutoa mahitaji mengine yatakayohitajika.

KILIMO CHA ALIZETI – JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI

Tukiwa tunaelekea katika msimu wa kilimo cha alizeti mwezi February 2018, ofisi ya Mbunge inaomba kuwatambua wakulima wanaohitaji mbegu za alizeti Jimboni.

Ofisi ya Mbunge kwa kushirikiana na maafisa kilimo wa Wilaya, Kata, Vijiji na viongozi wengine wanapokea maombi ya wakulima wanaohitaji mbegu hizo kwa ajili ya maandalizi.

Mawasiliano Piga Simu No:
+255765592828 // +255764239821 // +255762 626 881 // +255765 535 200

MBUNGE MUSOMA VIJIJINI AKAGUA MIRADI YA ZAHANATI NA SHULE

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini akisikiliza maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule ya msingi Nyausungu.

Na Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amefanya ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika vijiji vya Bukima, Kasoma na Nyasaungu inayotekelezwa kwa michango ya wananchi, fedha za mfuko wa jimbo pamoja na Mbunge.

Katika ziara yake hiyo, Prof. Muhongo amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Majita “B” iliyopo kijiji cha Bukima kata ya Bukima pamoja na jengo la akina mama na watoto linalojengwa katika zahanati ya kijiji cha Bukima ikiwa ni hatua ya awali ya upanuaji wa zahanati hiyo kuwa kituo cha afya.

Akiwa katika kijiji cha Kasoma kilichopo kata ya Nyamrandirira, Prof. Muhongo amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kasoma “A” na Kasoma “B” ambapo alitumia muda wa dakika 45 kuzungumza na wananchi wa kijiji cha Kasoma kuhusu shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Prof. Muhongo alisema, wananchi hao wamefikia hatua nzuri kinachotakiwa sasa ni kuondoa makundi ya kisiasa, kujituma katika shughuli za maendeleo, kujitoa katika michango mbalimbali ya kimaendeleo ili kufanikisha shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa na zahanati bila kutegemea serikali kuu na wafadhili peke yao.

Akikamilisha ziara yake jimboni katika kijiji cha Nyasaungu kata ya Ifulifu, Prof. Muhongo alikagua miradi ya vyumba viwili vya madarasa ambavyo vinajengwa kwa nguvu za wananchi, saruji kutoka kwa mbunge, mabati kutoka kwa mbunge na fedha za mfuko wa jimbo; mchango ambao kwa pamoja umekamilisha ujenzi na upauji wa vyumba hivyo viwili vya madarasa shuleni hapo.

Kwa upande wa ujenzi wa zahanati, Prof. Muhongo ameahidi kupitia ofisi yake jimboni kufuatilia ili kupata ufumbuzi wa kufanikisha shughuli za ujenzi katika kijiji hicho na yeye yupo tayari kuungana na wananchi katika shughuli zote hizo.

Hata hivyo, amewaahidi wananchi wa jimbo lake kuwa, atatoa mchango wake katika shughuli yoyote ya maendeleo ambayo ni moja ya vipaumbele vyake jimboni.

Alisema, ni lazima wananchi waoneshe mfano kwanza kabla ya serikali au wafadhili wengine na kusema, yupo bega kwa na wananchi waliokwishaanza kazi hizo, sasa anasubiria taarifa ya kurudi tena ili aweke mchango wake katika maeneo yote yanayojenga zahanati na vituo vya afya na zahanati kama vile Bukima, Nyasaungu, Nyambono na maeneo mengine jimboni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa jimbo la Musoma vijijini wamemshukuru mbunge wao Prof. Muhongo kwa kuwaunga mkono katika kuboresha huduma ya afya jimboni pamoja na elimu na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikia maendeleo bora katika sekta ya elimu na afya.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Bukima, diwani wa kata ya Bukima January Simula alisema, jitihada za wananchi wa kijiji cha Bukima zimeanza kuonekana kwa vitendo, ndio maana tayari hatua za maendeleo zimeanza kwa kasi kubwa.

Diwani huyo alisema, tayari vyumba viwili vimekamilika katika ujenzi wa shule mpya ya Majita “B” kwa kushirikiana na Mbunge wao pamoja na upanuzi wa zahanati ya Bukima.

“Wananchi wangu wana hamasa kubwa ya kushiriki katika maendeleo na hata jitihada hizi za ukamilishaji wa vyumba viwili ni sehemu ya michango yao na michango ya mbunge. Tutaendelea kutoa ushirikiano Mheshimiwa mbunge na ujio wake hapa leo kama alivyosema ni lazima tumrudishe kama si kuweka jiwe la msingi basi vyote pamoja na msaada wake” alisema Simula.

Kwa upande wake Juma Maungo ambaye ni mwananchi wa kijiji cha Kasoma, amemshukuru mbunge wao Prof. Muhongo kwa jitihada ambazo ameshazifanya na anazoendelea kuzifanya katika jimbo la Musoma vijijini ikiwa ni pamoja na sekta ya elimu, kilimo na afya na wamemuahidi mbunge wao kumpa ushirikiano mkubwa katika shughuli zote za maendeleo.

“Mheshimiwa mbunge kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu kwako kwa jitihada zote unazozifanya na hata unavyoendeleza shughuli za maendeleo jimboni. Kwa kusema hivyo, napenda nitamke wazi kwamba sisi tutakuunga mkono kwa nguvu zote ili tulisukume gurudumu la maendeleo jimboni” alishukuru mwananchi huyo.

Hadi sasa Prof. Muhongo tayari amechangia madawati 8,000 ambayo yameshasambazwa katika shule zote za msingi katika jimbo la Musoma vijijini, amechangia mabati na saruji kwenye shule za masingi na sekondari jimboni.

Aidha, mbunge huyo ametoa magari matano ya wagonjwa katika zahanati nne na kituo cha afya kimoja cha Murangi.

Hata hivyo, katika kuhakikisha hatua za mapambano katika kufanikisha maendeleo ya elimu jimboni mwake, Prof. Muhongo ameshagawa vitabu zaidi ya 10,000 katika awamu nne kwa shule zote za sekondari na msingi za jimbo lake na vitabu zaidi ya maboksi 2500 ambavyo aligawa kwa wabunge wengine wa mkoa wa Mara.

PROF. MUHONGO AZINDUA UJENZI WA KITUO CHA AFYA NYAMBONO

Mratibu wa mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Nyambono Dkt. Majura Songo (kushoto) akisoma taarifa ya mradi huo. Kulia ni mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, akifuatilia kwa makini taarifa hiyo.

 Na Fedson Masawa

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amezindua ujenzi wa Kituo cha afya katika kijiji cha Nyambono kata ya Nyambono kwa kuweka jiwe la msingi.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa jimbo la Musoma vijijini wakiwemo madiwani na wananchi wa kata ya Nyambono, imefanyika Disemba, 25, 2017 katika viwanja vya kituo cha afya Nyambono kinachojengwa kijijini hapo.

Awali akifungua hafla hiyo, Kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Nyambono Sostenes Majura alisema, wananchi wa kijiji cha Nyambono wana hamasa kubwa ya kushiriki shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuchangia nguvu kazi na michango mbalimbali itakayokuwa inahitajika.

Majura alitumia hadhara hiyo kuwaomba viongozi mbalimbali na wananchi wenye moyo wa kujitolea waishio nje ya kijiji na kata ya Nyambono wawaunge mkono ili kufanikisha shughuli hizo za ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa na vyumba vya uangalizi maalum na vyumba vitatu vya madaktari.

Akisoma taarifa ya mpango na utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa kituo hicho cha afya, mratibu wa mradi huo Dkt. Majura Songo ambaye pia ni mzawa katika kijiji cha Nyambono alisema, kijiji cha Nyambono kina watu zaidi ya 5,000 ambao wamekuwa wakipata huduma za matibabu katika zahanati ya kijiji cha Saragana ambayo nayo imeelemewa na wagonjwa.

Mratibu huyo aliendelea kusema, lengo la mradi huo ni kuwaondolea usumbufu wananchi wa Nyambono na umebuniwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na wazawa wanaoishi nje ya kijiji cha Nyambono na kwa umoja na mshikamano huo, tayari wameungana na zoezi la uchangiaji limekwishaanza na fedha hizo zinachangwa moja kwa moja kwenye ofisi ya Mbunge zilizopo Saragana.

Dkt. Songo alisisitiza kuwa, mradi wa ujenzi wa kituo cha afya ni shirikishi ambapo unawahusisha wananchi wa kijiji cha Nyambono walioko ndani na nje ya kijiji, marafiki, viongozi wote wa Musoma vijijini na Halmashauri ya wilaya ya Musoma, huku wananchi  wanashiriki nguvu kazi kama vile kusomba mawe, mchanga na mafundi, wananchi waishio nje ya Nyambono wanashiriki kutoa michango ya saruji 350 ambayo tayari imepatikana mifuko 69 na zoezi bado linaendelea.

“Ndugu mgeni rasmi, mradi huu ni shirikishi ambapo unajumuisha wananchi walioko nje na ndani ya kijiji cha Nyambono, viongozi wa kata na kijiji pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Musoma” alieleza Dkt. Songo.

Hata hivyo, kituo cha Nyambono kimekadiriwa kugharimu shilingi za kitanzania bilioni 2.2 na kitakuwa na jumla ya majengo 12 likiwemo jengo la OPD ambalo tayari ujenzi wake umeanza kutekelezwa, jengo la mama na mtoto na majengo mengine yote kulingana na muongozo kamili wa ujenzi unaostahili kwa mujibu wa taratibu.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo aliwashukuru wananchi wa kijiji cha Nyambono kwa kubuni mradi huo mzuri na ameahidi kuchangia shughuli nzima ya uezekaji wa majengo hayo mara tu yatakapokuwa yamekamilika ujenzi wake.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya wananchi wa kijiji na kata ya Nyambono, Mkoyongi Masatu amewashukuru viongozi wote na wananchi waliojitolea kuchangia michango yao ili kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha afya.

Aidha, Masatu alimshukuru Prof. Muhongo kwa kujitolea kuwaezekea majengo hayo na ameahidi ushirikiano mkubwa ili kufikia Juni 2018 ujenzi huo uwe umekamilika.

“Nitumie fursa hii muhimu kuwashukuru viongozi, Mbunge na wananchi kwa ujumla kwa jitihada zao na michango yao ili kuhakikisha kituo hiki kinakamilika katika muda muafaka. Nami naahidi kutoa ushirikiano mkubwa ili nisimuangushe wala kuupoteza mchango wa Mbunge na ifikapo Juni 2018 kituo kiwe kinaanza kazi” alishukuru na kusema Mkoyongi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa kijiji cha Nyambono wamesema, suala la kujenga kituo cha afya ni jitihada pekee za kuondoa usumbufu, kuleta maendeleo na kupunguza vifo vya mama na mtoto kwani huduma hiyo tayari itakuwa imesogea karibu na jamii hizo ukilinganisha na huduma ya awali inayopatikana katika kijiji cha Saragana na kata za jirani.

Hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la Msingi ilienda sambamba na sherehe za sikukuu ya Krismasi ambapo Prof. Muhongo aliungana na marafiki zake Dkt. Christa na Wolf kutoka Ujerumani walioungana na wananchi wa jimbo lake kuazimisha sikukuu hiyo kwa kushiriki chakula cha pamoja na wananchi wake.

Kabla ya kushiriki hafla za uwekaji wa jiwe la msingi, Prof Muhongo na marafiki wake walipata fursa ya kuhudhuria misa takatifu katika kanisa la Menonite lililopo kijiji cha Nyambono.

ZAIDI YA MILIONI 100 YAPATIKANA KWENYE ZOEZI LA KUCHANGIA ELIMU

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Anney akizungumzia miradi ya ujenzi wa maabara na vyumba vya madarasa kwenye kikao alichoshirikisha madiwani, wenyeviti pamoja na watendaji wa kijiji cha Chumwi.

Na. Verdiana Mgoma

WANANCHI wa vijiji mbalimbali vya Jimbo la Musoma vijijini wanaendelea kuitikia wito wa Mkuu wa Wilaya Dkt. Vicent Anney aliyewataka kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara ambapo zaidi ya shilingi milioni 100 imepatikana.

Dkt. Anney alitoa wito huo mapema mwezi Mei, mwaka huu na kuelekeza kila kaya katika Halmashauri ya Musoma vijijini kutoa mchango wa shilingi 15,000 kwa ajili ya ujenzi huo.

Maelekezo hayo yalipelekwa kwenye vikao vya ngazi ya vijiji na kata na kupata ridhaa ya wananchi ambao walikubaliana kuchangisha kila mwananchi mwenye umri zaidi ya miaka 18 na vijiji vingine vimekubaliana kuchangisha kaya kama ilivyoelekezwa.

Hivi sasa michango hiyo inaendelea kukusanywa kwa vijiji vyote 68 na kusimamiwa na serikali za vijiji, ingawa kasi ya uchangiaji hairidhishi, mpaka sasa fedha iliyokusanywa ni shilingi 108,539,900 ikilinganishwa na kiasi cha fedha kilichokisiwa kukusanywa shilingi 520,710,000 kwa makadirio ya fedha hizo ni sawa na asilimia 21 tu ya fedha iliyo kusanywa.

Kwa maelekezo yaliyotolewa hadi kufikia tarehe 31, Disemba, 2017 halmashauri ikamilishe ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Kutokana na changamoto hiyo, halmashauri iliandaa kikao kilichojumuisha watendaji na viongozi wa halmashauri ili kutatua changamoto na kuunga nguvu kwa ajili ya kazi iliyo mbele ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma vijijini Dkt. Mgema Rutema, akitoa taarifa ya mahitaji ya madarasa na maabara kwa shule za msingi na sekondari alisema, shule za msingi zina upungufu wa vyumba 8,00 vya madarasa, shule za sekondari zina upungufu wa vyumba 56 vya madarasa na vyumba 40 vya maabara.

“Kutokana na mapungufu hayo, malengo tuliyojiwekea ni  kuhakikisha kuwa vyumba vyote vinakamilika ifikapo tarehe 8, Januari, 2018 siku ambayo shule zitafunguliwa” alisema Rutema.

Aidha, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Mkuu wa wilaya juu ya hamasa ya uchangishaji wa mchango wa shilingi 15,000 kwa kaya na shilingi 10,000 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na shilingi 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa maabara.

Kupitia michango hiyo, kuna baadhi ya vijiji vilivyo hamasika na kufanya vizuri zaidi katika ukusanyaji, vijiji hivyo ni Murangi, Busekera, Busamba, Kwikuba, Buira, Bukumi, Kome, Buranga, na Butata, huku vijiji vinavyotajwa kuwa na kasi ndogo ni Mhoji , Mayani, Nyabaengere, Kiriba, Kakisheri, Kinyang’erere na Buanga.

Kupitia kikao kilichofanywa na halmashauri, kwa lengo la  kujifunza kwa waliofanikisha zoezi la uchangishaji, kupata msaada wa uzoefu na mbinu zinazotumika ili iwepo fursa ya viongozi wa vijiji ambavyo zoezi la uchangiaji linasuasua, kuona namna ya kutoa msaada hasa katika uhamasishaji.

Katika kikao hicho, baadhi ya sababu zilizo tajwa kupunguza kasi ya uchangiaji ni pamoja na baadhi ya viongozi wa vijiji kutofafanua vizuri lengo la michango hiyo kwenye mikutano yao, kuingizwa siasa katika michango hiyo ambapo wanasiasa wamekuwa wakiwaambia wananchi kwamba hakuna haja ya kuchangia kwasababu elimu ni bure.

Sababu nyingine zinazotajwa kuteteresha zoezi hilo ni historia ya michango ya nyuma ambayo mapato na matumizi hayajasomwa, hivyo wananchi kuingiwa na wasi wasi wa kupoteza fedha zao na nyingine ni kutokuwepo kwa stakabadhi halali za serikali kwa ajili ya uchangishaji, watendaji kutosimamia ukusanyaji wa michango na baadhi ya vijiji kutokuwa na watendaji.

Hata hivyo, ipo mikakati ya kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa ambapo imeundwa tume kwa ajili ya kusimamia kazi hiyo na kuongeza nguvu kwenye timu za ukusanyaji ngazi za vijiji na kata kwa kubuni mifumo na utaratibu ili kuhakikisha kila kaya inatoa mchango na kusimamia matumizi yake na kuandaliwa mfumo wa ukusanyaji wa fedha kwa kutumia stakabadhi halali za serikali.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa wilaya Dkt. Vicent Anney alisema, changamoto walizonazo ni nyingi katika idara ya elimu, lakini malengo yaliyopo ni kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara na kuwataka viongozi wa kata na vijiji kusimamia shughuli za maendeleo ili kuboresha elimu.

Dkt. Anney alisema, sababu zilizotolewa na baadhi ya viongozi juu ya fedha wanazochangisha kama changamoto ya kutofikia malengo hayo, isiwe visingizio vya wao kukwamisha michango na kuwataka kufanya kazi za maendeleo kwa bidii.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema, ofisi yake itatoa ushirikino kwa viongozi na wananchi ili kuwezesha miradi hiyo yote na kukamilika kwa wakati, huku akiwataka kufikia Januari, 2, 2019 wahitimishe zoezi la uchangishaji, na matumizi ya michango iliyo kwisha kuchangishwa yatajadiliwa kupitia vikao vya WDC, tayari kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara.

OFISI YA MBUNGE YAMJULIA HALI MAMA ALIYEANGUKIWA NA NYUMBA AKIWA MJAMZITO

Msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa (kulia) akiwa amembeba mtoto wa Roza Nyangasi (aliyekaa), kushoto ni Tabu Munibhi ambaye ni wifi wa Roza na mmoja wa watu wanaomuuguza mgonjwa huyo.

Na. Mwandishi Wetu

MMOJA wa majeruhi aliyeangukiwa na nyumba kufuatia mvua kubwa na upepo mkali uliovikumba vijiji mbalimbali vya Jimbo la Musoma Vijijini Roza Nyangasi mkazi wa  kitongoji cha Stoo kijiji cha Kurukerege kata ya Nyegina amesema anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu.

Roza ambaye wakati anapatwa na ajali hiyo alikuwa mjamzito amefanikiwa kujifungua mtoto wa kike anayeitwa Rehema na anaendelea vizuri.

Akizungumza na msaidizi wa mbunge Fedson Masawa aliyemtembelea kujua maendeleo yake, Roza alimshukuru Prof. Sospeter Muhongo kwa mchango wake ambao umemsaidia kugharamia matibabu na hadi sasa anaendelea vizuri.

“Namshukuru Mungu naendelea vizuri japo bado kuna maumivu sehemu za shingo ambapo matofali yalinidondokea. Lakini pia shukrani nyingi sana zimuendee Mbunge wangu Prof. Muhongo kwani bila mchango wake hali yangu ya matibabu haya ingekuwa mbaya” alisema na kushukuru Roza ambaye baada ya kuangukiwa na matofali aliumia miguuni huku akiwa mjamzito na baada ya siku nne alijifungua.

Awali, Kabla ya kuwasili katika kijiji cha Kurukerege kata ya Nyegina, msaidizi huyo wa mbunge aliendelea na zoezi maalum la kufanya tathimini ya uharibifu wa nyumba uliosababishwa na kimbunga na kubahatika kufika nyumbani kwa Roza Nyangasi.

Mapema mwezi uliopita, Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo alimtembelea mama huyo na kumsaidia mchango wa shilingi 200,000 kwa ajili ya huduma ya matibabu ambazo anakiri zimemsaidia kwa kiasi kikubwa.

MBUNGE MUSOMA VIJIJINI AIWEZESHA FAMILIA KUPITIA KILIMO

Msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa (kulia) akikagua shamba la mke wa mzee Kocha baada ya kukamilika kulimwa. Kushoto ni Buinda Kocha ambaye analimiwa shamba hilo akiwa na Chikopa Manumbu (katikati) ni mmoja wa vibarua waliokuwa wakilima shamba hilo.

Na. Mwandishi Wetu

HATUA ya awali ya ulimaji wa shamba la marehemu mzee Kocha aliyekuwa mkazi wa kijiji cha Busekera imekamilika na wakati wowote zoezi la upandaji wa mbegu litafanyika.

Shamba hilo lenye ukubwa wa heka nne, limeandaliwa kwa ajili ya kusaidia familia ambayo imeachwa na mzee huyo ili ijimudu kiuchumi na chakula.

Wakati wa ziara yake kwenye kijiji cha Busekera, Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo alitembelea familia hiyo kutoa pole baada ya kupatwa na msiba ambapo mke wa marehemu mzee Kocha alielezea ugumu wa maisha unaoikabili familia yake na kuomba msaada wa mbunge.

Kutokana na ombi hilo, Prof. Muhongo alitoa ushauri wa kulima shamba hilo na kupanda mahindi na mtama ili familia hiyo ipate chakula na kuuza mazao ya ziada na kujipatia fedha za kukidhi mahitaji mengine muhimu.

Msaidizi wa mbunge Fedson Masawa, akikagua maendeleo ya shamba hilo alisema, wakati wowote wanaweza kuanza kupanda mbegu kuwahi mvua zilizoanza kunyesha ili kwa siku za usoni familia hiyo iweze kujikwamua kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

“Wakati wowote tutaanza kupanda mbegu ili tuwahi mvua ambazo zimeanza kunyesha na mbunge ameahidi kutoa gharama zote za ulimaji pamoja na kununua mbegu” alisema Masawa.

PROF. MUHONGO ACHANGIA MATIBABU YA MPIGA KURA WAKE

Msaidizi wa Mbunge, Fedson Masawa (wa pili kushoto) akimkabidhi Muriti Mafuru fedha taslimu shilingi 300,000 ambayo ni ahadi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ili kufanikisha huduma ya matibabu ya Mzee Mafuru anayesumbuliwa na tatizo la kibofu cha mkojo na tatizo la mguu.

Na Mwandishi Wetu

MSAIDIZI wa Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Fedson Masawa amekabidhi kiasi cha fedha za matibabu kwa familia ya Mzee Mafuru Kati ambaye anasumbuliwa na matatizo ya mguu na kibofu cha mkojo.

Wakati alipotembelea kijiji cha Busekera kuangalia madhara yaliyotokana na mafuriko yaliyovikumba vijiji vingi jimboni humo, Prof. Sospeter Muhongo aliahidi kumsaidia mzee huyo shilingi 300,000 kwa ajili ya matibabu.

Akikabidhi fedha hizo, Masawa aliwataka wanafamilia wanaomuuguza mzee huyo kuwa na uvumilivu na kujituma katika kuendelea kumuhudumia Mzee Mafuru ambaye ni mkuu wa kaya hiyo.

“Ndugu zangu mbunge ametimiza ahadi yake aliyoiahidi. Kuuguza ni kazi ngumu, kinachotakiwa kwenu ni kuwa na moyo wa uvumilivu na kujituma ili kurejesha afya ya mzee wetu” alisema Masawa.

Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo, mmoja wa watoto wa mzee huyo Muriti Mafuru alimshukuru Prof. Sospeter Muhongo kwa kuungana na familia yao ili kuhakikisha afya ya mzee wao inaimarika.

Muriti aliongeza kuwa, watajitahidi kutumia fedha hizo katika kufanikisha matibabu ya mzee wao na si kwa matumizi tofauti.

“Tunamshukuru Prof. Muhongo kwa kuungana nasi kwa mchango wake ili kuimarisha afya ya mzee wetu, mwenyezi Mungu ambariki sana Mbunge. Pia tutajitahidi kutumia fedha hizi kwenye matibabu wala siyo kazi nyingine” aliahidi kijana huyo.

MRADI WA UJENZI WA KITUO CHA AFYA KIJIJINI NYAMBONO

Wazaliwa na Wakazi wa kijiji cha Nyambono wakishirikiana na ndugu na rafiki zao, na wapenda maendeleo kwa ujumla wameamua kujenga kituo cha afya kwa njia ya kujitolea. Mradi huu mkubwa utazinduliwa rasmi na Mh. Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Muhongo, tarehe 25/12/2017, Musoma Vijijini.

Kwa maelezo zaidi ya mradi wasiliana na Majura Amon Songo (0765 300 900)

Msaidizi wa Mbunge: Hamisa Gamba (0762 626 881)

Michango yote itumwe kwa Msaidizi wa Mbunge

www.musomavijijini.or.tz

MBUNGE MUSOMA VIJIJINI ATIMIZA AHADI YAKE KIJIJI CHA SEKA

Diwani wa kata ya Nyamrandirira Ruteli Maregesi (aliyesimama kushoto) na msaidizi wa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Verdiana Mgoma (wa kwanza kulia), wakikabidhi misaada ambayo iliahidiwa na mbunge Prof. Sospeter Muhongo kwa familia ya Nyambita Nyambea wakazi wa kijiji cha seka. 

Na. Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ameendelea kutimiza ahadi ya kuzisaidia familia zilizoomba msaada kufuatia maafa yaliyotokea hivi karibuni kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Wakati wa ziara yake, baadhi ya wahanga akiwemo Nyambita Nyambea mkazi wa Seka, alimuomba mbunge amsaidie kulipa kodi ya nyumba ili aishi na familia yake kwa kipindi ambacho atakuwa kwenye maandalizi ya kujenga makazi mapya.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo na msaidizi wa mbunge Verdiana Mgoma, Nyambita alimshukuru Prof. Muhongo kwa msaada wake na kumuomba aendelee na moyo huo wa kujitolea kwa watu wasiojiweza.

“Mbunge aliahidi kunilipia kodi ya nyumba kwa muda wa miezi sita baada ya nyumba yangu kuanguka kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali, hivi leo nimepokea kiasi cha shilingi 84,000 ambayo ni kodi ya miezi sita, hivyo kupitia msaada huu, hadi kipindi cha kodi kuisha nitakuwa nimepata nguvu za kuanza ujenzi na kurudi kwenye nyumba yangu kama awali” alisema Nyambita.

Aidha Nyambita aliongeza kuwa, mbunge alitoa ahadi ya kumnunulia mwanae Nyafuru viatu vya shule, tayari amepokea jozi mbili za viatu kwa ajili ya masomo na mtoto huyo ameahidi kufanya vizuri zaidi katika masomo yake.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamrandirira Ruteli Maregesi ambaye alishuhudia makabidhiano hayo, alimshukuru Prof. Muhongo kwa dhamira na nia ambayo ameonyesha kwa wananchi wake hasa kuwa na moyo wa kujitolea, huku akikiri kwamba kwa muda aliofanya naye kazi amejifunza mambo mengi.

“Kwa niaba ya wakazi wa kata ya Nyamrandirira tunatoa shukrani zetu na kumuombea kheri” alisema diwani Maregesi.

TATHIMINI YA ATHARI ZA MAFURIKO YAANZA MUSOMA VIJIJINI

Baadhi ya kaya zilizopata maafa kutokana na kimbunga zikichukuliwa tathimini mpya kwa ajili ya maandalizi ya ripoti kamili ya Jimbo zima la Musoma vijijini. Pichani ni Mtendaji wa kijiji cha Bukumi Fred Jeremia ambaye ameambatana na ofisi ya Mbunge kuchukuwa tathimini ya uharibifu huo.

Na Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kuagiza wasaidizi wake kwa kushirikiana na viongozi wengine kuanza kupitia upya tathimini ya uharibifu uliosababishwa na kimbunga na mafuriko, tayari zoezi hilo limeanza.

Wasaidizi wa mbunge na watendaji mbalimbali wa kata na vijiji wameanza kupitia upya takwimu halisi ya maafa hayo katika maeneo ya jimbo la Musoma vijijini ambapo baada ya tathimini hiyo, ripoti kamili ya maafa itaandaliwa kwa ajili ya kuiwasilisha katika mamlaka husika.

Zoezi hilo lilianza 27, Novemba mwaka huu linatarajiwa kukamilika mapema wiki hii ambapo ripoti hiyo itajumuisha hali halisi ya uharibifu uliotokea katika kaya husika, uharibifu uliosababishwa na mafuriko katika mashamba mbalimbali kwa kanda zote za Majita, Mugango na Bukwaya pamoja na ramani halisi ya jimbo inayoonesha maeneo husika yalipotokea maafa hayo.

Ili kufanikisha zoezi hilo kwa haraka zaidi, ofisi ya Mbunge imewaomba wananchi na viongozi wa kata na vijiji husika ambao pia ni waathirika wa matukio hayo kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuharakisha ripoti hiyo.

WACHIMBAJI WADOGO WAELEZA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI

Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Karusenyi kijiji cha Suguti, Musoma vijijini wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa mgodi huo Mapigano Peter (mwenye fulana nyeusi).

Na. Verdiana Mgoma

WANANCHI wa Jimbo la Musoma vijijini wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini aina ya dhahabu, wameiomba serikali kuwasaidia kutatua changamoto wanazo kumbana nazo hasa kwenye sekta ya uchimbaji ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Mkurugenzi wa mgodi wa Karusenyi Mapigano Peter alisema, Jumuiya ya wachimbaji wadogo wana changamoto nyingi endapo serikali itazitatua, watafanya kazi zao kwa ufanisi, mzunguko wa fedha utaongezeka na maisha ya wachimbaji wadogo yatabadilika.

Katibu wa wachimbaji wadogo Hatari Bwatwa, alizitaja changamoto zinazowakabili kwenye shughuli zao za uchimbaji ikiwemo ugumu katika mchakato wa kupata ruzuku, ambapo inachukua muda mrefu kupata mkopo jambo ambalo linawakatisha tamaa na kuomba muda upunguzwe ili waweze kupata mikopo hiyo.

Mbali na hilo, Bwatwa alisema kutokana na kukosa mitaji, wanashindwa kupata pampu za maji zenye uwezo wa kutoa maji haraka wakati uchimbaji unaendelea, mashine za kisasa za kupasulia miamba (Jack harmmers na Compressor) ambavyo vinahitaji uwekezaji mkubwa.

“Tunahitaji crane kwa ajili ya kutoa mwamba au udongo wenye dhahabu hivisasa wachimbaji wanatumia ndoo ambapo wanatumia nguvu na muda mwingi. Pia tunakosa elimu ya kitaalamu kuhusu uchimbaji tofauti na walio wengi kutumia uzoefu” alisema Bwatwa.

Aidha, mbali na changamoto hizo za vifaa, Katibu huyo alisema soko la kuuza dhahabu limekuwa ni tatizo kubwa kwa wachimbaji wadogo, wengi wamekuwa wakiuza dhahabu yao kwa bei ya hasara kutokana na kukosa taarifa za viwango vya uuzaji wa dhahabu na hii inawafanya kila mmoja kuuza kwa bei yake na kuwanufaisha zaidi wanunuzi.

Hata hivyo, Katibu Hatari Bwatwa alisema mbali na changamoto hizo zinazogusa shughuli zao za uchimbaji, wanakabiliwa na hatari ya kuibuka kwa magonjwa yanayochangiwa na muingiliano wa watu, hivyo akaomba serikali iwasaidie kutoa elimu kwa wachimbaji hao na watu wanaoishi jirani na mgodi.

“Wachimbaji wadogo wa dhahabu ni wengi na sehemu kama hizi za machimbo suala zima la maadili lipo chini, maana ni sehemu ya mkusanyiko na watu wanaotoka sehemu mbali mbali, hivyo magonjwa ya zinaa yanashamiri, watoto kuacha shule, vitendo vya ubakaji, mabinti kujiuza, hivyo wakati serikali ikishughulikia namna ya kutatua changamoto za wachimbaji, kwa upande wa pili itengeneze mazingira rafiki yatakayo rekebisha maadili hasa sehemu hizi za migodi” alisema.

MBUNGE WA MUSOMA VIJIJINI ATEMBELEA WAATHIRIKA WA MAFURIKO

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukumi (hawapo pichani) mbele ya nyumba iliyoathirika na mafuriko, anayefuata ni Munubi Bunyinyiga ambaye ni mmoja wa waathirika wa janga hilo, kulia ni Katibu tarafa Adam Maungo.

Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo (kushoto) akiwa na Boazi Maingu, Diwani wa kata ya Rusoli (wapili kutoka kushoto) wakati wakizungumza na wakulima ambao mashamba yao yamesombwa na maji baada ya mvua kubwa iliyonyesha katika kijiji cha Rusoli kata ya Rusoli.  

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyeupe) akipiga picha ya pamoja na waathirika wa mafuriko katika kijiji cha Busekera kata ya Bukumi.

Prof. Sospeter Muhongo akimjulia hali muhanga wa mvua iliyoambatana na upepo mkali katika kijiji cha Kurukerege.

Wananchi wakionesha hali halisi ilivyokuwa wakati wa tukio la Kimbunga kilichoambatana na mvua kubwa katika kijiji cha Bukumi.

PROF. MUHONGO ATOA MSAADA WA CHAKULA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO

Mbunge wa Musoma vijijini, Prof. Sospeter Muhongo akiwa na baadhi ya wananchi wanaotoka kwenye vijiji vya Kata ya Ilifulifu mara baada ya kuwapatia chakula cha msaada kufuatia mazao na nyumba zao kuharibika kutokana na mvua kubwa na upepo mkali kuikumba kata hiyo.

Na. Ramadhani Juma

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ametoa msaada wa chakula kwa kaya 57 zilizoathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha na kuambatana na upepo mkali katika kijiji cha Kabegi kata ya Ifulifu.

Prof. Muhongo ametoa msaada wa kilo 570 zenye thamani ya shilingi 456,000 ambapo kila kaya imepewa kilo 10 za mahindi.

Akizungumza na waathirika wa tukio hilo kabla ya kukabidhi msaada huo, Prof. Muhongo aliwapa pole wananchi wa kijiji cha Kabegi ambao nyumba zao zimeezuliwa na nyingine kubomoka na kuwahimiza kujenga nyumba bora na imara pamoja na kupanda miti mingi katika maeneo ya makazi kwa kata na vijiji vyao ili kuepuka dhoruba kama iliyokumba.

Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kabegi Pilly Waryoba alimshukuru Prof. Muhongo kwa msaada wa chakula aliowapatia na kusema ni hatua nzuri ya kuanzia, kwani mvua iliyonyesha ilisababisha kaya zao kupoteza chakula chote walichokuwa nacho.

Kwa upande wake Magori Maregesi alitoa shukrani kwa Prof. Muhongo kwa moyo wake wa kuitambua vyema na kuijali jamii yake hasa inapokumbwa na majanga, ambapo amewapatia chakula na siyo fedha kama ilivyokuwa imezoeleka kwa viongozi wengine.

“Kiongozi wa namna hii lazima tumtumie vizuri kwani anajali watu hasa wanapopatwa na matatizo makubwa kama haya na ni utaratibu mzuri wa kutupa chakula kuliko hela kama tulivyozoea kwa watu wengine” alishukuru Maregesi.

Naye Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kabegi Charles Choto alimshukuru Prof. Muhongo na kumtakia kheri na baraka katika kazi zake anazozifanya na kuendelea kuwakumbuka na kuwa karibu na wananchi wa jimbo lake la Musoma vijijini.

Choto aliongeza kuwa, wananchi wake wamebomokewa nyumba zao na wengine kuezuliwa nyumba na hivyo kaya nyingi hazina makazi na nyingine zimepoteza chakula, lakini kwa faraja aliyoionesha Prof. Muhongo imeleta matumaini kwa familia hizo.

“Namshukuru sana Prof. Muhongo na ninamtakia kheri katika kazi zake anazozifanya na aendelee na moyo huo wa kuwakumbuka wananchi wake. Ni nyumba nyingi zimebomolewa na kuezuliwa, lakini kwa msaada huu umetutia faraja” alishukuru Mwenyekiti Charles Choto.

PROF. MUHONGO AWEKA WAZI MATUMIZI YA FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Musoma Charles Magoma (kushoto) wakati wa kikao cha kujadili matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo 13, Novemba, 2017 katika kijiji cha Kabegi kata ya Ifulifu.

Na. Fedson Masawa

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ameweka wazi matumizi ya fedha za mfuko wa Jimbo la Musoma vijijini kwa kufanya kikao maalum na viongozi na wananchi wa jimbo hilo.

Kikao hicho kilichoongozwa na Prof. Muhongo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha za Mfuko wa Jimbo, kilihudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Mara Adamu Malima, Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, madiwani wa Musoma vijijini, viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri ya wilaya ya Musoma, wananchi na viongozi mbalimbali wa kata na vijiji kutoka Musoma Vijijini.

Akisoma taarifa ya matumizi na mgawanyo wa fedha hizo afisa mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Joldan Hojode alisema: “kutokana na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi wa jimbo la Musoma vijijini na viongozi mbalimbali wa kata na vijiji walipendekeza fedha hizo zielekezwe katika kuezeka vyumba vya madarasa ambapo maoni hayo yameheshimiwa na kuifanya kamati  ielekeze fedha za mfuko wa jimbo kwenye uezekaji wa vyumba vya madarasa kama walivyopendekeza wananchi.”

Hata hivyo Hojode alisema, fedha hizo zitatumika kununua mabati ya kutosha kuezeka vyumba 17 vya madarasa kwani kila chumba kitapewa jumla ya mabati 54.

Kwa upande wake Prof. Muhongo amewataka madiwani kujituma na kusimamia vyema fedha hizo ili zifanye kazi iliyolengwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia miradi yote iliyofadhiliwa na mfuko wa jimbo.

Prof. Muhongo pia amewasisitizia wananchi na viongozi kujituma katika kuongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, kilimo cha chakula na biashara ikiwa ni pamoja na alizeti na pamba ili kuinua kiwango cha elimu, upatikanaji wa chakula pamoja na kuinua uchumi wa jimbo.

Sambamba na hayo, Prof. Muhongo alipata fursa ya kuungana na Mkuu wa mkoa wa Mara, Mkuu wa wilaya na viongozi mbalimbali kuwapa pole wananchi ambao zaidi ya nyumba 40 ziliezuliwa na kubomolewa baada ya upepo uliombatana na mvua kubwa na kusababisha baadhi ya kaya kukosa makazi katika kata ya Ifulifu kijiji cha Kabegi.

Aidha, akijitambulisha kwa wananchi wa Musoma vijijini Mkuu wa mkoa wa Mara Adamu Malima, aliwataka viongozi na wananchi kutimiza majukumu yao katika kufanya shughuli za maendeleo kuliko kusubiri kusukumwa na ngazi ya juu.

Wakishukuru kwa nyakati tofauti wananchi waliohudhuria kikao hicho wamemshukuru Prof. Muhongo na uongozi wa Mkoa na wilaya kwa uamuzi mzuri wa kugawa fedha za mfuko wa jimbo na kuridhika na mgawanyiko wa fedha hizo katika kanda zote za jimbo la Musoma vijijini.

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa kijiji cha Kabegi Charles Choto, aliwashukuru viongozi wa wilaya na mkoa kwa kuwahi kuwafikia wananchi wa kijiji chake hasa katika matukio ya kubomoka na kuezuliwa nyumba zao na akaahidi kutoa ushirikiano katika kutekeleza vyema shughuli za maendeleo.

“Nakushukuru sana Mheshimiwa DC kwa moyo wa huruma uliouonesha hasa baada ya kupata taarifa ya maafa haya kwenye kijiji changu na kufika kwa wakati. Nawashukuru Mbunge, Mkuu wa mkoa na viongozi wengine kwa kuwafikia wananchi wangu. Tutashirikiana zaidi na zaidi katika kusimamia na kutekeleza shughuli za maendeleo jimboni” alishukuru Choto.

MKUU WA WILAYA YA MUSOMA ATEMBELEA WAATHIRIKA WA MAFURIKO

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano (wa pili kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Bugunda Manyama Malembo (kulia) wakati alipofika kuangalia athari zilizosababishwa na kubwa iliyonyesha siku kadhaa zilizopita (Picha na Fedson Masawa).

Na. Mwandishi Wetu

MKUU wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amewatembelea waathirika wa mafuriko katika kijiji cha Kastam kilichopo kata ya Bukima wilaya ya Musoma vijijini.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya aliongozana na viongozi mbalimbali wa kata ya Bukima na kijiji cha Kastam pamoja na msaidizi wa Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini.

Awali akiwasilisha taarifa fupi ya uharibifu uliotokea, Mtendaji wa kijiji cha Kastam Joseph Phinias alisema,  jumla ya kaya 19 nyumba zao zimebomoka wakati kaya 17 zilikumbwa na mafuriko na nyingine zaidi zikipata nyufa kubwa huku akisisitiza kuwa, kaya zilizobomolewa nyumba zao tayari kaya mbili tu hadi sasa zimekwisha hama maeneo hayo.

Phinias alisema, pamoja na kuwepo kwa uharibifu katika majengo, mazao mengi yamesombwa na maji jambo ambalo linaweza kusababisha tatizo la njaa hapo baadaye.

Akigusia suala la barabara, mtendaji huyo alisema, barabara ya kuingia Kastam kwa sasa imekatika, hivyo hairuhusu tena gari lolote wala pikipiki kuingia na kushauri mamlaka husika kuiwahi barabara hiyo ili kuepusha kukwama kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Naye Diwani wa kata ya Bukima, January Simula alisema, mvua iliyonyesha kwa kipindi cha siku mbili, kata yake ilikumbwa na madhara makubwa, lakini kijiji cha Kastam ndicho kilichokumbwa na madhara makubwa zaidi kwani nyumba nyingi, mashamba yaliyokuwa na mazao takribani ekari 300 yameharibiwa na mvua.

Diwani Simula ameweka wazi kuwa, tayari serikali imeshawaagiza wananchi ambao nyumba zao zipo mabondeni wahame mara moja na kuelekea kwenye makazi mengine.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, amewapa pole wananchi na viongozi wa kata ya Bukima na kijiji cha Kastam kwa tatizo lililowapata na kuwaagiza wananchi walioko mabondeni wahame mapema ili kuepuka mafuriko yanayoweza kujitokeza zaidi.

“Nawaomba wananchi wenzangu, nawaagiza serikali ya kijiji na vitongoji wahame kwenye maeneo ya mabondeni mpaka mvua itakapopungua lasivyo watakuja kupata madhara makubwa sana” aliagiza Dkt. Naano.

Mkuu huyo wa wilaya alisisitiza, wananchi ambao wanaendelea kuishi kwenye nyumba zilizo na nyufa pia wahame ili kuepuka madhara zaidi hasa kupoteza maisha ya jamii.

“Kwahiyo maeneo yote muwaambie wananchi serikali za vijiji, wenyeviti wa vitongoji wananchi wasikae kwenye nyumba zile zilizopasuka kwa maana zitaleta madhara makubwa na hata kupoteza maisha” alisisitiza Dkt. Naano.

Aidha, Dkt. Naano aliwaagiza watendaji kuorodhesha kaya zote zisizo na vyoo vya kudumu hasa kipindi hiki cha mvua na kuzifikisha kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua kwa lengo la kuepukana na madhara ya kipindupindu.

Hata hivyo, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Karebu Musululi ameishukuru serikali kwa wepesi wake na ushauri wao na kusema hali hiyo inaleta faraja na matumaini kwa watu wake na sasa wao wataufanyia kazi ushauri wa serikali ili kuokoa maisha yao

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amemuagiza Mhandisi wa wilaya ya Musoma kwa kushirikiana na wakala wa usimamizi na ujenzi wa barabara (TANROADS) kuharakisha ujenzi wa daraja kubwa lililopo mpakani mwa kijiji cha Bulinga (kata ya Bulinga) na kijiji cha Bugunda (kata ya Bwasi).

Mkuu wa wilaya ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo hilo na kushuhudia daraja hilo ambalo lilivunjika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha 7, Novemba na kusababisha barabara ya Bukima hadi Kome kutopitika.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Bugunda Manyama Malembo alisema, kuharibika kwa daraja hilo kumechangia shughuli nyingi za kiuchumi kukwama, hivyo ni muhimu serikali kuharakisha ujenzi mpya wa daraja hilo.

“Toka daraja hili livunjike, shughuli nyingi za kiuchumi zimekwama, tunaomba tu serikali itusaidie kulishughulikia suala hili.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi wa sekondari ya Nyanja wanaotoka kata ya Bulinga walisema, wana wasiwasi wa kukosa masomo na hata kuhatarisha maisha yao kwani barabara hiyo inapitika kwa shida na wengine ilifikia hatua wakaanza kutoa fedha kwa ajili ya kuvushwa hadi upande wa pili.

TIMU YA SOKA YA BIASHARA MUSOMA MJINI YAFANYA ZIARA BUNGENI

Viongozi na wachezaji wa Timu ya Biashara ya Musoma mjini, Mkoani Mara wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo na Mathayo Manyinyi wa Musoma mjini, leo 10, Novemba timu hiyo ilipowatembelea wabunge hao wanaoshiriki vikao vya bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.

MVUA YAHARIBU NYUMBA, MAZAO NA MIUNDO MBINU MUSOMA VIJIJINI

Diwani wa Kata ya Bukima January Simula (wa pili kutoka kulia) akiwa na Mtendaji wa Kata ya Bukima (wa pili kutoka kushoto) na Mtendaji wa kata ya Katata Charles Buremo (wa kwanza kutoka kushoto) wakiwa kwenye ziara ya kutembelea waathirika wa mvua.

Na. Fedson Masawa

MVUA kubwa iliyodumu kwa takribani masaa sita imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali katika vijiji vya kata ya Bukima.

Mvua hiyo iliyonyesha 7, Novemba mwaka huu ilianza kunyesha asubuhi hadi mchana imesababisha familia nyingi kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka na nyingine kupata nyufa.

Aidha, mvua hizo zimesababisha vyoo vya shule ya sekondari Bukima kutitia, mazao kusombwa na maji pamoja na barabara kukatika.

Mtendaji wa kata ya Bukima Peter Magesa alisema, kijiji cha Kastam ndicho kilichokumbwa na mafuriko zaidi kwani maji yalivamia kaya mbalimbali.

Hata hivyo Magesa alifafanua kuwa, kijiji cha Butata na Bukima, waathirika wake ni wa nyumba kubomoka wala siyo kujaa maji kama ilivyo Kastam.

“Wakulima wengi katika kijiji cha Kastam wameharibikiwa na mazao yao kama vile mihogo, mahindi na viazi kwani mashamba yao yamefunikwa na maji” alisema Magesa.

Magesa aliendelea: “mvua hiyo pia imeharibu miundo mbinu ya barabara hasa katika daraja ya Nyegugu, Kurumonyo (mpakani mwa Butata na Bukima) pamoja na daraja kubwa ya Bukima (barabara ya kuelekea Busekera) jambo lililosababisha huduma ya usafiri kufungwa kwa muda.”

Akizungumzia idadi ya kaya zilizoathirika na mvua hizo, Magesa alisema, ndio kwanza serikali za vijiji na kata zinapita kuchukua orodha baadaye itatolewa takwimu iliyo sahihi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bukima January Simula aliwapa pole waathirika wote kwa tukio lililowapata na kutoa agizo kwa mtendaji wa kata ya Bukima awaandikie barua watendaji wote wa vijiji vya kata hiyo ili kuwapa barua wananchi wanaoishi kwenye maeneo hatarishi wahame mapema na hata wale ambao nyumba zao zimeonesha dalili za nyufa wachukue tahadhari na kupisha nyumba hizo haraka sana.

KILIMO CHA MPUNGA CHATOA FURSA NYINGINE KWA WANANCHI MUSOMA VIJIJINI

Mmoja wa wakulima wa mpunga Amina Masatu akihamisha mbegu kutoka kwenye kitalu kupeleka kwenye majaruba tayari kwaajili ya kupandwa.

Na. Verdiana Mgoma

IDADI ya wakulima wanaojitokeza kulima mpunga kwa kutumia njia ya umwagiliaji inaongezeka kutokana na hamasa inayoendelea kutolewa na wataalamu mbalimbali wa kilimo na viongozi wa serikali.

Afisa kilimo wa kata ya Suguti Masinde Mjarifu alisema, awali haikuwa kazi rahisi kuwashawishi wananchi kulima mpunga kwa kuhofia uhaba wa mvua, lakini baada ya kuelimishwa kuhusu kilimo cha umwagiliaji, wengi wamejitokeza kulima huku wakiwa na matumaini ya kufanikiwa kupitia kilimo hicho.

“Mbali na kuwahimiza kulima kwa umwagiliaji, pia tunawahimiza kutumia mbegu za mpunga wa nchi kavu, fursa hii ya mbegu za mpunga wa nchi kavu ni fursa kwa wakulima wengi zaidi kuzalisha mpunga bila kulazimika kuhitaji maeneo yaliyozoeleka ya mabondeni” alisema Mjarifu.

Mmoja wa wakulima wa mpunga kijijini Suguti, Amina Masatu alisema, wameamua kuanzisha mashamba darasa yatakayowasaidia hasa upande wa kilimo, lengo ni kutambulisha kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya nafaka; mpunga wa nchi kavu.

“Kuwepo kwa mashamba darasa ni kufundisha vikundi mama ili kueneza elimu inayopatikana kwa malengo ya kuwepo kwa wakulima wengi kwenye kilimo cha umwagiliaji” alisema.

Aidha, mkulima huyo aliongeza: “Kilimo hiki cha mpunga kina hamasa kubwa kwetu, lakini changamoto tunazo kumbana nazo ni pamoja na upatikanaji wa elimu bora ya kilimo cha mpunga cha nchi kavu, kutokuwepo kwa wafadhili watakao saidia kutoa mbegu, upatikanaji wa mbolea bora itakayo saidia katika ukuaji na masoko kwaajili ya kuuzia mazao yao endapo kutakuwepo msaada wa kutatua changamoto hizo tuna imani kilimo kwetu kitakuwa ni fursa ya pekee.”

BUSAMBA WAFANIKISHA UJENZI WA CHOO CHA WATUMISHI NA MAKTABA

Mafundi wakiendelea na shughuli za ujenzi wa choo cha walimu katika shule ya msingi Busamba ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa matumizi ya mifuko 60 ya saruji iliyotolewa na Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo shuleni hapo. Kulia ni Maisha Tengeja, mwalimu wa shule ya msingi Busamba.

Na. Ramadhani Juma

SERIKALI ya kijiji cha Busamba wamefanikisha ujenzi wa choo cha walimu katika shule ya msingi Busamba iliyopo kata ya Nyegina, jimbo la Musoma vijijini.

Ujenzi huo unafuatia baada ya kijiji hicho kufanya maamuzi ya kujenga maktaba ya shule hiyo kwa kutumia mchango wa mifuko 60 ya saruji iliyotolewa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo na upo kwenye hatua nzuri.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwalimu wa taaluma wa shule ya msingi Busamba Anna Mweya kwa niaba ya mkuu wa shule hiyo alisema, mifuko 60 iliyotolewa na Mbunge ilifanya kazi ya ujenzi wa maktaba, maamuzi ambayo yalilenga kuboresha mazingira ya kutunzia vitabu pamoja na wanafunzi kujisomea.

Anna aliongeza kuwa, baada ya kukamilisha ujenzi huo, serikali ya kijiji iliamua kujenga choo cha walimu kwa kutumia matofali yaliyosalia ikiwa ni njia pekee ya kumaliza changamoto hiyo shuleni hapo.

Mwalimu Anna aliendelea kufafanua, maamuzi ya kujenga maktaba na choo cha walimu hakumaanishi kuwa shule ya Busamba haina upungufu wa vyumba vya madarasa, bali ni katika kuimarisha mazingira ya utoaji wa huduma ya elimu.

Alisema, kwa wastani shule ya Busamba ina jumla ya wanafunzi 1,025 na ina upungufu wa vyumba 18 na vilivyopo ni vyumba 10 tu, hivyo serikali ya kijiji hicho imekamilisha ujenzi wa chumba kimoja cha darasa na kimeshaezekwa.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Busamba Kadenge Maanya amethibitisha matumizi ya mifuko hiyo 60 ya saruji katika ujenzi wa maktaba na choo cha walimu ikiwa ni sehemu ya mahitaji makubwa ya shule yao kwa wakati huu.

Mwenyekiti huyo pia alisema, mbali na ujenzi wa maktaba na choo cha walimu, wananchi wa Busamba kwa kushirikiana na serikali yao wamekamilisha ujenzi wa chumba kimoja cha darasa.

MCHANGO WA MBUNGE WAFANIKISHA UEZEKAJI WA NYUMBA YA MWALIMU

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Bukumi (katikati) akiwa na mafundi wakati wa uezekaji wa nyumba ya mwalimu katika shule ya msingi Bukumi.

 

Na. Fedson Masawa

MCHANGO wa mabati 100 yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo katika shule ya msingi Bukumi, umefanikisha zoezi la uezekaji wa nyumba ya mwalimu mkuu katika shule hiyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Bukumi Nyaonge Maligo amemshukuru Prof Muhongo kwa mchango mkubwa alioutoa kijijini hapo kwa kuwa umewasaidia kupiga hatua nzuri ya maendeleo na wananchi wake kuwajibika kwa sehemu ndogo ya kukamilisha ujenzi huo.

“Kwa niaba ya wananchi wangu, namshukuru sana Prof. Muhongo kwa mchango huu, tumepiga hatua nzuri na wananchi wangu kuchangia sehemu ndogo, ni jambo la kushukuru” alishukuru mwenyekiti huyo.

Aidha, Mwenyekiti Maligo alisema pamoja na mchango wa mabati 100, Prof. Muhongo pia alitoa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo na chumba kimoja cha darasa ambacho pia kimekamilika na kuezekwa kwa mabati 54 kati ya hayo yalitolewa na mbunge.

Hata hivyo mwalimu wa shule ya msingi Bukumi Mabuba Makene alisema, kukamilika kwa nyumba hiyo ni hatua nzuri ya kupunguza tatizo la uhaba wa nyumba za watumishi shuleni hapo.

WANANCHI WA KIJIJI CHA CHITARE WAANZA UJENZI WA SHULE MPYA

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chitare wakishiriki katika shughuli za ujenzi wa shule mpya inayoendelea kujengwa katika kitongoji cha Mwikoko.

 Na. Mwandishi Wetu

WANANCHI wa kijiji cha Chitare kwa kushirikiana na serikali ya kijiji hicho wameanza ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kitongoji cha Mwikoko kilichopo kijijini hapo.

Hamasa hiyo inatokana na makubaliano baina ya wananchi wa Chitare na serikali yao kwa kuzingatia kigezo cha umbali wanaosafiri watoto kutoka vitongoji vya Kasia na Mwikoko hadi kitongoji cha Kumsima ilipo shule ya Msingi Chitare A na B.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti wa kijiji cha Chitare Zakayo Mbogora alisema, jiografia ya kijiji cha Chitare ni kubwa, lakini pamoja na kuwepo kwa shule mbili za Chitare A na B ambazo zimeungana pamoja, bado muundo huo hauwapunguzii umbali watoto wanaotokea vitongoji vya Kasia na Mwikoko, hivyo serikali ya kijiji na wananchi wamelazimika kujenga shule nyingine itakayokuwa karibu na vitongoji hivyo.

Mwenyekiti alisema, wameamua kuanza na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu, lakini malengo yao ni kufikisha idadi ya vyumba 10 vya madarasa pamoja na ofisi tano za walimu.

“Jiografia ya Chitare ni kubwa, tunazo shule mbili A na B, lakini shule hizi zipo pamoja. Sasa muundo huu bado unaleta shida kwani watoto wetu wanaendelea kusafiri umbali mrefu kutoka Kasia na Mwikoko hadi kitongoji cha Kumusima. Pia tumeamua kuanza na vyumba viwili na ofisi na tunalenga kufikisha vyumba kumi na ofisi tano” alisema mwenyekiti huyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa kijiji cha Chitare wamesema, wameamua kuchangia shughuli za ujenzi wa shule mpya na tayari wameanza kujenga, lakini bado wanahitaji mchango mkubwa kutoka kwa Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo na serikali kwa ujumla ili kufanikisha malengo yao na kuwaokoa watoto wanaoendelea kuumia na umbali kufuata elimu.

Kwa upande wake msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa, aliwashukuru wananchi wa kijiji cha Chitare na serikali yao kwa maamuzi mazuri waliyoyafikia na kuongeza kuwa, kama maamuzi hayo yangefanyika mapema basi leo kijiji cha Chitare wangekuwa wamefikia hatua nzuri kwani mpango huo aliuzungumza kwenye mikutano na vikao alivyowahi kufanya kijijini hapo.

Fedson alishauri serikali ya kijiji cha Chitare kukaa pamoja na kamati za shule ya Chitare A na B na kukubaliana ili michango yote inayoletwa kijijini hapo kwa ajili ya ujenzi, ielekezwe kwenye shule hiyo mpya kwani madarasa 14 ambayo yatabakia shuleni hapo yatakuwa yamekidhi uhitaji.

Alisema, bado yapo matofali yaliyotokana na saruji aliyotoa Prof. Muhongo na kama wakikubaliana matofali hayo yajenge shule mpya huku akisisitiza kuwa Mbunge yupo pamoja nao katika ujenzi huo wa shule mpya na shule zote za Jimbo lake.

“Ndugu zangu niwashukuru kwa jitihada mlizozifikia, ni maamuzi mazuri na kama mngeyazingatia toka mwanzo basi leo tungekuwa mbali. Mbunge yupo pamoja nanyi katika ujenzi wa shule hii mpya, ninachowashauri serikali ya Chitare ni kwenda kukaa na kamati ya Chitare A na B ili nguvu kubwa sasa tuielekeze katika kujenga shule hii mpya” alisema na kushauri msaidizi huyo.

KIJIJI CHA SARAGANA WAONGEZA CHANZO KIPYA CHA MAPATO

Baadhi ya akinamama wa kijiji cha Saragana waliojitolea kushiriki kwenye zoezi la ujenzi wa choo cha eneo la mnada wakiwa na ndoo za kuchotea mchanga kwa ajili ya ujenzi huo.

Na. Hamisa Gamba

WANANCHI wa kijiji cha Saragana wameanza rasmi shughuli za ujenzi wa choo katika eneo la mnada ulioko kijijini hapo.

Lengo la kujengwa kwa choo hicho mbali na kuzuia magonjwa ya mlipuko kutokana na eneo hilo kukutanisha idadi kubwa ya watu, pia una lengo la kuingiza mapato kwa serikali ya kijiji.

Kabla ya ujenzi huo, eneo hilo halikuwa na huduma hiyo baada ya choo cha awali ukuta wake kuanguka na paa kuezuliwa na upepo mkali.

Uamuzi wa kuanza ujenzi huo ulichukuliwa kwenye kikao cha wananchi hao na serikali ya kijiji ambapo walisomewa mapato na matumizi na ikabainika kijiji hicho hakina vyanzo vya kutosha vya mapato zaidi ya malipo ya minara ya simu na uchinjaji wa ng’ombe.

Kwenye kikao hicho Mwenyekiti wa kijiji cha Saragana, Leni Manyama baada ya mtendaji wa kijiji Silivey Adam kusoma taarifa ya mapato na matumizi, aliwaomba wananchi kuchangia kuchangia nguvu kazi zao ili kukamilisha ujenzi huo ambao utasaidia kuongeza mapato ya kijiji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri Frola Yongolo aliweka msisitizo kwenye kauli ya mwenyekiti huyo na kuwataka wananchi kushiriki kwenye ujenzi huo ambao iwapo utakamilika utasaidia kuongeza mapato ya kijiji na hata kusaidia kupambana na magonjwa.

Hata hivyo, wananchi hao walipokea suala hilo na kuanza mara moja utekelezaji, ingawa waliomba Halmashauri iwasaidie maji kutokana na ukame wakati huu wa kiangazi.

MILIONI 236 ZATOLEWA KUGHARAMIA UJENZI SEKONDARI YA KASOMA

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Anney akishiriki kuchimba msingi wa mabweni ya sekondari ya Kasoma ambao ujenzi wake umegharamiwa na Halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini.

Verdiana Mgoma

HALMASHAURI ya wilaya ya Musoma vijijini kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Nyamrandirira wamejitolea katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo shule ya sekondari Kasoma.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kufadhili mradi huo unaogharimu shilingi milioni 236 zitazotumika kupanua shule hiyo.

Mkuu wa Shule ya sekondari Kasoma Nelson Makaro alisema, kwa muda mrefu shule yao inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa ambapo wana wanafunzi 890 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, lakini wana vyumba vya madarasa 13 na wana upungufu wa vyumba vinane.

Makaro alisema, kwa upande wa mabweni upungufu ni mkubwa zaidi maana yapo mabweni mawili yanayotumika kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita tu, hivyo  wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha nne wanaishi majumbani mwao ambako ni mbali na shule, hivyo kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kupunguza changamoto hizo.

“Pia tunakabiliwa na changamoto nyingine ya uhaba wa walimu wa sayansi na nyumba za walimu na chakula kwa wanafunzi” alisema mwalimu Nelson Makaro.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyamrandirira Ruteli Maregesi alisema, wananchi wa kata yake wamehamasika katika ujenzi huo na walianza ufyatuaji wa matofali na nasasa wapo kwenye hatua ya uchimbaji wa msingi.

“Tuliweka majadiliano na wananchi wangu tulipogundua kuna baadhi ya changamoto tunaweza kuanza kutatua ili kunyanyua kiwango cha elimu. Mabweni kwetu ni ya muhimu sana maana kuwepo kwa mabweni tutaondoa changamoto ya watoto kutoka umbali mrefu na kutumia muda mwingi kufika shule, hupunguza majukumu ambayo wakitoka shule mara nyingi hufanya nyumbani na kukosa muda wa kujisomea, lakini wakiwa shule watakuwa huru zaidi” alisema diwani huyo.

Aliongeza:”tutawakinga watoto wa kike na vishawishi wanavyokutana navyo na kukatisha masomo (mimba), itasaidia pia kwa matumizi ya lugha hasa ya kiingereza maana mazingira wanafunzi wanapotoka mara nyingi hutumia lugha ya asili”

Naye Mkuu wa wilaya Dkt. Vicent Anney aliwashukuru wananchi hao na viongozi kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya na kuwataka kuongeza bidii ili kukamilisha mradi huo mapema huku akitoa onyo kwa wanaogoma kushikiri kufanya shughuli za maendeleo kwamba, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hata hivyo, Dkt. Vicent Anney alisisitiza ushirikiano kati ya wadau wa elimu yaani walimu, wazazi, wanafunzi na viongozi wa kisiasa kuwekeza zaidi kwenye elimu ili kuinua sekta ya elimu na kusisisitiza: ‘ukimsomesha mtoto umesomesha jamii.’

BUKIMA, BUTATA NA KASTAM WAHAMASISHWA KUSAKA MAENDELEO

Na. Mwandishi Wetu

ZIARA ya kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo imefanyika katika vijiji vitatu vya kata ya Bukima ambavyo ni Bukima, Butata na Kastam ambapo wananchi wametakiwa kujitokeza kuunga mkono jitihada zinazofanywa na mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo.

Viongozi mbalimbali akiwemo Diwani wa kata ya Bukima, viongozi wa serikali kutoka kata ya Bukima na vijiji vyote vitatu vya kata hiyo pamoja na wataalamu mbalimbali wa na msaidizi wa mbunge walishiriki ziara hiyo.

Akizungumza kwenye moja ya mikutano ilifanywa wakati wa ziara hiyo katika kijiji cha Bukima, msaidizi wa Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Fedson Masawa alisema kwa kipindi kifupi tangu alipochaguliwa, mbunge amechangia saruji mifuko 60, madawati 41 katika shule ya msingi majita A na madawati 95 katika shule ya msingi majita B.

Prof. Muhongo pia ametoa msaada wa mbegu za alizeti, mtama na mbegu za mihogo kwa wakulima mbalimbali wa kijiji cha Bukima sambamba na kushirikiana kwa ukaribu na wananchi wake katika matatizo mbalimbali kama majanga ya asili yakiwemo kimbunga na misiba.

Msaidizi huyo alisema, katika sekta ya afya Prof. Muhongo ametoa magari madogo manne katika zahanati nne za jimbo la Musoma vijijini ambazo ni Kurugee, Nyasulula, Mugango na Masinono magari ambayo yanafanya kazi jimbo zima kutokana na uhitaji wake.

Mbali na magari hayo manne, Prof. Muhongo ametoa gari moja kubwa ambalo lipo katika kituo cha afya cha Murangi huku akiahidi kutafuta gari jingine kubwa kwa ajili ya kubebea wagonjwa.

Akizungumzia suala la maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, afya na kilimo Fedson alisema ili mbunge aweze kufanikisha kuondoa changamoto zinazozikabili sekta hizo, wananchi wanapaswa kumuunga mkono kwa hali na mali katika utekelezaji huo kwa wakati muafaka.

“Ndugu wananchi wa kijiji cha Bukima, Mbunge wetu anahitaji ushirikiano mkubwa sana kutoka kwenu wananchi na viongozi, michango yenu, nguvu zenu na moyo wenu wa kujitolea ndio utakaomfanya mbunge kumaliza changamoto zinazowakabili” alisema.

Aidha, aliwataka wananchi wa kijiji cha Bukima kujituma katika kuchangia ujenzi wa wodi ya akina mama na watoto ili kuharakisha kasi ya ujenzi wa zahanati ya Bukima kuwa kituo cha Afya kutokana na wingi wa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika zahanati hiyo.

Katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, aliwashukuru viongozi na wananchi wa kijiji cha Bukima kwa hatua nzuri ambayo wamefikia ya kujenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya mwalimu katika shule ya msingi Majita B.

Kwa upande wa sekta ya kilimo, amewasisitiza wananchi kujituma katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kujikwamua kiuchumi huku akiwataka kuwa tayari kwa mtambo wa kusindika alizeti ambao unafanyiwa utaratibu wa kufungwa katika kata ya Suguti.

Kaimu Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Bukima Benarld Mirobo akizungumza kwa niaba ya serikali ya kijiji hicho alisema, wananchi kwa sasa wapo pamoja na watafanya kila linalowezekana kwa hali na mali kuanza mara moja ujenzi wa wodi ya akina mama na watoto kama walivyoanza katika ujenzi wa vyumba vya madarasa.

NYUMBA ZA WAGANGA ZAZINDULIWA KITUO CHA AFYA MURANGI

Mkuu wa WIlaya ya Musoma vijijini Dkt. Vincent Naano Anney (wa kwanza kulia), Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida na Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo wakifungua kitambaa kwenye jiwe la msingi kuhashiria uzinduzi rasmi wa nyumba za waganga wa kituo cha afya cha Murangi ambazo zimejengwa kwa ufadhili wa serikali ya Japan kwa gharama ya milioni 170.

Na. Fedson Masawa

NYUMBA kwa ajili ya makazi ya waganga wa kituo cha afya cha Murangi zimezinduliwa rasmi leo kijijini hapo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na kijiji hicho.

Uzinduzi huo ulioongozwa na Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, ulihudhuriwa pia na Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma vijijini Charles Magoma, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, madiwani na viongozi mbalimbali wa kijiji hicho.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Prof. Sospeter Muhongo aliwashukuru serikali ya Japan kwa kufadhili mradi huo mkubwa wenye lengo la kuboresha huduma za afya kituoni hapo uliogharimu milioni 170 huku akitumia hadhara hiyo kusisitiza kuendelea kwa kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Wananchi mbalimbali waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, walishukuru wote waliofanikisha ujenzi huo ambao walisema utawasaidia kupata huduma ya uhakika na haraka wakati wowote tofauti na awali ambapo walipata wakati mgumu kutokana na waganga kuishi mbali na eneo hilo na hivyo kukosa huduma ya haraka inapotokea dharura.

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo akihutubia wananchi wake (hawapo pichani) waliohudhuria kwenye sherehe za uzinduzi wa nyumba za waganga wa kituo cha afya cha Murangi huku viongozi wengine wakimsikiliza kwa makini.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma vijijini Charles Magoma akimkabidhi zawadi Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida wakati wa sherehe za uzinduzi wa nyumba za waganga wa kituo cha afya cha Murangi huku zoezi hilo likishushudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Murangi waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa nyumba za waganga wa kituo cha afya wakishangilia na wengine wakifuatilia kwa makini hotuba za viongozi mbalimbali waliopata nafasi ya kuzungumza kwenye sherehe hizo ambazo zilifana.

MWENGE WA UHURU WAWASILI MUSOMA VIJIJINI, MIRADI YAZINDULIWA

Pichani ni mwenge wa uhuru baada ya kuwasili kwenye viwanja vya kijiji cha Chirorwe kwa ajili ya uzinduzi na kuweka jiwe la msingi wa zahanati ya kijiji hicho.

Na. Verdiana Mgoma

MSAFARA wa mbio za mwenge wa Uhuru umewasili kwenye Jimbo la Musoma vijijini na kufanikiwa kukimbizwa kwenye baadhi ya vijiji vya jimbo hilo.

Mbio za mwenge kwa mwaka huu zina kauli mbiu ya “shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu” ambapo ndani ya jimbo hilo miradi ya maendeleo na huduma za kijamii zimezinduliwa na nyingi zitaendelea kuzinduliwa kwa kipindi ambacho mwenge huo utakuwepo.

Akizungumza katika uzinduzi wa zahanati ya kijiji cha Chirorwe, kiongozi wa mbio za mwenge mwaka huu Amour Hamad Amour amewataka watanzania kuweka nguvu katika kujenga taifa la viwanda ili kutimiza azma ya serikali ya awamu ya tano ambayo imedhamiria kuinua uchumi kwa kujenga viwanda.

Amour alisema, wananchi wanapaswa kujikita katika kilimo ili kuwepo kwa ajira ya kukuza uchumi wa viwanda na kusisitiza kuwajibika na kuepukana na uvivu na kufanya kazi kwa mazoea.

“Kila mmoja wetu anapaswa kuwajibika katika ujenzi wa taifa na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kurudisha maendeleo ya taifa nyuma” alisisitiza Amour na kuongeza kuwa, hayo hayatofanikiwa ikiwa watanzania watasumbuliwa na maradhi na kuwataka kuongeza mapambano dhidi ya malaria kwa kutumia vyandarua kujikinga na mbu waenezao ugonjwa huo.

“Pia tujiepushe na rushwa, tujikinge na ugonjwa wa Ukimwi na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya hasa kwa vijana ambao hawajatumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya, wasijiingize kwenye matumizi ya dawa hizo” alisema Amour Hamad Amour.

Hata hivyo, Kiongozi huyo wa mbio za mwenge alielezea miradi mbalimbali iliyotekelezwa kwa kushirikiana halmashauri pamoja wahisani ambayo itazinduliwa wakati wa mbio hizo.

Moja ya miradi hiyo ni uzinduzi wa kituo cha afya cha Murangi ambao umefadhiliwa na Japan ikiwa ni ishara ya urafiki kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Ujenzi wa zahanati hiyo ulihusisha nyumba mbili za wafanyakazi wa kituo hicho, ujenzi wa miundo mbinu ya hospitali ambayo ni choo cha wagonjwa, sehemu ya kuhifadhia takataka na sehemu ya kutupa takataka.

MBUNGE WA MUSOMA VIJIJINI AFANIKISHA NDOTO YA MWANANCHI WA KIRIBA

Johnson Nyeura akiwa nje ya nyumba yake ambayo ujenzi wake umefikia kwenye hatua nzuri.

Na. Ramadhan Juma

BAADA ya kuishi kwenye ofisi ya kijiji cha Kiriba kwa muda mrefu akiwa na familia yake kwa kukosa makazi, mlemavu wa ngozi Johnson Nyeura amehamia kwenye nyumba yake.

Nyeura amefanikiwa kukamilisha nyumba yake kwa msaada wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo ambaye alijitolea kumsaidia baada ya kumkuta akiishi kwenye ofisi hiyo ya kijiji.

Kwasasa Nyeura anaishi kwenye nyumba yake ambayo kwa kiwango kikubwa imekamilika na tayari imefungwa hanamu, milango na madirisha na kazi iliyobakia ni kupigwa lipu na sakafu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi akiwa nyumbani kwake, Nyeura alimshukuru Prof. Muhongo kwa msaada aliompatia na kufanikisha ndoto yake ya kuishi kwenye nyumba yake.

Hata hivyo, Johnson Nyeura licha ya furaha aliyonayo ya kupata makazi hayo, aliomba msaada wa kujengewa choo kwani hivisasa yeye na familia yake wanalazimika kupata huduma hiyo kwa majirani.

KIKAO CHA KWANZA CHA BARAZA LA MADIWANI CHAFANYIKA MURANGI

Wananchi waliohudhuria kikao cha madiwani (full council) kilichofanyika kwenye viwanja vya Murangi.

Na. Verdiana Mgoma

MADIWANI wa Musoma Vijijini wamekubaliana kuhamisha rasmi shughuli zake kwenye Makao Makuu ya Halmashauri hiyo yaliyopo kwenye kijiji cha Murangi.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Charles Magoma alisema, wameamua kuhamia rasmi nyumbani ambako ni Murangi na kuanzia sasa vikao vyote vitafanyika huko.

Magoma alisema, watahakikisha wanatafuta ofisi hata kama ni mbovu, lakini wataanza hivyo hivyo: “maana mwanzo huwa mgumu inabidi tukubaliane na kasi ya awamu ya tano”

Mkurungenzi wa Halmashauri ya Musoma Vijijini Flora Yongolo alisema, hilo ni tukio la kihistoria kwa Halmashauri hiyo kuchukua maamuzi ya kuhamia Murangi ambako ndipo kwenye makazi yao.

“Kwa historia kikao hiki kitafanyika wazi kwa wananchi ili wajue nia na madhumuni yetu ni kuhamia rasmi Murangi. Lengo letu siyo kuhamia Murangi tu, tunahitaji pia kujenga halmashauri yetu na kujitegemea kwa kuwa tumedhamiria kufanya hili, tutahitaji kupata msaada wa pesa kutoka serikalini tayari kwa kuanza ujenzi” alisema Yongolo.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Nyamrandirira, Ruteli Maregesi amewakaribisha madiwani hao kwenye kijiji cha Chumwi endapo kutakuwa na shida ya sehemu ya kufanyia vikao.

Diwani huyo ameshukuru kwa uamuzi huo waliochukua madiwani wenzake na kuungana kwa pamoja kufanikisha zoezi walilopigania kwa muda mrefu.

“Imefika tamati, tumefanikisha kurudi Murangi hili ni jambo la kheri kwetu na kwa wananchi wa jimbo la Musoma vijijini” alisema diwani Maregesi.

Naye Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Anney alisema, anaunga mkono maamuzi yaliyochukuliwa na Halmashauri ya Musoma vijijini ya kuhamishia makazi yake rasmi Murangi, jambo ambalo linaonesha nia ya kukubaliana na mabadiliko ya awamu tano.

“Hata Rais aliposema anahamia Dodoma watu hawakuamini, lakini na sisi pia tumejifunza kutoka kwa mkuu wetu kama ameweza kuhamia Dodoma, kwetu inakuwaje ngumu kuhamia Murangi?” alihoji Mkuu wa wilaya.

Mkuu wa Wilaya Dkt. Vicent Anney alisema, kwa kuonesha wamedhamiria kwa maamuzi hayo, ameahidi kutoa taarifa kwa ngazi za juu ili waweze kupata pesa kwa ajili ya ujenzi wa Halmashauri hiyo.

Hata hivyo, alisisitiza maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, hali ya chakula na matumizi ya fedha kwa ajili ya kuimarisha vikundi vya akina mama na watoto.

WAZAZI, BODI ZA SHULE YA NYANJA NA BULINGA WAKUBALIANA KUBORESHA ELIMU

Wazazi waliofika kwenye kikao maalum cha kujadili namna ya kuinua kiwango cha elimu kwa shule ya Nyanja na Bulinga ambapo wamekubaliana kuchangia chakula kwa ajili ya kuwapikia watoto wao wanapokuwa shuleni.

Na Fedson Masawa

BODI ya shule ya sekondari Nyanja na Bulinga zimekubaliana na wazazi kuweka mikakati mipya ili kuinua kiwango cha elimu ya sekondari kwa shule hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa hivi karibuni kwenye kikao cha bodi za shule hizo, kilichofanyika katika shule ya Sekondari Bulinga.

Kikao hicho cha pili, kinafuatia kikao kingine kilichofanyika katika shule ya sekondari Nyanja iliyopo kata ya Bwasi, ambapo wazazi wote wa kata hizo wamekubaliana kuanzisha utaratibu maalum wa kuwaandalia watoto wao chakula cha mchana ili wanafunzi hao watumie muda wa kutosha katika masomo.

Wazazi hao wamekubaliana kuchangia Mahindi kilo 12, Maharage kilo 6, mafuta ya kupikia pamoja na chumvi, mchango ambao wazazi wamekubaliana kuutoa kwa awamu pamoja na vyombo vya kupikia na kulia chakula.

Sambamba na michango ya chakula, wazazi hao pia wamekubaliana kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maabara kwa ajili ya kuboresha huduma ya masomo ya sayansi kwa watoto pamoja na kujenga jengo la utawala katika shule ya sekondari Bulinga.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hizo Abel Bogohe alisema, kamati ya bodi iliyopo kwa sasa ni kamati inayosimamia shule mbili;shule ya sekondari Nyanja iliyopo kata ya Bwasi na shule ya sekondari Bulinga iliyopo kata ya Bulinga ambayo kwa sasa inahesabika kama tawi la sekondari ya Nyanja.

Bogohe alisema, ni majukumu makubwa kwani kamati inayo kazi ya kusimamia shule mbili na hii yote ni kwa sababu shule ya sekondari Bulinga bado haijapata usajili kutokana na mapungufu ya jengo la utawala.

“Pamoja na majukumu yote hayo, ndugu wazazi hapa Prof. Muhongo haepukiki na ni lazima tumuombe atufikirie kwenye ukamilishaji wa maabara, kwani sekondari ya Nyanja tayari jengo la maabara zote tatu limekamilika na kuezekwa kwa nguvu za wananchi kilichobakia ni sakafu na miundombinu ya ndani. Bulinga bado jengo la maabara linaendelea kujengwa pia kwa nguvu za wananchi, tunaomba Mbunge atusaidie kuyafanikisha haya” alisema  Bogohe.

Hata hivyo, Bogohe ameeleza pamoja na changamoto zote hizo wazazi, kamati na walimu wa shule hizo wanalo jukumu la kushirikiana pamoja ili kuinua taaluma ya wanafunzi wanaosoma katika shule hizo kwa kubuni, kupanga na kujiwekea utaratibu maalumu wa kuinua kiwango cha taaluma kwa watoto wao.

“Tunazo changamoto nyingi, lakini wazazi lazima mshiriki kikamilifu ili kuinua taaluma ya wanafunzi hawa. Tunapaswa sasa kuwatengenezea utaratibu wa kutumia muda mrefu katika masomo na wazazi kutumia muda mwingi kufanya maendeleo ya miundo mbinu ya watoto kujifunzia” alisema Bogohe.

Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo na Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Nyanja, Charles Ndebele amewaomba wazazi kuwaunga mkono walimu wao kwani walimu peke yao hawawezi kuleta mabadiliko katika elimu bila ushirikiano kutoka kwa wazazi hasa kuboresha miundo mbinu ya elimu kwa kuwa na maandalizi bora ya mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kutoa muda wa kutosha na uhuru wa mwanafunzi kujisomea.

Naye Mtendaji wa Kata ya Bulinga Gudrack Mazige ameieleza bodi na kumshukuru Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa jitihada zake za kupambana na changamoto za elimu na kusema, pamoja na kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa lakini bado ameisaidia kata ya Bulinga mifuko 70 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika sekondari ya Bulinga.

Mazige amewataka wazazi kuwa pamoja na kuwa na mwamko mzuri katika elimu, wanapaswa kujitahidi kumuunga mkono Mbunge wa jimbo lao kwa ajili ya kufanikisha mipango yao mizuri.

“Ndugu wananchi na viongozi wa bodi, sambamba na mapambano na kuinua kiwango cha elimu, shule ya sekondari Bulinga imepokea saruji 70 kutoka kwa Prof. Muhongo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala ili shule yetu iweze kusajiliwa. Tumshukuru sana Prof Muhongo lakini sasa tunao wajibu wa kumuunga mkono kwa kuwajibika kikamilifu hata kwa kuchangia nguvu kazi” alieleza Gudrack.

MASHINDANO YA NYAMBONO NDONDO CUP YATIMUA VUMBI

Wachezaji wa moja ya timu zinazoshiriki michuano ya Nyambono Ndondo Cup timu ya Muhoji FC wakiwa kwenye picha ya pamoja.

MASHINDANO ya mpira wa miguu yanayohusisha timu 15 kutoka vijiji vya Nyambono, Bugoji na Bugwema yameanza rasmi kwenye kijiji cha Nyambono.

Mratibu wa mashindano hayo Gerlad Mbogora ambaye ni mlezi wa Urafiki FC alisema, ameamua kuanzisha mashindano hayo yanayojulikana kama Nyambono Ndondo Cup ili kuleta hamasa kwa vijana, kujitengenezea ajira, kukuza urafiki na zaidi kuwa na timu moja imara itakayoshiriki katika michuano ya mashindano ya mpira wa mguu sehemu mbalimbali jimboni na nje ya jimbo.

Mbogora alisema, pamoja na kuendesha mashindano hayo kuna changamoto ya upungufu wa mipira, hivyo mashindano hayo yanategemea mpira mmoja tu.

Mratibu huyo alimuomba Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo na wadau wengine wamuunge mkono kwa kuwasaidia mipira miwili kwa ajili ya mashindano hayo.

KIJIJI CHA BUKIMA WATEKELEZA MAAGIZO YA WARD C, WAANZA UJENZI

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa shule ya msingi Majita B.

Na. Fedson Masawa

VIONGOZI wa serikali ya kijiji cha Bukima kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho wameanza kutekeleza maagizo ya Ward C ya kufanikisha mahitaji ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu hasa ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Hatua hiyo ya utekelezaji imefikiwa siku chache baada ya kikao cha Ward C Bukima kuagiza viongozi wa serikali ya kijiji cha Bukima kuanza haraka ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Majita “B”.

Kijiji cha Bukima kwa sasa kimeanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu ukiwa ni mpango wa ujenzi wa vyumba saba vya madarasa katika shule mpya ya Majita “B”.

Ujenzi huo wa vyumba vya madarasa unafadhiliwa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ambaye anachangia saruji ili kufanikisha ujenzi huo.

Kwa awamu ya kwanza, Mbunge huyo amechangia mifuko 60 ya saruji ambayo imefyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Bukima Murungu Murungu amefafanua kuwa, baada ya serikali kukubaliana kuihamisha shule B, zoezi la ujenzi limeanza kwa kasi na wanatarajia kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo viwili ndani ya mwezi huu wa Septemba au mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

Murungu amekiri kwamba serikali yake ilifanya makosa mwanzoni, lakini hatarajii makosa hayo yajirudie tena kwani ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa siyo kazi rahisi na bila kuendana na kasi ya Mbunge wao yeye na serikali yake wanaweza kuchukua miaka mingi bila kufanikisha mahitaji hayo.

“Serikali yangu imefanya makosa hapo nyuma, lakini kamwe sitarajii wala sitavumilia makosa hayo yajirudie. Tuna mzigo mzito wa ujenzi wa vyumba 7, lakini bila kuungana na Mbunge wetu na kasi yake mimi na serikali yangu hatutaweza kwa kipindi hiki kifupi” amekiri na kueleza Murungu.

Akizungumza kwa njia ya simu Diwani wa kata ya Bukima January Simula alisema, jitihada za wananchi na viongozi wa Bukima kwa sasa zimeonekana, lakini kuna saruji mifuko 60 iliyotolewa na Prof. Muhongo imebakia ambayo viongozi wa Butata wanatakiwa wakamilishe upigaji lipu vyumba vyao vya madarasa walivyovijenga.

“Kama watashindwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku 10, mifuko hiyo tutaihamisha na kuwapelekea Bukima ili iwaongezee nguvu” alisema Simula.

Naye msimamizi wa shughuli za ujenzi huo Mnubi Mahindi ambaye pia ni mjumbe wa serikali ya kijiji cha Bukima alisema, serikali yao tayari imeweka pembeni tofauti zao kwa sasa wanafanya kazi kwa pamoja kwani wanacho kibarua kigumu cha ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa.

“Hatuna tofauti yoyote kwa sasa, kazi tuliyo nayo ni ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa, hiki ni kibarua kigumu ni muhimu sasa kuungana na Mbunge ili tufanikishe kutatua changamoto za elimu katika shule zetu” alisema Mahindi.

RUSOLI WAKARIBISHA OFISI YA MBUNGE KUKAGUA MASHAMBA YAO

Mbunge wa viti maalum Agness Chinuno (aliyesimama) akizungumza na baadhi ya wakulima wa bustani baada ya kuvuna nyanya tayari kwenda sokoni.

Na. Mwandishi Wetu

VIKUNDI vya vijana na akina mama Musoma vijijini vimekaribisha uongozi wa ofisi ya mbunge kufika katika mashamba yao yaliyoko katika kata ya Rusoli kwa ajili ya kujiridhisha na hatua iliyofikiwa na vikundi hivyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Diwani wa kata ya Rusoli Boazi Nyeula alisema, kata ya Rusoli peke yake ina mashamba makubwa ya kutosha huku kukiwa na vikundi vingi vinavyojishughulisha na kilimo cha bustani za mbogamboga na matunda, lakini wanashindwa kupanua mashamba hayo kutokana na upungufu wa vitendea kazi.

Boazi alisema, pamoja na changamoto hizo, kati ya vikundi hivyo vinavyojishughulisha na kilimo hicho ni kikundi kimoja peke yake kwenye kata yake kilichojitahidi kwa sasa kununua mashine ya kumwagilia na mipira, vikundi vingine vilivyobakia vinatumia ndoo kumwagilia bustani zao.

Diwani wa viti maalum Agness Chinuno aliyeongozana na Msaidizi wa Mbunge katika mashamba hayo ya bustani, alisema kata ya Rusoli ni moja ya kata zilizo na mashamba ya kutosha kulima bustani na hilo linadhihirika kutokana na hali halisi iliyopo, ambapo vipo vikundi vitatu vimeanza kuandaa mashamba yenye ukubwa wa hekari sita kwa ajili ya kilimo cha matikiti maji, lakini bado yapo mashamba mengine ya kutosha.

Mbunge huyo alisema, mwanzoni wananchi wa kata hiyo hawakuwa na hamasa yoyote kuhusu kilimo cha bustani, lakini kwa sasa akina mama wengi na vijana wamekimbilia kwenye vikundi na ndio maana wamefikia hatua baadhi waliotangulia kununua mashine ya kumwagilia.

Mmoja wa vijana wanaojishughulisha na kilimo cha bustani Malofu Mjinja alisema, vijana wanawaza kupanua zaidi maeneo ya kilimo chao na tayari kazi imeanza katika mashamba yaliyo kandokando mwa ziwa, lakini changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa zana za kuwarahisishia kazi ikiwemo mashine za kumwagilia, na kuahidi iwapo watapata watahakikisha hakuna njaa katika kata ya Rusoli na maeneo ya jirani.

“Tunakushukuru sana ndugu yetu maana umesikia wito wetu na kama tumekuona wewe basi tunajua tumefikiwa na Prof. Sospeter Muhongo ambaye ni Mbunge wetu. Kilio chetu kikubwa kwako ni kwamba tuna malengo ya kujilisha wenyewe Musoma Vijijini kwa maana maeneo makubwa tunayo, nguvu tunazo na tunaomba Mbunge na serikali watusaidie vitendea kazi na mashine ili kurahisisha kazi” alishukuru na kuomba Mjinja.

Hata hivyo, Masami Lucas ambaye ni moja kati ya wanavikundi wa kata ya Rusoli alisema, kikundi chao kwa sasa kipo katika mavuno ya nyanya na wanamshukuru mwenyezi Mungu kwani mavuno yao yametoka vizuri na sasa wanaelekea kuanza msimu mwingine.

Masami aliomba Mbunge wao kuwawezesha katika vitendea kazi na mbegu bora kama alivyofanya katika vikundi 15 vya jimbo la Musoma vijijini ili waweke nguvu hizo pamoja wataweza kulilisha jimbo.

“Prof. Muhongo ni Mbunge wa watu, tunaamini kama akijitahidi kutuwezesha kama alivyofanya kwa vikundi 15, basi tukiunganisha nguvu zetu kama wanavikundi jimbo zima na maeneo tuliyo nayo yenye maji ya kutosha, Musoma vijijini hatutazungumzia ukosefu wa chakula” alisema Lucas.

Kwa upande wake Msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa, aliwapa pole na kuwapongeza vijana na akina mama hao kwa mipango yao na malengo yao mazuri waliyo nayo na kuwahasa waendelee na jitihada hizo huku wakisubiri taratibu nyingine za vifaa zikifanyika.

“Ndugu zangu wana Rusoli, poleni na hongereni sana kwa mipango na malengo mazuri ama kweli mmeona mbali, kweli tukiamua tutajilisha wana Musoma vijijini. Jimbo letu lina vikundi vingi na kusema ukweli si rahisi Mbunge kutusaidia kwa wakati mmoja na mkilinganisha na miradi anayoendelea kuitekeleza kwenye sekta ya elimu hasa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi Jimboni” alisema Masawa.

Msaidizi huyo wa mbunge aliongeza: “Kutokana na wingi wa vikundi vilivyopo Jimboni, kitakachowezekana basi Mbunge atakifanyia kazi na taarifa ya maombi yenu nitaifikisha. Lakini pia ikitokea mmesaidiwa vifaa hivyo, basi nanyi mjitume zaidi kuhakikisha vifaa vinavyotolewa na Mbunge vina uwezo wa kufanyiwa kazi na kunufaisha walioko ndani na nje ya vikundi hasa matokeo ya mwisho wa shughuli zenu.”

NGUVU KAZI WAKABIDHIWA MASHINE YA UMWAGILIAJI

Kikundi cha nguvu kazi kutoka kijiji cha Nyabaengere wakikabidhiwa mashine ya umwagiliaji na diwani wa kata ya Musanja Elias Ndaro (mwenye fulana ya kijani na njano) na Afisa kilimo kata Majura mfungo (wa kwanza kulia) Masatu Manyama, kwaajili ya kuongeza ufanisi katika kilimo chao na kuacha kutegemea mvua ambazo hazina uhakika.

Na. Verdiana Mgoma

UONGOZI wa kikundi cha Nguvu Kazi kilichopo kijiji cha Nyabaengere kata ya Musanja, umekabidhiwa mashine ya umwagiliaji kwaajili ya kuongeza tija ya kilimo chao.

Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye shamba la kikundi hicho na kuongozwa na diwani wa kata ya Musanja Elias Ndaro, Afisa Kilimo wa kijiji cha Nyabaengere Majura Mfungo na baadhi ya wanachama wa kikundi hicho akiwemo Kiongozi wao Masatu Manyama.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Majura Mfungo alisema, watu wengi wanashindwa kuanza kilimo cha umwagiliaji kwa kukosa mtaji wa kununua vifaa na hata ambao wanaendelea na kilimo hicho kwa kutumia ndoo, hawapati mavuno bora.

“Hizi ni baadhi ya changamoto zinazotokea katika jamii zetu hasa kwenye upande wa kilimo cha umwagiliaji, sisi viongozi tumeamua kuunga mkono sera ya kuinua kilimo hicho cha umwagiliaji na kuna mambo tunayozingatia kwenye uhamasishaji ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi kwenye kilimo hiki” alisema Mfungo.

Afisa Kilimo huyo aliongeza: “pia tunahamasisha matumizi bora ya maji katika kilimo, maendeleo yatakayoonekana kwenye kilimo cha umwagiliaji kiuchumi, kijamii na kimazingira na zaidi kilimo hicho cha umwagiliaji kuwa endelevu”

Kwa upande wake diwani Elias Ndaro alifafanua kuwa, mashine hiyo ni mwendelezo wa matumizi sahihi ya fedha za mfuko wa jimbo ambapo mwaka jana Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo alizindua mpango huo kwa kukabidhi mashine za umwagiliaji kwa vikundi 15.

“Maamuzi tuliyofikia ni kwamba, kwenye kata yetu kila baada ya mwaka na nusu mashine ya umwagiliaji inahamishiwa kijiji kingine kwa malengo kuwa kata nzima wanufaike na mashine hiyo” alisema diwani Ndaro.

Diwani Ndaro alisema, ili kupata maendeleo na fursa mbalimbali vikundi vilivyopo ndani ya kata yake vinapaswa kujisajili na kuandaa katiba na kufungua akaunti benki ambayo itawasaidia kuhifadhi fedha zao.

“Tunamshukuru sana mbunge wetu kwa msaada huu mpaka sasa vijana wengi wamejikita zaidi katika kilimo” alisema diwani huyo.

Kwa upande wake kiongozi wa kikundi cha Nguvu Kazi Masatu Manyama aliwashukuru viongozi mbalimbali wanaowaunga mkono katika shughuli zao za kilimo hali ambayo inawafanya wazidi kuongeza juhudi.

Manyama alisema, viongozi wao wamekuwa msaada mkubwa katika kukabili changamoto wanazokutana nazo hasa kwa upande wa kilimo, lakini zinatatuliwa na kuwafanya wasonge mbele zaidi.

Kiongozi huyo alisema, awali kabla ya kukabidhiwa mashine hiyo, walikuwa wanatumia mashine ya kukanyaga kwa mguu na wakati mwingine walikuwa wanamwagilia kwa kutumia mikono, lakini sasa watakuwa wakulima bora baada ya kupata mashine hiyo.

SERIKALI YA KIJIJI CHA BUKUMI YAKUBALIANA KUCHANGIA MFUKO WA MAENDELEO

Mtendaji wa kijiji cha Bukumi Alfred Onyango akisoma ajenda za kikao cha kujadili maendeleo ya kijiji hicho, kulia kwake (mwenye kofia) ni Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Bukumi Nyaonge Masatu na anayefuatia ni Mtendaji wa Kata ya Bukumi Leftinant Mkama. 

Na. Fedson Masawa

SERIKALI ya kijiji cha Bukumi imekubaliana kuchangia fedha kwa ajili ya mfuko wa maendeleo kwa shule za msingi na sekondari.

Mtendaji wa Kijiji cha Bukumi Alfred Onyango akizungumza kwenye kikao maalum cha kujadili mfuko wa maendeleo alisema, shughuli za utekelezaji wa maendeleo ya ujenzi yanaenda vizuri kwani tayari chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi Bukumi kimekamilika na katika ujenzi huo, mifuko mitano ya saruji imebaki huku vyumba vyote vikiwa vimepigwa lipu nje na ndani.

“Katika shule ya msingi Burungu utekelezaji wa shughuli za maendeleo unaendelea, ukamilishaji wa kupiga lipu ndani na nje pamoja na sakafu umefikia hatua nzuri na saruji iliyopo itakamilisha kabisa chumba hicho” alisema Onyango.

Aidha, wakichangia kipengele cha agizo la Mkuu wa Wilaya, wajumbe wa serikali ya kijiji cha Bukumi wakiongozwa na Koporo Chirongo alisema, Mkuu wa wilaya ni kama amewatangulia kwa kuwa michango hiyo tayari kijiji cha Bukumi wanayo na wanaendelea nayo hadi hapo watakapofikia hatua ya kumaliza uhaba wa madarasa na maabara katika kijiji na kata yao.

Hata hivyo, akiweka msisitizo kwenye hoja hiyo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Burungu na mjumbe katika serikali ya kijiji cha Bukumi Bahati Tengule alisema, suala la mtoto kupata elimu bora si la kufikiria, ni kitu cha kukubaliana na agizo na hata kama asingesema Mkuu wa Wilaya, bado wazazi na viongozi wanatakiwa kuwajibika.

Tengule alisema, wanachohitaji ni kuona watoto wanafaulu masomo ya Sayansi siyo kuendeleza changamoto za Sayansi kama walizoziacha shuleni hapo ikizingatiwa masomo hayo ndio yenye ajira ya uhakika.

“Nimesoma kwenye shule ile na kero ya maabara naijua sana. Na leo bila kusoma masomo ya Sayansi, utajiriwaje? Sisi ni wazazi tukubaliane twende kwenye utekelezaji” alisema Tengule.

Kwa upande wake mmoja wa wajumbe kwenye kikao hicho Mangerepa Misana aliibua wasiwasi wa mchango wa maabara wa shilingi 5,000 na kusema fedha kama hizo zilichangwa na mrejesho wa matumizi yake haujawahi kurudishwa tangu mwaka 2014 yapata takribani minne.

Mangerepa aliomba kama kuna uwezekano mtendaji aliyehusika kukusanya michango hiyo arudishwe Bukumi awasomee wananchi taarifa ya mapato na matumizi ili roho zao zirudi pamoja na waendelee na mchango mwingine kama alivyoagiza Mkuu wa Wilaya.

KIJIJI CHA CHIRORWE WAOMBA MSAADA WA KUMALIZIA JENGO LA ZAHANATI

Mafundi wakiwa katika zoezi la uezekaji wa jengo la zahanati ya kijiji cha Chirorwe kata ya Suguti

Na. Verdiana Mgoma

KAMATI ya afya Halmashauri ya Musoma vijijini kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Chirorwe, wamekusudia kuboresha huduma ya afya kwa kukamilisha jengo litakalotumika kwa ajili ya zahanati ya kijiji hicho.

Mwenyekiti wa kijiji cha Chirorwe Maingu Msai, alisema wameamua kujitolea katika ujenzi wa zahanati hiyo ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya inayowakabili kwa muda mrefu.

Mwenyekiti huyo alisema, wananchi wameamua kuchangia nguvu kazi hadi hatua waliyofikia, na hatua iliyobaki wameomba msaada kwa serikali na wadau mbalimbali ili waweze kumalizia.

“Tuliomba msaada serikalini tukafanikiwa kupaua, tulipokea milioni 30, lakini bado tunahitaji msaada mkubwa ili kukamilisha jengo hili kwa kuwa lengo letu ni kuwepo na huduma ya afya kijijini hapa” alisisitiza Msai.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Nyakwesi Masatu, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo alisema, moja ya changamoto kubwa wanayokumbana nayo hasa akina mama, ni umbali wa kufuata huduma ya afya.

Nyakwesi alisema, kijijini kwao huduma ya afya ya uzazi wa mama na mtoto ambazo ni upimaji wa mama wajawazito na watoto, kuzalisha na kufatilia makuzi ya watoto, hazipatikani, hivyo husababisha akinamama kupoteza maisha au kiumbe kinachozaliwa.

Alisema, akinamama pia kwa kukosa huduma za karibu wanapata magonjwa mengine kama fistula, ikizingatiwa kijiji chao hakina gari la kubebea wagonjwa.

“Hatuna usafiri ambao unaweza kutufikisha kituoni kwa wakati, watoto wanaozaliwa kukosa huduma za afya kama chanjo na ukuaji wa shida, ombi langu kwa serikali tuweze kupata msaada wa mahitaji yetu na kukamilika kwa jengo hili utasaidia, maana sehemu tunapofuata huduma ni kijiji cha jirani kutoka tunapoishi” alisema Nyakwesi.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Suguti Danford Gaudance alisema, kata hiyo pekee ndio ambayo haina zahanati, hivyo inawapa wakati mgumu wakazi wa kijiji hicho kufuata huduma ilipo.

Afisa Mtendaji huyo alisema, nia yao ni kusogeza huduma karibu na walengwa hasa akina mama wajawazito, watoto na wazee, lakini bado wanahitaji msaada mkubwa ili kukamilisha jengo hilo.

Miongoni mwa msaada wanaohitaji ni saruji, milango, madirisha na vifaa vya hospitali, huku akifafanua kuwa, fedha walizopokea ni kwa ajili ya kuezeka tu, hivyo mahitaji bado ni mengi na lengo lao ni kuondoa adha ya wakazi wa kijiji hicho kuwa mbali na huduma ya afya.

ZOEZI LA UPIMAJI WA ENEO LA ZAHANATI BURUNGU LAKAMILIKA

Viongozi wa serikali ya kijiji, kata na Halmashauri wakijadiliana mara baada ya kukamilika kwa zoezi la upimaji wa eneo ambalo itajengwa zahanati ya kitongoji cha Burungu.

 Na. Fedson Masawa

MGANGA Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Thadeus Makwanda amehudhuria zoezi maalum la upimaji wa eneo linalotarajiwa kujengwa zahanati katika kitongoji cha Burungu, kijiji cha Bukumi kata ya Bukumi.

Zoezi hilo liliongozwa na Mhandisi wa wilaya aliyekuwa ameambatana na Mganga Mkuu wa wilaya ya Musoma pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri ya wilaya ya Musoma akiwemo Afisa ardhi kutoka Halmashauri ya Musoma.

Akizungumzia hali halisi ya eneo lililopimwa kwa ajili ya zahanati, mhandisi Mkuu wa wilaya Maige Gibai alisema, eneo lililotengwa na kijiji ni kubwa na linatosheleza kujenga zahanati pamoja na nyumba za waganga.

Maige aliwaomba wananchi wajitume na kuanza kusogeza mawe, matofali, kototo na mchanga wakati wakisubiri mchoro ili kuhakikisha zoezi la ujenzi linaenda kwa kasi na serikali ianze kuiweka zahanati yao kwenye bajeti.

Naye Mganga Mkuu Dkt. Thadeus Makwanda alisema, wananchi wameteseka kupata huduma hiyo kwa kutembea umbali mrefu kuifuata jambo ambalo hapendi kuliona likiendelea, kwani hali hiyo ndio inayochangia vifo vingi vya akinamama wajawazito, watoto na wazee.

“Ndugu wananchi mmeteseka sana, namimi sipendi muendelee kuteseka. Unakuta mama anaumwa na uchungu usiku, akikaa kuanzia saa 3 hadi saa 4 bila huduma yoyote na hasa ikitokea kama mimba ina matatizo, basi tunaweza kumpoteza mtoto au mama” alisema Dkt. Makwanda.

Aidha Dkt. Mwakwanda aliongeza kuwa, kwa sasa wananchi wanatakiwa waungane ili kuhakikisha zoezi la ujenzi linaenda kwa kasi na wawe na hali ya kuhamasishana kutoa michango mbalimbali pamoja na kushiriki katika zoezi zima la ujenzi.

“Kwahiyo sasa mnatakiwa muwe na moyo kweli kweli. Muwe na Moyo wa kuhamasishana, kuchanga na kujenga. Vyote hivyo mkiwa navyo hii zahanati haichukui miaka mingi” alisema Dkt. Makwanda.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Bukumi na kitongoji cha Burungu, Magreth Deus ambaye ni mkazi wa eneo hilo,  alishukuru ujio wa serikali kwa lengo la kuwasogezea huduma karibu.

Magreth alisema, huduma hiyo ilikuwa ikisubiriwa na kuhojiwa kwa kipindi kirefu kupitia kwa viongozi wao, hivyo jukumu lao sasa ni kutekeleza maagizo ya wataalamu, kusogeza mawe, mchanga na michango mingine inayohitajika na kuwaomba wataalamu wawaishe ramani ya majengo hayo ili ujenzi uanze mapema.

“Kwa niaba ya wananchi wa eneo hili, ninapenda kuwashukuru sana wataalamu kwa kuja kusogeza huduma hii. Pia jukumu letu sasa ni kutekeleza maagizo mliyotuagiza. Tutasomba mchanga, matofali na tutachanga kwa kuhamasishana” alisema Magreth.

Akifunga kikao hicho cha wataalamu na wananchi kilichofanyika baada ya zoezi la upimaji wa eneo la zahanati, Mwenyekiti wa kijiji cha Bukumi Nyaonge Maligo alishukuru idara ya afya, ardhi na ujenzi kwa kuona umuhimu wa kufika na kuthibitishia wananchi wake kwa vitendo kwamba, sasa kazi ya ujenzi wa zahanati imeanza.

MATARAJIO YA KUPATA MBEGU BORA YA MIHOGO YAANZA KUONEKANA MUSOMA VIJIJINI

Moja ya mashamba ya mbegu za mihogo yaliyostawi vizuri katika kijiji cha Maneke.

Na. Ramadhani Juma

MSAADA wa mbegu za mihogo zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa ajili ya kuzalisha  mbegu za ziada katika mashamba darasa, zimeanza kuonesha mafanikio katika baadhi ya maeneo ndani ya jimbo hilo.

Katika maeneo mbalimbali ikiwemo kijiji cha Maneke, mbegu hizo zimestawi vizuri na kuleta matumaini ya kuwapo kwa mbegu za kutosha kwa siku za usoni.

Kaimu Afisa Kilimo Wilaya ya Musoma vijijini, Godfrey Nyambwe akizungumza baada ya kukagua mashamba ya mbegu, alimshukuru Afisa Kilimo wa kijiji hicho Mwaliki Muyengi kwa jinsi alivyosimamia kazi zake vizuri hadi wananchi wa kijiji hicho kuvunja rekodi ya kustawisha mbegu bora za mihogo.

“Nakushukuru sana ndugu Muyengi kwa jinsi ulivyosimamia mbegu hizi tangu mwanzo wa ugawaji, upandaji na sasa zimestawi vizuri, pia niwashukuru wana kikundi wa Keuma na Mzee Mafuru Geremo walivyoamua kutengeneza mashamba darasa kwa ajili ya kustawisha mbegu hizi, hivyo nawaomba wazitunze mbegu hizo hadi pale zitakapotosha kuvunwa” alisema Nyambwe.

Katika kijiji hicho cha Maneke, Jumla ya heka tatu za mihogo zimestawishwa katika mashamba darasa mawili, ambapo heka moja na nusu imestawishwa na mkulima binafsi Mafuru Geremo na heka nyingine moja na nusu imestawishwa na kikundi cha Keuma.

KIKUNDI CHA ‘HAKI SAWA’ KURWAKI WAFURAHIA MAVUNO YA MAHINDI

Wanachama wa kikundi cha Haki sawa wakishiriki kuhifadhi mahindi waliyovuna (Picha Na. Ramadhani Juma)

Na. Mwandishi Wetu

KIKUNDI cha kilimo cha umwagiliaji cha Haki Sawa kutoka Kijiji cha Kurwaki wameanza kunufaika baada ya kuvuna zaidi ya magunia 50 katika msimu wao wa kwanza wa kilimo.

Wakizungumza kwa furaha mbele ya msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Ramadhani Juma wanakikundi hao wamesema kwa sasa wamegundua mbinu ya mafanikio ni juhudi na kujituma.

“Hakika hatukutarajia kama tungeweza kuvuna kiasi hiki cha mahindi, tumejifunza kuwa juhudi huzaa mafanikio, tulianza kimchezomchezo tu, lakini leo tuna furaha kwa kile tulichokipata” alisema Mwenyekiti wa kikundi hicho  Kudra Charles.

Katibu wa kikundi cha Haki Sawa Stephano Cosmas alisema, mahindi hayo nusu yake yatatumika kwa ajili ya chakula kwa wanakikundi na nusu yatauzwa ili kupata fedha za kutunisha mfuko wa kikundi.

“Tumekubaliana kugawana nusu ya mavuno yetu kwa maana kwa sasa tunakabiliwa na janga la njaa, hivyo mahindi haya yatatusaidia sana na yatakayobaki tutayauza kwa ajili ya kununua vitendea kazi ili tuweze kupanua kilimo chetu” alisema Cosmas.

Wakitoa ombi lao kwa msaidizi wa Mbunge la kusaidiwa vitendea kazi kutoka Ofisi ya Mbunge, mweka hazina wa kikundi hicho Selemani Minangi alimwomba msaidizi huyo amfikishie Mbunge ombi hilo.

“Sisi tumejitolea kufanya kazi ya kufa na kupona tutahakikisha tumeondoa umasikini katika familia zetu kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji kama tulivyofanya, tunakuomba mtusaidie japo mashine ya umwagiliaji kama mlivyotoa msaada kwa vikundi vingine” alisema mweka hazina huyo.

Kwa upande wake msaidizi wa Mbunge Ramadhani Juma, aliwaomba wanakikundi hao kuongeza juhudi na kutokuwa na tamaa ya kugawana mara tu wanapofanya uzalishaji.

“Kikundi chenu bado ni kichanga, mnahitaji kuzalisha kwa wingi ili muweze kufikia mafanikio, epukeni kuwa na tamaa, hivyo kiasi mtakachouza jitahidini kununua baadhi ya vitendea kazi ili muepukane na kazi za sulubu za kumwagilia kwa mikono” alisema.

MKULIMA JEMBE WAPANIA KUFANYA MAKUBWA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA

Wanachama wa kikundi cha Mkulima Jembe wakitayarisha mashine ya umwagiliaji inayotumia mionzi ya jua, tayari kwa kuanza zoezi la kumwagilia bustani yao.

Na. Fedson Masawa

KIKUNDI cha Mkulima Jembe kilichopo kijiji cha Kastam, Kata ya Bukima ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini, kimesema kwa sasa wana mpango mathubuti wa kuanzisha kilimo kwa ajili ya mazao ya chakula ili kupambana na hali mbaya ya upungufu wa chakula ndani ya jimbo hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi alipotembelea shamba la kikundi hicho, Mwenyekiti wa Mkulima Jembe Festo Obedi alisema, kikundi chao kilianza kwa kutumia teknolojia ya asili; yaani walitumia kubeba ndoo za maji kwa ajili ya kumwagilia bustani ndogo ndogo, lakini baadae walipokea mashine kutoka kwa Mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo na kuanza kilimo cha kumwagilia kwa kutumia zana za kisasa.

“Kwa jitihada kubwa za kikundi, kwa sasa tumenunua mashine mbili ambazo zinatumia teknolojia ya umeme wa jua (Mashine zinazovuta na kusukuma maji kwa kutumia mionzi ya jua)” alisema Obedi.

Obedi alisema, kikundi chao kina mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia mashine tatu walizonazo ili kufanya mambo makubwa na ya kushangaza, mambo hayo ni pamoja na kupanua mashamba kwa ajili ya kuanza kilimo kikubwa cha umwagiliaji ili kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi ikiwa ni hatua njema ya kupambana na tatizo kubwa la upungufu wa chakula ndani ya jimbo la Musoma vijijini.

Kiongozi huyo alisema, wanafikiria kupata mashamba makubwa ya kukodi kwa ajili ya kufanikisha malengo waliyojiwekea. Pamoja na mipango hiyo muhimu Festo amesema changamoto kubwa ni mtaji wa kutekeleza na kufanikisha mipango yao ambapo ameomba serikali, wadau mbalimbali pamoja na Mbunge wao wa Jimbo la Musoma Mjini Prof. Sospeter Muhongo kuwasaidia kutatua changamoto hizo.

“Tuna mpango wa kukodi mashamba makubwa zaidi ili kufikia malengo tuliyoyaweka, lakini changamoto kubwa inayotusibu ni mtaji. Tunaomba kama serikali na wadau wengine kwa kupitia mbunge wetu watusaidie mtaji” aliomba Obedi.

Akizungumzia hali ya kujituma kwa vikundi vingine, Obedi alisema endapo vikundi vingine vilivyonufaika na mfuko wa jimbo na vile ambavyo havikunufaika na fedha hiyo kwa sasa, vikiwezeshwa kwa mashine hizo za kutumia mionzi ya jua, basi wanaamini jimbo la Musoma vijijini halitakuwa jimbo la kuomba na kuagiza chakula kutoka maeneo ya nje.

“Mashine hizi ni nzuri, tunaomba serikali kama itaamua kutuwezesha tena pamoja na vikundi vingine basi watununulie mashine kama hizi ili wanavikundi wengine waweze kushiriki kikamilifu” alisema.

Kwa upande wake Witness John amewaomba akinamama kuchangamkia fursa ya kilimo cha umwagiliaji kwani hakuna tena kilimo kitakachomkomboa mwanamke wa kijijini tofauti na kilimo cha umwagiliaji.

Witness aliongeza kuwa, hali ya hewa imekuwa ya kubadilika badilika, mwanzo walitegemea mvua za vuli na masika, lakini bado zimekuwa za kusuasua.

“Sisi wanawake, tunafanya kazi kwa bidii na inatusaidia kusomesha watoto, nawaombeni wanawake wenzangu tuchangamkie kilimo hiki cha umwagiliaji kwenye vikundi vingine ili tujikwamue katika umaskini tulionao na tuwasomeshe watoto wetu” alisema Witness.

Hata hivyo, Witness aligusia suala la viongozi wa kilimo kushindwa kuwafikia wana vikundi wakati wote wa kuanza kilimo hadi wakati wa mavuno, jambo ambalo alidai linachangia kushindwa kutatua changamoto za kitaalamu zinazowakabili wanapokumbana nazo ikiwa ni pamoja na ushauri wa kitaalamu, madawa yanayoweza kudhibiti magonjwa tofauti tofauti na namna ya kukabiliana nayo.

KIKAO CHA ‘WARD C’ CHATOA TAMKO UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO BUKIMA

Wajumbe wa kikao cha Ward C wakiwemo wataalamu na wazee mashuhuri waliokaribishwa kwenye kikao hicho, wakifuatilia kwa makini mijadala mbalimbali iliyokuwa ikiendelea ndani ya kikao hicho.

Na. Mwandishi Wetu

KIKAO cha Ward C Bukima kimetoa agizo kwa viongozi wa kijiji cha Bukima pamoja na vijiji vingine vya kata hiyo kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika vijiji hivyo inatekelezwa na kukamilika kwa wakati.

Maamuzi hayo yamechukuliwa ili kuwapa moyo wafadhili mbalimbali wanaotoa michango yao akiwemo Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ambaye ametoa mifuko ya saruji, mabati na hata vitabu vinavyohitaji maktaba kwa shule zote za sekondari na msingi.

Tamko hilo limetolewa katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Kata ya Bukima na kuhudhuriwa na wajumbe wa Ward C, wataalamu mbalimbali pamoja na wazee mashuhuri wa kata ya Bukima, ambapo ajenda 12 zilijadiliwa ikiwemo “Tathimini ya Mipango ya Maendeleo Ndani ya Nusu Mwaka kwa Vijiji vitatu vya Kata ya Bukima” ambavyo ni Bukima, Butata na Kastam.

Katibu wa kikao hicho ambaye pia ni Mtendaji wa kata ya Bukima Peter Magesa alisema, kati ya vijiji vitatu vya kata ya Bukima; Bukima, Butata na Kastam, ni vijiji viwili peke yake ambavyo vimefanikiwa kukamilisha mipango yao kwa kipindi chote hicho cha nusu mwaka.

Magesa alisema, Kijiji cha Bukima ambacho kimebaki nyuma kwa kila kitu hali ya kuwa fedha za kutekeleza miradi wanazo na ni kijiji chenye uwezo mkubwa ukilinganisha na vijiji vingine.

Alisema tayari kijiji cha Kastam kimekamilisha ujenzi wa vyumba vinne na ofisi na tayari kati ya hivyo, vyumba viwili vimekwisha kuezekwa kwa msaada wa Mbunge (chumba kimoja na ofisi) na Halmashauri chumba kimoja.

Aidha, kijiji cha Butata tayari wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili kwa msaada wa mifuko 60 ya saruji iliyotolewa na Mbunge, huku Bukima pamoja na kufyatua matofali, lakini bado wanasuasua katika utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na wodi ya akinamama na watoto katika zahanati ya Bukima.

Wajumbe wa kikao hicho kupitia kwa Karebu Masuluri, waliwataka viongozi wa kijiji cha Bukima kuweka wazi matatizo na changamoto zinazowafanya wasitekeleze mipango hiyo ya maendeleo kwa wakati kabla ya kikao kutoa maamuzi na ushauri dhidi ya viongozi wa serikali ya kijiji cha Bukima.

“Kwanza tupate maoni kutoka kwa viongozi wakuu wa eneo husika ili waweze kutueleza matatizo yanayowasibu, kisha nasi tuweze kupata sehemu ya kusaidia. Tukiangalia hata kwa hali ya kawaida kijiji cha Bukima ni kijiji tajiri kuliko vijiji vingine vya kata ya Bukima na kina matajiri wanaoweza kuchangia michango yao. Tuwaombe viongozi watuelezee Mheshimiwa Mwenyekiti” alisema na kuomba Masuluri.

Akieleza changamoto zinazowakabili na kushindwa kutekeleza, kukamilisha miradi hiyo kwa wakati, Mwenyekiti wa kijiji cha Bukima Murungu Murungu alisema ni wajumbe wa serikali wengi wao kuwa na itikadi za kivyama, kuwepo na makundi kwa wenyeviti wa vitongoji pamoja na baadhi ya wajumbe kutohudhuria vikao vya serikali ya kijiji tangu wachaguliwe na kuapishwa, hivyo kubakia kuwa wakosoaji na wakwamishaji wakuu wa maendeleo na kutofautiana katika maamuzi ya kimaendeleo.

Wajumbe wa kikao hicho cha Ward C Bukima chini ya Mwenyekiti wa kikao hicho January Simula (diwani wa kata ya Bukima) baada ya kumsikiliza mwenyekiti wa kijiji hicho, waliagiza serikali ya kijiji cha Bukima kukaa chini ili kumaliza tofauti zao na kufikia 24, Julai mwakahuu tayari wawe wamekwisha kujenga na kutekeleza miradi hiyo kwa kasi na kamati itapita kukagua hatua itakayokuwa imefikiwa.

“Suala hili tumelijadili sana kwenye vikao kuanzia vikao vyao vya serikali ya kijiji, lakini tunaona ni kama tunaumiza vichwa bila mabadiliko yoyote sasa chakufanya sisi kama wajumbe wa kikao hiki cha Ward C, tunawapa muda kufikia Julai 24, 2017, tunahitaji kukuta kazi imekwishafanyika na ikamilike kwa wakati. Hatutaki tena porojo wala stori. Kinyume na utekelezaji wote mtawajibishwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria” aliagiza na kusisitiza Simula.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe walipendekeza kuwa, ikiwezekana katibu wa kikao awaandikie barua viongozi wote wa vyama vilivyowaweka madarakani wawajadili na kuwashauri wawajibike katika majukumu yao ikishindikana basi vyama vyao vichukue hatua kali dhidi yao au kushitakiwa kwa mujibu wa taratibu za nchi.

WANANCHI MUSOMA VIJIJINI WAUNGA MKONO AGIZO LA MKUU WA WILAYA  

Mtendaji wa kata ya Bukumi Leftinant Mukama akizungumza na wananchi (hawapo pichani) waliojitokeza kwenye mkutano wa kuhamasisha maendeleo ya elimu, uliofanyika kwenye kijiji cha Buraga. Kushoto ni diwani wa Kata ya Bukumi John Kurwijira, anayefuatia ni Mwenyekiti wa kijiji hicho Giriad Mageta na Mtendaji wa kijiji cha Buraga Gabriel Chacha (mwenye fulana ya njano).

Na. Mwandishi Wetu

WANANCHI wa kijiji cha Buraga, Kata ya Bukumi wamekubali na kuunga mkono agizo la Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney la kuwataka kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara.

Hatua hiyo muhimu imeonesha mafanikio chanya katika mkutano wa kwanza wa wananchi na viongozi mbali mbali wa kata na kijiji cha Buraga pamoja na ofisi ya Mbunge uliofanyika 10, Julai, 2017 ikiwa ni moja ya mikutano iliyopangwa kufanyika mfululizo kwenye kata ya Bukumi kuhamasisha zoezi la kuchangia maendeleo ya elimu.

Mtendaji wa kata ya Bukumi Leftinant Mukama akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara alisema, Mkuu wa Wilaya ameagiza watoe michango yao kwa nia njema ili kuungana na serikali pamoja na Mbunge wao katika kunusuru suala la elimu katika jimbo la Musoma vijijini.

Akichangia katika uwasilishaji wa agizo hilo, Fedson Masawa ambaye pia ni Msaidizi wa Mbunge alisema, endapo wananchi wakiwa na utaratibu wa uchangiaji huo, ni njia muafaka ya kuweka mfuko hai kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na maabara.

Masawa alisema, mfuko huo utatoa fursa nzuri katika utumiaji wa vifaa vya ujenzi vinavyotoka kwa Mbunge tofauti nasasa ambapo baadhi ya vijiji vinapokea vifaa hivyo mapema, lakini vinakaa muda mrefu bila kutumika kutokana na ukosefu wa fedha.

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Mbega Kerenge akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Buraga alisema, agizo la Mkuu wa wilaya ni zuri kwa maana limelenga zaidi kuwasaidia na kuwaondolea usumbufu, hivyo wanalikubali na watalitekeleza.

“Mimi naona wazo hili ni zuri tu kwa maana litatusaidia kupunguza usumbufu, na sasa sisi wananchi wa kijiji cha Buraga tutachangia tu” alisema Kerenge.

Naye Msabha Matara, mkazi wa kijiji cha Buraga alisisitiza kuwa, wazo la kuchangia michango hii mapema ni zuri kwa kuwa litawapunguzia majukumu na kupoteza muda hasa wakati wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

“Tumekuwa tunapoteza muda mrefu kusubiria michango, kwahiyo tukienda na wazo hili la kuchangia mapema na kuhifadhi fedha kwenye mfuko maalum, tutapiga hatua nzuri tena ya pamoja” alisisitiza Msabha.

Kwa upande wake Abiudi Matekele alitoa tahadhari kwa viongozi wa kijiji na kata kuwa makini katika kufuatilia michango hiyo na kuhakikisha kila kaya inachangia bila kuacha kaya hata moja na kisha fedha zitakazopatikana zielekezwe kwenye matumizi sahihi.

MKUU WA WILAYA YA MUSOMA AFANYA ZIARA KUHAMASISHA MAENDELEO

Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney akizungumza na viongozi mbalimbali ndani ya wilaya yake kuhusu maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara unaoendelea kwa kasi.

Na. Juma Shabani

MKUU wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amefanya ziara kwenye kanda ya Bukwaya na Mugango kwa ajili ya kuhamasisha shughuli za maendeleo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Naano aliyeambatana na viongozi mbalimbali wa halmashauri, alifanya mazungumzo maalumu na viongozi wa vijiji, kata na wenyeviti wa vitongoji wa wilaya ya Musoma vijijini kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu na afya.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma vijijini Charles Magoma, akifungua mkutano wa Mkuu wa wilaya na viongozi hao, alitoa taarifa ya fedha zilizotolewa na Halmashauri kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa zahanati na vyumba vya madarasa.

“Tumetoa pesa kwa ajili ya zahanati na shule zilizokuwa zimefikia katika hatua ya upauwaji, tumetoa milioni 20 Chirorwe, milioni 20 Nyegina, milioni 15 Kigera Etuma na shule za msingi baadhi, hiyo yote ikiwa ni pesa ya halmashauri iliyokuwa imekusanya kwenye ushuru” alisema Magoma.

Mwenyekiti Magoma aliendelea kusema, ipo miradi mbalimbali iliyopo na inayotarajia kufunguliwa ambayo ikikamilika itasaidia kuongeza mapato ya halmashauri.

“Tupo katika hatua za mwisho za kujenga stendi kubwa ndani ya halmashauri hii ikiwa ni Busekera, Murangi na Mugango, nina imani kuwa hizo stendi zitakapokamilika tutakuwa tumejiongezea sehemu za ukusanyaji wa mapato” alisema.

Aidha, Magoma alisema wana mpango wa kuanzisha mwalo kwenye eneo la Nyamrinda kijiji cha Etaro kwa ajili ya kuboresha biashara ya samaki ambapo hatua hiyo itasaidia kuinua uchumi wa eneo hilo.

“Kwenye mwalo huo kutakuwa na maegesho ya maboti yanayovua samaki na sehemu ya kupaki magari yanayosimama kwa ajili ya kusubiri kusafirisha samaki kwenda kwenye maeneo mbalimbali, hivyo tutakuwa tumeongeza mapato ndani ya halmashauri yetu, halmashauri imejipanga vizuri kuhakikisha tunajenga mwalo mkubwa na wakisasa kabisa utakao kuwa na uwezo mkubwa wa kuingiza watu wengi na biashara mbalimbali”

Mwenyekiti Magoma aliwataka viongozi hao kusaidia jitihada za kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ili vijiji ambavyo havina zahanati vipate huduma hiyo kutokana na mapato hayo.

“Kuna vijiji vingi havina zahanati, hivyo ni jitihada zetu viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha tunasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ili tufanye maendeleo mengi katika halmashauri yetu ikiwemo kujenga zahanati” alisisitiza Charles Magoma.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney alitoa shukrani zake za dhati kwa viongozi wanaomuunga mkono katika kuhakikisha wilaya hiyo inapata maendeleo.

“Nawashukuru sana wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa vijiji watendaji wa vijiji na kata kwa kuonyesha moyo wa kusimamia maendeleo yetu na kuhakikisha tunapata maendeleo kwa kasi. Ndugu zangu viongozi katika halmashauri hii hatuna madarasa ya kutosha, kuna wanafunzi bado wanasomea nje wakati tuna uwezo mkubwa kabisa wa kujenga vyumba vya madarasa hata tukijiwekea malengo kwa mwaka tukiwa tunajenga vyumba viwili vya madarasa ndani ya muda mfupi tutakuwa tuna vyumba vingi na vya kutosha hivyo watoto hawatasomea nje” alisema Dkt. Naano.

Mkuu huyo wa wilaya pia alisema, ndani ya wilaya yake hakuna maabara katika shule za sekondari, jambo ambalo litaikosesha wilaya hiyo wataalamu wa sayansi kwasababu wanafunzi watashindwa kufanya vizuri masomo yao ya sayansi na kuishia mitaani.

“Vijana wengi wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri masomo ya sayansi na kubaki kuwa mtaani bila kazi na kuzurura hovyo bila kazi, hivyo sisi wenyewe ndo inatakiwa tujenge maabara, hakuna mtu atakaye toka Kilimanjaro kuja kutujengea maabara hapa, hivyo ni juhudi zetu viongozi kuwakikisha tunawahamasisha wananchi vizuri ili kuhakikisha tunajenga maabara tena za kisasa kabisa” alisema.

Hata hivyo, Dkt. Naano alisema kuna vitu kwasasa wilaya hiyo haina tatizo navyo vikiwemo vitabu na madawati ambayo yaliwekewa mkakati maalum na mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo na kumaliza matatizo hayo.

“Sisi viongozi tumuunge mkono mheshimiwa mbunge katika mambo mengine na sio kila kitu kumuachie yeye na kuna viongozi baadhi naona mmesha jisahau kabisa kufanya majukumu yenu na kumtegemea mbunge kwa kila kitu, kwa maana mnaona analeta saruji, mabati na misaada mbalimbali nasema tufanye kazi wote” alisisitiza Mkuu huyo wa wilaya.

Katika kuunga mkono jitihada hizo za Prof. Muhongo, Dkt. Naano alipendekeza mchango wa Shilingi 15,000, kwa kaya ili kuhakikisha wanajenga vyumba vya madarasa na maabara katika vijiji vilivyopo wilayani humo, na kufafanua kwamba shilingi 5,000 itatolewa kwa ajili ya maabara na Shilingi 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.

Viongozi wote walikubaliana na suala la mchango huo wa Shilingi 15,000 kwa kaya na kuahidi kuhamasisha wananchi wao kuchangia maendeleo ya elimu.

Mbali na masuala hayo ya elimu, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney aliongelea suala la uvuvi haramu na kuweka wazi kwamba wapo viongozi ambao wameshindwa kulisimamia ipasavyo kwenye maeneo yao na kuacha uvuvi huo uendelee.

“Natoa onyo tena kwa wale viongozi ambao mmeshindwa kusimamia na kukomesha suala la uvuvi haramu, nitawakamata nyie mkae jela maana haiwezekani mshindwe kudhibiti suala hilo, kuna baadhi ya maeneo uvuvi haramu umeisha kabisa, lakini bado kuna baadhi ya maeneo viongozi mnakula rushwa na kuachia wavuvi wanaendelea kufanya uvuvi haramu, nasema hakikisheni mnakomesha uvuvi haramu, wavuvi wasiotaka kufuata sheria nipeni taarifa ili tuwashughulikie” alisema.

KILIMO CHA MUHOGO CHAPIGA HATUA NZURI MUSOMA VIJIJINI

Wanafunzi shule ya msingi Lyasembe wakipalilia shamba la mihogo kwa kung’oa maotea shambani hapo huku wakipata maelekezo kutoka kwa mwalimu wao wa kilimo Samora Manyika.  

Na. Verdiana Mgoma

ZAO la Muhogo ni moja ya mazao muhimu. Zao hili ambalo hulimwa zaidi na wakulima wadogo, hutumika zaidi kwa matumizi ya chakula na biashara.

Wakulima walio wengi wamejikita kwenye zao hili kwasababu hustawi zaidi kwenye maeneo ya mvua ya wastani, ardhi yenye kichanga, pia hustahimili ukame.

Wakitoa sifa zaidi za zao hilo la Muhogo, wakulima wanasema ni rahisi kulima na hubaki ardhini kwa muda mrefu bila kuvunwa na upatikanaji wa mavuno ni wa uhakika zaidi kuliko mazao ya nafaka.

Kushamiri kwa kilimo hiki ni jitihada za Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, ambaye baada ya kutokea malalamiko ya kuwepo upungufu wa chakula kwenye vijiji mbalimbali ndani ya jimbo lake, aliamua kuhamasisha kilimo cha muhogo.

Prof. Muhongo aligawa mbegu za Mihogo kwa wananchi wake na kuwataka kuweka nguvu kubwa kwenye kilimo hicho chenye tija badala ya kuomba chakula cha msaada.

Mbali na wakulima wengi kujitokeza kulima muhogo, hamasa ilifanywa hata mashuleni ambapo shule nyingi zimelima na kutumia vizuri fursa ya mbegu kutoka kwa mbunge.

Yapo mashamba darasa yanayomilikiwa na shule, taasisi, vikundi na wananchi wa kawaida ambao ni wakulima wazuri, lakini pia lengo la kugawa mbegu hizo katika makundi ilikuwa ni kuandaa mbegu bora kwa matumizi ya kata nzima kwa baadaye.

“Tulipokea jumla ya kilo 50 mbegu za mtama na magunia 19 ya vipando vya mihogo kutoka ofisi ya mbunge” anasema Maricha Mgono, Afisa kilimo kata ya Murangi.

Mwalimu wa Kilimo wa shule ya msingi Lyasembe, Samora Manyika anasema lengo la shule hiyo kujikita katika kilimo ni kulima mazao ya chakula na biashara na kutumia mazao hayo kwa ajili ya wanafunzi.

“Endapo tutashirikiana vizuri na wananchi, tutatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi na hiyo itasaidia kupunguza tatizo la utoro shuleni na kuongeza pia kasi ya ufaulu wa wanafunzi” anasema mwalimu Manyika.

Mmoja wa wazazi waliopo kwenye kamati ya shule na mkulima wa kijiji cha Lyasembe, Sospeter Mfungo anasema, wamechangamkia fursa hiyo ya kilimo cha muhogo lengo ili mazao hayo yaweze kusaidia upatikanaji wa chakula shuleni na kuongeza maarifa ya uelewa kwa wanafunzi.

“Kilimo cha mihogo kina faida nyingi ikiwa ni pamoja na mizizi ya mihogo ni tegemeo kubwa la wakulima, majani ya mihogo hutumika kama mboga na miti ya mihogo hutumika kama kuni maalumu kwa kupikia. Tunamshukuru sana mbunge wetu kutusaidia katika upande wa kilimo, kwa sasa tumejipanga upya na mazao yanayo vumilia ukame tofauti na hapo nyuma tulilima kwa msimu” anasema Sospeter Mfungo.

PROF. MUHONGO ATOA FUTARI KWA WAUMINI WA KIISLAMU JIMBONI KWAKE

Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini, Ramadhan Juma akihakiki baadhi ya vyakula vya futari vilivyotolewa na Prof. Sospeter Muhongo kwa ajili ya waumini wa kiislamu Jimboni kwake.

Na. Mwandishi Wetu

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ameungana na waislamu wa jimboni kwake kwa kuwapa futari katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza na waumini wa kiislamu wakati wa zoezi la usambazaji wa chakula hicho, Msaidizi wa mbunge Ramadhan Juma amewaeleza waumini hao kuwa, Prof. Muhongo yupo pamoja na amewataka kuiombea nchi amani katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

Akifafanua kuhusu mgawanyo wa chakula hicho, msaidizi huyo amesema, vyakula vilivyotolewa na mbunge ni mchele (kilo 930), maharage (kilo 475), sukari (kilo 350), mafuta (lita 195) na tambi (Katoni 35).

Vyakula hivyo vimegawanywa kwenye misikiti 36 iliyopo katika jimbo la Musoma vijijini na mgawanyo huo umezingatia idadi ya waumini katika kila msikiti.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa upokeaji wa chakula hicho, waumini hao wamemshukuru mbunge wao kwa jinsi anavyowajali bila kuangalia itikadi ya dini.

“Hakika huyu kiongozi ni mwema, yeye ni mkristo lakini anawajali hadi waislamu na kuutambua huu mwezi mtukufu, Mwenyezi Mungu amzidishie na ampe afya njema” alisema kiongozi wa msikiti wa Montah al-qalaf (Nyakatende) ustaadh Mzidalifa Ayub.

Naye kiongozi wa msikiti wa Taq’wa (Rukuba) Shekhe Mzamiru Yahya alimshukuru Prof. Muhongo kwa jinsi anavyowajali wananchi wa jimbo lake.

“Kwa mara ya kwanza nilimwona akija hapa Rukuba kukabidhi madawati kwa shule yetu ya msingi, akaleta saruji na mabati kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, na sasa amegeukia upande wa kugawa futari, hakika huyu amefunuliwa na Mungu ili awaokoe watu wake. Daima Mungu yuko pamoja nae” alisisitiza Shekhe Yahya.

Kwa upande wake, Shekhe wa Wilaya, Shekhe Bakari Ekonjo alibainisha kuwa, Waislamu hawana la kusema juu ya mbunge tofauti na kumshukuru na kumwombea maisha marefu na yenye Baraka tele.

Pia amesema, majaribu anayoyapata ni mipango ya Mungu na Mungu ndiye atamwonyesha njia ya kutokea,  alimwomba msaidizi wake kuwa, siku moja mheshimiwa mbunge afike jimboni kwa ajili kumwombea dua.

“Tufikishie salamu zetu kwa Mheshimiwa, hakika huyu ndo nabii wetu kwa watu wa Musoma vijijini na Mkoa wa Mara kwa ujumla, aliyokwishayafanya ni picha tosha kwa watanzania wote. Mungu atamwinua daima” alimalizia Shekhe Bakari.

KATA YA BUSAMBARA YATAJWA KUWA MFANO WA KUIGWA KWENYE KILIMO

Afisa kilimo wa kata ya Busambara, Benard Otieno (kulia) akitoa maelekezo kwa Mwalimu Magreth katika moja ya mashamba darasa ya zao la mtama.

Na. Mwandishi Wetu

IMEBAINIKA kata ya Busambara ni miongoni mwa Kata zilizofanya vizuri katika kilimo cha mazao ya alizeti, mtama na Mihogo kutokana na wakulima wa vijiji vilivyopo kwenye kata hiyo kufuata maelekezo ya kitaalamu na kulima kisasa.

Hali hiyo imedhihirika hivi karibuni wakati wa ziara ya Msaidizi wa Mbunge la Jimbo la Musoma vijijini, Ramadhan Juma wakati akikagua mashamba darasa ya mazao ya mtama na mihogo katika kijiji cha Kwikuba, Mwiringo na Maneke..

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wakati wa ziara hiyo, afisa kilimo wa kata ya Busambara Benard Otieno alisema, baada ya kupokea msaada wa mbegu hizo kutoka kwa Mbunge, aliitisha vikao katika vijiji vyote vitatu vya kata ya Busambara na kuwahimiza wananchi kulima mazao hayo kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora.

“Niliwagawia wananchi mbegu za alizeti kwa maana zilikuwa nyingi sana, mbegu za mihogo na mtama zilikuwa chache, hivyo tulikubaliana na wananchi kuwa zielekezwe kwenye taasisi na kwa baadhi ya wakulima mashuhuri na tukafanikiwa. Hakika najivunia mafanikio ya kilimo katika Kata yangu, tuna zaidi ya heka thelathini za alizeti, hekakumi na moja za mtama na heka nane za mihogo. Heka za mtama na mihogo ni kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za baadae, yaani ni mashamba darasa” alisema Otieno.

Aidha, afisa kilimo huyo alimshukuru Mtendaji wa Kata hiyo Victor Kasyupa kwa kuleta chachu ya kilimo cha alizeti baada ya kuamua kulima heka mbili kama shamba la mfano.

“Shamba lake limestawi vizuri sana kwa maana alifuata ushauri wa wataalamu wa kilimo, hakika atapata mavuno mengi” alisisitiza Otieno.

Pamoja na mafanikio hayo, afisa kilimo huyo alisema zipo changamoto zilizowakabili baadhi ya wakulima wa alizeti ikiwemo upungufu wa mvua, hali iliyosababisha baadhi ya mazao kukauka.

Hata hivyo, Afisa kilimo huyo aliwatupia lawama wakulima hao kwa kuchelewa kupanda kama alivyokuwa amewaelekeza, huku akimuomba msadizi wa mbunge kufikisha ombi lao kwa Mbunge la kupata mashine ndogo ya kukamulia alizeti ili wauze mafuta badala ya kuuza alizeti ambayo haijakamuliwa.

VIKUNDI VYA BURUDANI VYANOGESHA ZIARA YA MAKAMU WA RAIS

Kikundi cha Kwaya kutoka Kata ya Bugoji wakitumbuiza katika uwanja wa Mukendo, Manispaa ya Musoma wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani.

Na. Ramadhan Juma

VIKUNDI vya burudani kutoka jimbo la  Musoma vijijini, vimekonga nyoyo za wengi katika ziara ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassani wilayani Musoma.

Vikundi hivyo vilipata nafasi ya kutumbuiza katika maeneo mbalimbali, ambapo kikundi cha ngoma kilipata nafasi ya kutumbuiza wakati wa uzinduzi wa barabara ya lami Kilomita 9.9 kutoka Buhare hadi Mutex na kilipata nafasi tena katika uwanja wa Mukendo wakati wa mkutano wa hadhara.

Kikundi cha kwaya kilipata nafasi ya kutumbuiza kabla ya mkutano na baada ya mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa Mukendo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, washiriki wa vikundi hivyo, kikundi cha ngoma (Kiwajaki) kutoka kata ya Kiriba na kikundi cha kwaya kutoka kata ya Bugoji, wamemshukuru Mbunge wao Prof. Muhongo kwa kuwapatia fursa ya kuonyesha vipaji vyao.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa mbunge kwa kutupa nafasi ya kuja kuonyesha vipaji vyetu, hakika tunaweza, tunamwomba aendelee kutufadhili hata kwenye matamasha ya kitaifa tuwaonyeshe watanzania uwezo wa Musoma vijijini, hatutamwangusha milele. Tunajiamini” alisema Wanyanja Masatu, kiongozi wa kikundi cha ngoma.

MVUA NA UPEPO MKALI WASABABISHA UHARIBIFU WA NYUMBA 45 BUKUMI

Moja ya nyumba zilizopata madhara kutokana na upepo mkali ulioambatana na mvua na kusababisha kaya 45 kukosa makazi kwenye vijiji vitatu vya kata ya Bukumi.

Na. Fedson Masawa

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali imesababisha kaya 45 kukosa makazi katika vijiji vitatu vya kata ya Bukumi.

Majengo mengine yaliyoezuliwa katika tukio hilo lililotokea 2, Juni, majira ya usiku, ni pamoja na jengo moja la ghala la kijiji cha Bukumi pamoja na jengo la Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lililojengwa na kikosi hicho kijijini Busekera.

Jumla ya nyumba zilizoezuliwa kwa kila kijiji ni 10 pamoja na jengo moja la stoo ya kijiji cha Bukumi, nyumba moja katika kijiji cha Buraga na kijiji cha Busekera ni nyumba 33 na jengo moja la kikosi cha JKT.

Akitoa taarifa kwa mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa kijiji cha Bukumi Nyaonge Masatu alisema, alipata taarifa alfajiri ya 3, Juni kutoka kwa waathirika wa tukio hilo na kuagiza ipigwe ngoma ya kuwajulisha wananchi wote wasitishe shughuli zao kwa siku hiyo ili washiriki kuwapa msaada wenzao waliopatwa na matatizo hayo.

Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, mzee Malima Maira alisema upepo ulianza kuvuma ukionekana wa kawaida, lakini ghafla ukaongezeka nayeye alishtukia paa lote la nyumba likinyanyuliwa kwa upepo huo na kutupwa mbali na nyumba yake.

“Kilichofuata ni mimi na familia yangu kuloa kwa mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha, lakini tulijitahidi kuwaondoa watoto waliokuwemo ndani ya nyumba” alisema mzee Maira.

Aidha aliongeza, mbali na mke wake ambaye aliumia kidogo kwa kupigwa na tofali, anamshukuru Mungu kwani hakuna mtu aliyeumia vibaya katika ajali hiyo, japo chakula kama unga uliokuwemo ndani wote uliharibika kwa mvua hiyo.

Naye Nyamweko Chui maarufu kwa jina la ‘Nyakajore,’ alisema tukio hilo ni mara ya kwanza kumtokea na ilikuwa usiku, hivyo hakuwa na namna yoyote ya kutoa msaada kwa familia yake iliyokuwemo ndani na kuomba msaada kwa majirani.

Alisema, mbali na mali zilizoharibika na kupotea, watoto wameumia kwa kiasi kikubwa kwani wengine walikuwa wanalaliwa na matofali na tayari wamechukuliwa na diwani wa kata ya Bukumi na kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

“Sijawahi kutokewa wala kushudia hili linatokea, ni mara yangu ya kwanza, tena hii ni usiku sasa, hata watoto wangu siwaoni nikashindwa kabisa kutoa msaada kwao na mali zangu. Watoto wangu wamejeruhiwa, namshukuru Mungu diwani amewapeleka hospitalini” alisema Nyamweko.

Kwa upande wake Juliana Manumbu, alisema haelewi kabisa kilichotokea na anaona ni kama miujiza tu itokee ili kuirudisha nyumba yake katika hali iliyokuwepo, kwani hana kitu chochote anachokitegemea ili kufanikisha kuiezeka nyumba yake na kuishi humo tena kama awali.

Diwani wa kata ya Bukumi, John Kurwijira ameelezea kusikitishwa na tukio hilo na kuongeza kuwa tayari uongozi wa kata na vijiji wameshachukua hatua za kupeleka kwenye matibabu majeruhi pamoja na kuwaomba wananchi walioguswa na tukio hilo waweze kuchangia chochote ili waathirika wapate huduma ya chakula.

Diwani huyo alisema, tayari wananchi na wasamalia wameshajitokeza kuwasaidia makazi baadhi ya waathirika hadi watakapofanikisha makazi yao tena na kuomba msaada zaidi kutoka serikalini na wasamalia wema ili kuwasaidia waathirika hao.

“Ndugu wananchi nimalizie kwa kuwasihi mjitahidi kujenga nyumba imara na kuziezeka kwa ubora. Hii itapunguza kasi ya uezukaji wa nyumba zetu. Lakini pia tujitume kupanda miti katika makazi yetu na kuzunguka maeneo ya jirani ili kupunguza kasi ya upepo mkali” aliwasihi diwani John Kurwijira.

VIKUNDI VYA NGOMA NA KWAYA KUPAMBA ZIARA YA MAKAMU WA RAIS MUSOMA

Kikundi cha ngoma cha Bwai kinachotarajiwa kutumbuiza kwenye mapokezi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani anayetarajia kuwasili Wilayani Musoma 7, Juni mwaka huu.

Na. Mwandishi Wetu

VIKUNDI vya ngoma na kwaya kutoka kijiji cha Bugoji na Bwai vinatarajia kupamba mapokezi ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassani anayetarajia kuwasili wilayani Musoma 7, Juni mwaka huu.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo ameahidi kuchangia usafiri na chakula kwa vikundi hivyo ili vikatoe burudani kwenye mapokezi hayo.

“Kwaya ya Jimbo (kutoka Kijiji cha Bugoji) na Kikundi cha Ngoma (kutoka Kijiji cha Bwai) cha Jimbo la Musoma Vijijini vitatumbuiza siku hiyo ya Ugeni huo mkubwa Wilayani mwetu.  Tudumishe Utamaduni wetu na Tujitume” alisema Prof. Muhongo.

Vikundi hivyo maalum viwili vilipatikana kwenye michuano ya ngoma na kwaya ya kilele cha sherehe za nane nane za mwaka jana zilizofanyika kwenye kijiji cha Suguti.

SHEHENA NYINGINE YA VITABU YAWASILI MUSOMA VIJIJINI

Na. Mwandishi Wetu 

KONTENA la futi 40, lenye vitabu zaidi ya 22,000 limewasili Musoma vijijini kwa ajili ya kusambazwa kwenye shule za sekondari za jimbo hilo.

Vitabu hivyo vyenye thamani ya dola za Kimarekani 350,000 vitatolewa bure kwenye shule za Sekondari (20) na Msingi (111).

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo, amewahimiza wakuu wa shule mbalimbali za jimbo hilo na viongozi wa serikali zilipo shule hizo kukamilisha ujenzi wa maktaba na wale ambao hawajaanza, waanze ujenzi ili wapate mgao wa vitabu hivyo.

Prof. Sospeter Muhongo alisema, muda bado upo kwa ajili ya zoezi hilo kwani vitabu hivyo vitaanza kugawiwa 1, Januari 2018 na moja ya vigezo vya kupata mgao ni kuwa maktaba ya kuhifadhi vitabu hivyo.

Hii ni mara ya 5 kwa shule za jimbo hilo kupokea vitabu kutoka Marekani na Uingereza ambapo vitabu vingi ni kwa ajili ya masomo ya Sayansi na Kiingereza, lengo likiwa ni kuwaongezea wanafunzi uelewa na kupandisha kiwango cha ufaulu ndani ya jimbo hilo.

Shule mbalimbali tayari zimepokea vitabu hivyo kwa awamu zilizopita, ambapo mbali na shule za Jimbo la Musoma vijijini, shule nyingine za Mkoa wa Mara zimefaidika na mgao huo.

Mwaka jana, Prof. Muhongo alikabidhi vitabu vya sayansi na hesabu 25,000 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 kwa wabunge wote wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya shule za msingi na sekondari mkoani humo.

Wabunge waliokuwepo kwenye makabidhiano hayo ni Ester Matiko (Tarime Mjini, Chadema), John Heche (Tarime Vijijini, Chadema), Boniphace Mwita (Bunda Vijijini, CCM), Kangi Lugora (Mwibara, CCM) na ambao hawakufika walituma wawakilishi.

MUSOMA VIJIJINI WAHAMASISHWA KULIMA ZAO LA DENGU

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha Suguti farmer’s wakiwa katika zoezi la umwagiliaji wa dawa katika shamba la dengu. Katikati (mwenye fulana nyeusi) ni Afisa kilimo wa kijiji cha Kusenyi, Majura Chikumbiro akitoa maelekezo ya kitaalamu kwa wakulima hao.

 Na. Verediana Mgoma

KIKUNDI cha Suguti Farmer’s kilichopo kwenye kijiji cha Kusenyi wamejitosa kulima zao la dengu ili kuhamasisha wanakijiji wenzao kulima zao hilo.

Kiongozi wa kikundi hicho Mathayo Masatu alisema, wameamua kulima zao hilo kutokana na kuwepo tabia ya jamii yetu kuzoea kulima msimu, badala yake wao wanalima msimu wote hata kukiwa hakuna mvua.

Masatu alisema, shamba lao wanatarajia litakuwa darasa ambalo linaweza kuwavutia walio wengi na kujikita zaidi kwenye kilimo bila ya kujali msimu.

“Sisi vijana tumeona ni vyema tukawa waanzilishi kwenye suala zima la kilimo na mpaka sasa tumelima heka tatu za alizeti tulizopokea kutoka ofisi ya mbunge, pia tumelima heka moja ya maharage na hizo heka nne za dengu ambazo tuna imani haya ni baadhi ya mashamba darasa tulioamua kuanza nayo” alisema kiongozi huyo na kuongeza kuwa, wapo tayari kuelimisha na kuhamasisha watu kujikita zaidi kwenye kilimo bila kusubiri.

Afisa kilimo kijiji cha Kusenyi, Majura Chikumbiro akizungumzia zao hilo la dengu alisema ni moja ya nafaka kama zilivyo nafaka nyingine na ni miongoni mwa zao muhimu kwa biashara pia hulimwa ukanda wa ziwa.

Chikumbiro alisema, dengu hutumika kama mboga mchanganyo wa wali mseto na makande na kwa upande wa kanda ya ziwa hili ndio zao linalotegemewa zaidi likiongozwa na choroko kwa kuwa na thamani kubwa hivyo zao hilo ni muhimu kwa uchumi wa kanda ya ziwa.

“Kilimo hiki hakina usumbufu kama yalivyo mazao mengine hasa ukifuata taratibu, hupendelewa kulimwa zaidi kwenye maeneo ya mbuga ambayo huwahi kukauka, hivyo msimu mzuri wa kilimo cha dengu ni mwezi wanne mwishoni au wa tano mwanzoni kuhusu soko la dengu ni uhakika zaidi kwa maana uhitaji wake ni nje na ndani ya nchi” alisema Majura Chikumbiro.

MKUU WA WILAYA YA MUSOMA AHITIMISHA HUDUMA YA MATIBABU YA BURE

Madaktari bingwa kutoka China wakiwa katika maandalizi ya kuanza kutoa huduma ya matibabu katika zahanati ya Kwikuba.

Na. Fedson Masawa

MKUU wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney amefunga huduma ya matibabu iliyokuwa ikitolewa na madaktari bingwa kutoka nchini China katika zahanati mbili za Musoma vijijini.

Huduma hiyo iliyoanza 7, Mei, 2017 katika zahanati ya Nyambono na kuendelea kwa muda wa siku nne, imehitimishwa rasmi 10, Mei katika zahanati ya Kwikuba.

Akitoa taarifa ya huduma hiyo kwa niaba ya Mganga mkuu wa zahanati ya Kwikuba, Elly Hassan ambaye ni mganga muuguzi katika zahanati hiyo, alisema wananchi waliojitokeza kupata vipimo na matibabu kwa siku nne ni 2,034 ambapo 844 walijitokeza kwenye zahanati ya Kwikuba na 1,190 zahanati ya Nyambono.

Akizungumza wakati wa kufunga huduma hiyo, Dkt. Anney kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameishukuru serikali ya China na timu ya madaktari hao kwa ushirikiano mzuri waliouonesha kwa kukubali wito kutoka kwa Prof. Muhongo kuja kutoa huduma ya matibabu ndani ya jimbo lake.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa, huduma iliyotolewa na timu hiyo ni huduma ambayo kwa asilimia kubwa isingekuwa rahisi kwa jamii ya watu maskini kuimudu, lakini wamefanikiwa kuipata bila malipo.

“Na nzuri zaidi wamekuja kutibu akina mama ambao wanaishi vijijini ambao kwa namna yoyote ile wasingeweza kupata hiyo huduma. Sasa tumewatembelea huku na wameonwa, na hiyo imesaidia wenzetu wachina kufahamu wananchi wenye matatizo makubwa ambayo wanakaa nayo nyumbani bila kupata matibabu. Mfano, akina mama 20 wamepata rufaa kwenda hospitali ya mkoa wakatibiwe” alisema Dkt. Naano.

Aidha, Dkt. Naano aliwasisitiza wananchi wa Musoma na Tanzania kwa ujumla kuuendeleza na kuudumisha uhusiano na urafiki uliopo baina ya serikali hizo mbili kwani wanatambua umuhimu na kazi kubwa inayofanywa na serikali ya China nchini Tanzania.

“Urafiki wetu kati ya China na Tanzania ulianza siku nyingi sana mpaka tukawa na kiwanda kinaitwa Urafiki, wachina walitujengea reli ya kati. Hili linadhihirisha kwamba urafiki wetu ni wa shida na raha na bado wanaendelea, wanajenga bandari ya Bagamoyo. Kwa hiyo hawajaishia tu katika kutoa matibabu” alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.

Hata hivyo, katika kupiga hatua ya maendeleo zaidi ndani ya wilaya ya Musoma, Dkt. Naano amewasihi wananchi na viongozi kumuunga mkono kikamilifu mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutumia fursa zinazopatikana ndani ya wilaya yao ili kujihakikishia maendeleo chanya hasa katika mpango wa serikali kuu wa uchumi wa viwanda.

Dkt. Naano alisema, kutokana na serikali kupungukiwa katika sekta ya afya hasa upande wa madawa, wilaya ya Musoma imepewa fursa ya kujenga kiwanda cha kutengeneza bandeji na maji ya dripu ambayo yatakuwa yananunuliwa na MSD.

“Sisi serikali tunapungukiwa, hasa madawa na huduma mbalimbali, ndugu zetu wachina mlioko hapa, sisi tumepewa fursa kama wilaya tumeombwa tujenge kiwanda cha kutengeneza maji ya dripu, hicho kiwanda soko lake tumepewa na MSD. Tunahitaji tuwe na uchumi wa viwanda, sisi Musoma tunahitaji tuwe na kiwanda cha kutengeneza bandeji na maji ya dripu” alisema na kutoa changamoto kwa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Halmashauri ya Wilaya ya  Musoma vijijini kuandaa fedha kwa ajili ya kuanza zoezi la kujenga kiwanda hicho haraka iwezekanavyo.

“Kiwanda hicho, kitakuwa kimetengeneza fursa mbalimbali za ajira kwa jamii ya watu wa Musoma pamoja na Tanzania kwa ujumla. Vile vile kiwanda kitakuwa kimezuia kabisa hela nyingi zinazopelekwa nje kama vile Uganda na India ambako maji hayo yanayotumika kwenye hospitali zote nchini yanatoka huko” alisema.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Kwikuba Kamunyiro Kubega kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho na Jimbo la Musoma vijijini, ametoa shukrani za dhati kwa Prof. Muhongo kwa jitihada kubwa anazozifanya kwa wananchi wake ikiwemo kuleta madaktari bingwa na kutoa huduma ya matibabu.

“Ninamshukuru sana Prof. Muhongo kwa kutuletea madaktari bingwa ili kutoa huduma kwenye zahanati yetu, tuko pamoja na yeye. Naishukuru pia serikali ya Tanzania na China na timu ya madaktari bingwa kutoka China kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha huduma ya matibabu inawafikia wananchi na kuhudumiwa bure kabisa na huduma hii imewafikia karibu na tayari afya zao zitakuwa na auheni hivyo zitawawezesha kuendelea na shughuli zao za maendeleo.” alisema Mwenyekiti Kubega.

WANANCHI MUSOMA VIJIJINI WATAKIWA KUWEKA KANDO SIASA NA KUCHAPA KAZI

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo (wa kwanza kushoto waliokaa) akiwa na viongozi mbalimbali wa serikali, aliyesimama ni Thereza Rusweka, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kurugongo A.

Na. Mwandishi wetu

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ametaka wananchi na viongozi jimboni kwake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa linakwisha jimboni humo.

Prof. Muhongo ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kurugongo A na Kurugongo B zilizopo katika kata ya Bulinga ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kukutana na kuwapa pole wananchi walioathiriwa na kimbunga katika kijiji cha Musanja ambapo jumla ya nyumba 21 ziliezuliwa na upepo.

Akiwa katika shule ya msingi Kurugongo, Prof. Muhongo alishuhudia na kujiridhisha na hali halisi ya upungufu wa jumla ya vyumba 6 vya madarasa kwa shule zote mbili, hivyo kusababisha jumla ya madarasa 10 kusomea nje kwenye vivuli vya miti ya shule hiyo.

Awali akiwasilisha taarifa ya upungufu wa madarasa na mwenendo mzima wa taaluma ya shule hiyo, mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kurugongo A, Thereza Rusweka alisema, shule hizo zote zina uhaba wa vyumba 16, na kusababisha madarasa 10 kupata elimu wakiwa katika vivuli vya miti.

“Kwa kipindi kirefu tumekuwa katika mazingira haya haya, wanafunzi wengi waliopita wamesomea kwenye madarasa haya haya…cha ajabu sasa mvua ikija hakuna shule tena” alisema Mwalimu Thereza.

Akiwa katika hatua ya kupambana na tatizo la upungufu wa madarasa, Prof. Muhongo amewataka wananchi wa kata ya Bulinga na kata zote za Musoma vijijini kuwekeza nguvu zao katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha wanamaliza tatizo sugu la upungufu huo wa vyumba vya madarasa.

Prof. Muhongo aliongeza kuwa, yupo bega kwa bega na wananchi wa Musoma vijijini katika kusukuma gurudumu la maendeleo jimboni mwao na kuwataka wananchi waachane na itikadi za kisiasa kwa kipindi hiki cha utekelezaji wa maendeleo kwani si muda wake, kwa sasa waungane pamoja katika kufanya maendeleo kwenye maeneo yao.

“Tuwekeze nguvu kwenye madarasa, mimi Mbunge wenu nipo pamoja nanyi kwa kila kitu. Saruji ikija chapeni kazi, mabati yakija chapeni kazi. Ndani ya miaka miwili au mitatu mtaona mabadiliko. Wakati wa maendeleo mfanye kazi ya maendeleo, siasa wekeni pembeni” alisema na kusisitiza Prof. Muhongo.

Kata ya Bulinga ni moja ya kata 21 za jimbo la Musoma vijijini ambazo tayari Prof. Muhongo amekwisha kuchangia vifaa vya ujenzi kwa ajili ya vyumba vya madarasa ambapo katika shule ya Msingi Kurugongo A, Prof. Muhongo amechangia jumla ya mifuko 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa. Shule ya msingi kurugongo “B” amechangia jumla ya mifuko 110 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa.

Pia, mbunge huyo amechangia jumla ya mifuko 60 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili katika shule ya msingi Busungu na kuchangia mifuko 70 ya saruji katika shule ya sekondari Bulinga ili kusaidia ujenzi wa jengo la utawala kwa ajili ya kukamilisha mahitaji ya sekondari mpya ya kata ya Bulinga kusajiliwa.

Aidha Prof. Muhongo amechangia vifaa vya uezekaji wa chumba kimoja cha darasa katika sekondari hiyo ambapo jumla ya mabati 52 na mbao 85 vimekwisha kutolewa na ofisi ya mbunge.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya Bulinga, Diwani wa kata hiyo Mambo Japan (CHADEMA), amemshukuru mbunge wa jimbo la Musoma vijijini kwa jitihada kubwa anazozifanya jimboni yeye na serikali ya awamu ya tano kwa ujumla katika kuhakikisha wanatekeleza na kusimamia vyema maendeleo ya jimbo, taifa na hatimaye kuleta mabadiliko ya kweli.

Diwani huyo alisema, mambo yanayofanywa na serikali ya sasa ndio hayo hayo waliyokuwa wakiyataka, hivyo wapo tayari kuungana pamoja na kufanya kazi za maendeleo kwa ushirikiano ili kuleta maendeleo wanayoyahitaji wananchi.

MADAKTARI BINGWA KUTOKA CHINA WATOA HUDUMA ZA AFYA MUSOMA VIJIJINI

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Nyambono wakisubiri kupata huduma ya afya na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa kutoka China.

Na. Mwandishi Wetu

MBUNGE jimbo la Musoma na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, kwa mara nyingine ameleta timu ya madaktari bingwa kutoka China kwa ajili ya kutoa matibabu katika Zahanati mbalimbali za Jimbo hilo.

Huduma hiyo ya matibabu ilianza kwenye kata ya Nyambono na kuendelea kwenye kata ya Kwikuba ambapo wananchi walijitokeza kwa wingi kupima afya zao na kupatiwa matibabu.

Akizungumza kabla ya kuanza zoezi hilo kwenye zahanati ya Nyambono, Prof. Muhongo alisema, matibabu hayo yanatolewa bure ambapo mbali na vipimo, wananchi watakaogundulika wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali, watapatiwa dawa bila malipo yoyote.

“Hapa Nyambono madaktari wapo kwa siku mbili, nadhani kwa hizi siku mbili wagonjwa wa maeneo haya watapata matibabu, na ndugu zetu hawa wachina hamlipii chochote, ni kwamba wagonjwa mtapata matibabu bure, isitoshe watawapatia dawa” alisema Prof. Muhongo.

Aidha, madaktari hao wametunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao kwa jimbo hilo; tayari wameshatoa huduma hiyo kwenye kata ya Murangi, Mugango na Nyasusura.

Wakati huo huo katika jitihada za kuboresha huduma za afya, Prof. Muhongo alisema gari jipya la wagonjwa litafika jimboni na hivyo kufikisha jumla ya magari sita ya wagonjwa.

Hii ni baada ya gari moja kubwa kutoka Japan kupelekwa kituo cha afya cha Murangi na mengine manne kupelekwa katika zahanati za Mugango, Masinono na Nyasurula na Kurugee.

Prof. Muhongo aliwahimiza wananchi na viongozi kuwa makini na wasimamizi wazuri wa magari ya wagonjwa yanayoletwa jimboni ili baadaye kila zahanati ya Musoma ipate gari ya kubebea wagonjwa.

“Nanyi ndugu zangu wananchi na hata viongozi kuweni wakali sana kwenye haya magari na wale madereva wazembe wawajibishwe. Tunataka baadae kila zahanati ya jimbo letu ipate gari lake la wagonjwa endapo mtaendelea kuzitunza vizuri hizi zinazoletwa” alisema Prof. Muhongo.

Diwani wa kata ya Nyambono Mkoyongi Masatu, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata ya Nyambono na Musoma vijijini, ameshukuru ujio wa madaktari bingwa kutoka China kwa ajili ya kutoa matibabu katika kata yake na kuahidi kutoa ushirikiano na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa utaratibu unaofaa katika kata yake.

WANANCHI SUGUTI WAPATA MBADALA WA ZAO LA MAHINDI AMBALO LINASUASUA

Mkulima wa kijiji cha Kusenyi, Idefonce Max akiwa na kijana wake Martin wakipalilia mtama.

Na. Verediana Mgoma

BAADHI ya wananchi wa vijiji vya Kata ya Suguti wameamua kujitosa kulima zao la mtama baada ya mahindi kushindwa kustahimili ukame.

Mmoja wa wakulima hao Idefonce Max alisema, baada hali ya hewa kubadilika na kuwepo kwa mvua za kusuasua, alichukua maamuzi ya kulima mtama kwa kuhofia huenda zao la mahindi lisingeweza kustahimili mabadiliko ya msimu wa hali ya hewa.

Mkulima huyo alisema, baadhi ya wanakijiji wenzake waliolima mahindi wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kuwepo kwa mvua chache na wadudu walioshambulia mazao yao, hivyo imebidi yeye kuwa mfano kwa wengine kuhusu kilimo hicho cha mtama.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kusenyi, Magesa Mashauri amekiri kuwepo kwa changamoto kwenye zao la mahindi hasa kwa wakulima waliozoea kilimo hicho, ambapo msimu uliopita hawakuweza kufanikiwa kwenye mavuno ya mahindi na kusababisha tatizo la njaa kwenye eneo lake.

“Baada ya kumueleza mbunge kuhusu suala la msaada wa chakula aliona njia pekee ni kubadilisha mazao ya chakula kuwa mtama na mihogo, haya ni mazao yanayoweza kustahimili ukame hivyo akachukua jukumu la kuendelea kuhamasisha wananchi katika kilimo hicho na baadhi wameanza kunufaika” alisema Mashauri.

Mashauri aliongeza: “mbunge hakuishia tu kuhamasisha kilimo cha mtama na mihogo, lakini pia ametoa msaada wa mbegu za mtama na mihogo ambazo zimegawanywa kwa wanakijiji na taasisi kwa dhumuni la kutunza mbegu kwa mahitaji ya kijiji kizima kwa msimu ujao”

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Suguti, Masinde Mjarifu alisema kuna aina ya mbegu 30 za mtama zinazolimwa kama chakula na hustawi kwenye aina zote za udongo.

“Maeneo mazuri ni udongo wa mfinyanzi, lakini pia kwenye udongo ambao una kiasi kidogo cha mchanganyiko wa kichanga na huvumilia udongo wenye chumvi kuliko mahindi, hapo nyuma watu walipenda zaidi kulima mahindi kwa sababu huleta mazao mengi kwa ekari, lakini wakati wa ukame watu hurudi kwenye mtama kwasababu huvumilia zaidi ukame” alisema Mjarifu.

Aidha, afisa kilimo huyo alitaja matumizi ya mtama; ni kwaajili ya kupikia uji, mikate na pombe, lakini pia majani na mabua ya mtama hutumika kama lishe ya mifugo na matumizi mengine ni kutandikia paa ya nyumba.

“Nilipokea jumla ya kilo 50 ya mbegu za mtama na magunia 42 ya vipando vya mihogo kutoka ofisi ya mbunge, mbegu hizi nimezigawa kwa usawa kabisa kwenye vijiji vinne kwa wananchi, vikundi na taasisi ambazo hao waliopata ndio watakaotupatia mbegu kwa msimu unaofuata hivyo shukrani za pekee zimwendee mbunge wetu na mpaka sasa mabadiliko katika sekta ya kilimo yanaonekana” alimaliza Masinde Mjarifu.

Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo.

AMBULANCE MPYA KUTOKA INDIA: Tunazo Ambulance 5. Mgawanyo na matumizi ya Ambulance zetu lazima tuzingatie JIOGRAFIA na WINGI wa WANANCHI wanaohudumiwa na Zahanati zetu. Kwa hiyo Ambulance Mpya kutoka India itapelekwa ZAHANATI ya WANYERE. Bado naendelea kutafuta Ambulance nyingine. Tushukuru Serikali ya India. TUZITUNZE
S Muhongo, Mbunge

MUSOMA VIJIJINI WATAKIWA KUJITUMA NA KUFANYAKAZI KWA BIDII

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Muhongo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiriba.

Na. Ramadhani Juma

MBUNGE wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter  Muhongo, amewataka wananchi wa jimbo hilo kujituma na kufanyakazi kwa bidii ili kukabiliana na njaa.

Prof. Muhongo alitoa kauli hiyo wakati wa sherehe za pasaka ambapo alipata fursa ya pekee ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Mwiringo, Bwai Kumusoma na shule ya msingi Kiriba.

Katika kusheherekea sikukuu hiyo, Prof. Muhongo pia alipata fursa muhimu ya kushiriki chakula cha pamoja na wananchi wa jimbo lake katika viwanja vya shule ya msingi Kiriba kijijini Kiriba na kuhudhuriwa na wananchi wengi.

Awali, akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Bwai Kumusoma, Prof. Muhongo alijiridhisha na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi moja iliyojengwa kwa nguvu za wananchi ambapo katika ujenzi huo, Mbunge alichangia mabati 54 na mbao 149.

Baada ya kuguswa na jitihada za wananchi wa kijiji cha Bwai Kumusoma, Prof. Muhongo aliwaomba wananchi waliohudhuria katika ziara hiyo kujitokeza kwa moyo mmoja ili kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo, ambapo wananchi hao walichangia kiasi cha 1,500,000/= na Prof. Muhongo alichangia mabati 200 kwa ajili ya kukamilisha zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

Akizungumzia suala la kuinua elimu jimboni, Prof. Muhongo ameitaka jamii ya Musoma vijijini isimame kidete kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora katika mazingira bora ili kuboresha ufaulu na kuongeza idadi ya wasomi wa elimu ya juu na hatimaye kuondokana na umaskini na njaa katika familia zao.

Pia Prof. Muhongo aliongeza kuwa, haina haja ya kuwa na shule nyingi zisizo bora, ni bora kuwe na shule chache zilizo na ubora kitaaluma na kimazingira ya kujifunzia na kufundishia.

“Tukisomesha watoto wetu tutaondokana na umaskini na familia iliyo na msomi hawana njaa. Pia tusiwe na utitiri wa shule zisizo na ubora” alisema Prof. Muhongo.

Aidha, Prof. Muhongo aliwahimiza wananchi wa Musoma vijijini kujituma katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na tatizo la njaa katika maeneo yao.

Prof. Muhongo alisema, inasikitisha kuona mikoa mingine inapata chakula cha kutosha wakati Musoma walio katika eneo la kandokando mwa ziwa wanakosa chakula.

“Ni jinsi gani tunavyochekwa na watu wa mikoa mingine kuona tunalia njaa wakati tuna ziwa. Tujitume kufanya kazi, serikali haiwezi kulisha watu milioni 50” alisema Prof. Muhongo.

MBUNGE MUSOMA VIJIJINI AFANYA ZIARA YA KUKAGUA UJENZI WA MADARASA

Mtendaji wa kijiji cha Bugoji Yuda Magoma (kulia) akitoa taarifa ya maendeleo ya shughuli za ujenzi katika shule ya msingi Kanderema. Kushoto, aliyevaa fulana ya kijani ni Prof. Muhongo.

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea kwa kasi kubwa ndani ya jimbo lake.

Katika ziara yake hiyo, Prof. Muhongo aliongozana na  viongozi mbalimbali wa serikali na vyama, ambapo walipokelewa kwa nyimbo kutoka kwa Miriam Mwangwa (8), akihamasisha wazazi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, kuachana na majungu ya vijiweni pamoja na kuwaasa wanafunzi kujituma katika masomo yao.

Tukio hilo liliwashangaza wananchi wengi na viongozi waliohudhuria katika viwanja hivyo na kuhamasika kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo huku Prof. Muhongo akielezea kuvutiwa na ujumbe wa binti huyo na kuahidi kuungana na wananchi wa Bugoji ili kutatua changamoto ya vyumba vya madarasa.

Akiwasili katika kata ya Bugoji, Prof. Muhongo alikagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, ofisi mbili za walimu na jengo la maktaba katika shule ya msingi Kanderema ambapo ujenzi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa msaada wa mbunge aliyetoa mifuko 120 ya saruji huku wananchi wakijitolea kufanya kazi mbalimbali za kusaidia ujenzi huo.

Akizungumzia shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa, diwani wa kata ya Bugoji Ibrahimund Malima, alimshukuru mbunge wao kwa msaada aliowapatia hususani saruji na mabati.

Vilevile diwani alimshukuru kwa kuwasaidia mbegu za alizeti na mihogo, na kuahidi kusimamia kikamilifu na kuhakikisha vifaa vyote vilivyotolewa na mbunge na wahisani wengine vinafanya kazi iliyopangwa.

Akiwa katika kijiji cha Muhoji, Prof. Muhongo alikagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya msingi Muhoji vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho ambapo wananchi walichangia ununuzi wa saruji na mbao.

“Vyumba vyote vinne vimejengwa kwa nguvu za wananchi pia mbao zote ni nguvu za wananchi, hivyo tunaomba mbunge kama kuna uwezekano tunaomba utusaidie bati 108 tukamilishe ujenzi huu kama ulivyotusaidia bati za kuezeka chumba kimoja kilichokamilika” alisema mtendaji wa kijiji cha Muhoji, Mohamed Hamza.

Aidha, mtendaji huyo aliongeza kuwa, kijiji cha Muhoji kina changamoto ya ukosefu wa zahanati jambo ambalo lilimgusa pia Prof. Muhongo na kuamua kuungana na wananchi wa kijiji hicho kuanzisha harambee kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.

Katika harambee hiyo, jumla ya 480,000/= zilipatikana. Prof. Muhongo pia aliwaunga mkono kwa kuwasaidia jumla ya mifuko 100 ya saruji na kuwataka wafuate taratibu zote za kitaalamu katika ujenzi wa zahanati hiyo.

Mbali na zoezi hilo la ukaguzi wa ujenzi wa madarasa, Prof. Muhongo alihudhuria zoezi la kuaga mwili wa mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chumwi Edward Kohe, lililofanyika shuleni hapo.

Katika kumuenzi mwalimu huyo, Prof. Muhongo aliahidi wananchi wa kijiji cha Chumwi kuwajengea vyumba 9 vya madarasa kwa kuwapatia mifuko 405 ya saruji. Prof. aliwataka wananchi kujituma kwa kujenga vyumba hivyo kama ishara ya kumkumbuka mwalimu huyo daima.

“Mwalimu amefariki lakini historia yake haitopotea milele. Tukijenga hivyo vyumba vya madarasa, mwalimu hatosahaulika milele” alisema Prof. Muhongo.

JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI – SALAMU ZA MBUNGE WENU

Tunaposherehekea PASAKA ya 2017, naomba niwakumbushe MAAMUZI tulìyoyafanya: (1) Kuboresha Elimu ya Shule za Msingi na Sekondari, (2) Tuwe na Kilimo chenye kutumia maarifa mapya na ubunifu mpya, (3) Kuboresha Miundombinu ya Matibabu ya kisasa (4) Kufufua Utamaduni wetu. Ardhi, Umeme, Maji na Miundombinu ya Usafiri na Mawasiliano ni nyezo za kujenga uchumi imara. TUTAFANIKIWA.

VIJANA WA SERENGETI KUFUNDISHWA KUTENGENEZA CHAJA NA TAA ZA UMEME JUA

SOLAR LAMP & SOLAR CHARGER: Baada ya vijana 100 wa Jimbo la Musoma Vijijini kufuzu kutengeneza taa na charger za Jua, Mbunge wa Musoma Vijijini amempeleka Mtaalamu Dr H K Choi (S Korea) Wilayani Serengeti akatoe mafunzo hayo kwa vijana wa Serengeti. Mradi huu wa vijijini utatekelezwa ndani ya Wilaya zote za Mkoa wa Mara.

MBEGU ZA MKOMBOZI ZALETA MATUMAINI KWA WAKULIMA MUSOMA VIJIJINI

Afisa kilimo kutoka idara ya kilimo halmashauri ya wilaya ya Musoma (kushoto) akikagua moja ya mashina yaliyo ng’olewa katika shamba la mbegu bora aina ya mkombozi katika shamba la shule ya msingi Butata kijijini Butata. Kulia ni Charles Buremo afisa mtendaji wa kijiji hicho na katikati ni Mshangi Salige, afisa kilimo kata ya Bukima na Rusoli.

Na Mwandishi Wetu

MBEGU bora za mihogo aina ya Mkombozi ambazo zilisambazwa mwishoni mwa mwaka jana, zimeonekana kustawi na kuleta matumaini kwa wakulima wa Musoma vijijini.

Hayo yamebainika wakati wa zoezi la usambazaji wa mbegu za awamu ya pili ambazo zimetolewa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, zoezi ambalo limefanywa na Afisa kilimo kutoka halmashauri ya wilaya ya Musoma na Msaidizi wa Mbunge Fedson Masawa.

Baada ya zoezi hilo kukamilika, viongozi hao waliomba kutembelea baadhi ya mashamba darasa yaliyopo shule ya msingi Kwikerege pamoja na shule ya msingi Butata na kujiridhisha na maendeleo ya mbegu hizo zilizotolewa na Halmashauri kwa mara ya kwanza.

Akitoa taarifa ya ustawi wa mbegu hizo, mwalimu Maregesi Malima ambaye ni mwalimu wa bustani katika shule ya msingi Kwikerege alisema, mbegu aina ya mkombozi zinastawi vizuri ila changamoto kubwa iliyowakabili ni ukosefu wa mvua kwa kipindi kirefu.

Mwalimu Malima alisema, hali hiyo imechangia mbegu kukauka, ingawa wana imani ya kupata mavuno mazuri hasa kwa awamu ya pili.

Akizungumzia kuhusu namna ya utunzaji na usimamizi wa mashamba hayo, Afisa kilimo wa kata ya Rusoli na Bukima Mshangi Salige alisema, wanafuatilia kwa ukaribu na kusimamia kuanzia hatua ya uandaaji wa mashamba, mbegu na upandaji.

Salige aliongezea kuwa, kwakuwa wafanyakazi wakuu wa mashamba hayo ni wanafunzi, wanatumia muda mwingi pia kuwa karibu nao hasa wawapo shambani wakati wa kupanda na kupalilia.

“Mimi kama msimamizi wa kilimo kwenye kata hizi mbili wajibu wangu ni kusimamia hatua zote kuanzia kuandaa shamba hadi kupalilia. Pia kuwasimamia vizuri wanafunzi katika hatua ya upandaji na upaliliaji ili wasiende kinyume na kanuni za kilimo” alisema Salige.

Naye afisa kilimo kutoka wilaya ya Musoma Godfrey Katima, alielezea kukerwa na kitendo cha baadhi ya wananchi wa kijiji cha Butata kung’oa mihogo hiyo mashambani bila utaratibu wowote hali ya kuwa haijafikia hatua ya kuvunwa na kusema hivyo ni vitendo visivyovumilika.

“Viongozi msiwavumilie hata kidogo wale wote watakaobainika kung’oa mihogo hiyo na hatua kali zichukuliwe dhidi yao na kila raia awe mlinzi wa mbegu hizi ili zitusaidie wengi hapo baadae” alisema Katima.

Akizungumza wakati wa kukamilisha zoezi la ukaguzi wa mashamba hayo, Mtendaji wa kijiji cha Butata Charles Buremo kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Butata na jimbo la Musoma vijijini, amemshukuru Prof. Muhongo kwa kuwathamini wananchi wake na kuwaletea mbegu bora zaidi za mihogo ili kuondokana na upotevu wa zao hilo jimboni.

Pia Buremo amekiri kuwepo kwa vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu katika mashamba hayo ya mbegu bora na kuahidi kuyashughulikia matendo hayo ili kuhakikisha yanakoma hapo kijijini kwake.

“Kwanza nimshukuru Prof. Muhongo kwa namna anavyowajali wananchi wake na kuwaletea mbegu hizi bora za mihogo ili kuendelea kulinda heshima ya zao hili jimboni. Ni kweli, matendo haya yatakuwa yanafanywa na watu wasio na maono na nia njema ya kuthamini umuhimu wa mbegu hizi. Mimi nina ahidi kulishughulikia suala hili kwa ajili ya manufaa ya wengi hapo baadaye” alisema Buremo.

MIFUKO MINGINE 2,560 YA SARUJI YAKABIDHIWA MUSOMA VIJIJINI

saruji

Msaidizi wa mbunge Ramadhan Juma (kushoto) akiwakabidhi viongozi wa ngazi mbalimbali mifuko ya saruji. Kutoka kulia ni Mwalimu Biego Marogoi, Diwani wa Kata ya Bwasi Masatu Nyaonge na Mtendaji wa kijiji cha Busekera Dorica Togora.

Na Mwandishi Wetu

MIFUKO 2,560 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari za jimbo la  Musoma vijijini imekabidhiwa kwa walengwa.

Hiyo ni awamu ya pili ya mpango huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa unaofadhiliwa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, ambapo awamu ya kwanza mifuko 2,560 pamoja na mabati 1,296, yalitolewa kwa shule za msingi 39 na shule tatu za sekondari.

Katika awamu hiyo ya kwanza, zaidi ya vyumba 60 vimejengwa, katika awamu hii ya pili, shule za msingi 27 na shule za sekondari 4 zimepata mgao wa saruji hiyo ambapo utekelezaji wa ujenzi unaanza.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mifuko hiyo ya awamu ya pili, msaidizi wa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Ramadhani Juma, amewaomba viongozi wa vijiji na kata mbalimbali walioshiriki kuchukua saruji hiyo kuitumia kwa muda muafaka na kwa matumizi yaliyokusudiwa ambayo ni ujenzi wa vyumba vya madarasa na si vingine.

“Ndugu waheshimiwa viongozi mliochukua saruji hii, tunawaomba mjitahidi sana kuhakikisha inatumika kwa haraka sana na kwa kazi lengwa ikiwa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa” alisema msaidizi huyo.

Aidha, aliongezea kwa kuwataka viongozi hao wajitume katika usimamiaji na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo ili kuendana na kasi ya awamu ya tano na hatimaye kukamilisha hatua hiyo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuingia kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

“Vile vile viongozi mjitahidi na mjitume sana kufuatilia na kusimamia kuhakikisha shughuli za maendeleo zinaenda kwa kasi ili tuweze kukamilisha hili zoezi la vyumba vya madarasa. Pia hatutakubaliana na ubadhilifu wowote utakaojitokeza juu ya matumizi ya saruji hii, atakayefanya vitendo hivyo atawajibika” alisisitiza.

Akizungumza baada ya kupokea mifuko hiyo, diwani wa kata ya Bwasi, Masatu Nyaonge alisema, mifuko 120 aliyopewa kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili ambazo ni shule ya msingi Bwasi B pamoja na kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi Kome B, utakuwa umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuahidi kusimamia matumizi sahihi ya saruji hiyo.

“Kwa idadi hii ya mifuko 120 mlionikabidhi, ujenzi wa shule hizi Kome B na Bwasi B utafanikiwa kwa kiasi kikubwa na ninakuhakikishia kuwa saruji hii itatumika kwa wakati na kwa matumizi sahihi” alisema diwani Nyaonge.

Naye Mtendaji wa kijiji cha Busekera Dorica Togora, ameshukuru kwa mchango huo wa mifuko 60 ya saruji na kusema ana uhakika wa kukamilisha zoezi la ujenzi wa vyumba viwili mapema mwezi wa nne kama hali ya hewa itakuwa nzuri.

Mtendaji Dorica aliongezea kuwa, ana imani na wananchi wake kuhusu ushiriki wao katika maendeleo kwani mpaka sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili na ofisi moja kwa nguvu na michango yao wenyewe.

Kwa upande wake, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Makojo Biego Marogoi kwa niaba ya viongozi na wananchi wa jimbo la Musoma vijijini, ametoa shukrani za dhati kwa Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini kwa jitihada zake za kuboresha miundo mbinu katika sekta ya elimu.

“Kwa niaba ya viongozi wote wa jimbo hili la Musoma vijijini na wananchi wote, napenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kabisa kwa mbunge wetu Prof. Muhongo kwa jitihada anazozifanya katika miundo mbinu ya elimu. Nasi tunaahidi kumuunga mkono na kuanza ujenzi huu mapema zaidi” alishukuru na kuahidi mwalimu Marogoi.

Baada ya awamu hii ya pili kukamilika, zaidi ya vyumba 100 vya madarasa vitakuwa vimejengwa. Upatikanaji wa vyumba hivi utasaidia kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani hali inayochangia kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu.

WADUDU WAHARIBIFU WASHAMBULIA MAHINDI, HATUA ZA HARAKA KUCHUKULIWA

Untitled2

Afisa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Godfrey Katima (aliyesimama) alipotembelea baadhi ya mashamba ya wakulima ili kushuhudia uharibifu wa zao la Mahindi kwa baadhi ya mashamba yaliyopo kijiji cha Murangi. Kulia ni Abel Biswalo akiwa katika hatua ya palizi.

Na Mwandishi wetu

IDARA ya kilimo kupitia Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Musoma Godfrey Katima wamejiridhisha kuwepo kwa wadudu waharibifu wanaoshambulia zao la mahindi katika mashamba mbalimbali ya wakulima yaliyopo Musoma vijijini.

Hayo yamebainika kufuatia ziara ya afisa huyo kwenye mashamba ya mahindi na kukutana na baadhi ya wakulima kijijini Murangi katika kata ya Murangi ambapo alishuhudia kuwepo kwa tatizo hilo.

Awali akizungumza na afisa kilimo huyo, mmoja wa wakulima wa mahindi Christopher Magoti alisema, mahindi yao yameanza kupatwa na tatizo la kushambuliwa na wadudu mapema tu baada ya zao hilo kufikia katika hatua ya palizi.

Mkulima huyo alisema, wadudu hao wanashambulia zaidi majani laini yanayochipua, pamoja na kutoboa majani ya zao hilo jambo ambalo limekuwa endelevu na sasa linaonekana kuwa sugu kwani hawajapata ufumbuzi wowote wa kuweza kudhibiti tatizo hilo.

“Tukienda kwa maafisa kilimo wanatuelekeza dawa za shilingi arobaini elfu (40,000) wakati mimi hata chakula kwa siku ninashindia uji, tunaomba wakulima tusaidiwe hili, bila kusaidiwa basi hata hii mvua inayonyesha haitakuwa na faida kwetu na tutakufa na njaa kabisa” alisema na kuomba Mzee Magoti.

Mkulima mwingine Abel Biswalo alitahadharisha serikali kuwa endapo idara ya kilimo ya wilaya ya Musoma isipokuwa makini na kutimiza wajibu wake basi wilaya yao itakuwa na matukio ya njaa yasiyokoma kutokana na kupuuza majukumu yake, kwani kumekuwa na matukio ya muendelezo hasa katika sekta ya kilimo katika wilaya ya Musoma.

“Zao la muhogo lilishambuliwa, zao la viazi likavamiwa na wadudu kama ilivyo sasa kwenye mahindi na sasa mahindi nayo yamefikiwa na kama kawaida ya viongozi husika hatujajua tatizo hili litaisha lini” alibainisha Abel.

Kwa upande wake, Nyangai Ching’oro hakusita kulinganisha hali halisi iliyopo kwenye jamii zao na tatizo lililowakumba wakulima kwa sasa na kusema: “kwa kipindi kirefu jamii ya Musoma imekumbwa na tatizo la upungufu wa chakula uliosababishwa na ukame wa muda mrefu, lakini kwa sasa mvua imenyesha na wakulima wamelima kwa wingi. Tatizo kubwa lililopo ni mazao kushambuliwa na wadudu waharibifu kitu ambacho kitapelekea kuwepo na ukosefu wa chakula zaidi”

“Tumelia sana na tatizo la upungufu wa chakula kwani mvua ilikuwa hainyeshi. Mvua imenyesha, tumelima lakini mazao yanaharibiwa. Tusipokuwa makini tatizo la njaa halitokwisha na mimi naomba idara ya kilimo itimize majukumu yake kwetu wakulima ili matatizo haya yatatuliwe” alisema na kuomba Ching’oro.

Akizungumza baada ya kusikiliza vilio vya wakulima hao, Godfrey Katima aliahidi kuwasilisha taarifa ya tatizo hilo katika idara yao ya kilimo kwa ajili ya kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuokoa zao hilo huku akiwataka maafisa kilimo wa kata na vijiji kuwa karibu na wakulima kwa ajili ya msaada na ushauri zaidi.

“Poleni sana kwa tatizo hili linalowakabili. Kweli ni tatizo linalostahili hatua za haraka zaidi na mimi nitaliwasilisha kwenye idara yetu kwa ajili ya hatua zaidi. Pia niwatake maafisa kilimo wa kata na vijiji wawe karibu na wakulima na wawe tayari kutoa ushauri na msaada pale panapostahili” alisema na kuagiza Katima.

SHULE ZA MSINGI JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI KUBORESHA MAKTABA ZAKE

Untitled

Moja ya maktaba zinazopatikana kwenye shule za msingi za jimbo la Musoma vijijini ambazo zipo kwenye mkakati wa kuboreshwa.

Na Fedson Masawa

SHULE za msingi zenye maktaba katika jimbo la Musoma vijijini zimeahidi kuboresha maktaba zao ili kuziweka katika mazingira mazuri zaidi ya kujisomea watoto pamoja na wananchi wenye uhitaji wa kujisomea kutoka nje ya shule hizo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Burungu, Mkama Ng’aranga, alisema shule yake ina mpango wa kupanua maktaba hiyo ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kuingia na kujisomea.

“Shule yangu ina mpango wa kupanua maktaba hii ili kutoa fursa kwa watoto kutoka shule nyingine na wananchi wa kawaida kuingia na kujisomea bila shida yoyote. Pia utaratibu huu utakuwa ni kivutio kwa vijana wa vijijini kuja kujisomea na niombe walimu wenzangu wakilifanya hili basi tutakuwa mfano wa kuigwa” alisema Mwalimu Ng’aranga.

Akizungumzia umuhimu wa kuwepo kwa maktaba bora, Mwalimu Paschal Aloyce ambaye ni msimamizi mkuu wa taaluma shuleni hapo, alisema maktaba hiyo itatoa hamasa kwa wanafunzi wa shule hiyo kwani mazingira bora ya wanafunzi kujisomea ni njia moja wapo ya kuwa na ufaulu bora katika shule, hivyo basi kuwa na maktaba kubwa na bora ni kuongeza ufaulu bora kwa wanafunzi wao.

“Maktaba bora shuleni ndio ufaulu bora wa wanafunzi. Kuwa na maktaba bora hapa shuleni naamini kabisa vijana watajituma na hawatotumia muda wao mwingi kuzurura mitaani. Hivyo matokeo yao yatakuwa mazuri zaidi” alieleza mwalimu Aloyce.

Aidha, Magreti Trutumbi ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba shuleni hapo, ametoa shukrani zake za dhati kwa viongozi wa serikali na shule kwa kuwajengea maktaba na kujaza vitabu kwani haikuwa hali ya kawaida kwa wao kupata eneo sahihi la kujisomea na sasa wamelipata.

Kwa upande wake Filimon Elifath alishukuru kwa mchango mkubwa anaotoa Mbunge wao Prof. Muhongo ikiwa ni pamoja na vitabu, madawati, mifuko ya saruji na mabati kwa ajili ya kufanikisha mazingira bora ya taaluma yao katika shule zote za jimbo lao.

“Tunamshukuru mbunge wetu Prof. Muhongo kwa mchango wa mabati, saruji na vitabu anavyotupa. Itatusaidia katika kufaulu masomo yetu. Nasisi wanafunzi tunaahidi kufanya vizuri zaidi kwenye mtihani wetu wa mwisho” alishukuru na kuahidi Filimon.

MBUNGE ATOA MBEGU ZA MIHOGO NA MTAMA KWA WAKULIMA JIMBONI

Untitled

Wananchi wa Kata ya Nyegina wakikabidhiwa mbegu za mihogo na mtama kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uzalishaji wa mbegu hizo.

Na Mwandishi wetu.

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, ametoa mbegu za mtama na mihongo kwa wananchi wa jimbo hilo ikiwa ni hatua muhimu ya kupambana na tatizo la njaa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo la ugawaji wa mbegu lililofanyika kwenye kijiji cha Nyegina, msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Ramadhani Juma alisema, hatua hiyo ya ununuzi wa mbegu ilichukuliwa baada ya Prof. Muhongo kupokea taarifa kutoka kwa wananchi wake waliohitaji msaada wa mbegu bora za mihogo na mtama.

“Kuna baadhi ya wananchi walimuomba mheshimiwa mbegu za mihogo na baadhi wakawa wamemuomba mbegu za mtama na mihogo. Prof. Muhongo aliagiza taarifa ya mahitaji ambapo Halmashauri wakawa wanahitaji gunia 700 ambazo ziligharimu Milioni 14. Baada ya kupokea taarifa hiyo tulienda kuwalipa Magereza Kiabakari Milioni 7 awamu ya kwanza ambayo sasa imeleta magunia 350 na ndio sasa yanasambazwa” alisema Juma.

Aidha, akizungumzia mbegu za mtama, msaidizi huyo alisema mbunge alitoa Milioni 1.2 ambazo zimetumika kununulia kilo 900 za mtama ambazo zitasambazwa  kwa wakulima.

“Kuhusu mbegu za mtama, kuanzia jana nimezigawa Majita, lakini pia tuna wasiwasi kwamba hizi mbegu za mtama, tutakapokuwa tunazigawa kuna wananchi wetu wataenda kusaga unga. Kwa hiyo tupate utaratibu, zile kaya zitakazochukua mtama ziandikwe na kwa kushirikiana hata na uongozi wa kijiji, wawe wanaenda kuwatembelea ili kujiridhisha kama kweli walipanda. Kwa hiyo niwaombe tuzitumie kama mbegu ili baadaye tupate mbegu nyingi zaidi” alisema Ramadhani Juma.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyegina Majira Mchele amewataka vijana wajitokeze kushiriki kikamilifu katika kufanya shughuli za kilimo mashambani kwa ajili ya kuzalisha kwa matumizi ya baadaye siyo kuwaachia wanawake huku wao wakizurura mitaani.

“Mimi naomba vijana twendeni mashambani. Ukienda saa 12 saa 3 umetoka utaendelea na majukumu yako ili tumvushe yule mama anayeenda shambani mwenyewe. Hii mvua ni ya kukimbizana nayo, tujitume” alisisitiza diwani Mchele.

Naye Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Musoma, Paul Makuli ambaye pia ni Afisa Kilimo wa wilaya alieleza utaratibu wa mgawanyo wa mbegu hizo kuwa zitapandwa katika ekari 87.5 kwa halmashauri nzima ambapo vikundi 9, taasisi 17 na kaya 100 zitapewa mbegu.

Akizungumza na wananchi wa Nyegina katika uzinduzi huo, Vicky Mbunde ambaye ni Kaimu mkuu wa Wilaya alimpongeza Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini kwa juhudi kubwa anazozifanya ndani ya jimbo hilo huku akikemea tabia ya wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba yaliyolimwa.

“Wale ambao mnafuga mifugo hakikisheni mifugo yenu mnaitengea maeneo ambayo hayajalimwa ili angalau tunayoyafanya hapa yaonekane yana faida, atakayekiuka utaratibu huu, basi sheria ichukue mkondo wake dhidi yao” alisema.

Pia Kaimu mkuu wa wilaya ametoa onyo kali kwa vijana wanaojihusisha na matendo ya ulevi huku wakishindwa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na kuwataka kila mmoja ashiriki kikamilifu katika uzalishaji.

“Najua mtu hawezi kwenda kulima akiwa ametumia dawa za kulevya au ametumia kilevi chochote, najua sasa hivi serikali inapambana vikali katika kudhibiti dawa za kulevya. Sasa wenye vilabu, vilabu vyote fungua kuanzia saa 9:30 jioni. Ukifungua kuanzia saa 4 au saa 5 asubuhi, mtendaji wa kata inabidi uwakamate na uwapeleke kwenye baraza la kata mara moja” alisema Vicky.

Akihitimisha zoezi la ugawaji wa mbegu hizo, Kaimu mkuu huyo wa wilaya amewasihi wananchi kushiriki kikamilifu kila mmoja na kila kaya kuwa na shamba lililolimwa na kupandwa.

“Ukaguzi utakuja kufanyika, kila kaya moja lazima iwe na zao la chakula, aidha ulime mtama ekari moja, ulime mahindi, viazi au mihogo. Tutafanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba, tutakuwa na mwenyekiti wa kijiji, mwenyekiti wa kitongoji ili kubaini kila kaya na shamba lake na tujitahidi sana kulima mazao yanayostahimili ukame na madiwani na viongozi wengine mtusaidie kuhamasisha” alisema Vicky Mbunde.

 

MKUU WA WILAYA AFUNGA RASMI MAFUNZO YA UTENGENEZAJI VIFAA VYA UMEME JUA

Untitled

Vijana waliohitimu mafunzo ya kutengeneza chaja za simu na taa kwa kutumia mionzi ya jua wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa kufunga mafunzo hayo katika kituo cha Nyegina. Waliosimama nyuma ni Dkt. Hong-kyu Choi (aliyevaa fulana nyekundu), anayefuatia kuelekea kulia ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney. Kushoto kutoka kwa Dkt. Choi ni Majira Mchele diwani wa kata ya Nyegina.

 

Na Fedson Masawa

MAFUNZO ya kutengeneza chaja za simu na taa zinazotumia mionzi ya jua yamefungwa rasmi huku vijana 97 wakihitimu mafunzo hayo ya siku 20.

Mafunzo hayo yamefungwa na Mkuu wa wilaya ya Musoma vijijini Dkt.Vincent Naano Anney katika kata ya Nyegina, ambapo yalitarajiwa kushirikisha vijana 100 kutoka jimbo la Musoma vijijini, lakini ni vijana 97 pekee wamehitimu baada ya vijana watatu kushindwa kushiriki kwa kutoa hudhuru.

Mbali na vijana hao,  viongozi mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa kijiji cha Nyegina, Diwani wa kata ya Nyegina nao walipata fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Dkt. Hong-kyu Choi kutoka Korea.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Nyafuru Magere kutoka kijiji cha Nyasulura alisema, ingependeza zaidi kama watajengewa kiwanda ili ujuzi walioupata kwa ajili ya uzalishaji na kujiajiri wenyewe.

“Mimi nampongeza Waziri na mbunge wetu Prof. Muhongo kwa kutuletea mafunzo haya, tumepata ujuzi wa kutosha na sasa tulikuwa tunaomba watujengee kiwanda ili tujiajiri. Vilevile napenda kuwasihi vijana wenzangu ambao hawajashiriki mafunzo haya, wasitegemee ajira kutoka serikalini, ajira ni wao wenyewe na ujasiliamali tunaoufanya ni ajira tosha” alisema Nyafuru na kuwasihi vijana wenzake wasipuuze fursa za kujiajiri.

Naye diwani wa kata ya Nyegina, Majira Mchele alimshukuru Dkt. Hong-kyu choi kwa kutumia muda wake mwingi kuwafundisha vijana wa Tanzania na Musoma vijijini na kumpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa na uhusiano mzuri na Dkt. Choi na ubalozi wa Korea kwani ndiye aliyefanya vijana hao kuelekea kutimiza ndoto zao.

“Namshukuru sana Dokta Choi kwa kutumia muda wake, yeye ni mtu wa Korea, lakini ameamua kuugawa muda wake kwa ajili ya kuja kuwasaidia watanzania. Nimshukuru pia mheshimiwa mbunge kwa kufanya urafiki na Dokta mpaka akaibua hiki tunachokuja kukivuna. Bila Prof. Muhongo Dokta asingeijua Tanzania, wala Musoma vijijini na wala elimu hiyo msinge ipata” alisema diwani Majura.

Kwa upande wake Dkt. Hong-kyu alisema, vifaa anavyofundisha na kuvitengeneza ni muhimu na ni rahisi mno, hivyo vitawasaidia vijana kutengeneza ajira, kutoa elimu na kuboresha maisha ya watu na hatimaye vijana kufikia ndoto na matarajio yao ya usoni.

Aidha, Dkt. Choi alimshukuru Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwani alipokutana naye kwa mara ya kwanza ofisini kwake akiwa na vifaa hivyo, mbunge huyo alivutiwa navyo na kumuomba  akawafundishe vijana wake 100 jimboni.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney, aliwashukuru  wasaidizi wa Mbunge kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuwaunganisha wananchi ndani ya jimbo hilo na hivyo kuharakisha maendeleo.

“Kwanza nawashukuru sana wasaidizi wa mbunge kwa kuweza kuwaunganisha wananchi wa Musoma. Hii ni kwa sababu nimejifunza kitu kutoka kwa Prof. Muhongo kwa kuweka watu wake katika maeneo yote ndani ya jimbo, nikimaanisha Nyegina, Mugango, Murangi, Saragana na Busekera. Hii inaleta mpangilio mzuri sana. Nawashukuruni sana” alisema Dkt. Naano.

Aidha, akizungumzia mafunzo hayo, Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka vijana hao kutumia ujuzi walioupata kujitanua kifkra na kujiona kuwa wana uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi iwapo watakabidhiwa vifaa vya kufanyia kazi na kusambaza elimu kwa vijana wenzao.

Dkt. Naano pia alipendekeza uundwaji wa vikundi vinavyotambulika kwa ajili ya kujiweka katika hatua nzuri ya kupata misaada kutoka serikalini ikiwemo Halmashauri ya Musoma.

“Maarifa na ujuzi mlioupata wa kutengeneza hizi sola ndogo, sasa mna uwezo wa kutengeneza sola kubwa endapo mkipata vifaa. Pia nawaomba mjitahidi haya maarifa muwafundishe na wengine na mkitoka hapa mkaunde vikundi na vikundi hivi tutavifadhili kwa fedha za mfuko wetu wa halmashauri”

Mkuu wa wilaya Dkt. Vincent Naano Anney  alimalizia kwa kumshukuru Dkt. Choi pamoja na ubalozi wa Korea kwa kufanikisha kazi nzuri aliyoifanya katika jimbo la Musoma vijijini na kuahidi kuwaweka vijana katika makundi na kumthibitishia mkufunzi huyo kuwa, serikali inajipanga kupitia ubalozi wa Korea nchini ili kuhakikisha vifaa vinapatikana kwa urahisi kwa ajili ya kuwaendeleza vijana nchini.

 

VIJANA 20 WAHITIMU MAFUNZO KITUO CHA BUKIMA, WAAHIDI KUWA WALIMU WAZURI

Untitled

Vijana walioshiriki mafunzo ya kutengeneza taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua.

Na Ramadhani Juma

VIJANA 20 kutoka kata 6 za jimbo la Musoma vijijini walioshiriki mafunzo ya kutengeneza taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua, wamehitimu mafunzo yao katika kituo cha Bukima.

Mafunzo hayo yaliyowashirikisha vijana kutoka kata ya Rusoli, Bukima, Makojo, Bulinga, Bwasi na Bukumi yamehitimishwa rasmi 4, Machi mwaka huu katika ukumbi wa ofisi ya kata Bukima.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, vijana hao wameshukuru kupewa fursa hiyo muhimu ya kushiriki mafunzo hayo na kuahidi kuwa hawatowaangusha viongozi waliowateua na wananchi waliofanikisha uteuzi wao kwa kuhakikisha kilichofundishwa kitawasaidia kuwa walimu wa vijana wengine.

“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa viongozi na wananchi waliofanikisha kutupata, elimu na ujuzi tulioupata hapa ni njia bora ya kuwafundisha hata vijana wengine zaidi” alishukuru Anthony Zephania, mmoja wa vijana hao.

Kwa upande wake Ester Aloys alisema, Dkt. Choi amefungua njia nzuri kwao vijana kujiajiri bila kutegemea ajira kutoka serikalini kama ambavyo imezoeleka kwa vijana wengi.

“Dokta Choi umetuonesha njia nzuri, tumejifunza mengi ambayo mwanzo hatukuyajua na ametupatia ujuzi wa kudumu na sasa tunaweza kujiajiri na siyo kutegemea kuajiriwa tena. Vilevile endapo tutapata uwezesho kidogo wa vifaa, tutakuwa tumeisaidia sana jamii yetu ya kipato cha chini” alisema Ester.

Akizungumza wakati wa kuagana na wanafunzi wake Dkt. Hong-kyu Choi amewaambia kuwa, hana shaka na wao anaamini ipo siku watakutana tena Musoma vijijini na kuwasimika rasmi vijana wake na kuanza shughuli za uzalishaji zaidi kwani tayari wamejifunza na kuelewa nini kinatakiwa kifanyike.

Hata hivyo, Dkt. Choi aliongezea kuwa, haoni ugumu wa yeye kuagiza vifaa vya kutengenezea kutoka Korea kuja Tanzania endapo vijana hao wakiwa tayari na serikali ikawaunga mkono.

JIMBO LA MUSOMA VIJIJINI – KILIMO CHA MTAMA NA MUHOGO

Mvua zinanyesha na wanavijiji wameomba mbegu za mazao ya chakula. Mbunge amekubali kuchangia upatikanaji wa mbegu hizo: (1) Mbegu za Mihogo za Sh Milioni 7 (saba) kutoka Magereza Kiabakari (Awamu I) na (2) Magunia 10 ya mtama (mbegu) ya Sh Milioni 1.2. Halmashauri itachangia usafiri na mengineyo.
Ofisi ya Mbunge

VIJANA WA MUSOMA VIJIJINI WAAHIDI KUJIAJIRI BAADA YA MAFUNZO

Vijana wa jimbo la Musoma vijijini wakiendelea na mafunzo ya kutengeneza taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua, pichani wanaonekana wakiwa katika hatua ya uunganishaji wa mfumo wa betri, taa na seli za sola katika kituo cha Murangi.

Vijana wa jimbo la Musoma vijijini wakiendelea na mafunzo ya kutengeneza taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua, pichani wanaonekana wakiwa katika hatua ya uunganishaji wa mfumo wa betri, taa na seli za sola katika kituo cha Murangi.

Na Fedson Masawa

VIJANA wanaopata mafunzo ya utengenezaji wa taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua katika kituo cha Murangi, wameahidi kujiajiri baada ya kumaliza mafunzo yao.

Wakingumza na mwandishi wa habari hizi, vijana hao wamempongeza mkufunzi wa mafunzo hayo Dkt. Hong-kyu Choi kutokana na jinsi anavyowafundisha na kuelewa.

Awali, akizungumza na wasimamizi wa mafunzo hayo, Ester Charles kijana kutoka kijiji cha Ryasembe kata ya Murangi, alisema anatarajia kutoka na ujuzi ambao utamsaidia kujiajiri na si kutegemea kuajiriwa tena.

“Ninafurahi sana kushiriki mafunzo haya, na kwa namna tunavyoendelea naamini binafsi ninatarajia kutoka hapa na ujuzi utakaoniwezesha kutengeneza ajira binafsi, siyo kutegemea kuajiriwa na mtu” alisema Ester.

Naye, Mugenyanda Mbasa kijana kutoka kata ya Rusoli, alimshukuru Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa kuwaona vijana wake jimboni na kuwatengenezea fursa zinazowapelekea kujiajiri na hivyo ujuzi watakaoupata katika mafunzo hayo utakuwa ni taa bora itakayowasaidia kumulika maisha yao yajayo.

“Binafsi nimshukuru sana mbunge wetu wa jimbo la Musoma vijijini kwa namna alivyotupa fursa tunayoweza kutumia na kuleta mabadiliko jimboni. Pia mafunzo aliyoyaanzisha ni taa itakayotusaidia kumulika maisha yetu ya usoni” alishukuru Mbasa.

Kijana mwingine Elisha Morice, kwa upande wake aliwahimiza vijana wenzake wanaoendelea na mafunzo, waliokwisha kamilisha na wale ambao hawajaanza mafunzo kuwa mwisho wa mafunzo hayo uwe ni mwanzo wa kueneza na kusambaza ujuzi huo kwa vijana wenzao ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo ili kupunguza utegemezi na uzururaji kwa vijana wa Musoma vijijini.

“Ndugu zangu, mimi napenda pia kuwahimiza vijana wote tunaoendelea na mafunzo, waliokwisha hitimu na wale ambao hawajaanza kwamba, mwisho wa mafunzo haya uwe ni mwanzo wa mafunzo kwa vijana wenzetu ambao hawakubahatika kushiriki mafunzo haya ili kuondokana na utegemezi na uzururaji” alisema kijana Elisha, anayetoka kijiji cha Chumwi.

Naye, Mkufunzi wa mafunzo hayo Dkt. Hong-kyu Choi kutoka Korea, amewasihi vijana kuwa wepesi wa kubadili mtazamo wao, fikra na kujiamini kwa kujali kile anachowafundisha kwani Prof. Muhongo ambaye ni mtu pekee aliyewafanya wafike jimboni hapo na Tanzania kwa ujumla ana nia njema na jamii yake na anaweza kuwasaidia na kuwainua vijana endapo wakiwa tayari kubadilika ili kuondokana na umaskini kwa kujitengenezea ajira binafsi.

MBUNGE WA MUSOMA VIJIJINI AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA MADARASA

 

Mbunge wa Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyeusi) akishirikiana na wananchi wa kijiji cha Kome kwenye ujenzi unaoendelea wa vyumba 10 vya Madarasa. Mbali na kushiriki ujenzi huo, Prof. Muhongo alitoa msaada wa mifuko na bati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo.

Mbunge wa Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyeusi) akishirikiana na wananchi wa kijiji cha Kome kwenye ujenzi unaoendelea wa vyumba 10 vya Madarasa. Mbali na kushiriki ujenzi huo, Prof. Muhongo alitoa msaada wa mifuko na bati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo.

Na Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Muhongo amekagua maendeleo ya ujenzi katika shule ya msingi Kome “B” iliyopo kijiji cha Kome kata ya Bwasi.

Akizungumza shuleni hapo, Prof. Muhongo alisema ameridhishwa na hatua nzuri iliyofikiwa na wananchi wa kijiji cha Kome, kwa kuweza kujenga jumla ya vyumba sita vya madarasa hadi usawa wa lenta huku malengo yakiwa ni kujenga vyumba 10.

“Tukitaka kufanikiwa lazima twende kwa mpango. Hatuwezi kuwa na maendeleo wakati tunakuwa na mipango ya kwenda na kurudi, kwenda na kurudi nyuma” alisisitiza Prof. Muhongo.

Aidha Prof. Muhongo amewathibitishia wananchi kuwa, mifuko mingine ya saruji itawasili Musoma baada ya wiki mbili na kuwasisitiza viongozi na wananchi kujituma kuhakikisha saruji hiyo ikifika inatumika haraka iwezekanavyo, tofauti na hivyo mifuko itahamishwa na kupelekwa kwingine.

“Baada ya wiki mbili nitatoa mifuko mingine ya saruji na mkipewa saruji au mabati, msipovifanyia kazi vitahamishwa” alisisitiza Prof. Muhongo.

Akizungumzia suala la umeme na kilimo cha umwagiliaji kama lilivyo wasilishwa na wananchi wa kijiji cha Kome, Prof. Muhongo amewaondoa wasiwasi na kusema watapata umeme wa kutosha kwa kuwa bado hatua ya kusambaza umeme vijijini inaendelea.

“Ndugu zangu kuhusu umeme msiwe na wasiwasi, umeme unakuja wa kutosha na suala la umeme tunaenda awamu kwa awamu, ndani ya miaka mitano vijiji vyote vya Tanzania vitakuwa vimenufaika na umeme” alisema Prof. Muhongo.

Kuhusu suala la kilimo, Prof. Muhongo amekiri kuwepo na ukame jimboni na maeneo mengine na kuona umuhimu wa kutumia kilimo cha umwagiliaji kwa jamii zote zinazoishi kando kando mwa ziwa ambapo amemuagiza Mwenyekiti wa halmashauri na madiwani wote kulijadili na kuona namna ya kuzisaidia jamii hizo ili kuondokana na tatizo la njaa kuliko kutegemea msimu wa mvua pekee.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Charles Magoma, amemthibitishia Prof. Muhongo kuwa suala la ujenzi wa vyumba vya madarasa wataendelea kulisimamia na kufuatilia matumizi sahihi ya vifaa hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa wakati.

Magoma ameahidi kuwasilisha hoja ya ununuzi wa mashine kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa jamii zinazoishi kandokando mwa ziwa Viktoria ili waweze kujinusuru na tatizo la njaa.

“Ndugu mheshimiwa, mimi naamini yote uliyoyazungumza tutayafanyia kazi, vifaa vya ujenzi tutaendelea kuvifuatilia na suala la mashine tutalijadili kwenye vikao vyetu vya mipango na fedha ndani ya siku mbili zijazo” alisema Magoma.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bwasi, Masatu Nyaonge, amemshukuru Prof. Muhongo kwa kuweza kufika kijijini hapo ili kujionea kazi nzuri inayofanywa na wananchi wake na kumhakikishia kuwa pamoja na wananchi wake kukumbwa na tatizo la njaa, lakini bado hawajakata tamaa ya kufanya maendeleo na bado wana uhitaji wa vifaa vya ujenzi kijijini hapo.

PROF. MUHONGO AZINDUA MAFUNZO YA KUTENGENEZA TAA, CHAJA KWA KUTUMIA MIONZI YA JUA

Na Ramadhan Juma

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amezindua mafunzo ya utengenezaji wa taa na chaja za simu zinazotumia mionzi ya jua.

Mafunzo hayo yanayofanyika kwenye kijiji cha Nyegina, yanawahusisha vijana 100 kutoka vijiji mbalimbali vya jimbo hilo, yana lengo la kutengeneza ujuzi na ajira kwa vijana hao.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Prof. Muhongo alisema mafunzo hayo mbali na kuzinduliwa Nyegina, yatafanyika kwenye kijiji cha Mugango, Bukima, Busekera na Saragana ambapo kila kituo kitakuwa na vijana 20 na mafunzo yatatolewa kwa siku tatu kwa kila kituo.

Prof. Muhongo alisema, baada ya mafunzo katika vituo hivyo vitano, vituo hivyo vitavunjwa na kuunda vituo viwili, kituo cha kwanza kitakuwa Nyegina na kingine kitakuwa Murangi ambapo kila kituo kitakuwa na vijana 50 kwa ajili ya kuwafanyia mazoezi ya mwisho.

Akizungumzia soko la vifaa hivyo, Prof. Muhongo alisema, baada ya vifaa hivyo kutengenezwa, vijana hao watakuwa wanaviuza kati ya 15,000 hadi 20,000 ambapo malighafi za kutengenezea vifaa hivyo watapelekewa, hivyo amewataka vijana jimboni humo kuchangamkia fursa hiyo.

Awali, Balozi wa Korea nchini Tanzania Song Geumyoung alisema, Korea itaendelea kudumisha uhusiano wao na Tanzania na sasa takribani miaka 20 toka mataifa haya yaingie katika uhusiano wao, bado wataendelea kudumisha uhusiano huo.

Aidha, Balozi Geumyoung alisema, vifaa hivyo vitasaidia kupunguza tatizo la umeme vijijini na hata mijini hususani kwa wale wasio na uwezo wa kupata umeme na kutoa ajira kwa vijana wengi.

“Miaka 20 ya uhusiano wa Korea na Tanzania, tutaendelea kudumisha uhusiano huu na tutasaidiana na Tanzania kusambaza umeme vijijini. Vilevile vifaa hivi vitawasaidia vijana hawa kujitengenezea ajira na pia vitasaidia wanafunzi kujisomea wakati wa usiku” alisema Balozi Geumyoung.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya Musoma Vincent Naano Anney, ameishukuru serikali ya Korea kwa hatua nzuri ya kuanzisha teknolojia ya utengenezaji wa taa na chaja zinazotumia mionzi ya jua kwani ni hatua pekee ya kuondoa utegemezi na umasikini kwa vijana wa Musoma na pia kuwaomba kuendelea na jitihada hizo ili kusaidia jimbo la Musoma vijijini na Tanzania kwa ujumla.

Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Dkt. Choi Hong Kyu, alisema hatua ya kwanza ya mafunzo hayo ni kuwajengea vijana hao uwezo wa kujiamini na kisha watafundishwa ujuzi wa utengenezaji wa vifaa hivyo.

“Tunataka kuwatengenezea vijana ajira binafsi na hatimaye kuacha utegemezi na kuondokana na shughuli nyingine zisizo halali. Hivyo nawaomba waonyeshe ushirikiano wa hali ya juu katika kupokea kile watakachofundishwa” alisema Dkt. Choi Hong Kyu.

WANANCHI KIJIJI CHA KIEMBA WAENDELEA KUJENGA MAKAZI MAPYA

 

Kiemba 1

 

Na. Juma Shabani

WANANCHI wa kijiji cha Kiemba kata ya Ifulifu, wanaendelea na ujenzi wa nyumba mpya baada ya zile za awali kubomolewa na upepo mkali uliokikumba kijiji hicho miezi michache iliyopita.

Wananchi hao walianza ujenzi huo baada ya kupokea vifaa mbalimbali kutoka kwa mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo ambaye aliahidi kutoa msaada huo alipotembelea kijijini hapo mwishoni mwaka jana.

Wakizungumza kijijini hapo, wananchi hao walimshukuru mbunge wao kwa kuwasaidia na kuwaondoa kwenye mazingira magumu waliyokuwa nayo baada ya nyumba zao kubomoka na nyingine kuezuliwa mabati na upepo mkali uliombatana na mvua kubwa.

“Nilikuwa na hali mbaya baada ya nyumba yangu kubomoka yote na kuishia chini na vyombo vyangu vya ndani kuharibika kabisa, nikakosa mahala pa kujihifadhi, nikawa naomba kwa majirani leo hapa kesho pale, lakini baada ya mbunge wetu kupata taarifa hizo kupitia kwa wasaidizi wake, aliweza kufika sehemu ya tukio na kujionea kilichotokea na kutuhaidi vifaa vya ujenzi siku hiyo hiyo nilipokea vifaa vya ujenzi ikiwa ni mabati, saruji na misumari” alisema Nyakaita Magati.

Magati aliendelea kusema: “hivi sasa nyumba imefikia kwenye hatua ya renta, naelekea kukamilisha nyumba yangu, kwa kweli tunamuomba mbunge wetu aendelee na moyo huo huo na Mungu ambariki sana pamoja na wasaidizi wake”

Naye, Tatu Richard alithibitisha kupokea vifaa vya ujenzi kutoka kwa mbunge na sasa nyumba yake imekamilika, jambo ambalo awali hakuamini kama lingewezekana.

“Jamani mimi mjane sijui ningefanyaje, niliona maisha yangu sasa yamekuwa magumu kupitiliza baada ya nyumba yangu kuezuliwa paa lote na kutupwa pembeni, sikuwa na mtu wa kunipa msaada kabisa, lakini Mungu sio Athumani, nilishangaa baada ya kuona watu wengi sana wakija kwangu na nikamuona mbunge wetu akiwa amefika kwangu kunipa pole na kunikabidhi vifaa vya ujenzi” alisema Tatu.

Mwandishi wa habari hizi alizungumza na wananchi wengine ambao aliwakuta kwenye maeneo yao wakiendelea na ujenzi wa makazi yao mapya na kurekebisha nyumba zilizopata nyufa, ambapo wamesema zoezi hilo litakamilika ndani ya mwezi mmoja na nusu.

VIJANA 100 KUPATA MAFUNZO YA KUTENGENEZA VIFAA VYA UMEME JUA

Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kulia) akionesha vifaa vya umeme jua ambavyo Balozi wa Korea nchini anatarajiwa kupeleka mtaalamu jimboni humo ili kuwafundisha vijana namna ya utengenezwaji wake.

Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kulia) akionesha vifaa vya umeme jua ambavyo Balozi wa Korea nchini anatarajiwa kupeleka mtaalamu jimboni humo ili kuwafundisha vijana namna ya utengenezwaji wake.

Na. Mwandishi Wetu

UBALOZI wa Korea Kusini nchini, unatarajia kutimiza ahadi yake iliyotolewa na balozi Song, Geum-Young kuwapatia mafunzo yatakayozalisha ajira vijana wa Musoma vijijini waliohitimu Kidato cha Nne.

Balozi Song, Geum-Young alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa mwaka jana, ambapo aliahidi kumpeleka jimboni humo mtaalamu kwa ajili ya kuwafundisha vijana namna ya kutengeneza taa na chaja ndogo kwa ajili ya kuchaji simu zinazotumia mionzi ya jua.

Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini, Prof. Sospeter Muhongo kupitia taarifa yake, alisema Dk. Hong K Choi kwa kushirikiana na Ubalozi wa Korea Kusini watatoa mafunzo hayo kwa vijana 100 kutoka jimboni mwake.

Prof. Muhongo alisema, vijana watakaopata nafasi hiyo ni wale waliomaliza kidato cha nne na wanaoishi kwenye vijiji vya jimbo hilo.

“Mafunzo yaanza tarehe 20 Feb 2017, Kijijini Nyegina. Wasaidizi wa Mbunge na Madiwani watachagua vijana watakaohudhuria mafunzo hayo” alisema Prof. Muhongo na kuongeza kuwa, kifaa hicho kikitengenezwa gharama yake ni 15,000, hivyo vijana watapewa mafunzo ya namna ya kuvitengeneza na watauza ili kujipatia kipato.

SHULE YA MSINGI KURUKEREGE WAPOKEA MIFUKO 180 YA SARUJI

Untitled

Diwani wa Nyegina Majira Mchele (kushoto) akiwa na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kurukerege Justine Masige, baada ya kupokea mifuko 180 ya saruji  kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Na Juma Shabani

WANANCHI wa kijiji cha Kurukerege wamepata matumaini ya kukabiliana na tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa, baada ya kupokea mifuko 180 ya saruji kutoka kwa mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo.

Mmoja wananchi wa kijiji hicho Justine Bugingo, akizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, alimshukuru mbunge huyo kwa kuona changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa na kuitafutia ufumbuzi.

“Tumekuwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule yetu, ila sasa kwa juhudi za mbunge wetu ametufanya kuwa miongoni mwa watu ambao sasa tunaona mwanga mkubwa wa maendeleo jimboni kwetu” alisema Bugingo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kurukerege Justine Masige alisema: “mimi na walimu wenzangu wote tutahakikisha tunasimamia suala la ujenzi wa vyumba vya madarasa, watoto wetu wameteseka kwa muda mrefu sana kwa kusomea nje na kusababisha kiwango cha elimu kushuka kutokana na mazingira na hali ya hewa mfano jua, mvua na upepo”

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nyegina, Majira Mchele alithibitisha kupokea mifuko 180 ya saruji ndani ya kata yake na kumshukuru Prof. Muhongo kwa hatua hiyo inayoonyesha wazi nia yake ya kutatua tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari ndani ya jimbo hilo.

“Shukrani nyingi sana zimfikie mheshimiwa mbunge, hii ni heshima kubwa sana anayotufanyia ndani ya kata, ninachoweza kusema ni kwamba, hakuna kitakacho haribika, nitahakikisha na nitasimamia vyema kabisa ujenzi wa vyumba vya madarasa yaliyo bora kabisa” alisema diwani huyo na kuongeza kuwa, atahakikisha saruji hiyo inafanya kazi iliyokusudiwa haraka.

MIFUKO 2,560 YA SARUJI YAWASILI MUSOMA VIJIJINI, YAANZA KUSAMBAZWA

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chumwi Lucia Mjengwa (kushoto) akiwa na wanafunzi wake Mfungo Manyama (katikati) na Mafwiri Yohana muda mfupi baada ya kupokea saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa shuleni kwao.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chumwi Lucia Mjengwa (kushoto) akiwa na wanafunzi wake Mfungo Manyama (katikati) na Mafwiri Yohana muda mfupi baada ya kupokea saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa shuleni kwao.

Na Fedson Masawa

MIFUKO 2,560 ya saruji iliyotolewa na Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo imewasili jimboni humo na kupokelewa na wasaidizi wa mbunge.

Saruji hiyo ilianza kuwasili kuanzia 13, January, 2017  imeanza kusambazwa kwenye shule mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule mbalimbali za msingi na sekondari Musoma vijijini ikiwa ni mkakati maalumu wa mbunge wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa jimboni mwake.

Wakati huo huo Verediana Mgoma anaripoti kuwa, shule ya msingi Chumwi imepokea mifuko ya saruji 120 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule hiyo yenye upungufu wa vyumba 13.

Mwalimu mkuu wa shule ya Chumwi, Lucia Mjengwa mara baada ya kupokea mifuko hiyo, alimshukuru mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo kwa kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu.

“Tunamshukuru sana mbunge, mpaka sasa tatizo la madawati limekwisha, lakini tuna changamoto kubwa ya upungufu wa vyumba vya madarasa, mpaka sasa shule imegawanywa kutokana na wingi wa wanafunzi, hivyo mahitaji ya vyumba ni 23 vilivyopo ni 10 na upungufu ni 13, kwahiyo tutaitumia saruji hii vizuri na kuanza ujenzi” alisema mwalimu Lucia.

Kwa upande wake mwanafunzi Mafwiri Yohana, alimshukuru mbunge kwa msaada huo ambao utawasaidia kutatua changamoto za vyumba vya madarasa.

“Sasahivi kutokana na uhaba wa madarasa, wakati mwingine tunalazimika kusomea nje na muda mwingine hali ya hewa inapobadilika, inatulazimu kubadilishana muda wa masomo, hivyo endapo changamoto ya vyumba ikipungua tutakuwa huru darasani na kusoma tufike mbali zaidi” alisema mwanafunzi huyo.

Mwenyekiti wa kijiji cha chumwi Mafwele Mkama, akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema, wamejipanga kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ushirikiano uliopo kati uongozi na wananchi.

“Mimi kama mdhamini mkuu katika kijiji hiki, nitakuwa bega kwa bega na wananchi wangu kumuunga mkono mbunge na kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi katika suala la taaluma” alisema mwenyekiti Mkama.

Hadi sasa, miongoni mwa shule zilizopo kata ya Nyamrandirira zilizopokea msaada wa saruji awamu ya kwanza ni pamoja na Rwanga, Nyamrandirira, Chumwi A na B ikiwa jumla ya mifuko ya saruji 240.

KIKUNDI CHA MWANGA WAVUNA MAZAO YAO, WAJIANDAA KUINGIA SOKONI

Untitled

Baadhi ya wakulima wa bustani ya Mwanga (wenye ndoo) wakionyesha mavuno yao kwa viongozi wa TANESCO na Msaidizi wa Mbunge (Mugango) walipotembelea wakulima hao wakati wakiendelea na ziara ya kuchukua takwimu za mahitaji ya umeme kwenye kata ya Nyambono.

 

 

Na. Hamisa Gamba

KIKUNDI cha vijana wanaojishughulisha na kilimo cha bustani kwenye kijiji cha Saragana, wamekamilisha msimu wa kilimo kwa kuvuna nyanya na vitunguu walivyopanda.

Kikundi hicho cha Mwanga (Mwanga Farmers), ni moja ya vikundi vilivyopata mbegu bora na mashine za kumwagilia kutoka kwa mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Amos Bwire akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema, licha ya mafanikio ya mavuno hayo bado wana changamoto ya ukosefu wa madawa ya kukidhi mahitaji ya mazao.

“Kuna changamoto mbalimbali zinatukabili licha ya mavuno tuliyopata, kubwa ni ukosefu wa madawa kwa ajili ya kuulia wadudu, lakini pia kushuka kwa bei ya nyanya na hali ya hewa kumetuathiri kwenye msimu huu” alisema mwenyekiti Bwire.

Naye mjumbe wa kikundi hicho Magesa Mauna alisema, licha ya changamoto walizokutana nazo kwenye kilimo hicho, bado wataendelea kulima bila kuchoka ili kuunga mkono jitihada za mbunge wa jimbo hilo aliyewahamasisha kuingia kwenye kilimo cha bustani kwa njia ya umwagiliaji.

“Tunaamini mbunge ana nia njema na sisi wakulima wa bustani, hivyo tunaomba pale tutakapokuwa tumekwama katika shughuli zetu za kilimo, aendelee kutuunga mkono kama kauli mbiu yake isemavyo hakuna kushindwa, hakuna kukata tamaa kwani kilimo ni uchumi”  alisema Magesa Mauna huku akinukuu kauli ya Prof. Muhongo.

SHULE ZILIZOJENGA MAKTABA ZAPEWA ZAWADI YA KRISMASI NA MWAKA MPYA

Na. Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini na waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amegawa vitabu kwa shule sita za sekondari na shule 24 za msingi zenye maktaba ikiwa ni zawadi ya Krismasi na mwaka mpya.

Awali kabla ya kuanza zoezi hilo lililofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Etaro, Prof. Muhongo alisema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa maktaba kwa shule zote za sekondari na msingi, hivyo alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma kukutana na madiwani wake ili kuhakikisha vitabu vya awamu inayofuata shule zote ziwe zina maktaba.

“Mimi kwenye suala la vitabu nitazidi kuleta, ikiwa sisi hatuna maktaba, hawa ni watoto wa watanzania wote, nitawapatia watu wengine wavipeleke maeneo mengine” alisema Prof. Muhongo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma na diwani wa kata ya Mugango, Charles Magoma, alikiri kuwepo na mapungufu katika safu ya ufuatiliaji wa ujenzi wa maktaba kwani shule nyingi jimboni hazina maktaba.

“Ni kweli ni aibu kwetu mheshimiwa, kati ya shule 20 za sekondari tunapata shule sita  zenye maktaba na kati ya shule 111 za msingi tunapata shule 24 ambazo zina maktaba. Kwa kweli ni aibu na ni kazi ngumu tuliyonayo sasa. Sasa waheshimiwa madiwani, nadhani hili tulione kuwa ni changamoto kwetu sisi ndio wahamasishaji wa shuguli za maendeleo” alisema Magoma..

Magoma aliendelea kusema: “Mheshimiwa nimeshaamua kufanya kazi, na hili tumeshaliona kwenye halmashauri yetu, tutajitahidi ili tukuunge mkono kama ulivyoamua kulihudumia jimbo lako. Mheshimiwa tukuombe radhi, tunaenda kujipanga”