MUSOMA VIJIJINI WAWEKA WAZI MATUMIZI YA FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO

moja

Katibu wa Mfuko wa Jimbo la Musoma Vijijini na Afisa Mipango wa Wilaya ya Musoma, Mukama Rugina (aliyesimama) akizungumza wakati wa mkutano wa kujadili matumizi ya fedha za mfuko huo.

Na. Mwandishi Wetu

WAJUMBE wa Kamati ya Mfuko wa Jimbo la Musoma Vijijini wameagizwa kuhakikisha wanakagua utekelezaji wa miradi ya kilimo ya vikundi vilivyokabidhiwa vifaa kutoka kwenye mfuko huo ili kujiridhisha.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati husika wakati wa mkutano wa hadhara wa kuainisha matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo kwa Awamu ya Pili uliofanyika katika kijiji cha Tegeruka, Musoma Vijijini.

Ilielezwa kwamba Awamu ya kwanza ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya Mfuko wa Jimbo hilo ni shilingi milioni 70,820,000 ambazo zilitumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo shilingi milioni 20,000,000 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Murangi.

Fedha nyingine ni milioni 27,500,000 ambazo zilitumika kwa ajili ya kurekebisha nyumba na madarasa yaliyokuwa yameezuliwa na upepo kwa shule mbili za msingi, milioni 22,500,000 ilitumika kununulia mashine za umwagiliaji, mbegu za mbogamboga na matunda pamoja na dawa za kilimo na shilingi 820,000 zilitengwa kwa ajili ya kuwezesha ufuatiliaji.

Profesa Muhongo alisema ni jukumu la Kamati husika kuhakikisha fedha imetumika kwa matumizi yaliyokubaliwa na aliagiza vikundi vyenye miradi ya kilimo ambayo haijaanza vinyang’anywe vifaa vilivyokabidhiwa na vipewe vikundi vingine vyenye vyenye nia dhabiti ya kuendeleza kilomo.

“Tembeleeni hivi vikundi, mkikuta havijaanza kutumia vifaa tulivyowapatia mvinyanga’anye na vifaa hivyo vigawiwe kwenye vikundi vyenye nia ya dhati,” aliagiza Profesa Muhongo.

Akizungumzia Awamu ya Pili ya Mfuko wa Jimbo, Profesa Muhongo alisema Mfuko wa Jimbo umepokea kiasi cha shilingi milioni 38,479,000 ambazo alisema Kamati husika kwa kushirikiana na wananchi pamoja na madiwani wamependekeza zitumike kwa ajili ya kuboresha kilimo.

Alisema shilingi milioni 16,000,000 zitatumika kwa ajili ya kununulia mbegu za kisasa za mihogo za mkombozi kiasi cha vipando 532,000 ambazo zitagawiwa kwenye Kata 21 kwa ajili ya vijiji 68, na shilingi milioni 21,900,000 itatumika kununulia mashine 21 za kukamulia alizeti.

Aliongeza kuwa hapo awali alisambaza mbegu za alizeti za majaribio kiasi cha kilo 4000 ambazo alisema zimeonesha mafanikio na hivyo aliongeza mbegu zilizoboreshwa kutoka Arusha kiasi cha kilo 5000 ambazo pia zilisambazwa.

Alisema ili kujiongezea kipato kutokana na kilimo cha alizeti, wameamua badala ya kuuza mbegu, wakulima hao watauza mafuta na ndiyo sababu ya kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya mashine hizo ambazo alizielezea kuwa ni za kuzungusha kwa mikono na hazihitaji mafuta wala umeme.

“Hizi nilitoa fedha yangu na sio katika mfuko wa jimbo; na kukitokea mapungufu nifahamisheni nijazilizie,” alisema.

Akizungumzia utaratibu wa mashine hizo, alisema kila Kata itakabidhiwa mashine yake na kwamba zitafungwa kwenye ofisi za kata chini ya usimamizi wa Afisa kilimo.

MASHINDANO YA MITUMBWI MUSOMA VIJIJINI YAMALIZIKA

sita

Vijana kutoka Kata ya Suguti ambao walishika nafasi ya Tatu wakishangilia mara baada ya mtumbwi wao kuwasili kwenye eneo la kumalizia mashindano.

Na. Hamisa Gamba

MASHINDANO ya mitumbwi Musoma vijijini yaliyoshirikisha timu 12 yamemalizika kwa Kata ya Etaro kuibuka na ushindi na hivyo kujinyakulia fedha tasilimu milioni moja pamoja na kombe.

Mashindano hayo yaliandaliwa na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo kwa ajili ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 ambapo washindi wa pili ambao ni Kata ya Nyakatende walijinyakulia shilingi 750,000 na washindi wa tatu ambao ni Kata ya Suguti kujinyakulia shilingi 500,000 na huku wanaofuatia walipata shilingi 20,000 kwa kila Kata.

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Musoma Vijijini na Diwani wa Kata ya Mugango, Charles Magoma, alimpongeza Profesa Muhongo kwa kuanzisha mashindano ya namna hiyo jimboni humo kwani yamekutanisha wananchi wa Musoma Vijijini kutoka pande mbalimbali za jimbo hilo.

Aliongeza kwamba mashindano hayo yameleta mwamko mkubwa miongoni mwa vijana hasa ikizingatiwa kuwa hakuna mashindano ambayo huwakutanisha vijana kwa wingi kama ilivyokuwa kwa mashindano hayo ya mtumbwi.

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo alisema aliamua kuandaa mashindano hayo na mengine ya ngoma za asili na kuimba kwaya ili kuwakutanisha wanamusoma vijijini kwa maendeleo ya afya zao na jimbo kwa ujumla.

Alisema njia mojawapo ya kuwa na afya bora ni kushiriki michezo mbalimbali na hivyo aliahidi mashindano mengine ya mieleka ambayo yatafanyika kwenye Kata ya Mugango mapema mwezi Aprili.

Aliwataka wananchi hususani vijana kujitokeza kwa wingi na kwamba washindi watapewa zawadi ambayo alisema ataitangaza siku nyingine.

Aidha, alisema kila Kata iandae washiriki wawili kwa ajili ya kushiriki mieleka na wananchi wajiandae kushuhudia mashindano hayo ya kihistoria kuwahi kutokea Musoma Vijijini.

Mashindano hayo ya mitumbwi jimboni humo yalishirikisha jumla ya Kata tisa huku kila mtumbwi ukiwa na washiriki kati ya watano hadi saba na vilevile timu moja ya kimataifa ya rafiki zake na mbunge huyo kutoka Ujerumani ilishiriki na kushika nafasi ya mwisho.

‘MSIWE NA WASIWASI, HAKUNA MTU ATAKAYEKUFA KWA NJAA’

unnamed

Wananchi wa Kata ya Nyakatende wakichukua chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya sherehe ya Krismasi.

Na. Fedson Masawa

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amewahakikishia wananchi wake kwamba, hakuna atakayekufa kwa njaa licha ya ukame wa muda mrefu unaowakabili.

Prof. Muhongo alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyakatende muda mfupi kabla ya chakula cha mchana cha pamoja na wananchi wa jimbo lake katika kusheherekea sikukuu ya krismasi.

Alisema, serikali imeshalitambua tatizo la njaa linalowakabili wananchi wa jimbo hilo na itawaletea chakula cha bei nafuu, hivyo hakuna hata mtu mmoja atakayekufa njaa.

“Kwa hiyo ndugu zangu, serikali inalitambua tatizo lenu, msiwe na wasiwasi, hakuna mtu atakayekufa kwa njaa, serikali itatatua tatizo hilo” alithibitisha Prof. Muhongo.

Aidha, akizungumzia kilimo cha alizeti, kilimo cha umwagiliaji pamoja na mbegu za mihogo, Prof. Muhongo amesisitiza kuwa, kwa mkulima yeyote anayehitaji mbegu za alizeti atoe taarifa ili kuongezea mbegu hizo.

Mbali na hilo, alisema fedha za mfuko wa jimbo zitaelekezwa kwenye vikundi vya umwagiliaji pamoja na kununua mbegu za mihogo ili kupambana na tatizo la njaa.

“Zile fedha za mfuko wa mbunge ambazo tumepata zaidi ya milioni 38, zote tutajadili kuziweka kwenye kilimo ili tutatue matatizo ya njaa kwenye jimbo lenu” alisema Prof. Muhongo.

MBUNGE MUSOMA VIJIJINI AKEMEA WIZI, UHARIBIFU WA MALI ZA UMMA

unnamed

Prof. Sospeter Muhongo akizungumza kwenye moja ya mikutano yake.

MBUNGE wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesikitishwa na wizi wa dawa na uharibifu wa baadhi ya vifaa katika Kituo cha Afya cha Murangi, Musoma Vijijini na kuagiza wahusika wachukuliwe hatua.

Agizo hilo alilitoa hivi karibuni wakati akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya afya ikiwemo vitanda maalum 10, baiskeli za wagonjwa na vifaa vingine kutoka kwa wafadhili wa Australia kwa ajili ya Kituo hicho na kushuhudiwa na wananchi mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya jimbo hilo.

Awali kabla ya makabidhiano ya vifaa hivyo, alipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusiana na wizi wa dawa uliomhusisha mlinzi wa Kituo hicho pamoja na tukio la kuharibiwa kwa gari la wagonjwa alilokabidhi mwezi Machi mwaka huu.

Taarifa husika ilimkasirisha Profesa Muhongo na hivyo kuagiza wahusika wote wachukuliwe hatua za kisheria haraka iwezekanavyo ili iwe fundisho kwa wenye tabia za namna hiyo.

Akizungumzia gari hilo, Profesa Muhongo alisema lilitolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini lengo likiwa ni kusaidia wananchi hao kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata.

Aliongeza kuwa Serikali hiyo ya Japan ilimuahidi magari mengine zaidi ikiwa gari hilo litatunzwa vizuri na kutumika kwa shughuli iliyokusudiwa.

“Hii ni aibu kubwa, hata wafadhili watatushangaa na kutucheka, dawa nyingi tulipewa na wafadhili na gari ile tulikabidhiwa ikiwa bado mpya na kwa Tanzania gari za namna hiyo zipo mbili tu, ni hapa na Muhimbili,” alisema.

Mbali na hilo aliongeza kuwa Serikali ya Japan ilitoa kiasi cha shilingi milioni 170 kwa ajili ya kuboresha Kituo hicho na kuongeza kuwa atamuomba Balozi wa Japan nchini kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hiyo.

Aliwaagiza Madiwani kufuatilia kubaini hatua iliyofikiwa ya matumizi ya fedha hiyo na alisema endapo itadhihirika kuna ubadhirifu wa aina yoyote hatua za kisheria zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kurejesha fedha hizo.

Profesa Muhongo alisema anashangazwa kupewa taarifa hiyo na wananchi huku viongozi wakiwa kimya bila kuonesha hatua walizochukua na hivyo aliwataka Madiwani kutokuwa waoga katika kuwachukulia hatua wanaofanya ubadhirifu.

Aidha, Profesa Muhongo aliwaagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Thadeus Makwanda na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Murangi, Dkt. Josephat Karambo kuhakikisha hadi kufikia 15 Januari mwakani gari hilo liwe limetengemaa.

MUSOMA VIJIJINI WAMMWAGIA SIFA MBUNGE WAO, WAMUOMBEA AFYA NJEMA

unnamed-jpg12

Mzee wa Kijiji cha Murangi- Musoma Vijijini, Clifford Biseko (kulia) akifungua rasmi mkutano wa kujadili uchumi na maendeleo ya Jimbo la Musoma Vijijini. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo.

Na. Mwandishi Wetu

WANANCHI wa Jimbo la Musoma Vijijini wamempongeza Mbunge wao Profesa Sospeter Muhongo kwa kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo ndani ya mwaka mmoja.

Pongezi hizo zimetolewa na wananchi wa jimbo hilo wakati wa mkutano wa Tathmini ya Maendeleo na Uchumi ya jimbo uliofanyika hivi karibuni katika Kijiji cha Murangi, Musoma Vijijini na kushirikisha wananchi wa jimboni humo, madiwani, wadau wa maendeleo na watendaji wa Halmashauri husika.

Awali akifungua mkutano huo mzee wa Kijiji cha Murangi, Musoma Vijijini, Clifford Biseko alisema wanamusoma vijijini wanajivunia maendeleo yanayodhihirika kila kukicha kutokana na mchango wa mbunge huyo.

Aliongeza kwamba Profesa Muhongo ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo na kuwa hawajuti kumchagua na wanamwombea afya njema ili azidi kushirikiana nao katika kusukuma gurudumu la maendeleo jimboni humo.

Alisema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, wameshuhudia masuala makubwa ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, sanaa na michezo.

Akizungumzia suala la afya, Biseko alisema, Musoma Vijijini haikuwahi kuwa na gari hata moja la wagonjwa, lakini tangu Profesa Muhongo awe Mbunge tayari jimbo hilo linayo magari manne.

Aliongeza kuwa Musoma vijijini haikuwahi kupata ugeni wa madaktari bingwa kwa ajili ya vipimo, ushauri na matibabu lakini kwa Profesa Muhongo hilo liliwezekana kwani alikaribisha madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi ambao walitoa huduma bila malipo.

Kuhusu suala la kilimo, Biseko alisema, tangu Profesa Muhongo achaguliwe, alisambaza tani kadhaa za mbegu za zao la mihogo na alizeti ili wananchi wajikwamue kwenye umasikini.

Aliongeza kuwa, Profesa Muhongo alipeleka wataalamu mahiri wa kilimo kutoka ndani na nje ya nchi ili kufanya tathmnini ya kilimo bora ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kilimo bora.

Aidha, suala la elimu, Biseko alisema kuwa kulikuwa na uhaba wa madawati 8,000 kwa shule zote zilizomo jimboni humo na hilo lilitatuliwa bila wao kuchangishwa pia kusambaziwa shehena ya vitabu vya sayansi kwa shule zote.

Biseko alimalizia kwa kuzungumzia sekta ya michezo na sanaa alisema kuwa Mbunge ameandaa mashindano mbalimbali na vilevile kugawa vifaa vya michezo kwenye vijiji mbalimbali jimboni humo jambo ambalo alisema limehamasisha sekta husika.

PROF. MUHONGO ASHEHEREKEA KRISMASI KWA KUFANYA MAKUBWA

unnamed

Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tatu kutoka kushoto waliokaa katika viti) katika picha ya pamoja na waumini wa Kanisa la Menonite mara baada ya kumalizika ibada.

Na. Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametoa mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Zahanati ya Kigeraetuma iliyopo Kijiji cha Kamuguruki, ikiwa ni zawadi ya sikukuu ya Krismasi.

Zawadi hiyo ilitolewa 25 Desemba kijijini humo katika hafla ya chakula aliyoiandaa kwa ajili ya wananchi wa Kijiji hicho pamoja na vijiji vingine.

Katika hafla hiyo Profesa Muhongo aliongozana na familia yake pamoja na rafiki zake kutoka Ujerumani ambao kwa pamoja walijumuika na wananchi wa Musoma vijijini kusherehekea.

Awali kabla ya hafla hiyo, Profesa Muhongo na ujumbe wake walishiriki ibada katika kanisa la Menonite lililopo katika kijiji cha Nyakatende na baada ya ibada hiyo walielekea katika kijiji cha Kamguruki kwa ajili ya chakula.

Mara baada ya kumalizika kwa ibada, Profesa Muhongo aliahidi kuchangia uendelezaji wa ujenzi wa kanisa hilo, na kuagiza tathmini ifanyike ya kubaini mahitaji ili achangie.

Akiwa katika kijiji cha Kamguruki, alielezwa changamoto na mahitaji mbalimbali ya kijiji hicho ikiwemo ya ukamilishwaji wa ujenzi wa zahanati husika.

“Ikiwa ni zawadi yangu ya Krismasi kwenu, nitatoa mifuko 300 ya saruji ili kuendeleza ujenzi wa zahanati,” alisema.

Profesa Muhongo alisema 26 Desemba kutakuwa na kikao cha wabunge wote wa Mkoa wa Mara kitakachofanyikia wilayani Butiama lengo likiwa ni kujadili kilimo na maendeleo ya pamoja ya Mkoa huo.

Alisema fedha za jimbo kiasi cha shilingi milioni 38 zimetumika kama ilivyokubaliwa kwa kununua mbegu za mihogo ambazo zitagawiwa kwa wananchi. “Nikimaliza huko kikao nitarudi huku kuwaletea mrejesho lakini pia kugawa mbegu za mihogo,” alisema.

Mbali na hilo, Profesa Muhongo alisema Balozi wa Korea Nchini, Song, Geum-Young anataka kutengeneza ajira kwa vijana waliohitimu Kidato cha Nne ambao hawakupata fursa ya kujiendeleza.

Alitambulisha teknolojia ya umeme jua kwa ajili ya taa na kuchaji simu ambayo alisema Balozi huyo kupitia mtaalamu wake anatarajia kuipeleka jimboni humo kwa kuwafundisha utengenezaji wake vijana hao.

“Hiki kifaa cha umeme jua kikitengenezwa gharama yake ni 15,000 kwa hiyo vijana watapewa mafunzo ya namna ya kuvitengeneza na watauza ili kujipatia kipato,” alisema.

Alisema Februari mwakani, Balozi huyo na mtaalamu wake watafika jimboni humo kwa ajili ya kutambulisha vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na kuandaa mafunzo na hivyo aliwataka wazazi wawaruhusu vijana wao kushiriki mafunzo husika.

MAMIA WAHUDHURIA KIKAO CHA KUJADILI MAENDELEO MUSOMA VIJIJINI

musomavijijiji

Baadhi ya wananchi wa Musoma Vijijini waliohudhuria mkutano huo wakimsikiliza Mbunge wao, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).

Na Fedson Masawa

MAMIA ya wananchi wamejitokeza kuhudhuria kikao maalumu cha kujadili uchumi na maendeleo ya jimbo lao kilichofanyika jana kwenye kijiji cha Murangi, Musoma vijijini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wa serikali, madiwani, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wasomi mbalimbali wakiwemo waliozaliwa ndani ya jimbo hilo.

Waliowakilisha serikali kwenye kikao hicho ni Mkuu wa wilaya ya Musoma Dk. Vincent Naano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma, Frola Yongolo.

Awali akizungumzia kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Mbunge wa Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo aliwataka viongozi wa idara zote na madiwani wajipange kwa sehemu zao na kuhakikisha kila kitakachojadiliwa kinafuatiliwa ndani ya miezi minne kwa ajili ya kupima utekelezaji wa maazimio ya kikao hicho.

Mambo yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na Elimu, Afya na kilimo kama yalivyoainishwa kwenye vipaumbele vya jimbo la Musoma Vijijini.

Elimu

Akianza na suala la Elimu, Prof. Sospeter Muhongo amefafanua kuwa, madawati bado hayajatosha kwani ukizingatia idadi ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba na wale walioandikishwa darasa la kwanza na upungufu wa madawati ya shule za sekondari, bado kutakuwa na upungufu wa madawati 5000 ndani ya jimbo zima.

Ili kufanikisha zoezi hili, Mbunge ameiagiza halmashauri kulisimamia na kuhakikisha hakutokuwa na upungufu wa madawati. Pia aliwaomba wote wenye moyo wa kuchangia wawasiliane na mkurugenzi wa halmashauri kupitia namba ya simu: +255754414441

“Kwa hiyo ndugu zangu hiyo kazi tunaiweka mikononi mwa halmashauri na watakaohitaji kuchangia, ni vizuri muwasiliane na mkurugenzi” alitoa utaratibu Prof. Muhongo.

Kwa upande wa ujenzi wa vyumba vya madarasa, Prof. Muhongo amebainisha kuwa, kuna upungufu wa vyumba 748 vya madarasa kwa shule zote za msingi na sekondari na tayari ameshafanya mazungumzo na JKT kwa ajili ya kupatiwa vijana watakaofanya shughuli za ujenzi wa vyumba hivyo jimboni.

Pia ameongeza kuwa vifaa ikiwemo saruji na mabati vitanunuliwa moja kwa moja kutoka viwandani na ameshakamilisha mazungumzo na makampuni mawili; TWIGA CEMENT kwa ajili ya saruji pamoja na ALUMINIUM AFRICA kwa ajili ya mabati.

Akizungumzia utaratibu wa kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, Prof. Muhongo amesisitiza kuwa, fedha zote zitakazochangwa zinakwenda moja kwa moja kwenye akaunti ya kampuni husika, jimboni vitaletwa vifaa tu na vifaa vikifika vielekezwe kwenye maeneo husika.

“Hatutoi hela mkononi, unapokea mabati na simenti, na simenti ikifika naomba iende moja kwa moja kwenye eneo husika isikae stoo” alisisitiza Prof. Muhongo.

Wakichangia kipengele cha ujenzi, wananchi na viongozi wa jimbo la Musoma vijijini wamekubaliana na Mbunge wao na kuahidi kuungana pamoja na pia kuacha malumbano ili kusukuma gurudumu la maendeleo ya jimbo hilo.

“Kinachotuumiza ni ubishi, lakini tunaamini tupo pamoja na wewe na tunaahidi kukupa ushirikiano. Pia hatutaweza kuwavumilia viongozi wazembe wa halmashauri watakaoonesha namna fulani ya kurudisha nyuma maendeleo ya Musoma vijijini” alisema Mambo Japan, Diwani wa kata ya Bulinga.

Kuhusu ujenzi wa shule za sekondari za elimu ya juu; Akigusia pia suala hilo, Prof. Muhongo amesisitiza ujenzi wa sekondari za mfano za sayansi; Mkirira, Mugango, Bugwema na Mtiro kuwa kasi iongezeke ili ifikapo mwaka 2018 ziwe tayari na ziwe zimeanza kutumika ambapo amesisitiza kuwa ni shule za masomo ya sayansi.

Kilimo

Suala la kilimo pia limezungumzwa ambapo Prof. Muhongo amesisitiza wananchi kuendelea kulima mazao ya biashara na chakula kwa ajili ya kuondokana na umaskini na kuongeza chakula kwa kila kaya.

Akizungumzia suala la mbegu za alizeti, Prof. Muhongo amesema tayari jumla ya tani 5 za mbegu za alizeti zimeshawasili jimboni na tayari wakulima wameshapewa mbegu hizo bure. Aliongeza kuwa endapo kutakuwa na wakulima wanaohitaji mbegu hizo basi watoe taarifa zinunuliwe nyingine.

“Tani 5 za mbegu za alizeti sawa na kilogramu 5000 zimeshagawiwa kwa wakulima. Kama kuna watu bado wanahitaji waseme mbegu ziagizwe tena” alisema Prof. Muhongo

Akizungumzia utaratibu wa soko la alizeti, Prof. Muhongo amewathibitishia wananchi kuwa soko la uhakika litakuwepo na pia mashine ndogo ndogo za kukamua zitatolewa kwa baadhi ya kaya ili wakamue na kuuza mafuta.

“Mwaka jana tuliuza, mwaka huu tutauza na tutakuwa na mashine ndogo ndogo za kukamua mafuta. Pia nimeshafanya mawasiliano na mmiliki wa kiwanda kikubwa cha mafuta na amenithibitishia kufika jimboni kwa ajili kununua alizeti” alithibitisha Prof. Muhongo.

Kilimo cha umwagiliaji na mbegu za mihogo; Prof. Muhongo mbele ya mamia ya waliohudhuria kikao hicho amependekeza fedha za mfuko wa jimbo Tshs. 38,479,000/= zielekezwe kwenye vikundi vya kilimo cha umwagiliaji pamoja na kununulia mbegu za mihogo na ameomba madiwani watayarishe orodha ya vikundi vitakavyonufaika na fedha hizo.

Aidha, Prof. Muhongo amependekeza pia kikao cha kuhidhinisha fedha hizo kifanyike 26, Disemba 2016 saa 9:00 alasiri kijijini Tegeruka.

Uvuvi, suala la ufugaji wa samaki; suala hili pia limesisitizwa kwa madiwani na halmashauri kutakiwa kuorodhesha maeneo ya ziwani yanayofaa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa wa samaki. Prof. Muhongo amependekeza kikao cha ufuatiliaji wa maazimio kifanyike kijijini Bugoji baada ya miezi minne kuanzia sasa.

Afya

Wakizungumza kuhusu ujenzi wa vituo vitatu vya afya jimboni; Bukima, Nyegina na Mugango, Madiwani wa kata hizo wamesema kuwa ujenzi wa vituo umeaanza na unaendelea vizuri.

“Nyumba ya mganga boma tayari limekamilika na maboma ya wodi yapo tayari hivyo naomba halmashauri itusaidie kuezeka kwani tunatarajia kufikia 2017 tutakuwa tumekamilisha” alifafanua Mchele Majira, Diwani wa kata ya Nyegina.

Kwa upande wake Prof. Muhongo ameongezea kuwa kila mwananchi awe mlinzi wa mali zinazoingizwa jimboni ili zitumike katika matumizi sahihi na kuendelea kuwapa moyo wale wanaojitolea kulisaidia jimbo la Musoma vijijini.

Alisema kwa wale madiwani watakaopewa msaada wowote kwenye kata zao ikiwa ni pamoja na magari na vifaa vya ujenzi na kushindwa kusimamia vizuri, hatosita kupeleka kata nyingine ambako wanajali.

Halmashauri kufanyia vikao vyote Murangi

Mbunge, Madiwani, Mkurugenzi kwa pamoja wamekubaliana kwa kauli moja mbele ya wananchi wa jimbo la Musoma vijijini kuwa vikao vyote vya halmashuri vitakuwa vinafanyika Murangi. Lengo kubwa ni kutaka kuijenga makao makuu ya halmashauri ya Musoma vijijini ambayo ni Murangi.

Akizungumza na wananchi na viongozi wa ngazi zote, Prof. Mukama Biswalo mwakilishi maalum wa umoja wa Afrika huko Sudan ya Kusini ambaye pia ni mzaliwa wa Musoma vijijini alisema: “hatuwezi kuijenga halmashauri yetu wakati vikao tunafanyia mjini badala ya Murangi. Bila kufanya hivi, haiwezekani kuijenga halmashauri ya Musoma Vijijini.”

“Mkurugenzi, make history kuwa mkurugenzi wa kwanza kuanzisha makao makuu ya Musoma vijijini Murangi. Hatuwezi kuijenga halmashauri wakati hatutaki kufanyia vikao vyetu Murangi” alisisitiza Prof. Biswalo.

MBUNGE MUSOMA VIJIJINI ATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA KIMBUNGA

untitled-33

Prof. Muhongo akimkabidhi vifaa Nyakaita Magati (mwenye fulana nyekundu) mifuko ya saruji 40, misumari kilo 10 na mabati 24 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba iliyoezuliwa na kubomolewa na kimbunga katika Kata ya Ifulifu.

Na Ramadhan Juma

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo, ametoa msaada kwa kaya tano zilizoathirika na kimbunga katika kata mbili za Ifulifu na Bukima.

Msaada uliotolewa ni pamoja na mabati 105, mifuko ya saruji 105, mbao za kenchi 15 na misumari Kilo 56.

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo vya ujenzi, Prof. Muhongo aliwataka wananchi waliokabidhiwa vifaa hivyo wavitumie kwa matumizi yaliyokusudiwa ya kuboresha makazi yao yaliyoharibiwa na kimbunga na si vinginevyo.

Mmoja wa wananchi waliopokea msaada huo, Tatu Richard alimshukuru mbunge kwa kuguswa na tukio lililompata na kusema kuwa pamoja na kuwa na watoto wengi bado hakuona mtoto wake hata mmoja aliyeguswa na tukio hilo.

“Mimi ni mzee, ninao watoto wengi, lakini hayupo hata mtoto mmoja kati ya wanangu aliyeguswa na tukio hili. Ninamshukuru sana mbunge wangu kwa kuniona na kunisaidia” alishukuru Tatu.

Naye Nyakaita Magati alishukuru kwa msaada wa mabati 24, saruji mifuko 40 pamoja na kilo 10 za misumari na kusisitiza kuwa hakuamini kwa kile alichokifanya Mbunge huyo kuwasaidia kurudisha nyumba zao kwenye hali nzuri baada ya kuharibiwa na upepo mkubwa.

“Siamini macho yangu kama hili linalofanyika hapa kwangu ni tukio halisi. Naona kama miujiza, hakika nina kila sababu ya kukushukuru mbunge wetu kwa kutujali, kumbe kura yetu tuliiweka panapostahili na leo tunayaona matunda yake” alisema Magati kwa furaha.

Mkazi mwingine Pili Mabele aliyekabidhiwa mabati 21, mifuko 5 ya saruji na kilo sita za misumari alimshukuru Mbunge kwa msaada aliompatia na kutoa somo kwamba ni vema kumheshimu na kumthamini kila mmoja bila kujali kama ni ndugu yako.

“Hakika ni jambo la kipekee na la kushukuru hata kama ni mbunge kuja kutoa msaada kama huu kwa mtu ambaye hana imani kama alimpigia kura. Hii imetuonesha njia kuwa kila mtu lazima amjali mwenzake hata kama siyo ndugu yake” alishukuru na kueleza Pili Mabele.

Sambamba na msaada huo, Prof. Muhongo amekabidhi Jefu Kibhisa taa moja inayotumia mwanga wa jua pamoja na chaja moja ya simu inayotumia mwanga wa jua.

Akikabidhiwa vifaa hivyo ambavyo vimeenda sambamba na msaada wa mabati 23, misumari kilo 20 na saruji mifuko 50, Jefu ameshukuru na kumpongeza Prof. Muhongo kwa jitihada za kuijali jamii ya jimbo lake.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi na uongozi wa kijiji cha Kiemba, Mwenyekiti wa kijiji hicho Golo Atanas alimshukuru mbunge kwa msaada alioutoa kwa watu walioathirika na kimbunga.

Akikamilisha ziara yake katika kijiji cha Bukima kata ya Bukima, Prof. Muhongo amemkabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi Perusi Turuka ambaye ni muhanga wa kimbunga katika kijiji cha Bukima kata ya Bukima.

Vifaa alivyokabidhiwa mkazi huyo wa Bukima ni Mifuko 5 ya saruji, mbao 15 za kenchi, mabati 10 na Kilo 10 za misumari.

Sambamba na msaada huo, Prof. Sospeter Muhongo amesisitiza suala la kilimo kuwa ndio mbinu pekee inayoweza kuondoa umaskini na njaa Tanzania hivyo wananchi wanatakiwa kulima mazao ya chakula kwa wingi na mazao ya biashara ili kuondokana na utegemezi.

“Ndugu zangu, mimi ninaamini kweli hali ya hewa haikuwa nzuri, lakini tunatakiwa tulime kilimo cha kisasa…” alisema Prof. Muhongo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Musoma vijijini, Yahana Mirumbe, alimshukuru mbunge kwa jitihada za kuwa karibu na jamii nzima ya jimbo lake na kuitaka jamii hiyo kujenga nyumba bora zenye hadhi ya kuwekwa umeme ili kuepuka madhara yatokanayo na umeme ikizingatiwa wakati wowote watawekewa umeme.

KILIMO CHA MPUNGA CHAANZA TENA BAADA YA VIBOKO WAHARIBIFU KUUAWA

untitled

Bi. Nyanjagi Michael akiwa katika shughuli za kupanua shamba lake kwa ajili ya kilimo cha mpunga.

Na Fedson Masawa

MASHAMBA makubwa ya mpunga yaliyotelekezwa kutokana na wakulima kuhofia viboko waharibifu yameanza kulimwa katika maeneo tofauti ya kata za kandokando mwa ziwa Viktoria, jimbo la Musoma vijijini.

Hatua hiyo imekuja mwezi mmoja baada ya mtaalamu aliyesaidia kudhibiti tatizo la viboko waharibifu jimboni na kuwahakikishia wakulima kuanza kutumia mashamba yao bila hofu yoyote.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mkazi wa kijiji cha Bukumi, Nyanjagi Michael alisema wanashukuru mafanikio ya mtaalamu huyo ambaye amewasaidia kurudi kwenye mashamba yao na kuendelea na kilimo cha mpunga.

“Tunamuamini sana mtaalamu wetu, amefanya kazi nzuri kwa maana ameweza kuua viboko wawili hadi sasa hatuwaoni tena kama ilivyokuwa awali, mashamba yetu tuliyoyatelekeza tunahakikisha tutalima bila hofu yoyote” alisema Nyanjagi.

Katika hatua nyingine, mkazi mwingine wa Bukumi, Nyasami Mgono ameishukuru ofisi ya Mbunge kwa kazi nzuri na yenye mafanikio iliyofanyika ya kumpata mtaalamu ambaye amekuja jimboni humo kutatua tatizo lililoshindikana kwa miaka mingi.

“Binafsi naishukuru sana ofisi ya Mbunge wetu, kwa kazi nzuri inayofanyika kwani ni kazi yenye mafanikio. Tuliangaika kwa kipindi kirefu na sasa tumerudia kilimo cha mpunga kwenye mabonde yetu” alisema Mgono.

Kwa upande wake Nyangaso Mabure, alisema kwa mafanikio yaliyopatikana baada ya kudhibiti viboko waharibifu, wakazi wa maeneo ya kandokando mwa Ziwa Viktoria wataanza kunufaika na maeneo yao na kuwaomba viongozi wao kudhibiti kila dalili zozote zinazoashiria uvurugaji wa mazao yanayolimwa na wakulima katika maeneo hayo.

“Kwa hatua iliyofikiwa ya kudhibiti viboko waharibifu waliotusumbua kwa muda mrefu, tunaamini kila mmoja wetu kwenye eneo lake ataanza kulitumia bila kuhofu” alisema Nyangaso.

“Tunachozidi kuwaomba na kuwasihi viongozi wetu wanaohusika na hili tatizo wazidi kuwa na moyo kuendelea kudhibiti dalili zote zinazoweza kuharibu na kuvuruga mazao yetu” aliongeza na kuomba Nyangaso.

Afisa kilimo wa kijiji cha Bukumi, Alex Mihambo amethibitisha jitihada za wakulima wa kandokando mwa ziwa Viktoria hasa kijiji cha Bukumi kwa kurudisha imani yao na kuwasihi wakulima kwa kuzingatia ushauri wa wataalam.

“Wakulima hawa kweli wamerudisha imani yao baada ya kusumbuka kwa kipindi kirefu, sasa wameamua kulima mpunga katika maeneo haya. Ninachozidi kusisitiza ni kulima kilimo cha kisasa kwa kufuata ushauri wa kitaalamu” alisema na kusisitiza Alex Mihambo.